|
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani akizungumza juzi na wananchi wa Kitongoji cha Lukungu Kijiji cha Lamadi wilayani Busega wakati wa ziara yake ya kukagua uhai wa Chama hicho na utekelezwaji wa Ilani ya uchaguzi. |
|
Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Titus Kamani, akimvisha aliyekuwa mmoja wa wanachama wa Chama cha Demkrasia na Maendeleo (CHADEMA) kati ya 47 waliyokihama chama hicho juzi katika Kijiji cha Lamadi kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mbunge huyo. |
|
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani, akipandisha bendera ya CCM kuashilia uzinduzi wa Shina mojawapo kati ya kumi aliyozindua katika ziara yake ya kukagua uhai wa chama hicho wilayani Busega juzi. Picha na Peter Fabian. |
NA PETER FABIAN, BUSEGA.
RAIS Dk Jakaya Kikwete ametakiwa kusaini haraka hati za watu waliopatikana na makosa ya mauaji ya Albino, ili adhabu ya kunyongwe hadi kufa itekelezwe jambo ambalo pia litasaidia kukomesha mauaji hayo yanayoibuka katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yalisomwa juzi kwenye risala ya wananchi wa Kijiji cha Mwamagigisi wilayani Busega mkoani Simiyu, kupitia Kikundi cha Wajasiriamali wa CCM kijijini hapo kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani alipofika kuweka jiwe la msingi la kufungua Ofisi na Shina lao la CCM .
Kikundi hicho kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Dk Kamani, kimetoa sh 110,000 kusaidia mawasiliano ya walemavu wa ngozi (Albino) pindi wanapoona wako hatarini au kuna watu wanaowatilia shaka na kuonekana kuna dalili za kuwanyemelea.
Dk. Kamani alilitoa fedha hizo juzi wakati wa uzinduzi huo na uwekaji wa jiwe la Msingi, wakati wa ziara ya kuimarisha uhai wa Chama wilayani humo ambapo pia aliwahutubia wananchi waliohudhuria ikiwemo kuwakumbusha kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu ili kuwawezesha kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Wakilaani mauaji ya Albino katika risara yao iliyosomwa na Odemba Bahai kwa Dk Kamani, wanakikundi hao walisema vitendo vya utekaji na mauaji ya walemavu hao vinawasikitisha, wanamuomba Rais Dk Kikwete asaini hati za adhabu za kifo za watu waliohumiwa kunyongwa hadi kufa, kutokana na mauaji hayo.
“Kuwafanya ndugu zetu Albino kuwa dili la kujipatia utajiri na kuwaua, ni kosa kubwa hata kwa Mungu, tunaomba mahakama ziharakishe kesi za watuhumiwa wa mauaji hayo na Rais wetu asaini hati za hukumu ya kuwanyonga watu waliohukumiwa kifo ili wanyongwe haraka hadi kufa.”
“…….Kuheshimu haki za binaadamu wenzetu hao tunatoa sh10,000 japo ni kidogo tulichonacho ili ziwasaidie walemavu wetu kununulia vocha za kupiga simu kwenye vyombo vya dola pindi wanapoona mtu aliye kwenye mazingira ya kuwanyemelea maeneo anayoishi,”. Ilisema sehemu ya risara hiyo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwamagigisi na kujibu risara hiyo baada ya uzinduzi wa kikundi hicho, Dk Kamani alisema serikali ya CCM inalaani vikali mauaji ya walemavu hao na vikongwe na vyombo vya dola vimekuwa vikijitahidi kuwakamata wahusika na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.
DK. Kamani aliunga mkono mchango wa fedha za vocha zilizotolewa na wanakikundi hao na kuongeza sh 100,000 na kufanya mchango huo ufikie sh 110,000 ambazo zitakabidhiwa kwa viongozi wa Albino wa wilaya ya Busega.
Mwenyekiti huyo, pia katika ziara yake hiyo wilayani Busega alifungua mashina kumi ya wakereketwa wa CCM wakiwemo wana kikundi hao ambao aliwapiga jeki kwa kuwachangia sh milioni 1 huku mashina mengine akiyachangia kati ya sh 500,000 hadi 1,000,000 kila moja.