ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, February 17, 2026

KILI TRUST YAANDAA WARSHA KUWAJENGEA UWEZO WANUFAIKA WAKE ILI KUIMARISHA UWAJIBIKAJI NA UHAKIKI WA KINA

Kwa uongozi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omar Sukari (aliesimama pichani), wadau (ikiwemo GGML, TACAIDS, LGAs, na washirika wengine)  wanaratibu mbinu zitakazokuwa za kijamii, endelevu na zenye matokeo yanayopimika.


Mwanza, Tanzania

Geita Gold Mining Limited kupitia mpango wake wa Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS Trust (Kili Trust) imeandaa warsha ya kuwajengea uwezo wanufaika wake, inayofanyika jijini Mwanza kuanzia Februari 16–20, 2026. Warsha hiyo inawakutanisha wanufaika, wadau wa utekelezaji, washirika na wadhamini kwa lengo la kuimarisha utawala bora, uwajibikaji wa kifedha na kuongeza matokeo chanya ya programu.



Warsha hii ni hatua muhimu ya kiutawala kabla ya utoaji wa fedha kupitia Kili Grants Portfolio ya mwaka 2024/2025, inayolenga kusaidia miradi ya uwezeshaji wa kiuchumi, uimarishaji wa afya za jamii na mipango endelevu. Kupitia mpa…


Majadiliano ya kimkakati yakiendelea ili kubuni afua mahsusi zitakazowafikia wachimbaji wadogo katika Mkoa wa Geita, kundi lenye changamoto na hatari za kipekee katika mapambano dhidi ya VVU.

MSIBA WA ASKARI WA USALAMA BARABARANI WAACHA SIMANZI MWANZA

 

Na, Ernest Magashi

Jijini Mwanza kumeghubikwa na simanzi kufuatia kifo cha askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo wa Polisi (CPL) Tumsifu Wilson Kileo (F7768), ambaye mwili wake umeagwa na mamia ya waombolezaji kabla ya kusafirishwa kwenda Lyamungo mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.Marehemu alifariki dunia baada ya kugongwa na daladala iliyopoteza mwelekeo wakati akiwa kazini akiongoza magari na kusimamia usalama barabarani. Ajali hiyo ilitokea Februari 10, 2026 majira ya saa 2:00 asubuhi katika mzunguko wa Mwanza Hotel katikati ya Jiji la Mwanza.Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Buhongwa, Lucas Baskely, aliyeongoza ibada ya kuuaga mwili wa marehemu, aliwataka madereva kuacha uzembe barabarani na kutotumia vyombo vya moto kama silaha ya kuhatarisha maisha ya wengine. Alisisitiza kuwa hakuna safari iliyo na thamani kuliko uhai wa binadamu.Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, akieleza kuwa CPL Tumsifu alikuwa askari mwenye nidhamu, weledi wakati wote kazini, ambaye Jeshi la Polisi bado lilikuwa linamuhitaji katika kulinda usalama wa raia na mali zao.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Februari 16, 2026 aliongoza mamia ya maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali pamoja na wananchi katika kuuaga mwili wa marehemu. CPL Tumsifu alifariki dunia Februari 13, 2026 katika hospitali ya Rufaa Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu.Akizungumza na waombolezaji, Mkuu huyo wa Mkoa aliwahimiza askari na wananchi kuenzi maisha ya marehemu kwa kuendeleza mema aliyoyaacha katika kulitumikia Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla.

DC AWATAKA MADIWANI KUHAMASISHA WAZAZI KUPELEKA WATOTO SHULENI KABLA YA KUANZA MUSAKO

 

Na, Ernest Magashi

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kuhamasisha wazazi na walezi kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kuanza shule wanaripoti kwa wakati, kabla ya kuanza kwa msako wa kuwachukulia hatua wazazi watakaokaidi agizo hilo.Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskas Mragili, wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani. Amesema amepokea taarifa kuwa kasi ya uandikishaji na uripoti wa wanafunzi, hususan wa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza, bado hairidhishi.Ameeleza kuwa idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti shuleni iko chini ya asilimia 80 ukilinganisha na idadi ya waliofaulu darasa la saba mwaka jana.“Waheshimiwa madiwani, nawaombeni sana muhamasishe wazazi na walezi wapeleke watoto shule. Tumeanza mwaka vizuri tangu shule zilipofunguliwa Januari 2026, lakini mwitikio wa darasa la awali, la kwanza na kidato cha kwanza bado ni mdogo. Kuanzia wiki ijayo, kila mzazi au mlezi mwenye mtoto aliyeandikishwa na hajafika shule atachukuliwa hatua kupitia serikali za vijiji na kata,” alisisitiza Mragili.Aliongeza kuwa Serikali imeboresha miundombinu ya kujifunzia na inaendelea kutekeleza Sera ya Elimu Bila Malipo, hivyo jukumu la mzazi ni kuhakikisha mtoto anapata haki yake ya elimu. Alionya kuwa Serikali haitavumilia kuona watoto wanabaki nyumbani bila sababu za msingi, na wazazi watakaobainika watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.Mkuu huyo wa wilaya alisema licha ya Bukombe kufanya vizuri kitaaluma mkoani Geita, juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni ili kufikia lengo la Serikali la kutoa elimu bora kwa kila mtoto.Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, aliwapongeza wataalamu wa idara mbalimbali, hususan za elimu ya msingi na sekondari, kwa juhudi zao zilizoifanya wilaya hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika matokeo ya mitihani.

Dkt. Biteko aliwahimiza madiwani na wataalamu kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha wazazi kusomesha watoto wao ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta ya elimu.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliahidi kuwa wataalamu wataendelea kushirikiana na madiwani kuhakikisha malengo ya elimu yanafikiwa.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri, Erick Kagoma, aliwataka madiwani kwenda kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto shule kabla ya kuanza rasmi kwa msako huo.