ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 3, 2019

WAFANYAKAZI TIGO KIZIMBANI KWA KUINGILIA MIAMALA YA FEDHA ZA WATEJA.


Wafanyakazi wanne wa kampuni ya mawasiliano ya  Tigo na wananchi sita wanaodaiwa kushirikiana nao wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya kujipatia mamilioni ya fedha kwa kuingilia miamala ya fedha za wateja, udanganyifu na kutakatisha fedha.

Waliofikishwa mahakamani ni Raia wa Burundi, Hamis Singa (30) ambaye ni kiongozi wa wafanyakazi wa Tigo mjini Babati na wenzake wanne (si wafanyakazi wa kampuni hiyo) ambao wanatuhumiwa kujipatia Sh milioni 26 kutoka kwa wateja wa Vodacom na Airtel  kwa njia ya ulaghai.

Wengine ni wafanyakazi watatu wa Tigo Mlimani City na wenzao wawili (si wafanyakazi wa kampuni hiyo) ambao wanadaiwa kujipatia zaidi ya Sh milioni 20 na kutakatisha fedha hizo huku wakijua ni zao la uhalifu.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salim Ally.

Wakisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ilidaiwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka saba likiwemo moja la kutakatisha fedha.

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni Hamis Singa, Jailos Joseph (33), Singa Mnunga (32), Japhet Mkumbo (33) na Omari Omari (33) wote ni wakulima wanaishi Babati na Arusha.

Alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa tarehe isiyofahamika kati ya Januari na Julai, 2019 maeneo ya Arusha, Manyara na sehemu nyingine nchini walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la pili washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho kwa ulaghai walijipatia Sh 26,432,441 kwa kuhamisha fedha hizo kutoka kwa wateja wa Vodacom na Airtel.

Washtakiwa wanadaiwa katika shtaka la tatu walisambaza ujumbe usemao ‘Tuma pesa kwenye namba hii’ huku wakijua ujumbe huo wa uongo wenye nia ya kupotosha umma.

Shtaka la nne kwa washtakiwa wote, wadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwa watu mbalimbali ukielekeza kutuma fedha kwenye simu iliyosajiliwa kwa majina mengine.

“Mheshimiwa Hakimu shtaka la tano lina wakabili washtakiwa wote wanadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwa nia ya kujipatia fedha.

“Shtaka la sita linamkabili mshtakiwa Hamis, anadaiwa akiwa mwajiriwa wa Kampuni ya Tigo kwa ulaghai alipata uwezo wa kuingilia miamala ya fedha ya mawakala wa tigo kwa nia ya kujipatia fedha.

“Shtaka la saba kwa washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh 26,432,441 huku wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu,”alidai Wankyo.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu kesi hiyo imefunguliwa chini ya sheria ya Uhujumu Uchumi ambapo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Kesi itatajwa Agosti 15 mwaka huu.

MAAJABU YA MAZIWA YA MAMA KATIKA UBONGO WA MTOTO


WAKATI ulimwengu ukiadhimisha wiki ya kimataifa ya kunyonyesha mtoto (Agosti 1 hadi 7) na kuelezea faida zake kwa wazazi na taifa, wakazi wa jiji la Mwanza, kwenye kata mbalimbali na viunga vyake tofauti tofauti wanaendelea  kuhamasishwa kufahamu umuhimu wa maziwa ya mwanzo kabisa ya mama kwa mtoto .

Shirika la Amref Health Africa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) linatekeleza programu ya  Lishe kupitia programu ya 'Right Start Initiative' inayolenga kuboresha huduma za lishe kwa wakinamama wajawazito, watoto wachanga na watoto chini ya miaka miwili na wasichana wa rika balehe katika mikoa ya Mwanza na Simiyu.

SHUHUDIA YALIYOJIRI SIKU YA PILI YA UELIMISHAJI KATA YA MHANDU WILAYANI NYAMAGANA MKOANI MWANZA.  (CHUNGULIA VIDEO)

* DONDOO ZA AFYA NA KUNYONYESHA
Kunyonyesha ni moja ya njia sahihi ya kuhakikisha mtoto anakuwa mwenye afya na kuendelea kuishi.

Kama viwango vya kunyonyesha vingekuwa vya hali ya juu duniani , takriban maisha      820 000 ya watoto yangenusurika kila mwaka, linasema shirika la afya duniani (WHO).

Unyonyeshaji wa mtoto kwa miezi 6 kuna faida nyingi za kiafya kwa mama na mtoto.

Kumnyonyesha mtoto mara anapozaliwa kwa kipindi cha saa moja, humkinga kwa maambukizi yanayowapata watoto wachanga na kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Maziwa ya mama pia ni chanzo muhimu cha nguvu na virutubisho kwa watoto wa kati ya miezi 6 hadi 23.

Maziwa ya mama yanaweza kuchangia nusu au zaidi ya nguvu za mtoto katika umri wa miaka 6 hadi 12.

Watoto na vijana wadogo walionyonyeshwa wakiwa wachanga wana uwezekano mdogo wa kuwa na uzito wa mwili wa kupindukia .

Unyonyeshaji wa mtoto humsaidia kuboresha uwezo wa utambuzi wa akili (IQ), mahudhurio ya shule , na pia huhusishwa na mapato ya juu katika maisha yake ya utu uzima.

Kunyonyeshwa kwa muda mrefu pia huchangia afya na maisha bora ya mama kwani humpunguzia hatari ya kupata saratani ya mfuko wa mayai ya uzazi na matiti.

Kunyonyesha hutengeneza vichocheo vyamwili( hormone) ambazo humtuliza mama na mtoto.

Juma hili linaadhimishwa huku baadhi ya wanawake duniani wakishindwa kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo kutokana na sababu mbali mbali. .

Friday, August 2, 2019

NAMNA UNAVYOWEZA KUPOTEZA SIFA ZA KUINGIZWA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA



 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo Agosti 02, 2019 imekutana na wadau wa uchaguzi mkoani Mwanza wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, dini, asasi za kiraia, makundi ya watu wenye ulemavu, vijana, wanawake na wanahabari ili kupeana elimu kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni maandalizi kuelekea chaguzi zijazo. 

jEH wazijua sababu zinazoweza kukuondosha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura?

Nini lengo la kusanyiko hilo hapa jijini Mwanza? Huyu hapa Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk akifunguka zaidi, ambapo pia Mkurugenzi wa Idara ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Martin Mnyanyelwa anashiriki kuzibainisha sifa zinazo mwondoa mtu kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Thursday, August 1, 2019

TIGO YAIPA MSAADA WA KOMPYUTA 10 SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA KISUTU, DAR

 Afisa uwajibikaji kwa jamii wa Tigo , Halima Okash. (kushoto) akimkabidhi mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana Kisutu , Sylvia Lyimo (wa pili kulia) moja wapo ya kompyuta 10 zilizotolewa na kampuni ya Tigo katika hafla iliyofanyika shuleni hapo jijini Dar es Salaam (wa pili kushoto ni Diwani wa kata ya Kisutu Kheri Mohamed Kessy.
Afisa uwajibikaji kwa jamii wa Tigo , Halima Okash. Akionyeshwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Kisutu jijini Dar es Salaam,jinsi ya kutumia kompyuta mara baada ya kukabidhi msaada wa kompyuta 10 zilizotolewa na kampuni ya Tigo, kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Sylvia Lyimo. Baadhi ya wanafunzi wakifurahia kutumia kompyuta muda mfupi baada ya kukabidhiwa masada wa komuta 10 kutoka Kampuni ya Tigo.

Na Mwandishi Wetu.

Kampuni inayoongoza katika maisha ya kidigitali nchini Tanzania ya Tigo, leo imetoa msaada wa kompyuta 10 shule ya sekondari ya wasichana Kisutu, pamoja na kuwaunganisha na intaneti ya bure kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kupata elimu kupitia teknolojia ya kisasa.

Msaada huo umeenda sambamba na uzinduzi wa kituo cha kupata elimu kutumia njia za kisasa za kidigitali kwa shule za Sekondari mkoani Dar es Salaam.  Wanafunzi watawezeshwa kupata fursa ya kutumia kituo hicho kupata maarifa ya matumizi ya kompyuta na TEHAMA.

Akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo, Afisa Uwajibikaji kwa Jamii kutoka Tigo, Halima Okash alisema, “Msaada huu tuliotoa leo kusaidia shule ni moja ya ufanikishaji wa mkakati wetu wa kuwezesha matumizi ya kidigitali ambapo shule zikiwezeshwa kutumia teknolojia kufundisha wanafunzi, wataweza kupata maarifa sambamba na kunufaika kwa kutoachwa nyuma katika mapinduzi ya kiteknolijia ya Kisasa matumizi ya TEHAMA yanayoendelea duniani”.

Alisema kutokana na ongezeko la matumizi ya kompyuta nchini Tanzania, sio shule zote zinauwezo wa kutoa elimu ya matumizi ya teknolojia hii. Moja ya changamoto inayowakabili wanafunzi wa shule za sekondari nchini ni kukosekana kwa nyenzo za kuwawezesha kupata elimu inayohusiana na matumizi ya teknolojia za kisasa.

“Wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Kisutu, sasa wanaweza kupata mafunzo ya matumizi ya kompyuta katika mitaala ya masomo yao. Elimu ya TEHAMA inaweza kuleta mabadiliko haraka katika sekta ya elimu, ambapo wanafunzi wanaweza kupata maarifa kutoka kwenye mitandao na tovuti mbalimbali za kielimu, kujifunza mambo mengi na kupata ujuzi unaotakiwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi.” alisema.

Aliongeza kusema “Uzinduzi wa kituo hiki cha kutoa elimu kupitia TEHAMA, unadhihirisha dhamira ya kampuni ya Tigo, kufanya uwekezaji katika miradi ya kusaidia jamii hususani kuleta mapinduzi ya sekta ya elimu kuwa ya kisasa na ya kidigitali, sambamba na kufanya shule hii kuvutia wanafunzi wengi wa shule jirani wenye kiu ya kupata elimu ya matumizi ya kompyuta na TEHAMA.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Kisutu, Mh. Khery Kessy, ambaye alikuwa ni mgeni rasmi aliipongeza kampuni ya Tigo, kwa juhudi zake za kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kusomea nchini.

“Nawashukuru Tigo kwa msaada huu, kwa kuwa utawezesha wanafunzi kupata maarifa ya elimu kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa mapema wakiwa bado wako katika madarasa ya chini katika safari yao ndefu ya kutafuta elimu. Ujuzi watakaopata kupitia kompyuta hizi utawawezesha kwenda na wakati wa kisasa na kuweza kuwa na sifa ya kupata ajira.” alisisitiza.

Mmoja wa wahitimu wa programu ya Tigo inayojulikana kama Change makers, ya mwaka 2014, amejitolea kushiriki kuwafundisha wanafunzi wa shule hiyo na kushirikisha wanafunzi kutoka shule nyingine za sekondari, ufadhili huu wa kampuni ya Tigo utawezesha wanafunzi kushiriki na kuwavutia kutaka kujua matumizi ya TEHAMA katika kufanikisha ndoto zao katika masomo yao.

Katika miaka ya karibuni, kampuni ya Tigo imetoa msaada wa kompyuta 77 katika shule na vyuo vya Serikali, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma, Shule ya Sekondari ya Jangwani, iliyopo jijini Dar es Salaam, shule 3 za sekondari mkoani Mtwara na shule moja ya msingi mkoani Tanga.

HII HAPA NGOMA MPYA INAYOTIKISA DAVIDO NA MTU MZIMA CHRIS BROWN - BLOW MY MIND


Davido, Chris Brown - Blow My Mind (Official Video)

MASAUNI AKAGUA UANDIKSHWAJI VITAMBULISHO VYA TAIFA NA UTOLEWAJI WA PASI ZA KUSAFIRIA ZANZIBAR

 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wananchi waliofika Makao Makuu ya Uhamiaji Visiwani Zanzibar leo  kupata pasi za kusafiria za kielektroniki, wapili kulia ni Kamishna wa Uhamiaji Johari Suluhu.
 Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Zanzibar, Hassan Hassan ,akifafanua  jambo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia),alipofika ofisi za mamlaka hiyo  leo kukagua zoezi la utolewaji vitambulisho kwa wananchi.
 Mkazi wa Unguja  Salma Ali,  akizungumza  wakati  wa  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad  Masauni (hayupo pichani), alivyofika Ofisi za Uhamiaji Zanzibar leo  kukagua zoezi la utolewaji wa pasi za kusafiria za kielektroniki linavyoendelea.
Mkazi wa Unguja  Salim Hassan Makame,  akizungumza  wakati  wa  Naibu  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni(hayupo pichani), alivyofika  Ofisi za Uhamiaji Zanzibar leo  kukagua zoezi la utolewaji wa pasi za kusafiria za kielektroniki linavyoendelea.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

UHAMIAJI, NIDA WATAKIWA KUHUDUMIA WANANCHI.
Na Mwandishi Wetu
Naibu  Waziri  wa  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi  Mhandisi  Hamad Masauni  amewataka  watumishi  wa  Idara  ya Uhamiaji  na Mamlaka ya  Vitambulisho vya Taifa(NIDA) kuwahudumia wananchi walioiweka serikali madarakani ili  kuepuka baadhi ya mbinu zinazotumiwa na watu wasio na nia njema kuvuruga amani ya nchi.
Ameyasema hayo Makao Makuu ya Uhamiaji Zanzibar  baada ya kukagua zoezi la utolewaji vitambulisho vya taifa na ubadilishaji wa pasi za zamani za kusafiria baada ya kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi waliofika katika ofisi hizo
“Kuna sauti zinatembea katika mitandao ya kijamii zikieleza ubaguzi unaofanyika katika kutoa pasi na vitambulisho, bado siamini kama kweli watumishi wetu mnafanya hivyo. Muhimu fanyeni kazi kuhudumia wananchi hawa bila kubagua mtu yoyote yule muhimu awe na nyaraka zote muhimu zinazomtambulisha,” alisema Masauni
“......wananchi hawa wamezichagua serikali hizi mbili lazima tuwahudumie maana ndio waajiri wetu,hatuwezi kuwa tupo katika serikali kisha hatuhudumii wananchi ipasavyo au tunahudumia kwa ubaguzi” aliongeza Masauni
Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri Masauni wananchi waliofika katika ofisi hizo waliiomba wizara kuongeza idadi ya watumishi hasa katika kipindi hiki cha kukaribia mwisho wa kubadilisha pasi za kusafiria ili kupunguza kupoteza muda mrefu kufuatilia pasi hizo za kusafiria.
“Tangu asubuhi saa mbili tuko hapa na huduma zimekua zikienda taratibu sana,tunaomba kuwepo na uharaka wa kupata huduma hizi,wiki nzima tunakuja hapa lakini utolewaji umekua auridhishi sana,nadhan watumishi waongezwe” alisema Abdallah Kheri Said Mkazi wa Vuga
Akizungumza katika ziara hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA),Hassan Hassan  alisema matarajio mpaka mwisho wa mwaka huu ni kusajili watu Laki Nane Thelathini Sita Elfu huku akiweka wazi changamoto za wingi wa watu wanaofika kwa ajili ya kuchukua vitambulisho ambavyo vimekua vinatumika katika kupata pasi za kusafiria na usajili wa laini za simu
“Tutaletewa mashine 15 kutoka Tanzania Bara ili tuweze kuhudumia watu wengi kwa wakati mmoja ili kupunguza foleni na kuharakisha utolewaji wa vitambulisho hivyo” alisema Hassan
Nae Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Suluhu alitaja changamoto ya kipato  kwa  raia walowezi ambao gharama ya kupata kibali cha kuishi  ambayo ni milioni mbili kuwa ni  kubwa huku wakilalamika vipato vyao vikiwa vidogo.

iMES, Imekuja kwa wakati Muafaka

 Mataalam kutoka OR-TAMISEMI, Fatma Yusuph, akitoa msaada wa kiutaalam kwa wataalam wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, wakati wa zoezi la uingizaji wa taarifa katika mfumo wa iMES.
 Mtaalam wa TEHAMA, kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma nchini, Milton Ndosi, akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa zoezi la uwandani kwenye Jiji la Mwanza.
 Limi George, Afisa Ugavi Manispaa ya Ilemela, akiwa anaingiza takwimu katika mfumo wa iMES wakati wa zoezi la uwandani katika Manispaa hiyo. (Picha zota na Atley Kuni-TAMISEMI)
Afisa Takwimu kutoka OR-TAMISEMI, akitoa maelezo ya awali juu ya Mfumo wa iMES, kwa wataalam wa Jiji la Mwanza.

iMES, Imekuja kwa wakati Muafaka
Na. Atley Kuni- Mwanza
Wataalam kutoka Idara na Vitengo wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wamesema Mfumo jumuishi wa Ufatiliaji na Tathimini (integrated Monitoring and Evaluation System-iMES), umekuja kwa wakati na enzi muafaka, wakati huu ambao matumizi ya takwimu ni hitaji la kila nyanja katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Wakiwa katika zoezi la pamoja za uingizaji wa takwimu katika mfumo, wataalam hao wamesema, ile hali yakukimbizana na taarifa pindi zinapo hitajika sasa litakuwa mwanzo na mwisho wake.
Limi George, Afisa Manunuzi katika Manispaa hiyo anasema kwamba, kwakuwa mfumo ni web base, haita malazimu mtaalam kuanza kutembea kutoka ofisi moja kwenda ofisi nyingine kusaka taarifa bali kwakupitia mfumo wa iMES kila kitu mtu atafanya akiwa mezani kwake.
“Kwakuwa sisi watumiaji wote tumesha tengenezewa akaunti za kutuwezesha kuingia katika mfumo, hata kama kuna hoja za ukaguzi ambazo zilijitokeza kutoka kwa Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, nikiwa kwenye dawati langu nitaweza kuzifatilia na kuzifanyia kazi bila yakutembea toka Ofisi moja hadi nyingine cha msingi hapa nikwa wataalam kuutumia mafumo kwakuweka data kwa wakati” alisema Limi.
Naye Rose Nyemele, Afisa Muuguzi katika Manispaa hiyo, yeye anasema, pamoja na kutumia mfumo wa (Data Health Information System-DHIS-2) katika masuala ya mipango ya bajeti na MTUHA, ambayo yalianzia ngazi ya Kijiji bado anaona iMES imekuja kwa wakati mujarabu kujibu masuala mtambuka kutoka sekta zote.
“Kwetu sisi watu wa Afya data ni kila kitu, Masuala kama Mipango ya bajeti katika Dawa, Rasilimaliwatu, pamoja na vifaa tiba na vitendanishi vingine hutegemea sana uwepo wa taarifa sahihi na kwawakati, hivyo iMES tunaiona kama suluhu yakudumu, alisema Nyemele.
Mtazamo wa Nyemele, hautofautiani na Afisa TEHAMA katika Halmashauri hiyo Isac Tenguye, ambaye anasema katika Dunia ya sasa kuwa na Mfumo kama huo ni muarobaini wa matatizo ya taarifa.  
“Huu ni mfumo utakao kuwa na chanzo kimoja cha taarifa na utaepusha takwimu kutofautiana kama kipindi cha nyuma, mnaweza kwenda kwenye mkutano mmoja na wadau lakini wewe mtendaji na mdau taarifa zenu mkakuta zinakinzana, lakini kwa iMES tunaona kabisa kila mmoja atajikita kupata taarifa kutoka katika mfumo na hivyo kuondoa tofauti” alisema Tenguye.
Hata hivyo Wataalam hao, hawakusika kuipongeza Serikali pamoja na Wadau wa Maendeleo nchini USAID, chini ya Maradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma PS.3 kutokana na juhudi wanazo zifanya za uimarishaji wa mifumo ya Sekta za Umma.
“Uzalendo nikuwa na mapenzi mema na nchi yako hivyo tunawapongeza sana OR TAMISEMI pamoja na PS.3, kwa ushirikiano huu ambao unaonesha matunda ya wazi wazi kwa nchi hususan ni katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano ambayo imejipambanua katika kumjali mwananchi” alisema Nelson Rugaimukamu Daktari wa Mifugo katika Manispaa hiyp    
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, zimekuwa Mamlaka za mwanzo kabisa za majaribio ya mfumo huo wa iMES huku lengo likiwa nikuzifikia Halmashauri zote 185 nchini lakini pia kujumuisha  Wizara  za kisetakta kote nchini.

Shirika la NSSF lafungua milango zaidi kwa watanzania

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limewahimiza wananchi waliojiajiri na kuajiriwa katika sekta isiyo rasmi nchini, kutumia fursa iliyopo ya kujiunga na shirika hilo ili kunufaika na mafao mbalimbali ikiwemo ya uzazi na uzeeni.

Meneja Uhusiano Elimu kwa Umma NSSF, Lulu Mengele aliyasema hayo jana kwenye mkutano baina ya shirika hilo na waandishi wa habari mkoani Mwanza, uliolenga kutoa elimu kuhusiana na kampeni ya Marafiki wa NSSF yenye lengo la kuhakikisha wananchi wote wanajiunga na kunufaika na mafao ya jamii.
Tazama Video hapa chini

POLISI MWANZA YANASA MTANDAO WA WIZI WA BODABODA

KUFUATIA kuongezeka kwa vitendo vya unyang'anyi wa pikipiki na baadhi ya vijana kujeruhiwa na hata wengine kufariki dunia, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 18 wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio hayo ya wizi na uporaji.
Mbali na kukamatwa kwa watu hao, polisi pia limekamata pikipiki 16 zilizokuwa zikitumika katika wizi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano Julai 31, 2019 Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro amesema matukio hayo yametokea kati ya Januari hadi Desemba 2018,  na Januari hadi Julai, 2019.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika ni Nyakabungo,  Nyakato,  Buhongwa, Isamilo,  Ibanda,  Kiseke,  Kishiri,  Maduka tisa,  Nyamhongoro,  Ngudu wilaya ya Kwimba na Sengerema.

BALOZI IDDI AZINDUA MRADI WA MAJI KATIKA NYUMBA MPYA ZA ASKARI POLISI MAHONDA

 Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi  Seif Ali Idd, akifungua bomba kuashiria Uzinduzi wa Mradi wa Maji kwenye Eneo la Nyumba za Polisi, zilizoko katika Jimbo la  Mahonda, Mkoa wa  Kaskazini Unguja.Aliyevaa koti ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi  Seif Ali Idd, akimtwisha ndoo ya maji mwananchi wa Mahonda baada ya  Uzinduzi wa Mradi wa Maji kwenye Eneo la Nyumba za Polisi, zilizoko katika Jimbo la  Mahonda, Mkoa wa  Kaskazini Unguja.Katikati  ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi  Seif Ali Idd(kulia), akifurahia baada ya  kumtwisha ndoo ya maji mwananchi wa Mahonda baada ya  Uzinduzi wa Mradi wa Maji kwenye Eneo la Nyumba za Polisi, zilizoko katika Jimbo la  Mahonda, Mkoa wa  Kaskazini Unguja.Wapili kulia   ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Wednesday, July 31, 2019

VIDEO:- CCM YAPIGA MARUFUKU UJAZAJI RUMBESA NA VIPIMO VYA UJAZO VINAVYOMUIBIA MKULIMA.


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally amehudhuria Mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela  wa uwasilishaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM Jimbo la Ilemela-uwanja wa CCM Kirumba.


Mkutano huo maalum wa uwasilishaji wa utekelezaji wa Ilani, uliofanywa na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula umehudhuriwa viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakiongozwa Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Ndg. Kheri James Mwenyekiti wa Vijana wa CCM taifa na Mama Munde Tambwe, mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ndg. Jamal Babu, viongozi wa Mkoa, Wilaya, Kata, Matawi na wajumbe wote wa mashina  Wilaya ya Ilemela.

Katibu Mkuu akizungumza katika mkutano huo, ametoa maelekezo kwa viongozi wa serikali hasa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusimamia vipimo vya ujazo wa mazao ikiwemo kupiga marufuku ujazaji wa rumbesa na mizani isiyotenda haki kwa wakulima.

"Natoa maelekezo nchi nzima kwa wakuu wa mikoa na wilaya kwa niaba ya CCM, kama mnataka kazi ndani ya serikali hii ya CCM nisisikie malalamiko kuhusu ujazaji wa rumbesa kama ambavyo baadhi ya wafanyabiashara wanawafanyia wakulima wetu hivi sasa.  Rumbesa, na mizani isiyokuwa ya haki kwa wakulima wetu ni kosa kisheria, na kamati za siasa za mikoa, wilaya, kata na matawi simamieni hili na mtoe taarifa ili wananchi wanyonge wasiendelee kunyanyaswa." Dk. Bashiru ameelekeza.


 Wakati huo huo, Ndg. Kheri James akimkaribisha Katibu Mkuu, amewataka vijana wote nchini kuendelea kuwatetea viongozi kwa nguvu zote dhidi ya baadhi ya watu wasio itakia mema nchi yetu kwa kutoa kejeli na kuwakatisha tamaa viongozi wetu, licha ya kazi kubwa wanayoifanya kwa nchi yetu.

"Ninawaomba vijana nchi nzima, tuendelee kuwalinda viongozi wa chama na serikali dhidi ya yeyote anayetoa kejeli kwa kazi kubwa wanazofanya viongozi wetu usiku na mchana, hatutaruhusu mwenyekiti na Rais wetu, Katibu Mkuu wetu na viongozi wote wakatishwe tamaa na watu wachache wasioitakia mema nchi yetu."  Ndg. Kheri amesisitiza.
 Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella akitoa neno la utambulisho na makaribisho kwa wadau waliohudhuria mkutano huo.











Ziara hii ya siku tano, imeanza leo Mkoani Mwanza ikiwa ni muendelezo wa kutekeleza jukumu la viongozi wa CCM kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Tuesday, July 30, 2019

ANGELINE MABULA: WANANCHI WA KATA YA BUGOGWA SHIDA YA MAJI KUWA HISTORIA


Mara baada ya Mbuge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM Jimbo la Ilemela, shughuli iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dkt. Bashiru Ally, ikawa sasa fursa kwa mtangazaji wa Jembe Fm Mwanza Harith Jaha kuzungumza mawili matatu na mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania. 

Tumia hii tafadhali : MWENYEKITI WA CCMMKOA WA SHINYANGA AZINDUA 'KISHAPU YA KIJANI' AONYA CCM KUWEKA WAGOMBEA WASIOKUBALIKA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amezindua rasmi kampeni ya 'Kishapu ya Kijani', huku akionya viongozi na wanachama wa chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambao utafanyika mwezi Oktoba mwaka huu kutopitisha wagombea wasio na sifa.

KAMPUNI I ya Jatu PLC yaendesha mafunzo kwa vijana 100,yawaasa kuacha kutegemea kuajiriwa

KAMPUNI I ya Jenga Afya Tokomeza Umaskini (Jatu PLC), imeendesha mafunzo kwa vijana 100 lengo likiwa ni kutokomeza umaskini kupitia rasilimali watu.

Meneja mkuu wa Jatu, Mohamed Simbano akizungumza wakati wa mafunzo hayo alisema mkakati wa taasisi yao ni kusaidia kuondoa kutu vichwani mwa vijana kwa kuacha kutegemea kuajiriwa na badala yake waangalie fursa zilizopo na kuweza kujiajiri.

“ Tukiwa hapa kwenye mafunzo, una diploma, degree weka pembeni kwa sababu hazina maana sana kama huna uwezo wa kubuni wazo na kutengeneza pesa,” alisema Simbano na kuongeza

“Aliyejaribu na akashindwa, anafaida kubwa kuliko asiyejaribu, kufeli haina maana umeshindwa bali utatafuta namna nyingine ya kujaribu.” Alisema

Akimnukuu mwanafalsafa Joseph Chilton Pearce aliyeelezea thamani ya ubunifu aliyosema, ‘to live a creative life we must lose our fear of being wrong’ kwa tafsiri isiyo rasmi alimanisha kuishi maisha ya ubunifu kunahitaji kuondoa hofu ya kukosea.

Simbano alisema elimu ambayo wanawapatia vijana hao itawaondoa katika dhana ya kusaka ajira au kubweteka majumbani na badala yake watachukua hatua na kujiikingiza kwenye ujasiriamali wa kilimo na masoko.Alisema mafunzo hayo ni bure kwa kila kijana mwenye ndoto za kujikwamua kiuchumi,bila kujali elimu.

Alisema mara baada ya mafunzo hayo watatoa nafasi kwa vijana katika masoko kwa kuwaajiri na kuimarisha kitengo chao cha masoko, hadi kufikia mwaka 2022 kila anayetumia soko bidhaa za Jatu aweze kupata manufaa na kwamba chakula kinacholiwa kiwe suluhisho la masoko.

“Mafunzo haya ni endelevu, vijana 100 tutakaowapa ajira ni fursa pekee kwao kwa kuimarisha kitengo cha masoko cha Jatu, na kazi yao kubwa ni kuhakikisha kila mwanachama wa jatu aweze kutumia bidhaa.” Alisema

Alisema mafunzo hayo yanaenda sambamba na mpango mkakati na kufikia malengo, waliojiwekea ikiwemo kutokomezaz umaskini kupitia rasilimali watu, kilimo na viwanda, ikiwa ni pamoja na kuingia kwenye soko la hisa (DSE) mwezi Septemba.