ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 26, 2022

JAMII IMESHAURIWA KUWEKA UTARATIBU WA KUPIMA MAGONJWA YA SARATANI KWANI YANATIBIKA.

 


Waandishi wa habari Mkoani Mwanza wamejengewa uelewa juu ya magonjwa ya saratani ili wakaielimishe jamii yenye uelewa mdogo  katika maradhi hayo.

 

Taasisi ya Aga Khan kupitia mradi wa mtambuka wa saratani (TCCP) umetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 37 Mkoani Mwanza Machi 25,2022 katika ukumbi wa nyakahoja mradi huo unafadhiriwa na Shirika la Maendeleo la Ufarasa (AFD) kwa kushirikiana na  Taasisi ya Aga Khan (AKF) wenye thamani ya Euro13.3m.


 Akizungumza katika  mafunzo hayo Mwezeshaji, Brendalinny John amesema  lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya kuelimisha jamii namna ya kujiepusha na maradhi ya saratani sanjari na kuripoti taarifa sahihi.


 Amesema ni wajibu wa kila mwandishi wa habari kuandika taarifa za ugonjwa wa saratani kwa usahihi na uhakika kwa kufuata maadili na kutoa elimu kwa jamii ili waweze kutambua suala hilo na kufuata matibabu kwani ugonjwa huo unatibika.


Kwa upande wake Dkt.bingwa wa magonjwa ya Saratani alieyebobea katika magonjwa ya mionzi Beda Likonda aliyekuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo kutoka hospital ya Kanda Bugando amesema kuwa kila mwaka Tanzania inapata wagonjwa wapya elfu 40000 wa magonjwa ya Saratani  ikiwa Saratani ya shingo ya kizazi ikiwa inaongoza.

 

Amesema kuna changamoto mbalimbali za kupambana nazo kama Nchi wakipata takwimu halisi ,kutoa elimu kwa jamii na wadau wa afya juu ya njia za kuepuka na kujilinda na ugonjwa huo na tiba shufaa inatakiwa izingatiwe ilikupambana na ugonjwa huo wa Saratani.


Dkt. Bingwa wa upasuaji kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa ya Sekou toule, Athanas Ngambakubi mesema saratani ni ugonjwa unaosababishwa na kugawanyika kwa seli za kiungo chochote mwilini bila kufuata utaratibu wa kawaida.


Dkt. Ngambakubi amesema kuwa watoa huduma binafsi waweke bei rafiki kwa wagonjwa ili kuweza kuokoa maisha yao.


Ngambakubi ameishauri jamii kuweka utaratibu wa kuchunguza afya zao na kubaini mapema ugonjwa huo ambao unatibika.


 Amesema dalili za saratani kwa wanawake ni kutokwa damu ukeni, maji maji machafu yenye harufu kali, uvimbe, homa, kuathili mfumo wa hewa kupungua uzito, vidonda visivyo pona.


Naye Meneja ubia uwezeshaji na mawasiliano wa mradi wa mtambuka wa saratani,Sarah Maongezi amesema mradi huo wa miaka minne ambao unatekelezwa kwenye wilaya 13 za mkoa wa Mwanza na Dar es salaam kwa kushirikiana na timu za mkoa.


"Mradi huu utaboresha huduma za awali za saratani kwenye vituo 100 vya afya vya Mwanza 50 na Dar es saalam 50 japo kuwa upo katika mikoa miwili lakini manufaa yake yataenea nchi nzima"amesema Maongezi.


Amesema lengo la mradi huo ni kudumisha ushirikiano na tafiti kuhusu saratani, kuboresha miundo mbinu na vifaa tiba vya huduma ya saratani, kuendeleza na kukuza rasimali watu wa taaluma mbalimbali za matibabu ya saratani na uboreshaji wa huduma na uhamasishaji wa saratani katila jamii.


Amesema jamii inauelewa mdogo juu ya kutambua na kupima ugonjwa huo kwani ni vema wajitokeze kwa wingi kufanya matibabu mapema na kuweza kubaini tatizo.


Mradi huo ni wa miaka 4 unaotarajia kumalizika mwaka 2024 na unamatarajio ya kujenga hospitali ya Saratani yenye mashine mbili za kisasa za mionzi ya  nje na ya ndani ,gari la uchunguzi wa Saratani ambalo litakuwa na mashine ya uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti na kupata taarifa sahihi za Saratani ,viatarishi ikiwa ni pamoja na kupata huduma bora.

TASAC YATOA ELIMU JUU YA USALAMA WA SAFARI ZA MAJINI ZIWA VICTORIA.

 Shirika la uwakala wa meli nchini TASAC, limetoa wito kwa Wanafunzi nchini kuzingatia masomo ya sayansi ,Hisabati na Jiografia ili waweze kutimiza ndoto zao za kitaaluma ikiwemo ya kuwa mabaharia.

Akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya KAHANGARA, wilayani MAGU mkoani MWANZA Kaimu meneja masoko na mahusiano wa shirika hilo JOSEPHINE BUJIKU amesema hali hiyo inatokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya wafanyakazi katika sekta ya maji hapa nchini.

RAIS SAMIA KUOKOA JENGO LA HALMASHAURI LILILOSIMAMA UJENZI KWA ZAIDI YA MIAKA 10

 Kamati ya Bunge ya LAAc imekagua ujenzi wa ofisi ya Utawala ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu na kuahidi kuifikisha kiu ya wananchi wa wilaya hiyo kuona jengo lao linakamilika nazo huduma zikitolewa toka kwenye ofisi hizo.

Sambamba na kuridhishwa utekelezaji wa mradi huo, akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi, Kaimu Mwenyekiti Mhe. Aloyce Akwezi (Mb) ameipongeza Halmashauri kwa jengo imara litakalowafikishia huduma wananchi kwa karibu.
Pia amewataka TAMISEMI kuhakikisha inaleta fedha zilizobaki ili kuweza kukamilisha mradi uliochukua zaidi ya miaka kumi. Wakati huo huo, Naibu Waziri (TAMISEMI) Mhe. Dkt Festo Dugange amewahakikishia kamati kuwa amepokea maelekezo ya kuleta fedha kwa mradi huo uliogharimu takribani bil 7 na utaisha kwa wakati. Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa Ndg. Ngusa Samike amepokea salamu za pongezi na kusema ushirikiano wa viongozi wa Mkoa umeweza kuleta mafanikio. Kukosekana kwa migogoro ndio kumeleta mafanikio makubwa Halmashauri ya Magu.










RAIS WA UKRANE ATOA MWITO WA MATAIFA KUONGEZA UZALISHAJI WA NISHATI.

 


Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameyatolea mwito mataifa yenye utajiri wa mafuta na gesi kuongeza uzalishaji kufidia nakisi ya usambazaji wa nishati kutoka Urusi. 


Akihutubia kwa njia ya video kwenye jukwaa la Doha linalofanyika kila mwaka kujadili changamoto za ulimwengu, Zelensky amesema ni muhimu kwa mataifa kama Qatar kuongeza usambazaji wa gesi duniani ili kupunguza bei ya nishati. 


Amesema kutokana na uharibifu unaofanywa na Urusi nchini Ukraine, taifa lake litashindwa kusafirisha nje mazao na bidhaa zake hali itakayoathiri ulimwengu mzima. Matamshi yake yanakuja wakati Urusi inaendeleza mashambulizi yake ya kijeshi nchini Ukraine na kupuuza miito ya kukomesha vita kwa njia ya mazungumzo.

MKE ADAIWA KUMUUA MUMEWE.

 


Mwanamke mmoja mkazi wa Kitongoji cha Kililangwena wilayani Tanganyika mkoani Katavi, Fadhia anatuhumiwa kumuua mumewe Laurent Buchumi (36) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni.


Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame amesema tukio hilo limetokea Machi 24, 2022 saa 5:30 usiku nyumbani kwa wanandoa hao baada ya kutokea ugomvi baina yao.


“Walikuwa na ugomvi ndani, baada ya kutokea ugomvi  mwanaume alitoka nje na mtuhumiwa alimfuataa  na kumchoma na kitu chenye ncha kali” amesema


Mbali na hilo Kamanda Makame amesema Belta Fransisco mkazi wa mtaa wa Ilembo Manispaa ya Mpanda ameua kwa kupigwa na kitu kizito chenye ncha kali kichwani kwake alipokuwa shambani.


Kamanda Makame ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Machi 24 saa 3:30 asubuhi shambani kwake.

Friday, March 25, 2022

RAIS SAMIA; WAFUNGWA WANAWEZA KUITWA WANAFUNZI.

 


Rais Samia Suluhu Hassan amesema, wanaohukumiwa kufungwa jela wanaweza kupewa jina la wanafunzi kwa sababu shughuli kubwa ya Magereza ni pamoja na kujifunza na kurekebisha watu.


Amesema hayo leo Ijumaa Machi 25, 2022 katika uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi ya makao makuu ya Magereza jijini Dodoma.


“Ni kweli kabisa ndugu zetu wanaohukumiwa kufungwa ni wafungwa, lakini tunaweza kuwapa jina la wanafunzi kwa sababu shughuli kubwa ya Magereza pamoja na adhabu ni kujifunza na kurekebisha watu kwa shughuli wanazojipanga nazo,”amesema Rais Samia Suluhu Hassan


“Wakishirikishwa ipasavyo inakwenda kuwapa uzoefu na kwenda kuwapa taaluma, wakitoka waende kujitegemea haitaeleweka kama mfungwa anatoka hana la kufanya kama wale tulizoea kuwaona wakati wa msamaha,”amesema.


“Mfungwa anasamehewa leo nje hana la kufanya hana pa kukaa familia inamkana. Anaamua kwenda tena kuiba kwa makusudi ama kwenda kufanya jambo ambalo ataonekana kufanya akamatwe arudishwe tena. Huo sio mwendo mzuri mwendo mzuri ni wanafunzi hawa wanapotoka kwenda kuweza kujitegemea kutokana na taaluma na ujuzi watakaokuwa wanapata wakiwa ndani,”amesema.

SIFA ZINAZOIFANYA MWANZA SEC KUTOA VIONGOZI

 MKURUGENZI wa Taasisi ya Nitetee (Nitetee Foundation) ya jijini Mwanza, Dkt. Flora Lauwo amewaasa wadau mbalimbali wa elimu kushirikiana na Serikali kuboresha miundombinu ya elimu katika Shule ya Mwanza Sekondari hatua itakayosaidia kuinua zaidi ufaulu kwa wanafunzi.

Dkt. Laulo ametoa rai hiyo Machi 24, 2022 alipokuwa mgeni rasmi kwenye Mahafali ya 22 ya Kidato cha Sita yaliyofanyika shuleni hapo yakishirikisha wanafunzi 359 (wavulana 102 na wasichana 257) ambao wanatarajiwa kuhitimu masomo yao mwezi Mei mwaka huu 2022. Amesema licha ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za waalimu lakini bado kuna changamoto kwa wanafunzi wa kike kukosa chumba maalum kwa ajili ya kujistiri na kubadilisha taulo za kike wakati wa hedhi ambapo ametoa rai kwa wadau mbalimbali kusaidia kutatua changamoto hiyo. Dkt. ametumia fursa hiyo kukabidhi taulo za kike kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa kike shuleni hapo pamoja na kukabidhi jezi za michezo kwa ajili ya wavulana na wasichana shuleni hapo ikiwa ni sehemu ya taasisi yake kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo taasisi ya 'The Desk & Chair Foundation' kuhamaisha michezo mashuleni. Naye Mkuu wa Shule ya Mwanza Sekondari, Mwl. Sudi Gewa ameishukuru Serikali kwa uamuziwake wa kuzikarabati Shule kongwe nchini ikiwemo Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1959 ambayo kwa sasa wanafunzi wote wa kike wa kidato cha tano na sita wanaishi bweni. Aidha amepongeza uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni ambapo Shuleni hadisasa imepokea wanafunzi wawili ambao wameahidi kusoma kwa bidii huku wakijutia waliyopitia. Katika hatua nyingine Mwl. Gewa amebainisha kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyombo vya kukusanyia uchafu na kuupeleka dampo na kuomba wadau kusaidia upatikanaji wa vifaa hivyo ikiwemo bajaji ili kuwaondolea gharama kubwa zinazohitajika kuwalipa wazabuni wa kuzoa uchafu ambazo ni kati ya shilingi laki saba hadi laki tisa kwa mwenzi. Awali akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Scholastica Nchehe alisema Shule ya Mwanza Sekondari inakabiliwa na uhaba wa vifaa vya maabara na kuomba wadau wa elimu na Serikali kushirikiana kutatua changamoto hiyo ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza vyema.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Nitetee (Nitetee Foundation) ya jijini Mwanza, Dkt. Flora Lauwo pia alikabidhi zawadi kwa waalimu wa wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya vizuri katika mitihani yao ya majaribio.
Wanafunzi 359 (wavulana 102 na wasichana 257) katika Shule ya Mwanza Sekondari wanatarajiwa kuhitimu kidato cha sita mwaka huu 2022.
Wanafunzi wa kidato cha sita (kulia) wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao mwezi Mei mwaka huu 2022 katika Shule ya Mwanza Sekondari wakiwa kwenye mahafali yao. Kushoto ni wazazi na walikwa mbalimbali kwenye mahafali hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Mwanza Sekondari, Debora Ringo amewaasa wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajiwa kuhimu mwezi Mei mwaka huu 2022 kuzingatia kile walichojifunza na kufanya vyema kwenye mtihani wao ili kutimiza ahadi waliyoitoa ya kufaulu kwa daraja la kwanza zaidi ya 200.

Thursday, March 24, 2022

RAIS SAMIA ATAKA KUONDOLEWA KWA ALAMA YA MWENGE KATIKA DARAJA LA TANZANITE.

 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemwagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa kubadilisha alama ya mwenge iliyowekwa kwenye daraja mpya la Tanzanite na kuweka alama ya madini hayo itakayoendana na jina la daraja hilo.

Hayo ameyasema leo Machi 24, 2022 Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa daraja hilo lilogharimu Sh 243 bilioni.

Rais Samia amesema ushauri huo aliupata kutoka kwa wananchi kwamba wangependa daraja hilo walipoweka alama ya mwenge, basi kuwekwe alama ya Tanzanite ili kuendana na uhalisia wa jina la mradi huo.

“Niseme kidogo Waziri ushauri nilioupata kutoka kwa wananchi daraja hili tunaliita la Tanzanite lakini alama tuliyoiweka ni alama ya mwenge. Pamoja na kutambua mwenge ni tunu yetu adhimu wananchi wangependa sana kuona alama ya tanzanite pale ilipo alama ya mwenge ili liendane na jina la daraja hili,” amesema Rais Samia.  
Hata hivyo, Rais ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu.

“Nitoe wito kama ilivyo kawaida yangu kujitokeza kwa wingi wakati wa kuhesabiwa Agosti mwaka huu, twendeni tukahesabiwe,” amesema.

ACHENI KUTUPA BANDEJI NA MIFUKO KWENYE VYOO VYA HOSPITALI YA BUGANDO MNASABABISHA HAYA

KUNA maji taka yanayofuka kama chemchem katika kiunga cha kipita shoto kidogo cha Nata , kinacho gawanya barabara ya Nyerere na barabara ya Wurzburg inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, yakitapakaa barabarani na mengine kutitirika kwenye mitaro ya eneo hilo. Maji hayo machafu licha ya kuharibu hali ya hewa ya eneo hilo kwa kutoa harufu mbaya pia yanatajwa kuhatarisha afya za watumiaji wa barabara hizo kwamba huenda yakawa chanzo cha milipuko ya maradhi. Bila shaka mamlaka zinataarifa juu ya hili, lakini nini kauli yao?





 

MKE MPYA WA MREMA ASEMA ATAMRUDISHA UJANANI.

 

“Nataka kumrudisha Mrema kuwa kijana.” Hayo ni maneno ya mke wa mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labor Part (TLP), Augustino Mrema anayejulikana kwa jina la Doreen Kimbi, wakati wakiwa kanisani kwa ajili ya ibada ya kufunga ndoa.

Mrema ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, kuwa mbunge na kugombea urais wa Tanzania leo Alhamisi Machi 24, 2022 amefunga ndoa katika kanisa Katoliki Parokia ya Uwomboni Kiraracha mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Doreen amesema baada ya ndoa hiyo takatifu, ahadi yake ni kuzidi kumpendezesha Mrema kutoka hapo alipo hadi kuwa kijana.

“Kwanza watu waelewe kwamba mpaka kufikia wanamuona hivi, mimi ndio nimefanya hivi, kwani katika kipindi hiki cha uchumba nilikuwa nikimlea kwa muda mrefu sasa kuhakikisha anakuwa sawa na vitu vyote anavyovihitaji anavipata na anapata pia amani na ukimuona sasa na wakati ule unaweza kudhihirisha kwamba amebadilika.

“Kwa hiyo sitarajii kubadilika mimi kwa sababu ni kitu ambacho nimeamua na moyo wangu, sijashurutishwa na mtu na sina shinikizo lolote, kwa hiyo wategemee kumuona anapendeza zaidi kutoka ile hatua aliyokuwa nayo mpaka kumfikisha hapa na kwenda hatua nyingine ya kuwa kijana,”amesema Doreen.

Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labor Part (TLP), Agustino Lyatonga Mrema amesema familia ya mke wake ilimtaka alipie mahari ya Sh4.2 milioni ambapo hadi sasa ameweza kulipa  Sh1 milioni.

HRW YAITAKA ETHIOPIA KUCHUNGUZA SHAMBULIO LA ANGA DHIDI YA SHULE.

 


Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limeitolea mwito Ethiopia leo, kufanya uchunguzi wa shambulio la anga lililofanywa dhidi ya shule moja katika jimbo la Tigray ambalo liliuwa watu kadhaa. 

Shambulio hilo huenda likawa ni uhalifu wa kivita. Shirika hilo limesema mabomu matatu yalirushwa Januari 7 dhidi ya shule iliyokuwa ikiwahifadhi Watigrinya katika mji wa Dedebit na kuwaua kiasi watu 57 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 42. 

Human Rights Watch limesema serikali ya Ethiopia inapaswa kufanya uchunguzi wa kina na usioegemea upande kuhusu tukio hilo ambalo huenda lilikuwa uhalifu wa kivita na kuwachukulia hatua zinazostahiki waliohusika. 

Waliouwawa kwenye shambulio hilo walikuwa zaidi wazee, wanawake na watoto waliokuwa wakilala kwenye mahema yaliyotengenezwa kwa plastiki na shirika hilo limesema hakukuwa na ushahidi wa kuonesha walikuweko wanajeshi waliolengwa katika tukio hilo.

WAZIRI MKUU WA AUSTRALIA ATAHADHARISHA DHIDI YA PUTIN KUSHIRIKI MKUTANO G 20

 


Waziri mkuu wa Australia Scott Marrison amesema hii leo kwamba mpango wa Rais Vladmir Putin wa Urusi wa kutaka kushiriki mkutano wa kilele wa kundi la nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi la G20 licha ya kushuhudiwa mgogoro wake na Ukraine, ni hatua ya kuvuka mpaka. 

Mkutano huo utafanyika baadae mwaka huu huko nchini Indonesia. Morrison amewaambia waandishi habari mjini Melbourne kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni hatua ya kimabavu na ukiukaji wa sheria ya kimataifa na kwa hivyo fikra ya kukaa kwenye meza moja na Putin ni hatua ya kuvuka mipaka. 

Amesema tayari Marekani iko katika mwelekeo wa kuutaja uvamizi wa Ukraine kuwa uhalifu wa kivita. Jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema Marekani imebaini kwamba vikosi vya Urusi vimefanya uhalifu wa kivita ndani ya Ukraine akisema nchi hiyo iliwalenga makusudi raia na kutumia mbinu za kivita zilizoshuhudiwa Chechnya na Syria.

Wednesday, March 23, 2022

DC MOYO KUWACHUKULIA HATUA KALI ZA KISHERIA WATAKAO HARIBU VYANZO VYA MAJI.

 

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na baadhi ya wananachi wa wilaya ya Iringa kuhusu jukumu la kutunza vyanzo vya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na baadhi ya wananachi wa wilaya ya Iringa kuhusu jukumu la kutunza vyanzo vya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na baadhi ya wananachi wa wilaya ya Iringa kuhusu jukumu la kutunza vyanzo vya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na baadhi ya wananachi wa wilaya ya Iringa kuhusu jukumu la kutunza vyanzo vya maji.

Na Fredy Mgunda,Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo kuwachukulia hatua Kali za kisheria wananchi na viongozi wote watakao hatibu vyanzo vya Maji na kukata hovyo miti.


Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya maji wilaya ya Iringa yaliyofanyika katika Kijiji Cha magunga alipokuwa akishilikiana kupanda zaidi ya miti Mia tano ambayo ni rafiki ya maji.


Moyo alisema Kuwa Serikali imekuwa inatumia gharama kubwa kuhifadhi vyanzo vya maji na kuwapelekea maji Wananchi Lakini Wananchi wamekuwa wakiharibu vyanzo vya maji kwa makusudi bila kujali Serikali imetumia gharama kiasi gani.


Alisema kuwa maadhimisho ya wiki ya maji ya mwaka huu 2022 ambayo yameanza rasmi tarehe 16/03/2022 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22/03/2022 lengo kubwa ni kukumbushakutunza rasmali za maji ni maisha ya wanadamu wote.


Moyo  alisema kuwa wilaya ya Iringa inaendelea kutoa huduma ya maji safi na salama kwa maeneo yote ya vijijini kwa wastani wa asilimia 75.6 na Iringa mjini imefikia asilimia 97 na hayo yote yanaendelea kuboreshwa zaidi na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan.


Alisema kuwa mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan anatambua adha ambayo wananchi wanaipata hasa wanawake kwenda kufuata maji umbali mrefu na kusababisha kero nyingi kwenye familia.


Moyo alisema katika mwaka wa fedha wa 2021/2122 wilaya ya Iringa inaendelea kukarabati miradi mbalimbali ya maji ikiwepo ya vijiji vya Nyabula/Ulanda, Magunga/Itengulinyi, Makatapola, Mbweleli,na Makuka yote kwa lengo la kuhakikisha wanawatua ndoa wakinamama wa wilaya hiyo.


Alisema kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan amefanikiwa kupata fedha na kuanza kutekeleza miradi mingine zaidi kupitia Mpango wa Maendeleo ya ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko -19 ambayo imeanza kutekelezwa katika majimbo ya Kalenga na Isimani.


Moyo alisema kuwa katika wilaya ya Iringa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaendelea kuvilinda vyanzo vya maji na kupanda mti ambayo inasaidia kutunza maji yaliyopo ardhini kwa ajili ya matumizi.


Alisema kuwa wataendelea kuitumia kauli mbiu ya maazimisho ya maji mwaka huu inayosema kuwa “maji chini ya ardhi,hazina isiyoonekana kwa maendeleo endelevu” kwa kvitunza vyanzo vyote ya maji vilivyopo wilaya ya Iringa.



Kwa upande wake meneja wa RUWASA wilaya ya Iringa Eng Masoud Samila alisema kuwa katika maadhimisho ya siku ya maji wilaya ya Iringa yaliyofanyika katika Kijiji Cha magunga wamefanikiwa kupanda jumla ya miti mia tano (500) ambayo ni rafiki na maji.


Eng Samila alisema kuwa lengo la serikali kuhakikisha inamtua ndoo mama kichwani na kuwasaidia wananchi wa wilaya ya Iringa kupata maji safi na salama kwa ukaribu ambao utasaidia kuendelea kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.

TANGA UTALII FESTIVAL KUHAMASISHA ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI

 

MKUU wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa katikati akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Tanga ambao hawapo pichani kuhusu Tamasha la Utamaduni ( Tanga Utalii Festival) linalotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii Jijini Tanga kulia ni Meneja wa Bia ya Heineken Kanda ya Kaskazini, Swalehe Madjapa ambao ni mdhamini mkuu wa tamasha hilo kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Tanga


MKUU wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa katikati akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Tanga ambao hawapo pichani kuhusu Tamasha la Utamaduni ( Tanga Utalii Festival) linalotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii Jijini Tanga kulia ni Meneja wa Bia ya Heineken Kanda ya Kaskazini, Swalehe Madjapa ambao ni mdhamini mkuu wa tamasha hilo kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Tanga
Meneja wa Bia ya Heineken Kanda ya Kaskazini, Swalehe Madjapa ambao ni mdhamini mkuu wa tamasha hilo akizungumza wakati wa mkutano huo kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa 

 Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua matukio kwenye mkutano huop

 

NA OSCAR ASSENGA, TANGA.

TAMASHA la Utamaduni ( Tanga Utalii Festival) linalotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii Jijini Tanga litatumika pia kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linayotarajiwa kufanyika nchini Agosti mwaka huu ikiwemo kutangaza fursa za utalii, uchumi na utamaduni katika tamasha hilo.

 Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa katika mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika wilayani hapa kuhusu kuelekea Tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuwa na aina yake

 Mgandilwa amesema wamekusudia kufanya tamasha hilo kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana mkoani humo pamoja na kutangaza tamaduni mbalimbali za makabila yanayopatikana Tanga.

 "Watanzania moja ya jambo tunalojivunia na tunapaswa kuenzi ni tamaduni zetu,  sisi katika ngazi ya wilaya tumeliona hilo na tumeazimia kufanya tamasha liyakalohusisha tamasuni za watu wa Tanga, hivyo tutakuwa na ngoma mbalimbali," amesema.

Mgandilwa amezitaja ngoma za asili zitakazoshiriki katika tamasha hilo kuwa ni mdumange, baikoko, singeli pamoja na msanja pia kutakuwa na wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya akiwamo Matonya, Kassim Mganga na Dula makabila.

Kwa upande wake Meneja wa Bia ya Heineken Kanda ya Kaskazini, Swalehe Madjapa ambao ni mdhamini mkuu wa tamasha hilo, amesema wameamua kudhamini tamasha hilo kutokana na umuhimu wake kwa watu wa Tanga.


"Bia ya Heineken tumeona umuhimu wa tamasha hilo katika katika kuutangza Mkoa wa Tanga kimataifa tunaamini kuna fursa nyingi za kiuchumi hivyo tunaamini kupitia tamasha hili tutawavutia wawekezaji," Amesema Swalaehe.

 

 Naye Mratibu wa tamasha  hilo,Nasoro Makau ameviasa vyombo vya habari nchini  kuzitangaza nyimbo za asili ili kuendelea kuuenzi utamaduni wa mtanzania.

 

 "Vyombo vya habari vinatangaza sana muziki wa kizazi kipya sasa vione umuhimu pia wa kutangaza utamaduni wetu watoto wetu nao watambue kuwa tuna nyimbo zetu za asili wasije wakabobea kwenye tamadunii za kimagharibi na kuacha tamaduni zao.

 

"Tamasha litakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo mbio fupi, burudani kutoka kwa wasanii tofauti kwa hiyo kwa wenyeji wa Tanga tunawasihi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Jengo la Urithi, tamasha  litaanza saa 12 asubuhi na halina kiingilio.  Kauli mbiu ya tamasha hilo ni 'Tanga Festival, karibu mahabani," amesema

DC MOYO AMEUTAKA UONGOZI WA MBOMIPA KUACHA KUTUMIA MADARAKA VIBAYA

 

MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo  akiongeza na baadhi ya viongozi wa MBOMIPA pamoja na wadau wa jumuiya hiyo ya uhifadhi wa wanyama pori wilaya ya Iringa.
mwenyekiti wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (MBOMIPA) Jonas Mkusa akiongeza na baadhi ya viongozi wa MBOMIPA pamoja na wadau wa jumuiya hiyo ya uhifadhi wa wanyama pori wilaya ya Iringa.
Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (MBOMIPA) wakifuatilie semina ya uhifadhi wa wanyama pori wa jumuiya hiyo
Baadhi ya wadau wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (MBOMIPA) wakifuatilie semina ya uhifadhi wa wanyama pori wa jumuiya hiyo

Na Fredy mgunda,Iringa.

MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ameutaka uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (Mbomipa) kuacha mara moja kutumia madaraka yao vibaya na kuwa chanzo cha migogoro baina ya jumuiya hiyo na wawekezaji.

Akizungumza wakati mafunzo kwa viongozi na wadau wa jumuiya hiyo,Moyo aliwataka viongozi hao kutafakari zababu zilizopelekea kufutwa kwa MBOMIPA miaka mitano iiliyopita na kuzifanyia kazi ili kuwa funzo la kukomesha migororo katika awamu hii.

Kiongozi huyo wa Wilaya ya Iringa alisema Serikali haiko tayari kushuhudia viongozi wa MBOMIPA wakitumia madaraka yao vibaya kwa kukwamisha mipango na maendeleo ya jumuiya hiyo wenye lengo la kuvutia wawezekezaji wengi zaidi katika maeneo ya hifadhi kwa manufaa ya wananchi wa vijiji 21.

Moyo alisema Serikali ya Wilaya ya Iringa inapenda kuona mabadiliko ya haraka katika kuimarisha uhai wa Jumuiya ya MBOMIPA, na Ufanisi chanya wa watendaji wa kila siku huku akihimiza ushirikiano baina ya wananchi wa vijiji vinavyonufaika, viongozi wa MBOMIPA na serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alisema mafunzo wanayopatiwa viongozi na wadau wa Jumuiya hiyo ni mwanzo mzuri wa safari ya kuimarisha MBOMIPA mpya Kwani Wanahitajika wadau wa uhifadhi  ndani na nje ya nchi ili kuwezesha utaalam na Rasirimali fedha zitakazosaidia kuinua maendeleo ya wananchi.

Aidha Mkuu wa Wilaya Mohamed Hassan Moyo amewahimiza wadau wa Uhifadhi wa wanyama na Mazingira kuongeza jitihada za uhifadhi wa mazingira, misitu na vyanzo vya maji ambavyo utegemewa na watu, mifugo na wanyamapori hatua ambayo itasaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa na Tabia nchi.

“Tayari tumeanza kupata madhara makubwa katika maisha ya binaadam na pia kwa uchumi wa wananchi wetu na kuleta mzigo mzito kwa Taifa letu la Tanzania, Utafiti wa mabadiliko ya hali ya hewa na Tabia nchi umebaini ongezeko la hali ya joto pia ongezeko la tofauti la mienendo ya mvua na hasa upungufu wa rasilimali maji” Alisema Moyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (MBOMIPA) Jonas Mkusa alisema kuwa kusimama kwa shughuli za Jumuia hiyo kulikuwa na athari katika vijiji hasa kutokana na kukosa mapato yaliyokuwa yakipatikana awali kutokana na wadau walikuwa wamewekeza katika maeneo hayo

Mkusa alisema kurejea kwa jumuia hiyo ni jambo la faraja kwa wananchi wa vijiji 21 vinavyonufaika na MBOMIPA na kuhimiza ushirikiano utakaosaidia kuvutia wawekezaji na kuepuka kuzalisha migogoro isiyo na tija inayoweza kukwamisha maendeleo ya Jumuiya hiyo.

Mwenyekiti aliwahakikishia wananchi na wadau kuwa atahakikisha fursa zote zilizopo kupitia MBOMIPA zitakuwa wazi kwa ajili ya kufanikisha malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza kuwa uongozi wa Jumuiya hiyo hautokuwa kikwazo katika kufikia malengo.

 

Mbomipa ni Jumuiya inayoshughulika na uhifadhi wa Maeneo ya hifadhi ya wanyamapori ya jamii (WMA) nje ya mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Wilayani Iringa, Wanyama walioko katika eneo hilo wanatoka ndani ya hifadhi hiyo na hifadhi ya mikumi.

Vijiji vinavyounda Jumuiya hiyo ni Idodi, Ilolompya, Isele, Kinyika, Kisanga,Luganga, Mafuluto,Magozi,Mahuninga, Makifu, Mboliboli, Mkombilenga, Nyamahana, Itunundu, Kimande, Malizanga, Mbuyuni, Mapogolo, Kitisi na magombwe.

 

AHUKUMIWA KUNYONGWA KWA KUMUUA JIRANI YAKE.

 

Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma imemuhukumu kunyongwa hadi kufa mtu mmoja aitwaye Kinyota Kabwe mkazi wa Muzye wilayani Kasulu kwa kosa la kumuua kwa makusudi jirani yake kwa kumchoma mkuki mara tatu na kusingizia alikuwa amechanganyikiwa.


Kesi hiyo namba 105 ya Jamhuri dhidi ya Kinyota Kabwe imesikilizwa na Jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo Lameck Mlacha, inaelezwa mnamo Septemba 15, 2013 majira ya saa tisa alasiri mshtakiwa akiwa na mkuki alienda nyumbani kwa Lucia Tekena na kumchoma mkuki shingoni,kifuani na tumboni huku binti wa marehemu nae akijeruhiwa na mshtakiwa.


Inaelezwa kabla ya tukio hilo ambalo baada ya muda mfupi mwanamke huyo alipoteza maisha na yeye kukamatwa nikama kulikuwa na ugomvi na mvutano kati yake na mkewe nyumbani kwake ambao unahisiwa kuna uwezekano ulikuwa una muhusisha marehemu pia hivyo kusababisha mauaji hayo.


Upande wa Jamhuri uliongozwa na wakili Antia Julius na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Edna Aloyce. Upande wa utetezi uliwasilisha ushahidi wa mshtakiwa na kaka yake ulio eleza mshtakiwa ana matatizo ya akili na alikuwa anatumia dawa kwa muda hivyo kuna wakati hali ilikuwa inakuwa mbaya huku muhusika akisema hakumbuki tukio la kuchoma mkuki.


Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano akiwemo aliye shuhudia mauaji hayo na Daktari wa magonjwa ya akili aliye mpima na majibu yakawa kuwa hana ugonjwa wowote wa akili. Jaji Mlacha amesema inaonyesha mshtakiwa alikusudia kuua ndio maana alielekeza mkuki tumboni ,kifuani na shingoni na suala la ugonjwa wa akili hiyo ni namna ya kutafuta kujitetea na haina mashiko, hivyo akamhukumu adhabu kunyongwa hadi kufa.

ACT - WAZALENDO YAFYNGUKA MARIDHIANO YA KISIASA

 


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema chama hicho kimeingia katika maridhiano ya kisiasa kwa ajili ya kuimarisha amani na utulivu katika serikali ya umoja wa kitaifa.


Masoud ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema hayo wakati akizungumza na wanachama na wananchi katika mikutano ya hadhara Wilaya ya Kati Unguja na Magharibi katika ziara yake ya kujitambulisha.


“Maridhiano ya kisiasa yamefungua milango ya heri na maelewano ambapo siasa za chuki na uhasama zimeondoka na wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo,” alisema.


Masoud aliwataka wananchi kuendelea kutekeleza maridhiano hayo na kuyaenzi kuhakikisha yanakuwa endelevu kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar katika kupiga hatua ya maendeleo.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Ismail Jussa aliwataka wananchi kuiunga mkono ACTWazalendo kwani kipo kwa ajili ya kuleta maelewano na kuwaunganisha wananchi wote katika kukuza shughuli zao za kiuchumi na maendeleo.


Katika Kijiji cha Marumbi Wilaya ya Kati Unguja, Othman alizindua tawi la chama na kuwataka wanachama wake kukiunga mkono kuhakikisha kinashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.