ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 28, 2020

Tuesday, March 24, 2020

MWANAMUZIKI MANU DIBANGO AFARIKI KWA UGONJWA WA CORONA.


Mwanamuziki mashuhuri na mpiga saxophonist wa Cameroon, Emmanuel N'Djoke Dibango ‘Manu Dibango’, amefariki kwa ugonjwa wa corona.
Manu Dibango amefariki leo Jumanne asubuhi akiwa nje hospitali katika jiji la Paris, Ufaransa.

Dibango mwimbaji wa muziki wa jazz mwenye miaka 86, wiki iliyopita katika ukurasa wake wa Facebook alitangaza kupatwa na ugonjwa wa virusi vya corona.

Manu Dibango anakumbukwa kwa wimbo wake mashuhuri uliotamba mwaka 1972, ulioitwa Soul Makossa.

Monday, March 23, 2020

MAHAKAMA KUU TANZANIA YAAMUA HILI KUHUSU JANGA LA CORONA



MAHAKAMA kuu ya Tanzania, imesema ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona itahakikisha inatilia mkazo uendeshaji wa shughuli zake kwa njia ya mtandao jambo ambalo inadai litasaidia kujihadhari na ugonjwa huo. Imesema wadawaa na wananchi wengine watakuwa wanafuatilia mashauri ya kesi zao kupitia njia ya mtandao hatua ambayo pia itapunguza msongamano wa watu mahakamani. Kauli hiyo imetolewa na Jaji mkuu wa Tanzania, Professa IBRAHIM JUMA wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu kusikilizwa kwa kesi hizo kwa njia ya mtandao.

WASAFIRI WATAKAOPITA MPAKA WA TUNDUMA KUWEKWA KARANTINI SIKU 14

 Eneo la Tunduma ambapo ni Mpaka wa Tanzania na Zambia ambapo wasafiri wanao toka Nchi zenye Ugonjwa wa Virusi vya Corona kupitia mpaka huo watawekwa Karantini kwa gharama zao kwa muda wa siku 14.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando akinawa mikono kwa maji yenye dawa katika Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipokagua maandalizi ya kuwaweka karantini wasafiri wanao toka Nchi zenye Ugonjwa wa Virusi vya Corona.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Songwe wakinawa mikono kwa maji yenye dawa katika Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wakati wakikagua maandalizi ya kuwaweka karantini wasafiri wanao toka Nchi zenye Ugonjwa wa Virusi vya Corona
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Songwe imeanza utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli la kuwataka wasafiri waliotoka katika nchi zenye maambukizi ya Virusi vya Corona kukaa karantini kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao.
Mapema leo wajumbe wa Kamati hiyo wametembelea eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia uliopo eneo la Tunduma Mkoani Songwe ili kutathmini utayari wa kuanza zoezi la kuwaweka eneo tengefu yaani karantini wasafiri wote watakaotumia mpaka huo unao julikana kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi nchini kutoka nchi mbalimbali.
Wajumbe hao wamekubaliana kuanza mara moja zoezi la kuwatenga wasafiri wote watakaoingia nchini kupitia Mpaka wa Tunduma kwa gharama zao na kwa muda wa siku 14, ambapo zoezi hilo linatarajiwa kuanza leo Machi 23, 2020 usiku huku maandalizi ya maeneo na mahitaji mengine kwaajili ya kuwatenga yakiendelea kufanyika.
Pia wameweka mkakati wa kufanya kaguzi mbalimbali katika nyumba za kulala wageni ili kubaini endapo kuna wageni ambao wataingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na kukwepa kukaa karantini huku ulinzi ukiimarishwa Zaidi katika eneo lote la Mpaka.
Aidha wamewasihi wananchi wote kuendelea kuchukua hatua za tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kunawa kwa maji na sabuni, kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima kwani kinga ni bora Zaidi kuliko Tiba.

BURIANI Dkt. MAKONGORO MAHANGA

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ilala, Dk Milton


Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ilala, Dk Milton Makongoro Mahanga amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumatatu Machi 23, 2020 Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Hemed Ally amesema wamepata taarifa za msiba huo.

“Ni kweli taarifa hizo tumezipata kupitia katibu wa Chadema wa Mkoa wa Ilala maana yeye ndiye alikuwa anafanya naye kazi kwa ukaribu,” amesema.

Ally amesema leo Jumatatu walikuwa wamepanga kwenda Muhimbili kumuona lakini kabla hawajaenda walipata taarifa kuwa ameshafariki dunia.

“Ilikuwa twende tukamuone leo na taarifa zote zilikuwa zinapitia kwa katibu wake wa mkoa wa Ilala wa chama, sasa asubuhi alipofanya mawasiliano na mke wake akamueleza kuwa Dk Makongoro amefariki,” amesema.


WANAOFANYA MIZAHA YA CORONA KUCHUKULIWA HATUA


Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe katika Kikao cha Kutathmini utayari wa Kupambana na Ugonjwa wa Corona Endapo utatokea Mkoani Songwe, ambapo  amesema watu wanao fanya mizaha mitandaoni kuhusu ugonjwa wa Corona hao watachukuliwa hatua.
Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Songwe wakifuatalia mada mbalimbali kuhusu tathmini ya utayari wa Kupambana na Ugonjwa wa Corona Endapo utatokea Mkoani Songwe ambapo  moja ya maazimio ni kutoa elimu Zaidi kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari ya Corona.
Imebainika kuwa wapo baadhi ya watu ambao hutumia mitandao ya kijamii kutengeneza na kusambaza mizaha na taarifa za uongo juu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona huku wakiwaaminisha wengine kuwa ugonjwa huo hauwapati watu weusi.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe katika Kikao cha Kutathmini utayari wa Kupambana na Ugonjwa wa Corona Endapo utatokea Mkoani Songwe, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amesema watu hao watachukuliwa hatua kali.
Palingo amesema mizaha hiyo inadhoofisha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Corona na kuwafanya wananchi wengine kutotilia maanani maelekezo ya wataalamu wa Afya ya kuchukua hatua za tahadhari kwakuwa mapambano hayo ni vita ambayo inajumuisha jamii nzima.
Amesema kuwa licha ya Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kutangaza kuwachukulia hatua kali wote wanao sambaza mizaha na taarifa za uongo kuhusu Ugonjwa wa Corona, Uongozi wa Mkoa wa Songwe na Wilaya zote pia hauta wavumilia wote watakaofanya vitendo hivyo Mkoani hapa.
Palingo ameongeza kuwa wazazi na walezi wote wahakikishe wana waangalia watoto wote wasizagae mitaani, sokoni, minadani na katika mikusanyiko ya masomo ya ziada (Tuisheni) kwani serikali imefunga shule ili kuchukua tahadhari ya kuwakinga wanafunzi dhidi ya Ugonjwa wa Corona.
Amesema serikali inaendelea kusisitiza Sehemu ambazo lazima mikusanyiko iwepo kama katika nyumba za ibada na katika ofisi mbalimba, maji ya kunawa na sabuni yawepo na pia hatua zote muhimu za tahadhari zichukuliwe.
Aidha Palingo amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuacha masuala ya mila yanayoweza kuwawaweka katika hatari ya kuambukizana ugonjwa wa Corona hususani mila ya kusalimiana kwa kushikana mikono.
Amesema waanchi wanapaswa kuelewe kuwa wasisubiri ifikie hatua ya kutibu wagonjwa wa corona bali wazuie Kwanza kwa kuchukua tahadhari ya kujikinga kwani ikifikia hatua ya kutibu watu wengi wanaweza kupoteza maisha.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamadi Nyembea amesema Mkoa wa Songwe unatoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa wananchi kwa ngazi zote kwani ni njia mojawapo ya kupambana na ugonjwa huo.
Dkt Nyembea amesema Kamati za Afya za Wilaya hadi ngazi ya Kata zitahakikisha zinafikisha elimu ya kujikinga na Corona kwa wananchi pia maafisa wengine wa Serikali nao washiriki kuwaelimisha wananchi.
Sauli Ndambo Mkazi wa Ilembo Wilaya ya Mbozi ameishukuru serikali kwa kuchukua tahadhari na kufunga shule ili watoto wawe salama huku akiwataka wanao fanya mizaha kuacha mara moja kwani ugonjwa huo hauna mzaha na unaua.
Laurent Mwasile Mkazi wa Vwawa Wilaya ya Mbozi amewasihi vijana kuchukua tahadhari na kuacha mila ya kusalimiana kwa mikono na endapo watamuona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo watoe taarifa katika vituo vya Afya.

Sunday, March 22, 2020

WAZIRI MKUU AWATAJA WANAORUHUSIWA KUTOA TAARIFA KUHUSU CORONA.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameonya kuhusu upotoshwaji na utoaji holela wa taarifa kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababisha na virusi vya corona (COVID 19) unaofanywa na watu mbalimbali nchini.

Amesema kuanzia sasa taarifa hizo zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ikilazimika zitatolewa na Waziri Mkuu na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha mikanganyiko.



Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo Jumamosi, Machi 21, 2020 wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa kwa njia video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ifuatile watu wote wanaofanya upotoshaji kwa kupitia mitandao ya kijamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

“Watu wote wanaopotosha umma na kuleta taharuki kuhusu ugonjwa wa corona badala ya kuelimisha namna ya kujikinga, wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema licha ya hali ya maambukizi ya corona nchini kutia matumaini, viongozi hao hawana budi kupeana taratibu za namna ya kukabiliana na tatizo hilo.