ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 18, 2021

SAMIA ATAJA SABABU MGAO WA MAJI, ATOA MAAGIZO.

 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani amesema  uvamizi wa  vyanzo vya maji, kukata miti na kuchepusha maji kwa ajili ya matumizi ikiwemo kilimo na mifugo ni chanzo cha upungufu wa maji katika maeneo mengi nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando (BMC), Rais Samia amesema  anatambua miji mingi mikubwa inakabiliwa na uhaba wa maji unaosababisha mgao wa maji na upungufu wa umeme na kutaja sababu hizo.

“Kuna watu wanalima karibu na vyanzo vya maji haya yote mawili yanapelekea vyanzo vya maji kupungua. Yanapungua na hayaendi kule yanapotakiwa yaende."

“Kwa maana hiyo mtiririko katika maeneo  ambayo maji yanachukuliwa yanasafishwa na kupelekwa kwa matumizi ya watu yakiwa maji safi na salama unapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Ametaja sababu ya shida ya maji jijini Dar es Salaam ni kupungua kwa kina cha maji na kusababisha  kuathiri mchakato wa kupeleka maji kwa wananchi.

UPUNGUFU WA UMEME, TANESCO KUGEUKIA GESI ASILIA.

 


Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema linachukua hatua za haraka kwa kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia.

Hatua hizo ni kutokana na mabadiliko ya hali hewa, kupungua kwa kiwango cha maji katika mito na mabwawa nchini.

Taarifa ya Tanesco iliyotolewa leo Alhamisi Novemba 18, 2021 imesema hali ya upungufu huo imeathiri uzalishaji katika vituo vya kuzalishia umeme vinavyotumia maji.

“Athari kubwa imetokea katika vituo vyetu vya Kihansi, Kidatu na Pangani. Jumla ya upungufu wa uzalishaji ni nakribani megawati 345 ambayo ni asilimia 21 ya uzalishaji wote” imesema.

Hata hivyo shirika hilo limesema linachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kwa kuharakisha matengenezo ya baadhi ya mitambo yake ya Ubungo I inayozalisha megawati 25.

Vituo vingine ni Kinyerezi I megawati 185, Ubungo III megawati 112, pamojqa na kuwasha kituo cha Nyakato kinachozalisha megawati 36 hali itakayofanya kuwa na jumla ya megawati 358.

 “Kwakuwa kutakuwa na upungufu kwa baadhi ya mikoa taarifa zitatolewa kwa wakati ili wateja waweze kupanga kazi zao”. Imeeleza.

RAIS SAMIA AZINDUA MASHINE YA MRI BUGANDO.

 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua mashine ya kupima magonjwa mbalimbali (MRI) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) leo Alhamisi Oktoba 18, 2021.

 Rais Samia amezindua mashine hiyo baada ya kuwasili leo jijini Mwanza kuhudhuria Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Bugando iliyoanzishwa mwaka 1971.

Baada ya kufika hospitalini hapo Rais Samia amepewa taarifa ya miradi mbalimbali inayoendelea hospitalini hapo ukiwemo mradi wa jengo la saratani ambalo Serikali ilitoa zaidi ya Sh1 bilioni.Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Dk Fabian Massaga, jengo hilo la huduma za saratani litagharimu zaidi ya Sh5.2 bilioni ambalo litakuwa na chumba maalumu cha kufanya utafiti kwa wagonjwa wa saratani kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwingineko.

Dk Massaga pia ametoa taarifa kwa Rais Samia juu ya mradi wa jengo la mama na mtoto ambapo mpaka ujenzi wake ukamilike litagharimu zaidi ya Sh6.5 bilioni ambapo kwa sasa hospitali hiyo imetenga Sh500 milioni ya mapato ya ndani kuanza ujenzi huo.

Amesema pia hospitali hiyo inatekeleza ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa wenye matatizo ya macho, jengo kwa ajili ya wagonjwa wa nnje na wanafanya utafiti kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza.

WAFUNGWA WA 3 WALIOTOROKA JELA YA KAMITI KENYA WAKAMATWA.

 


Wafungwa 3 wanaohusishwa na ugaidi ambao walitoroka jela ya kamiti nchini Kenya siku ya Jumatatu wamekamatwa.

Watatu hao Musharaf Abdalla maarufu Alex Shikanda , Joseph Ouma na Mohammed Ali Abikar walikamatwa katika eneo la Kitui.

Kwa sasa washukiwa hao wanasafirishwa kurudi jijini Nairobi.

Walitoroka kutoka jela inayolindwa zaidi baada kutoboa ukuta wa jela hiyo.

Baadaye walitumia nguo aina ya blanketi na waya kutengeneza kamba ambazo walitumia kupanda kuta mbili ndefu za jela hiyo.

Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya maafisa wa jela ya Kamiti kukamatwa kwa madai ya kuwasaidia wahalifu hao kutoroka

Siku ya Jumatano, Rais Kenyatta alimwaagiza waziri wa masuala ya ndani Fred Matiangi kuhakikisha wanatumia kila mbinu kuwakamata wahalifi hao hatari.

Alivitaka vitengo vyote vya upelelezi kuwawajibisha maafisa wote waliodaiwa kuhusika na kutoroka kwao.

Kulingana na gazeti la Daily Nation, awali , vitengo vya usalama katika kaunti ya Kitui vilikuwa vimewekwa katika hali ya tahadhari baada ya wakaazi wa eneo hilo kuwaona wafungwa hao watoro.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kitui Leah Kithei mapema Alhamisi alithibitisha kwamba vitengo vyote vya usalama katika eneo hilo, wakiwemo machifu na manaibu wao walikuwa wamewekwa katika hali ya tahadhari.

''Habari hiyo pia imesambazwa kwa wenzetu katika kaunti jirani ya Tanariver na Garissa'', bi Kithei aliambia Daily Nation.

''Iwapo ni kweli ni wao, bila shaka tutawakamata, ni muda tu kabla ya hilo kufanyika''.

Wakazi waliowaona wanasemaje?

Wakaazi wa eneo hilo waliripoti kuwaona watatu hao , ambao wanawashuku kuwa wahalifu wanaosakwa baada ya kutoroka jela siku ya Jumapili, katika kituo cha maduka cha Malalani katika kaunti hiyo kubwa.

Walisema kwamba watatu hao , walioonekana kuchoka na wenye kiu, walinunua maziwa mengi , na maji , mkate na biskuti kutoka kwa maduka ya eneo hilo na kuplipa pesa.

Kwa mujibu wa gazeti hilo wakaazi walianza kuwashuku baada ya kutaka kuoneshwa njia ya kuelekea msitu wa Boni huko kaunti ya Lamu.

''Mmoja ya watoro hao alikuwa na kidonda katika mguu wake na alikuwa akichechemea pengine kwasababu ya kutembea mwendo mrefu. Walionekana kukanganyika na waliopotea, wasio na uelewa wowote wa eneo hilo''.

''Walikuwa wanauliza jinsi wangeweza kuelekea Garissa au Tanariver kutoka eneo hilo'', alisema mfanyabiashara katika soko hilo ambaye alizungumza na Nation kwa makubaliano kwamba hatotajwa kutokana na sababu za kiusalama.

Mfanyabiashara huyo aliwaelezea watatu hao kama mtu mmoja mwembamba mwenye asili ya kisomali na wanaume wawili Waafrika , maelezo ambayo ni sawa na watoro hao.

''Hawakuwa wamebeba mzigo lakini mmoja wao alikuwa amebeba begi dogo na kile kilichoonekana kama nguo''.

Soko la Malalani lipo kilomita 100 mashariki mwa mji wa Kitui na karibu na mpaka na kaunti ya Tanariver.

Linapakana na Mbuga ya wanyama ya Kusini mwa Kitui ambayo imekuwa maficho kwa washukiwa wa ugaidi.

RAIS AMTUNUKU CHETI DKT GWAJIMA.

 


DKT. GWAJIMA AMSHUKURU RAIS KWA CHETI NA NISHANI YA 'MEDAL OF GOLD'.

Na.WAMJW  DSM

Dkt. Dorothy Gwajima, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kushirikiana na Taasisi ya Skauti Tanzania hivyo, kumtambua kuwa miongoni mwa waliotunukiwa cheti na nishani ya "Medal of Gold".

Dkt. Gwajima amewashukuru watumishi na wadau wote wa sekta ya afya na kusema kuwa cheti na nishani hiyo ni heshima kwa Wadau wote wa Sekta ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na itachochea zaidi Ari na Kasi ya kazi katika kushirikiana na Skauti Tanzania.

USALAMA WAIMARISHWA KAMPALA BAADA YA MASHAMBULIZI YALIYOUA WATU 6

 


Usalama umeimarishwa katika mji mkuu wa Uganda Kampala, siku moja baada ya mashambulizi mawili ya mabomu kuutikisa mji huo na kusababisha vifo vya watu sita.

Maafisa wa polisi na wanajeshi waliojihami wameonekana wakishika doria katika maeneo mbalimbali ya mji huo/

Wito umetolewa pia kwa raia nchini humo kuwa katika hali ya tahadhari kufuatia mashambulizi ya jana, ikiwa ndiyo ya hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa mashambulizi ambayo yameshuhudiwa siku za hivi karibuni.

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na shambulizi hilo la kujitoa muhanga lililolenga kituo cha polisi na majengo ya bunge.Zaidi ya watu 33 walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya jana.

Wednesday, November 17, 2021

POLISI GOBA WAJERUHI KWA KIPIGO, MAJERUHI YUKO ICU MOI, ANAPUMULIA MASHINE, 'NDUGU WAELEZA KUPONA KWAKE UTATA'

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhani Kingai
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Muliro J. muliro


 *Majeruhi aomba IGP Sirro afikishiwe salamu.


Na Mwandishi Wetu

Jumatano, November 10, 2021, Polisi Goba walidaiwa kumkamata Issa Kassim (20), nyumbani kwao huko Goba kwa madai kwamba ameuziwa TV ya wizi, tukio ambalo mtuhumiwa alikana kulitenda.

 

Baada ya kumkamata mashuhuda wa tukio hilo walidai askari hao waliondoka naye wakidai wanampeleka kituo cha polisi Goba, lakini kabla ya kufika huko kituoni walimuomba awapigie simu ndugu zake waweze kumuokoa.

 

Mtuhumiwa (Issa Kassim), alipiga simu kwa mama yake akazungumza na mmoja wa polisi hao aliyefahamika kwa jina moja la Majuto.

 

Askari huyo wa jeshi la polisi kituo cha Goba, katika mazungumzo na Mama wa mtuhumiwa huyo inadaiwa alimuomba atume Sh.800,000 ili kijana wake waliyemshikilia kwa tuhuma ya kununua TV ya wizi waweze kumuachia.

 

Mama wa mtuhumiwa aliomba apunguziwe dau hilo, badala ya kuwapatia Tsh 800, 000 atume Tsh500,000, na  ombi lake lilikubaliwa na kutakiwa atume kiasi hicho cha fedha.

 

Wakati biashara hiyo ikiwa kwenye mazungumzo, mtuhumiwa issa ambaye alikuwa akisikia mazungumzo hayo alimzuia mama yake kuwatumia polisi hao fedha yoyote akidai hajatenda kosa lolote, anasingiziwa tu.

 

Baada ya mtuhumiwa huyo kuzuia fedha kutumwa kwa polisi hao,  polisi hao wakiongozwa na Majuto, na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Paul walidaiwa kumpiga sana, hasa maeneo ya kichwa kwa kutumia nyaya ngumu wakidai ni jeuri anazuia wao wasitumiwe fedha ili aachiwe.

 

Mashuhuda walidai baadaye tena, akiwa tayari amepokea kipigo cha kutosha kutoka kwa polisi hao, alitakiwa kumpigia simu ndugu yake mwingine mwenye uwezo kifedha ili atume fedha hiyo aweze kuachiwa. 

 

Alipigiwa simu binamu wa mtuhumiwa huyo aitwaye Tusekile Shadrack, ambaye alielezwa tukio hilo, na kutakiwa na afande Majuto, wa jeshi la polisi Goba atume fedha sh 800, 000 ili ndugu yake aweze kuachiwa na kufutiwa kesi inayo mkabili. 

 

Ndugu huyo wa mtuhumiwa ilidaiwa alimuomba polisi Majuto ampe namba yake ya simu amtumie fedha hiyo, aligoma kutoa namba yake, akamtaka atume kwenye simu ya mtuhumiwa au apewe namba ya wakala atoe kupitia huko, ilishindikana, fedha haikutumwa, mtuhumiwa kwa mara nyingine alimzuia asitume chochote sababu yeye anasingiziwa tu, hajatenda kosa hilo.


Alhamisi, November 11, 2021, asubuhi, Afande Majuto ilidaiwa alimpigia simu Mama wa mtuhumiwa akimtaka afike Hospitali ya Mwananyamala haraka, hali ya mwanaye ni mbaya.

 

Mama huyo wa mtuhumiwa aliongozana na Tusekile binamu wa Issa kwenda Mwananyamala Hospitali, walipofika kweli walimkuta mtoto wao taabani lakini, aliweza kuongea kwa shida sana na kuwasimulia mkasa mzima uliomkuta.

 

"Nimepigwa sana, sidhani kama nitapona, niombeeni sana kwa Mungu, nimeumizwa, nakufa bila hatia yoyote, polisi wakiongozwa na Majuto,  wamenitesa na wamenipiga kipigo kikali  wananiua eti kwa sababu nimewakosesha fedha za dhuruma walizotaka kuzipokea kutoka kwenu ndugu zangu, niombeeni, nami naomba, Mungu atanilipia" alisema Issa ambaye alikuwa akiongea kwa tabu akiwa wodini katika hospitali ya Mwananyamala.

 

"Cha ajabu, yule mwizi waliyedai ameniuzia TV ya wizi aliachiwa, hakufika hata kituo cha polisi, aliambiwa tukiwa njiani tuna karibia kituo cha Goba atambae, nakufa, nifikishieni salaam zangu kwa IGP Sirro, askari wake wanawatesa raia, wanawaua kwa kuwapiga wakitaka walipwe pesa kwa makosa ya kutengenezewa ili wapate fedha ya dhuluma, nakuacha mama, niombee kwa Mungu" aliongea Issa kwa majonzi makubwa huku akiwa hoi hospitalini hapo.

 

Katika hospitali ya Mwananyamala alifanyiwa kipimo cha cit-scan na MRI kichwani, wakadai mishipa ya mfumo wa fahamu kichwani imeathiriwa pakubwa, damu nyingi imevia, imeganda na kuikandamiza mishipa hiyo kwenye Ubongo.

 

Kutokana na hali yake kuendelea kuwa mbaya na kuanza kushindwa kuongea ilibidi haraka sana ahamishiwe MOI, ambapo alipokelewa na yuko ICU.


Kwa mujibu wa binamu wa Issa, Tusekile, maelezo ya madaktari bingwa wa MOI wa mifumo ya fahamu ya kichwa(Neurosurgery) wanaomhudumia, wamesema kupona kwake ni asilimia moja, muujiza tu wa Mungu ndio unasubiriwa.!


"Ndugu tumekata tamaa, hivyo tunaomba msaada wa kisheria na ushauri,"alisema Tusekile.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai alipoulizwa kuhusiana na tukio hili alidai kulisikia na kwamba ofisi yake inaendelea kufuatilia ili kujua ukweli wake na itatoa taarifa rasmi baada ya kubaini ukweli wake.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Novemba16, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro amesema askari wake wanachunguza tukio hilo na watakaobainika watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.


"Tumepokea malalamiko kutoka kwa wazazi wa mtuhumiwa mmoja anayejulikana kwa jina la Issa aliyekuwa akituhumiwa kwa wizi wa TV ambaye anadaiwa kupigwa na askari wetu wa kituo cha Goba, tunafanya uchunguzi kuhusu tukio zima, na vitendo vya rushwa, tukibaini ukweli hatua kali zitachukuliwa dhidi ya askari wetu,"amesema Kamanda Muliro.

BARAZA LA WAZEE KUKAMILIKA IFIKAPO 2022

 
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali inajiandaa kukamilisha uanzishaji wa baraza la wazee la Taifa ifikapo Mwaka 2022 kwa lengo la kuwawezesha wazee  kujadili changamoto zinazowakabiri.

Amebainisha hayo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Kutetea na kulinda haki za wazee nchini Tanzania Helpage, Smart Daniel wakati wakijadili mikakati ya uboreshaji wa huduma za wazee hapa nchini.

Aidha Dkt Gwajima Ametoa wito kwa shirika la Helpage International kuwaandaa vijana kufanya kazi kwa ajili ya kujiwekea akiba ya baadaye ili watakapo zeeka wasitegemee misaada ya serikali na taasisi za kimataifa na madara yake wawe na uwezo wa kujimudu kimaisha.

Amesema kuwa wazee wakiandaliwa vizuri watakuwa msaada mkubwa kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla kuwa watakuwa wameimika vizuri katika masuala ya Elimu,kiuchumi na usitawi wa jamii ili wasiende kulelewa kwenye kambi za wazee 

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Afya inayohusisha wazee hapa nchini, mkurugenzi wa shirika la kinataifa la kutetea na kulinda haki za wazee Tanzania Helpage,Smart Daniel ameiomba serikali kuandaa sheria ya wazee ili wapate huduma bora na kupewa nafasi zinazostahili ikiwemo ishirikishwaji katika vyombo vya maamzi.

amesema Helpage Intenational limeanzisha programu maalumu ya uelimishaji jamii ikiwemo wazee wajitokeze kwa wingi katika zoezi linaloendelea hapa nchini la chanjo ya uviko 19 kwa lengo la kulinda Afya zao,ambapo mikoa ya kigoma,Mwanza,Simiyu,Njombe na Ruvuma tayari wamepatiwa elimu na kwamba baadhi ya wazee wamewezeshwa kupatiwa miradi mbalimbali ya maendeleo ili waweze kujikimu kimaisha.

Aidha Daniel ameiomba serikali kuhudhiria katika mikutano ya kimataifa inayolenga kutetea haki za wazee kwa lengo la kupata uzoefu jinsi mataifa mengine yanavyoweza kuwahudumia wazee na kuwapatia sitahimi zao.

WATOTO 892 WAFANYIWA UKATILI ILEJE.

 

WATOTO 892 wafanyiwa ukatili kwa muda wa mwaka  mmoja katika wilaya ya Ileje mkoani Songwe na kupelekea kuhatarisha maisha yao ikiwa ni pamoja na kukosa haki yao ya kupata elimu.

Hayo yamethibitishwa na Afisa Ustawi wa jamii wa wilaya hiyo Methew Meisha alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili, kwa kudai kuwa Wilaya ya Ileje matukio ya unyanyasaji yamekuwa yakiongezeka kila mwaka na kuhatarisha ujenzi wa jamii bora kwa baadae.

Meisha aliyabainisha matukio yaliyokithiri kwa Ileje kuwa ni pamoja na ukitili wa Kingono, ukatili wa kimwili (kuchomwa na na kupigwa), ukatili wa kihisia na ukatili wa kutelekezwa watoto wadogo chini ya miaka mitano (5).

Alisema katika kipindi cha mwaka 2019 na 2020 jumla ya watoto 892 katika wilaya hiyo wamefanyiwa ukatili, huku akitanabaisha kuwa ukatili wa kingono ndio uliokithiri zaidi kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliofanyiwa ukatili.

Alitaja takwimu hizo kuwa jumla ya watoto 50 walifanyiwa ukatili wa kimwili kwa mawaka 2019 wakike wakiwa 28 na wakiume 22, watoto 122 walifanyiwa ukatili wa Kingono (kubakwa na kulawitiwa wakike wakiwa 89 na wakiume 33 na ukatili wa kihisia (madhara kiakili) watoto 196 wakike 121 wakiume 77.

Ukatili wa kutelekezwa (bila msaada ,mahitaji) watoto chini ya miaka mitano wataoto 77 walitelekezwa wakike 46 na wakiume 31.

“kwa  msimu wa 2020 takwimu ziliongezeka ambapo watoto 151 walifanyiwa ukatili wa kimwili kupigwa na kuchomwa , wakike 120 na wakiume 31, uktili wa kingono na ulawiti watoto 127, wakike 124 na watoto watatu wa kiume walilawitiwa.

Ukatili wa kihisia (madhara kiakili) watoto 532 walifanyiwa ,wakike 401 na kiume 131, kwa uopande wa ukatili wa kutelekezwa (bila msaada na mahitaji watoto chini ya miaka mitano watoto 82 wametelekezwa wakike 29  na kiume 53”Alieleza Meisha.

Alisema pamoja naelimu ambayo wamekuwa wakiendelea kuitoa kwa wananchi vitendo hivyo vuimekuwa vikiongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mikesha ya dini inayohusisha watoto wadogo ambapo baadhi ya wanaume hutumia mikesha kuwalaghai na kuwabaka watoto wa kike.

 Mkuu wa Wilaya ya Ileje Anna Gidarya amepiga marufuku mikesha ya dini hivi karibuni kwa watoto wadogo ili kuwalinda watoto dhidi yaunyanyasaji na ukatili uliokithiri wilayani humo kwa upande wa watoto wa kike.

Alitoa agizo hilo wakati wa Ziara yake ya kupokea kero za Wananchi katika vijiji vya  Ishinga  kata ya Ndola na Sapanda kata ya Ngulilo

 Alisema mikesha mingi ya makanisa inayofanyika katika Wilaya hiyo imekuwa miongoni mwa chanzo Cha watoto wa kike kufanyiwa vitendo vya ukatili usiku hasa ubakaji na kupelekea ongezeko la mimba za utotoni.

Gidarya alisema kuwavitendo vya ukatili kwa watoto vinaongezeka wilayani humo huku mikesha ya makanisa inayohusisha watoto ikishamiri siku hadi siku hali inayopelekea baadhi yao kutumia nafasi hiyo kushawishiwa kushiriki vitendo viovu.

"Baadhi ya watu wenye nia ovu wamekuwa wakitumia mwanya huo wa mikesha kuwalaghai na kuwabaka watoto na kuwasababishia mimba za utotoni na kuharibu kabisa ndoto za maisha kwa watoto wa kike,

Tunataarifa  zakutosha kuhusu watoto kufanyiwa ukatili na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa makanisa, naombeni kila mtu achukue jukumu la kumlinda mtoto wa kike , vitendo hivi havivumiliki kabisa" alihimiza Gidarya

Gidarya amewaagiza viongozi wa vijiji vyote na kata zote kuhakikisha, wanawachukulia hatua na kutoa taarifa za wazazi na walezi watakao kiuka na kuruhusu watoto wao kuhudhuria mikesha hiyo ya usiku.

NGOMA ZA USIKU ZAPIGWA MARUFUKU TANDAHIMBA.

 


Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala amepiga marufuku ngoma za usiku zinazochezwa katika wilaya hiyo akisema zimekuwa chanzo cha watoto wa kike kupata mimba na kushindwa kutimiza ndoto zao.

Akizungumza na wananchi alipotembelea Kata ya Mihambwe amesema kuwa wakati wa kuchezwa ngoma hizo watoto wengi wa kike wamekuwa wakipata ujauzito wakiwa na umri mdogo.

Amesema kuwa hali hiyo imemsukuma kupiga marufuku ili kuwasaidia watoto wakike waweze kusoma na kutimiza malengo yao bila kuwa na vizuizi vya ujauzito.

“Wakati wa kuchezwachezwa hizi ngoma mimba ndio zinakuwa nyingi kwa watoto shuleni mbali na wanaopata ujauzito shuleni hii inamdidimiza mtoto wa kike anashindwa kusoma anashindwa kufikia malengo yake na kukatisha ndoto zake”

“Kwa jambo hili hatutafumbia macho mimi sizuii mila na desturi kufanyika hapana na sijaja hapa kuzuia lakini twendeni na utaratibu sisi ni mashahidi mimba nyingi zinapatikana usiku” amesema Kanali Sawala na kuongeza

“Ndio maana nimeamua kuwa ngoma za usiku nimezuia kwa sasa msihangaike kuomba vibali mila zingine ziendelee kufanyika lakini sio ngoma za usiku”

AJALI BASI LA SAULI LAUWA BODABODA.

 


Mtu mmoja amefariki papo hapo na mwingine kujeruhiwa baada ya pikipiki waliyokua wakisafiria kugongwa na basi la kampuni ya Sauli.

Ajali hiyo imetokea usiku huu eneo la Kwa Mathias wilayani Kibaha, Pwani wakati basi lenye namba za usajili T668 DTF mali ya kampuni ya SAULI likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam kugonga bodaboda.

Mmoja wa mashuhuda Athuman Ramadhani amedai kuwa basi hilo ambalo lilikuwa limeongozana na magari mengine na ilipofika eneo pacha la barabara jirani na kituo cha daladala Kwa Mathias lilianza kuyapita magari mengine ambapo moja wapo iliyokua mbele ilihamia njia ya pembeni inayotumiwa na magari yanayoshusha abiria.

Wakati gari hilo iliposimama kushusha abiria, ndipo bodaboda yenye namba MC 606 CAQ ikiwa na abiria mwanamke ikakatisha mbele yake huku SAULI iliyokua imeshaanza kuyapita magari mengine ikiwa mwendo kasi na ndipo ilipokutana na pikipiki na kuigongwa ambapo, iliiburuza na kuingia uvunguni mwa basi hilo.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Pwani, Edson Mwakihaba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja abiria wa bodaboda aliyefariki kuwa ni Emma Mgole (37) mkazi wa Kwa Mathias huku dereva wa bodaboda hiyo Edwin Rodrick akijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Tumbi kwa matibabu ya haraka.

Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa Rodrick amehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzira, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Dereva wa basi la Sauli, Tito Gadau (32) anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.

Hata hivyo, baadhi ya vijana waliokua jirani na eneo hilo wamelishambulia basi hilo kwa mawe na kusababisha uharibifu mkubwa.

Monday, November 15, 2021

TUNAENDELEA KUJENGA NAFASI ZA AJIRA - RAIS SAMIA.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewatakia kheri wanafunzi wote wanaoanza mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne hii leo.

Kupitia ujumbe wake aliouandika hii leo Novemba 15, 2021, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia amesema serikali inaendelea kujenga nafasi zaidi kwenye nyanja mbalimbali yakiwemo mazingira bora ya ajira.

"Nawatakia kila la kheri wanafunzi wote wa kidato cha nne wanaoanza mitihani yao leo, tunaendelea kujenga nafasi zaidi kwao kusonga mbele kielimu, kiujuzi na kiajira, kwa kuongeza nafasi za kidato cha tano na sita, vyuo vya ufundi stadi na mazingira bora ya nafasi zaidi za ajira," ameandika Rais Samia.

FW DE KLERK WA AFRIKA KUSINI KUCHOMWA KATIKA MAZISHI YA FARAGHA.

 


Rais wa mwisho mzungu wa Afrika Kusini FW de Klerk, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 85 wiki iliyopita, atazikwa katika sherehe ya faragha siku ya Jumapili, kulingana na wakfu wake.

“Wakfu wa FW de Klerk unawatangazia kuwa kuchomwa kwa FW de Klerk’ na mazishi yake itafanyika Jumapili Novemba,21,” ilisema taarifa.

“Itakua shere ya faragha kwa familia na haitakua wazi kwa vyombo vya habari,” Wakfu huo uliongeza. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa.

De Klerk aliingia madarakani mwaka 1989 chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi, mfumo ambao ulihalalisha ubaguzi wa rangi, lakini baadaye akawa mtu muhimu katika kipindi cha mpito kuelekea demokrasia.

Mwaka 1993, alipata Tuzo ya Amani ya Nobel na rais wa zamani Nelson Mandela kwa kusaidia kujadili kukomesha ubaguzi wa rangi.

Kumekua na hisia mseto kuhusu utawala wake nchini Afrika Kusini.

Alifariki Alhamisi baada ya kupatikana na saratani mapema mwaka huu.

DKT GWAJIMA AMESEMA SERIKALI IMEJIPANGA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA IDARA YA RADIOLOJIA.

 Waziri wa Afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt Dorothy Gwajima amewataka watendaji kufanya kazi kwa bidhii kwa lengo la kuisaidia jamii iepuke kusafiri.kwenda  je ya nchi kufuata huduma wakati serikali imeboresha huduma za afya kwa kusambaza vifaa tiba.


Amebainisha hayo jijini Mwanza katika Kongamano na mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wataalamu wa mionzi na Tiba uliohusisha Radiolojia kutoka nchi wanachama wa Afrika mashariki Tanzania,Kenya,Uganda na Burundi.

Aidha amewakata kufanya kazi kwa ishindani katika utoaji wa huduma kwa jamii ili kukabiliana soko katika nchi wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki ambao wanatumia wataalamu wenye viwango vya kimataifa ili kuwezesha wananchi wanapata huduma inayo stahili hawa serikali itakapoanza kutoa huduma ya Bima ya afya kwa wote.