|
Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, akipungia mkono wananchi wa jijini Mwanza waliojitokeza hii leo kumlaki tokea airport hadi kwenye mkutano viwanja vya Magomeni Kirumba. |
MAELEZO: HISANI YA MWANANCHI
BAADA ya vuta vikuvute ya muda mrefu, hatimaye leo Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kumtangaza mgombea wake wa
urais katika mkutano maalumu utakaofanyika jijini Mwanza.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa chama hicho Kanda ya
Ziwa Magharibi na makao makuu zilisema kuwa leo mgombea huyo atatangazwa
mkoani hapa huku zikibainisha kuwa anayepewa nafasi kubwa ni Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa.
Taarifa hizo
zimekuja wakati kukiwa na tetesi kuwa chama hicho kilikuwa kinafanya
mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa anawania
urais kupitia CCM na kutemwa katika hatua za awali, huku vyanzo
mbalimbali vikisema mazungumzo hayo yanachukua muda mrefu na kuna
uwezekano mkubwa wa kutozaa matunda.
Jana, Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge walikaririwa
wakitoa matamko ya kumkaribisha Lowassa kuingia Chadema lakini kwa
sharti la kufuata kanuni na taratibu za chama hicho, lakini Dk Slaa
alisita kumzungumzia kiongozi huyo akiahidi kuzungumza mambo
yatakapokuwa sawa.
Mratibu wa Operesheni za Chadema
Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu alisema mgombea huyo (bila
kumtaja jina), atatangazwa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika
kwenye Viwanja vya Magomeni, Ilemela kuanzia saa nane mchana.
Njugu alisema katika mkutano huo, viongozi wakuu wa Ukawa wanatarajia kuwapo na maandalizi yake yamekamilika.
“Kesho
(leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Magomeni,” alisema
Njugu na kuongeza: “Mgombea urais kupitia Ukawa atajulikana hapo, kwani
tunatarajia viongozi wakuu wa Ukawa watamtangaza.”
Katika
mazingira tofauti, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Geita juzi,
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidokeza jina la Dk Slaa kama
mgombea urais wa chama hicho, kitendo kilichoibua hamasa na umati
kumshangilia, lakini akawapoza akisema ulimi umeteleza.
Alipoulizwa
kuhusu mkutano huo, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikiri kuwa
leo kulikuwa na mpango wa kumtangaza mgombea wa Ukawa, lakini alidhani
ingekuwa Dar es Salaam, hivyo kwa kuwa wameamua iwe Mwanza angefanya
utaratibu wa ndege ili aweze kuwahi.
Mwenyekiti wa
NCCR- Mageuzi, James Mbatia hakupatikana kuzungumzia mkutano huo, lakini
Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe alisema hakuwa na taarifa
hizo, hasa kwa kuwa vikao vya mwisho vilivyofanyika Jumapili na Jumatatu
vilihusisha wenyeviti wa vyama pekee.
|
Kiwia Ilemela (kushoto) Wenje Nyamagana (kulia) wote kugombea kupitia CHADEMA. |
Hata hivyo,
alisema ilibidi mgombea huyo atangazwe ama jana au leo. Chama cha CUF
kimekwishatangaza kuwa kinasubiri uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la
Uongozi litakaloketi Julai 25 kuamua juu ya hatima yake ndani ya Ukawa.
Alipotakiwa
kudokeza ni nani atasimama kuwakilisha Ukawa, Njugu alisema jukumu hilo
ni la viongozi wa juu na kwamba yeye akiwa kiongozi wa Kanda anatambua
mgombea urais wa Ukawa atatangaziwa Mwanza leo.
Lissu arusha watu roho Geita
Akihutubia
mkutano wa hadhara juzi, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida
Mashariki alisema mgombea wa Ukawa anafahamika ndani na nje ya nchi na
kinachosubiriwa ni kutangaza jina lake baada ya taratibu kukamilika
akisisitiza kwamba chama hicho hakitashindwa kwa goli la mkono.
Aliwaambia
wananchi wa Mji wa Geita waliokuwa wamefurika kwenye Viwanja vya Shule
ya Msingi Nyankumbu kuwa Ukawa wamechelewa kumtangaza mgombea huyo
kutokana na kuchelewa kupatikana mgombea mweza kutoka Zanzibar.
“Ndugu
wananchi mgombea wa Ukawa nimtaje, nisimtaje,” aliwauliza wananchi
waliofurika kwenye mkutano huo, nao wakaitikia, “mtajeee”
“Tumeshampata
mgombea urais wa Ukawa na mnampenda sana na mnamjua sana.
Ni mtu
anayefahamika nchi nzima na duniani kote,” alisema Lissu huku
akishangiliwa na wananchi.
Huku wananchi wakiwa na
shauku ya kujua jina la mgombea, Lissu alisema baada ya taratibu za
kumpata mgombea mwenza kukamilika, mgombea huyo atatangazwa.
“Siku tunamtangaza mtajua tu, tutaita vyombo vyote vya habari ili kumtangaza kwa hiyo mtamjua,” alisema Lissu.
Wakati
Lissu akitoa ufafanuzi huo, alijikuta akitaja jina la Dk Slaa na
kusababisha umati uliokuwa umefurika uwanjani hapo kushangilia.
“Kuna
mambo yametuchelewesha, lakini wakati tunashughulika kumtangaza Dk
Slaa... Wananchi (wakalipuka kushangilia)..., Lissu akaendelea,
“Samahani ulimi hauna mfupa, samahani sana naomba mniwie radhi
jamani…jamani, jamani, tulieni.”
Alisema umoja huo bado
una presha kubwa kuhusu kutaja jina la mgombea na kuwa wapo baadhi ya
viongozi wa Serikali na vyama hasimu ambao wanaombea Ukawa iparaganyike.
“Wapo
wanaotuombea mabaya Ukawa na wengine wanapewa fedha ili kuhakikisha
Ukawa inavunjika.
Kamwe Ukawa haitavunjika. Ninawahakikishia wananchi
kwamba Ukawa iko imara na haitavunjika hata wakituombea mabaya,” alisema
Lissu.
Amtaja Dk Magufuli
Akimzungumzia
mgombea wa CCM, Dk John Magufuli, Lissu alisema Ukawa haitishiki naye
kwa sababu hajawahi kuzungumzia kero zinazowakabiliwa wananchi, yakiwamo
mateso yaliyowapata wafugaji baada ya ng’ombe wao kuuawa na wengine
kuteswa wakati wa Operesheni Tokomeza.
Alisema tangu
kuibuka kwa tuhuma mbalimbali dhidi ya Serikali iliyopo madarakani
likiwamo sakata la Richmond na Tegeta Escrow, Dk Magufuli hajawahi
kusimama na kuutangazia umma nini msimamo wake kuhusiana na kashfa hizo.
Bulaya atajwa Chadema
Mkutano
huo utakaorushwa moja kwa moja katika televisheni, pia unatarajia
kumpokea Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyetangaza
kukihama chama hicho juzi bila kuweka wazi anakohamia.
Hata
hivyo, mbunge huyo ambaye tayari ameweka wazi kupitia ukurasa wake wa
Facebook kuwa atawania ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini, amekaririwa
na gazeti hili akisema hatima yake itakuwa hadharani leo.
|
Mbunge
wa Kahama (CCM), James Lembeli akiwa kwenye msafara ndani ya gari la wazi. |
Lembeli rasmi Chadema
Mbunge
wa Kahama (CCM), James Lembeli jana alihitimisha uvumi kuwa angehamia
Chadema baada ya kutangaza rasmi kujiunga na chama hicho na papo hapo
akatangaza kulitetea jimbo hilo kupitia chama hicho cha upinzani.
Lembeli
(58), ambaye pia anatarajiwa kutambulishwa rasmi katika mkutano wa
Mwanza, aliwaambia wanahabari Dar es Salaam jana kuwa amekihama chama
tawala baada ya kushindwa kuvumilia fitna na rushwa.
“Nimekaa,
nimetafakari, nimezungumza na mama yangu kwa muda wa zaidi ya saa 10,
mke wangu na watoto na kwa kusikia kilio cha wananchi wa jimbo la zamani
la Kahama nimeamua yafuatayo; kwanza ni kujiondoa uanachama wangu ndani
CCM.
“Sikupenda ila nimelazimika kuchukua uamuzi huu,
najua umewauma wengi na kuwakera wengi lakini nawaomba nao waangalie
hali ya viongozi wa wilaya wa Kahama waliosababisha hayo… ni uamuzi
mgumu sikupenda iwe hivyo na pili, kuanzia leo najiunga na Chadema,”
alisema Lembeli aliyeambatana na binti yake ambaye pia alijiunga nacho.
Mbunge
huyo aliyeitumikia CCM katika nafasi hiyo kwa miaka 10, aliwataka
wananchi wa Jimbo jipya la Ushetu alikozaliwa kutovunjika moyo na kuunga
mkono safari yake mpya akiahidi kuwa atakuwa nao bega kwa bega kama
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alipoulizwa kwa nini aliamua
kuhamia Chadema na siyo vyama vingine vya upinzani, Lembeli alisema ni
chama cha pili kwa nguvu na kina mtandao nchini, hivyo asingependa
kuhamia chama ambacho angeanza upya safari yake ya kisiasa.
“Mimi
nimeonyesha nia kutoka rohoni ya kuhamia Chadema, nitapitia mchakato
wote wa kumtafuta mgombea ili nipate ridhaa ya kupererusha bendera ya
chama hicho na nina uhakika kwa Kahama kwa asilimia 100 nitapita… iwapo
nitafeli mimi sina mpango mbadala na nimeshajiunga Chadema mpaka
mwisho,” alisema.
Si mtandao wa Lowassa
Huku
akizungumza kwa umakini, Lembeli alisema Watanzania wanapaswa kufahamu
kuwa yeye si miongoni mwa makada wanaoihama CCM kutokana na kukatwa kwa
Lowassa, bali kutokana na rushwa iliyokithiri, hivyo hatua hiyo (ya
kukimbia rushwa), itamsaidia kukwepa fedheha.