NA ANNASTAZIA MAGINGA, Mwanza
WAKAZI wa kijiji cha Kakola na Bushing'we wa Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, wamelalamikia Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu kutotoa ajira kwao na badala yake kuwapatia wageni ajira ambazo hata wao wanaweza kuzifanya.
Hayo yamebainishwa na wakazi hao wakati wa ziara ya kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na uwekezaji wa migodi ili kuimarisha na kutetea demokrasia na uwajibikaji bora katika sekta ya madini iliyoratibiwa na shirika la Action for Democracy and Local Government (ADLG).
Wakizungunza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi hususan vijana waliohojiwa wamesema kuwa licha ya kuwepo kwa kazi ambazo wanamudu kuzifanya katika mgodi huo, lakini wamekuwa wakinyimwa na badala yake wakipewa wageni kutoka nje ya kijiji chao na kupewa ajira hizo.
Malimi Mbulya amesema vijana ambao ni wakazi wa kijiji Kakola wamekuwa wakiambulia ajira za ulinzi tu kwa kisingizio kuwa hawana elimu wakati wanatambua kuwepo kwa kazi ndani ya mgodi ambazo haziitaji elimu ya juu na wamekuwa wakipewa wageni wan je ya wilaya yao ambao pia hawana elimu kubwa kama wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa huduma za jamii kijiji cha Kakola, Muhidini Ibrahimu, amesema mgodi huo umekuwa ukitoa ajira za sungu sungu ambazo hufanywa kwenye mazingira magumu na kwamba hulipwa Sh 150,000 kwa mwezi na kudai fedha hiyo haiwezi kukidhi mahitaji ya muhusika hasa ikizingatia ugumu wa kazi yenyewe.
Naye Apton Mshobozi ambaye amewahi kufanya kazi katika mgodi huo anasema licha ya kutoa ajira kwake kama mkazi wa kijiji hicho na kutumikia kwa muda wa miaka 10, aliachishwa kazi baada ya kupata ugonjwa wa ngozi kutokana na kemikali za sumu akiwa kazini bila ya kulipwa stahiki zake.
"Nilipata ugonjwa wa ngozi mwaka 2007 sikuwa peke yangu maana tulikuwa kama wafanyakazi tisa, lakini hakuna ambacho nimekipata kutoka Acacia, walinipeleka kwenye hospitali yao kwa uchunguzi baada ya hapo walinitelekeza hapa kijijini bila hata ya fedha za kununulia dawa za kutibu ngozi hivyo naiomba serikali itusaidie" amesema Mshobozi.
Aidha mtandao huu ulihojiana na Katibu wa Chama cha Wafanyakzi wa Tasnia ya Nishati na Madini (NUMET) Kanda ya Ziwa, Yusuph Kalyango ambaye pia ni Afisa Afya, Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) Taifa amesema sheria ya kazi ya mwaka 2006 (6) na kanuni zake, zinawabana wafanyakazi wa migodini wanapokuwa wakidai haki zao.
"Sheria zetu za wafanyazi wa migodini bado zinatubana kwa sababu mwajiriwa anaeleza anachokilalamikia na mwajili anasema anachokukatalia kwa hiyo kunakuwa na mgongano hii inawapa mwanya kutowalipa na hapa ninachokiona sidhani kama kuna uelekeo wa watu hawa kulipwa stahiki zao kwa sababu anaewachunguza kiafya ni daktari wa Acacia hivyo hawezi kusema ukweli, sio rahisi itabaki kuzungushana tu,” amesema Kalyango.
Hata hivyo licha ya sheria na kanuni kuwabana lakink numet iko tayarikuwasaidia na kwamba wanachokifanya ni mwajili kuwatambua watu hao kuwa walikuwa wafanyakazi wake ili aweze kuwalipa stahiki zao.