Mwamuzi ambaye alipiga kipyenga cha mwisho mapema kabla ya kumalizika kwa muda kamili wa mechi katika mechi la Kombe la mataifa ya Afrika anadai angekufa kwa joto kali.
Mzambia Janny Sikazwe alimaliza mechi ya Tunisia dhidi ya Mali sekunde 13 kabla ya kumalizika kwa dakika 90 za mechi, ambapo awali alipiga kipyenga cha kumaliza mechi dakika tano mapema, kabla ya kuangalia muda na kuanzisha tena mechi.
"Nimewaona watu wakienda kufanya majukumu nje ya nchi na kurejea nyumbani wakiwa ndani ya jeneza," alisema.
"Nilikaribia kabisa kurudi kama hivyo "Nilikuwa na bahati sikupoteza fahamu. Ingekuwa hadithi nyingine tofauti sana.
"Madaktari waliniambia mwili wangu haukuwa unapoa. Ilibakia muda kidogo tu ningekuwa nimeingia hali ya kupoteza fahamu , "Ninafikiri Mungu aliniambia nimalize mechi. Aliniokoa."
Mechi ya kundi F huko Limbe iliyochezwa siku ya Jumatano, tarehe 12 Januari ilimalizika kwa utata huku makocha kutoka Tunisia, ambao walikuwa wamefungwa bao 1-0 na kucheza dhidi ya wachezaji 10, wakikimbilia ndani ya uwanja kumkabili Sikazwe na wasaidizi wake baada ya kumaliza mechi mapema.
Hatahivyo, Sikazwe alishikilia uamuzi wake na alihitaji maafisa wa usalama kumsindikiza nje ya uwanja.
Dakika ishirini baada ya shindano waandaaji waliamuru mechi ichezwe mpaka ikamilike ,lakini wachezaji wa Tunisia hawakurudi uwanjani na Mali wakatangazwa washindi.
Baadaye Tunisia iliwasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la soka Barani Afrika, lakini hilo lilikataliwa na matokeo yakaidhinishwa.
Hali ya joto ya Cameroon ambayo imesababisha baadhi ya mechi kuchezwa katika nyuzi joto 30 na unyevunyevu,imesababisha matatizo katika Kombe hilo- huku watetezi wa kombe hilo Algeria wakielezea kuwa ni sababu ya wao kutoka sare ya 0-0 na Sierra Leone.
Akizungumza na vyombo vya habari vya Zambia wakati alipowasili nchini, Sikazwe alisema athari za hali ya hewa katika Limbe ilikuwa ni sababu ya kucheza vibaya katika kipindi cha mwisho.
"hali ya hewa ilikuwa ya joto sana, na unyevunyevu ulikuwa ni karibu 85%," alisema.
"Baada ya kupasha misuli nilihisi vingine. Tunajaribu kunywa maji lakini hatukuweza kuhusu maji yanakata kiu - hakuna kitu.
"Lakini sisi [maafisa wa mechi] tunaamini sisi ni wanajeshi na tunaendelea mbele na kupambana.
"Kila kitu nilichovaa kilikuwa na joto. Hata vifaa vya mawasiliano, Nilitaka kukitupa. Nilihisi joto sana."
Kipindi cha pili cha mchezo kilishuhudia kusitishwa mara kadhaa kwa mchezo ikiwa ni pamoja na waamuzi wawili wasaidizi kutathmini (VAR), mapumziko ya kunywa vinywaji na madirisha matano ya kubadilisha wachezaji na walau dakika tano za majeruhi zilitarajiwa kuongezwa.
Hatahivyo, Sikazwe alisema hakuweza kuwasiliana na maafisa wenzake wa mechi.
"Nilianza kuchanganyikiwa. Sikuweza kumsikiliza yeyote," alisema.
"Nilifika wakati ambapo nilianza kusikia kelele fulani na nilidhani mtu fulani alikuwa anawasiliana na mimi na watu walikuwa wananiambia 'hapana umemaliza mechi'.Ilikuwa ni hali ya ajabu.
"Nilikuwa ninajiuliza kichwani kujua ni nani aliniambia nimalize mechi. Labda nilikuwa najiongelesha mwenyewe, sijui. Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa mbaya ."
Siku moja baada ya mechi ya Tunisia na Mali Sikazwe alikwenda hospitali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya moyo, damu na mwili-lakini vipimo vilikuja vikiwa vya kawaida.
Pia aliwapokea hotelini kwake maafisa wa soka ikiwa ni pamoja na Rais wa Caf Patrice Motsepe na Andrew Kamanga, Rais wa shirikisho la soka la Zambia.
Sikazwe alirejea kazini katika Kombe la Mataifa ya Afrika Jumanne tarehe 18 Januari, akisimamia mashine ya VAR kwa kundi la mechi baina ya Gabon na Morocco.
Awali alisimamia mchezo wa fainali za Kombe la mataifa mwaka 2017 na mechi mbili za makundi katika Kombe la dunia la mwaka 2018,na aliapa kuendelea kuwa mwamuzi.
Sikazwe anatarajia kusimamia mechi katika kombe la Shirikisho la Afrika mwishoni mwa mwezi wa Februari.
"Familia yangu, watu wa Zambia, mna bahati ninaongea nanyi sasa hivi ," alisema.