Aliyekuwa mfalme wa muziki wa taarab nchini, Mzee Yusuph amefunguka na
kueleza kuwa watu wote walio na nyimbo zake kwenye simu zao wafute na
kuacha kusikiliza ili kuepuka dhambi.
Katika mahojihano na kipindi cha Mitikisiko ya Pwani cha Times Fm, Mzee
Yusuph ameelezea maisha yake ya ndoa, kidini na kiuchmi yalivyo kwa sasa
ukilinganisha na hapo awali.
“Mimi nikikubali watu wacheze nyimbo zangu ina maana nimeruhusu dhambi
tena ni bora nirudi kuimba muziki tena hivyo, watu wote waliokuwa na
nyimbo zangu kwenye simu zao wafute na kuacha kusikiliza kuepuka
dhambi,” amesema Mzee Yussufu.
Mzee Yussufu amesema yeye hayupo kwenye kundi lake la ‘Jahazi Modern
Taarab’ kama baadhi ya watu wanavyodhani na wala hafuatilii kabisa kundi
hilo.
“Nilitaka kulivunja Kundi la Jahazi lakini sheria za nchi haziruhusu
nikaliacha na haya niliambiwa na Basata wenyewe. Vyombo vya bendi ya
Jahazi havikuwa vya kwangu tulikuwa tunasaidiana na mabosi,” amesema.
Katika hatua nyingine Mzee Yusuph amesema maisha ya kiuchumi kwa sasa ni
toufauti na kipindi alichokuwa anafanya muziki kwani hapo awali kwa
wiki alikuwa anaweza kutengeneza milioni moja na nusu mpaka mbili ila
sasa kushika laki tano au milioni inaweza kumchukua miezi miwili.
Ameongeza kuwa wake zake wanne bado anaendelea kuishi nao kama kawaida,
na kuwa na wake ni jambo ambalo amehimizwa na sio amri, na kwa sasa
wanamjua ni mtu wa namna gani na mambo yote yanaenda sawa hakuna hata
mmoja anayefanya sivyo.