Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amezindua rasmi kampeni ya 'Kishapu ya Kijani', huku akionya viongozi na wanachama wa chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambao utafanyika mwezi Oktoba mwaka huu kutopitisha wagombea wasio na sifa.
Uzinduzi wa kampeni hiyo wilayani Kishapu umefanyika leo Julai 28, 2019 katika kata ya Maganzo kwenye Uwanja wa michezo, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM, wilaya na mkoa , wanachama, wananchi wakiongozwa na mbunge wa jimbo a Kishapu Suleiman Nchambi.
Mlolwa ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi amesema lengo la Kampeni ya Kijani ni kuhakikisha kuwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2020, wagombea wote wa CCM wanashinda kwa kishindo na kutowapatia hata kiti kimoja wapinzani.
Amebainisha kuwa ili adhma hiyo ipate kutimia ni marufuku viongozi wa CCM pamoja na wanachama kupitisha wagombea watakaowania viti vya uongozi kwenye chaguzi hizo, ambao watakuwa hawana sifa na wasiokubalika kwa wananchi, bali wapitishe wagombea wenye vigezo ambao watarahisisha uchaguzi na hatimaye kupita bila ya kupingwa.
“Tunaposema kampeni ya kijani maana yake ni kushinda viti vyote vya ugombea kwenye chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, na kutowapa nafasi wapinzani sababu CCM ndiyo chama pekee ambacho kinaleta ukombozi kwa wananchi, nadhani mnaona nyie wenyewe mambo anayo yafanya Rais wetu Dkt. John Magufuli,”amesema Mlolwa.
“Hivyo ili tupate kushinda viti vyote vya uongozi ni lazima tupitishe wagombea wote ambao wana sifa na kukubalika kwa wananchi, na siyo kupitisha tu watu ambao hawana vigezo wana maskendo machafu huko kwa wananchi kisa tu wana pesa, nawasihi msipitishe watu wa namna hiyo watatuangusha,”ameongeza.
Katika hatua nyingine alionya makundi ndani ya chama katika kuelekea kwenye kipindi hiki cha uchaguzi, na kuwataka wawe kitu kimoja katika kuendeleza mapambano ili waweze kupata ushindi wa kishindo, na baada ya hapo, pale penye mapungufu ndipo wakae kuyamaliza na kusameheana.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kishapu Suleimani Nchambi, alimtoa wasiwasi mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Shinyanga, kuwa jimbo hilo hakuna mgombea wa upinzani ambaye atashinda kwenye chaguzi zote, kwani wananchi wana imani na CCM kutokana na kuwatekelezea maendeleo yakiwamo maji safi na salama kutoka ziwa Victoria.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilayani Kishapu Joseph Kwilasa, amewataka vijana kutotumika kuvuruga amani kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka ujao, bali wajiandikishe kwa wingi na kupiga kura kwa kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo ambao wanatoka CCM.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizindua kampeni ya "Kishapu ya Kijani" na kuonya kuweka wagombea wasio na sifa wala kutokubalika kwa wananchi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM Mkoa wa Shinyanga Barack Shemahonge, akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Kishapu ya Kijani.Amewataka vijana kutofanya makosa bali wachague wagombea wote wa CCM, na pia wajiunge kwenye vikundi ili waweze kupata mikopo na kujipatia kipato kuliko kusubili kutumika kwenye uchaguzi na kupewa vitu vidogo.
Diwani wa Kata ya Maganzo wilayani Kishapu Mbalu Kidiga, akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake ambapo amesema kuwa kwenye chaguzi zote zijazo CCM itashinda kwa kishindo na hatimaye kuifanya Kishapu kuwa ya kijani.
Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.