ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 18, 2021

WAFUNGWA WA 3 WALIOTOROKA JELA YA KAMITI KENYA WAKAMATWA.

 


Wafungwa 3 wanaohusishwa na ugaidi ambao walitoroka jela ya kamiti nchini Kenya siku ya Jumatatu wamekamatwa.

Watatu hao Musharaf Abdalla maarufu Alex Shikanda , Joseph Ouma na Mohammed Ali Abikar walikamatwa katika eneo la Kitui.

Kwa sasa washukiwa hao wanasafirishwa kurudi jijini Nairobi.

Walitoroka kutoka jela inayolindwa zaidi baada kutoboa ukuta wa jela hiyo.

Baadaye walitumia nguo aina ya blanketi na waya kutengeneza kamba ambazo walitumia kupanda kuta mbili ndefu za jela hiyo.

Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya maafisa wa jela ya Kamiti kukamatwa kwa madai ya kuwasaidia wahalifu hao kutoroka

Siku ya Jumatano, Rais Kenyatta alimwaagiza waziri wa masuala ya ndani Fred Matiangi kuhakikisha wanatumia kila mbinu kuwakamata wahalifi hao hatari.

Alivitaka vitengo vyote vya upelelezi kuwawajibisha maafisa wote waliodaiwa kuhusika na kutoroka kwao.

Kulingana na gazeti la Daily Nation, awali , vitengo vya usalama katika kaunti ya Kitui vilikuwa vimewekwa katika hali ya tahadhari baada ya wakaazi wa eneo hilo kuwaona wafungwa hao watoro.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kitui Leah Kithei mapema Alhamisi alithibitisha kwamba vitengo vyote vya usalama katika eneo hilo, wakiwemo machifu na manaibu wao walikuwa wamewekwa katika hali ya tahadhari.

''Habari hiyo pia imesambazwa kwa wenzetu katika kaunti jirani ya Tanariver na Garissa'', bi Kithei aliambia Daily Nation.

''Iwapo ni kweli ni wao, bila shaka tutawakamata, ni muda tu kabla ya hilo kufanyika''.

Wakazi waliowaona wanasemaje?

Wakaazi wa eneo hilo waliripoti kuwaona watatu hao , ambao wanawashuku kuwa wahalifu wanaosakwa baada ya kutoroka jela siku ya Jumapili, katika kituo cha maduka cha Malalani katika kaunti hiyo kubwa.

Walisema kwamba watatu hao , walioonekana kuchoka na wenye kiu, walinunua maziwa mengi , na maji , mkate na biskuti kutoka kwa maduka ya eneo hilo na kuplipa pesa.

Kwa mujibu wa gazeti hilo wakaazi walianza kuwashuku baada ya kutaka kuoneshwa njia ya kuelekea msitu wa Boni huko kaunti ya Lamu.

''Mmoja ya watoro hao alikuwa na kidonda katika mguu wake na alikuwa akichechemea pengine kwasababu ya kutembea mwendo mrefu. Walionekana kukanganyika na waliopotea, wasio na uelewa wowote wa eneo hilo''.

''Walikuwa wanauliza jinsi wangeweza kuelekea Garissa au Tanariver kutoka eneo hilo'', alisema mfanyabiashara katika soko hilo ambaye alizungumza na Nation kwa makubaliano kwamba hatotajwa kutokana na sababu za kiusalama.

Mfanyabiashara huyo aliwaelezea watatu hao kama mtu mmoja mwembamba mwenye asili ya kisomali na wanaume wawili Waafrika , maelezo ambayo ni sawa na watoro hao.

''Hawakuwa wamebeba mzigo lakini mmoja wao alikuwa amebeba begi dogo na kile kilichoonekana kama nguo''.

Soko la Malalani lipo kilomita 100 mashariki mwa mji wa Kitui na karibu na mpaka na kaunti ya Tanariver.

Linapakana na Mbuga ya wanyama ya Kusini mwa Kitui ambayo imekuwa maficho kwa washukiwa wa ugaidi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.