Na Peter Fabian, MWANZA.
AGIZO la Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa, Rais Dk John Magufuli kwa viongozi na wanachama wa Chama hicho kuweka wazi mali za Chama ngazi za matawi, Kata, Wilaya na Mkoa pamoja na kutolewa taarifa ya mapato na matumizi yake kwa wanachama imeanza kuzaa matunda na kuwa chungu kwa wawekezaji na wapangaji kwenye majengo yake.
Hatua hiyo imepelekea Mahakama ya Baraza la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Mwanza kumuamru mwekezaji wa aliyekuwa mpangaji wa jengo la biashara la Kirumba Resort linalomilikiwa na CCM Kata ya Kirumba katika Wilaya ya Ilemela, Benson Temba kuondolewa baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango katika jengo hilo kinyume cha mkataba.
Uamuzi wa Mahakama hiyo unatokana na kesi namba 176 ya mwaka 2013 iliyofunguliwa na Bodi ya wadhamini wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo Abubakar Kweyamba dhidi ya mwekezaji huyo akidaiwa kuingia mkataba tata na kushindwa kulipa kodi ya pango kama ilivyo kwenye mkataba wa upangaji wa jengo hilo.
Mlalamikiwa Temba katika utetezi wake alidai kuwa aliingia makubaliano na wamiliki wa jengo kufanya ukarabati kwa shilingi milioni 60 na akaomba baraza hilo kutupilia mbali shauri hilo dhidi yake hoja na ambayo ilikataliwa na baraza.Awali alifungua shauri namba 36 la 2016 akipinga kuondolewa kwenye jengo.
Akisoma hukumu hiyo juzi kwa muda wa saa moja (Agosti 26, 2016) Mwenyekiti wa baraza hilo, James Sillas alisema kuwa shauri hilo lilikuwa gumu kutokana na mvutano wa kisheria uliokuwepo baina ya mawakili wa wadai na mdaiwa ambapo alidai kuwa mdaiwa (Temba) alivunja mkataba kwa kulipa kodi ya pango kidogo kidogo kwa miezi mitatu kinyume cha kifungu cha 3 (b) cha mkataba.
Sillas alieleza kuwa baraza hilo kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na mashahidi wa pande zote mbili na kwa kuzingatia maoni ya wazee wa baraza na sheria namba 2 ya baraza hilo ,maoni yao yalifanana kuwa mdaiwa alivunja mkataba na bazara hilo liligundua kuwa hakuwa tena na uwezo wa kifedha.
Sillas aliendelea kueleza kuwa baraza liligundua kuingiwa kwa mkataba wa giza wa miaka mitano huku kukiwa na mwingine wa mwaka mmoja, na hivyo baraza kujiuliza kulikuwa na nini wakati fedha hazijalipwa za mkataba wa awali.
“ Kipengele cha 3( b) kinachomtaka mdaiwa (Temba) kulipa kodi ya pango kwa miezi mitatu mfululizo kiasi cha shilingi milioni 1,000,000 kila mwezi badala yake alikuwa akilipa kidogo kidogo, hivyo kipengele hicho kilimyima uhalali wa kuendelea kuwa mpangaji,” alisema mwenyekiti huyo kwenye hukumu hiyo.
Kwamba hakuna ubishi kuwa kodi ililipwa Novemba 2015 lakini Desemba 2015 hadi Februari 2016 kodi haikulipwa na wadai kushindwa kuvumilia na hivyo wakaamua kufunga jengo ambalo tayari lilionekana kuchakaa.
Sillas alieleza kuwa baraza hilo limeridhika bila shaka,bila giza na wasiwasi kwamba kulikuwa na mkataba wa kinyemela na kuamuru Temba kuondolewa kwenye jengo hilo na kukabidhiwa mali zake,pia azuiwe kufika kwenye jengo hilo baada ya kukabidhiwa mali zake aondoke huku Mahakama hiyo ikimuondolea gharama za kesi na kudai kuwa mtu ambaye hajaridhika na uamuzi huo rufaa iko wazi.
.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kirumba Abubakar Kweyamba akizungumza na waandishi baada ya uamuzi huo kutolewa na Mwenyekiti Sillas alisema kuwa wameridhika na uamuzi huo kwani mahakama imetenda haki na kumpongeza baraza hilo (Sillas) kwani shauri hilo lilichukua muda mrefu kumalizika kutokana na nguvu aliyokuwa nayo mdaiwa na mabishano ya kisheria kwa mawakili wa pande mbili.
Kweyamba alidai kuwa kesi hiyo ni ya nne kufunguliwa kwenye baraza hilo na mwenyekiti aliyesikiliza kwa mara ya nne alilazimika kufanya kazi hata nje ya muda kutokana mawakili wa mdai kuweka visingio vya kuwa na kesi kwenye mahakama zingine.
“Tulikuwa tukihujumiwa na viongozi wetu wa juu Benard Ndutta (Wilaya na Mkoa) waliopita katika kusimamia shauri hili wakishirikiana na mwekezaji.Wakati kesi ikiendelea, lakini tumpongeze Katibu wa CCM Mkoa Miraji Mtaturu (DC wa Ikungi Singida) na Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela, Acheni Maulid kwa ushirikiano wao hadi leo uamuzi umetolewa na huu uwe mfano kwa viongozi wengine,”alisema.
Wito wangu kwa wanachama kushirikiana na viongozi kuwa watulivu wakati huu na waepuke kusikiliza baadhi ya wanachama na watu ambao wamekuwa wakijitokeza kutumia fursa za kuwachonganisha na kuwagawa kwa masilahi yao binafsi hivyo wawakatae na kujipanga kukitumikia chama ili kufikia malengo ya utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2015/2020.