ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 4, 2021

RAIA WA KENYA AHUKUMIWA MIAKA 27 JELA

 


Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, imemhukumu raia wa Kenya, Samwel Murwa (25) kutumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kosa la kupatikana na mafurushi saba ya kilo 259 za Mirungi.


Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Jaji Imaculeti Banzi baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi watano na vielelezo saba vya upande wa mashitaka, ambao alisema ulikuwa ni ushahidi mzito na haukuacha mashaka yoyote.


Awali mawakili wa upande wa mashitaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Sabitina Mcharo na Grace Kabu waliieleza mahakama mshitakiwa alikamatwa na mirungi hiyo Agosti 19,2018 katika kijiji cha Mnoa wilaya ya Mwanga.


Siku hiyo ya tukio, mshitakiwa alikamatwa porini akiwa amekalia mfuko wa Sandarusi ukiwa na mirungi na pembeni yake kulikuwa na mifuko mingine sita yote ikiwa imesheni mirungi ambayo huingizwa nchi kutoka  Kenya.


Katika utetezi wake ambao mahakama iliukataa, raia huyo wa Kenya alijitetea kuwa siku hiyo alikamatwa na polisi kwa kuingia nchini bila kibali lakini alivyofikishwa katika gari ya polisi ndio akakuta magunia hayo saba ya Mirungi.


Akisoma hukumu yake, Jaji Banzi alisema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka ulijitosheleza na haukuacha mashaka na kwamba utetezi wake hauna mashiko kwani hakuwadodosa mashahidi juu ya hicho alichojitetea nacho.


Hukumu hiyo ni mfululizo wa hukumu za vifungo dhidi ya wanaojihusisha na biashara ya Mirungi ambapo wiki hii pia mzee wa miaka 71, Patrick Malya alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na kilo 83 za Mirungi.


Adhabu hizo imetolewa wakati mkoa wa Kilimanjaro hasa wilaya za Rombo, Moshi, Hai, na Mwanga zikitikiswa kwa biashara ya mirungi inayoingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya, kupitia njia za panya zilizopo mpakani katika wilaya hizo.

SAMIA MGENI RASMI MKUTANO VYAMA VYA SIASA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa vyama vya siasa pamoja na wadau mbalimbali wa siasa.


Mkutano huo ambao awali ulitakiwa kufanyika Oktoba 21, mwaka huu lakini ukahairishwa, imeelezwa kuwa utafanyika Desemba 16 na 17, mwaka huu jijini Dodoma.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Desemba 4, 2021 Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa, Juma Ally Khatib amesema mkutano huo utatanguliwa na semina kwa wajumbe wa baraza la vyama vya siasa kuhusu historia na majukumu ya baraza hilo, ambayo itafanyika Desemba 15.


Khatib amebainisha kuwa mkutano huo utakuwa na mada tatu zinazohusu masuala ya kisheria, demokrasia, siasa, uchumi na maadili ya kitaifa, yanayohusiana na demokrasia ya vyama vingi vya siasa.


"Baraza la vyama vya Siasa linatumia fursa hii, kushauri vyama vya siasa vyote vyenye usajili kamili, kuhudhuria mkutano huo, kwani ni fursa adhimu ya kubadiishana mawazo kuhusu mambo yanayotuhusu. Siasa ni ushawishi na ushawishi hufanikiwa kapitia njia ya mijadiliano," amesema Khatib. 


Naye mwanasiasa Mkongwe na Mjumbe wa baraza la vyama vya siasa, John Cheyo ametoa wito kwa watanzania pamoja na serikali kuendelea kudumisha Uhuru na umoja. 


"Nawaomba vijana na Watanzania tuipende nchi yetu na tumlaani mtu yoyote anayedhihaki nchi. Pia naiomba serikali iendelee kudumisha uhuru na umoja katika Taifa letu kupitia baraza la vyama vya siasa... wale wanasiasa wanaohamasisha vitu vya ajabu huwezi kupata kwa njia hiyo unayoitaka, hata Mwalimu Nyerere aliipata nchi hii kwa njia ya mazungumzo," amesema Cheyo. 


Mwenyekiti wa kamati ya maadili na mahusiano wa baraza hilo, Doyo Hassan Doyo amesema baraza hilo liko kisheria hivyo linauwezo wa kutatua na kuondoa matatizo ambayo yanavikabili vyama vya siasa.


"Kwahiyo nitoe wito mwanasiasa yeyote atakayekiuka taratibu na sheria, tutamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na kanuni ambazo tumejiwekea. Hivyo tunatoa wito viongozi wasiwe maneno  ya maudhi kwa wengine, viongozi wa nchi pamoja na usalama wa Taifa," amesema Doyo.

Friday, December 3, 2021

WAZIRI DKT GWAJIMA AZINDUA MPANGO MKAKATI WA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA UVIKO-19 KWA MKOA WA DAR ES SALAAM.


Na WAMJW - DSM


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Mpango Mkakati wa kudhibiti maambuzi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa Mkoa wa Dar es Salaam wenye lengo la kuthibiti kuenea kwa wimbi la nne la maambukizi hayo.


 Dkt Gwajima amezindua Mpango huo leo Jiji Dar Es Salaam wakati wa Mkutano wa wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Sekta ya Afya.


Dkt Gwajima amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika Sekta ya Afya kwa kuhakikisha huduma za Afya zinaboreshwa kwa kujenga miundombinu mbalimbali na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za Afya.



Ameongeza kuwa bado kuna changamoto katika kuhakikisha huduma za Afya zinatolewa katika ubora zikiwemo uhaba wa watumishi, vifaa tiba na miundombinu katika ujenzi na ukarabati ili kuimarisha utoaji wa huduma za Afya kwa Mkoa wa Dar Es Salaam na Tanzania nzima.


Aidha,Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Mkutano huo uliowakutanisha wadau hao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa Sekta ya Afya utasaidia kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za Afya na yatatoa majibu na muelekeo katika kuhakikisha huduma bora za Afya zinapatikana.



Akielezea kuhusu wimbi la nne la maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 amesema Wadau hao wasaidia katika kutoa elimu kawa wananchi katika kuhakikisha wanazingatia ushauri wa wataalam wa afya katika kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa huo.


 "Wadau mliopo hapa mtaona sehemu gani muhimu ya kusaidia hasa katika elimu kwa Umma ili wananchi waweze kujikinga na maambukizi hayo ambapo njia mbalimbali zinashauriwavkatika kujikinga na ugonjwa huu" alisema  Dkt Gwajima.



Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid  Mfaume ameeleza kuwa Mkoa umejipanga katika kuhakikisha unapambana na maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa wimbi la nne na hasa kuhakikisha utoaji wa huduma za Afya katika vituo vya Afya vilivyopo mkoani humo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Grace Mbwilo amesema Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali itaendelea kushirikiana na wadau hao kwa kusajili na kuratibu Mashirika hayo katika kuhakikisha yanasaidia na Serikali kutoa huduma kwa wananchi.



Mkoa wa Dar Es Salaam umekutanisha wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa Sekta ya Afya kujadili na kuona namna ya kuboresha utoaji wa huduma za Afya mkoani hapo

DECEMBER TUNAKIWASHA SERENGETI.

 


Kampuni yetu ya AFRICAN PRINTEMPTS CULTURAL AND TRAVELS LIMITED ya jijini Mwanza 


18 December Tunakiwasha ni FUNGA MWAKA NA BATA LA SERENGETI huku ikiwa special kabisa kwa uzinduzi rasmi wa kampuni yetu ya @apc_travels 


Kutakuwa na mambo mazuri mengi ya tofauti na tour ambazo ushawahi kuzifanya au ulizisikia zikifanyika kwani hii ni UTALII NA BATA yani unatalii huku unakula bata 2 days 1 night. 


Bei zetu zipo hapo juu kwenye posta☝️ 


Kifupi tutakuwa na Tata bus na Cruiser na bei zake zitakuwa tofauti. 


Tata bus kwa Mtanzania au Eafrica utalipa 150k tu 


Cruiser kwa Mtanzania au Eafrica utalipa 255k tu hizo bei ni pamoja na malazi, malipo ya getting, kulala, usafiri n.k 


Kwa wale international maelezo yanajieleza kwenye posta au cheki nasi kwa namba za cm zilizopo hapo juu☝️ 


TWENZETU SERENGETI TUKATREND ILE KI #WORLDWIDE #ACHATUTREND

SERIKALI HAITOSITA KUFUTA LESENI VITUO BINAFSI VITAKAVYOTUMIA WATUMISHI WAKE MUDA WA KAZI.



Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali haitasita kuwafutia leseni wamiliki wa Vituo Binafsi vya Afya Nchini watakaobainika kuwashawishi watumishi waliopo kwenye taasisi za umma muda wa kazi kwenda kufanya kazi kwenye vituo vyao kinyume na sheria na taratibu za nchi hali inayosababisha kuzorota kwa huduma kwenye taasisi za serikali.


Rai hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam leo 03. Desemba 2021 katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Binafsi vya Afya Nchini ukihusisha watoa huduma za afya kutoka mataifa mbalimbali. Amesema Wafanyakazi waliopo katika Taasisi za umma kwenda kufanyakazi katika Sekta Binafsi muda wa kazi lazima ifanyike kwa utaratibu mzuri usiathiri huduma za upande mwingine kwani kufanya hivyo sio tu kuwa ni kosa kisheria bali ni kitendo kisicho na utu kwani tunawanyima haki wateja wengine waliofika kupata huduma.


Dkt Gwajima amesema kuwa inakadiriwa  36% ya gharama za uendeshaji inapotea kutokana na kukosa ufanisi katika mifumo ya kiutendaji.

Habari njema ni kwamba ikiwa tutafanya kazi kwa ufanisi na kuokoa 36% ambayo tunapoteza, tunaweza kupunguza gharama ya huduma ya afya kwa 36% ambayo inapotea na hivyo kutoa huduma kwa watu wetu kwa kiwango kikubwa na gharama za huduma kuwa nafuu zaidi ili kuwapunguzia gharama wananchi.


Nitoe Rai kwa watoa huduma binafsi kuwekeza katika teknolojia bunifu zitakazotusidia kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa kupunguza gharama za utoaji huduma za Afya kwa wananchi ili wafurahie matunda ya Taifa lao amesema Dkt.Gwajima


Aidha Dkt Gwajima amesisitiza APHFTA kuendelea kushirikiana na Serikali kuzuia ubadhirifu wa mali za unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu wa upande wa serikali na sekta binafsi kwa kununua au kuhamisha mali za umma na kuzipeleka kwenye Sekta Binafsi kinyume na utaratibu. Amesema kitendo hiki ni sawa na uhujumu uchumi na kinazorotesha juhudi za Serikali.

"Tanzania imefika mbali sana katika kukidhi mahitaji ya afya ya watu kwa kutambua ukweli kwamba sekta ya afya binafsi ina mengi ya kutoa, na kwamba kwa pamoja tunaweza kukabiliana vyema na mahitaji ya afya ya sasa na ya baadaye ya Watanzania hivyo

 tunahitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika utoaji huduma zikiwemo chanjo mbalimbali na ya Uviko 19, huduma za matibabu ya VVU/UKIMWI na kifua kikuu, uzazi wa mpango na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza" Amesema Dkt Gwajima


Dkt Gwajima amesema kuwa Wizara ya Afya imefurahishwa na kazi ambayo APHFTA inafanya katika Kuzuia Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs) na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza ambacho kinahusishwa na programu za afya shuleni ni kielelezo kinachotia matumaini kuwa  APHFTA ni mshirika muhimu  katika mpango wa Kitaifa wa kuzuia na kudhibiti  magonjwa yasiyoambukiza, haswa kupitia programu yake ya shule, ambayo hivi karibuni itapanuliwa kitaifa.

RONALDO HAKAMATIKI, KAFUNGA MABAO 801

 


Mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Manchester United Cristiano Ronaldo ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha idadi ya mabao 800 kwenye michezo rasmi kwa ngazi ya klabu na timu ya taifa.


Ronaldo amefikia rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal, mchezo ambao Manchester United iliibuka na ushindi wa mabao 3-2. Mabao hayo mawili yamemfanya Ronaldo kufikisha mabao 801 na kuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo katika historia ya mchezo huu pendwa.


Mchezaji huyo bora wa Dunia mara 5 amefunga idadai hiyo ya mabao akiwa na vilabu vinne tofauti pamoja na timu ya taifa ya Ureno. Katika mabao hayo amefunga mabao 130 akiwa na Manchester United ya England, mabao 450 akiwa na Real Madrid ya Hispania, mabao 101 akiwa na Juventes ya Italia na ameifungia timu yake ya taifa ya Ureno mabao 115.


Ronaldo mwenye umri wa miaka 36 msimu huu wa 2021-22 unaoendelea kwenye mashindano yote amefunga mabao 12 katika michezo 16 na mabao 6 kati ya hayo ni ya Ligi Kuu England (EPL).

TWITTER YAONDOA KARIBU AKAUNTI 3,500 ZA PROPAGANDA ZINAZOUNGWA MKONO NA SERIKALI

Twitter inasema imeondoa akaunti 3,465 zinazofanya kazi kama "operesheni za habari zinazoungwa mkono na serikali" ambazo ilizihusisha na nchi sita: Uchina, Mexico, Urusi, Tanzania, Uganda na Venezuela.


Nchini Uganda, Twitter iliondoa mtandao wa akaunti 418 "zilizokuwa zikishiriki katika shughuli zisizo halali" za kumuunga mkono Rais Yoweri Museveni na chama chake, National Resistance Movement.


Takriban akaunti 270 pia zilifungwa nchini Tanzania baada ya kupatikana kuwasilisha ripoti za nia mbaya kwenye Twitter, zikiwalenga wanachama na wafuasi wa FichuaTanzania, kikundi cha kutetea haki za kiraia.

SERIKALI YAPOKEA DOZI 115,200 ZA JANSSEN.


Na WAMJW-DSM 


Tanzania imepokea shehena ya Chanjo aina ya Janssen Dozi 115,200 zitakazotumika kuchanja wananchi 115,200 kwa ufadhili wa Serikali ya Ubeligiji kupitia mpango wa COVAX Facility kwa lengo la kuwakinga wananchi dhidi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa virusi vya UVIKO-19. 


Akizingumza na waandishi wa habari katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya kupokea Chanjo kutoka kwa Balozi wa Ubeligiji nchini Tanzania Peter Van Acker Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika vituo mbalimbali vya Afya hapa nchini kwa mujibu wa miongozo iliyopo ili kuwezesha wananchi kujikinga dhidi ya UVIKO-19. 


Amesema kuwa, awamu ya kwanza Serikali ilipokea dozi 1,058,400, awamu ya pili dozi 169,000 na leo Desemba 3, 2021 hivyo kufanya jumla ya Chanjo aina ya Janssen zilizopokelewa hapa nchini kufikia Dozi 1,342,600 na kufanya jumla ya chanjo zote zilizopokelewa kuwa  dozi 4,421,540 zikiwemo chanjo ya Sinopharm na Pfizer ambazo zitachanja watu 2,882,545 . 


Aidha Dkt Gwajima amewaagiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano wa hali ya juu kuhamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo na  kisha kujikinga kwa kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko 19 ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono (Sanitizer), kufanya mazoezi na kuepuka misongamano isiyo yalazima. 

Thursday, December 2, 2021

MADUDU UCHAGUZI MKUU 2020.

 


Ripoti ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) imebainisha kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 haukuwa na mazingira sawa ya ushindani, jambo ambalo liliathiri ushiriki wa vyama vya upinzani.


Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana, imeandaliwa na Redet chini ya Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) baada ya kuangalia uchaguzi uliopita katika mikoa yote wakiwa na waangalizi 2,353.


Akizungumzia yaliyojiri kwenye uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Redet, Profesa Rwekaza Mukandala alibainisha mambo mbalimbali yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo, ikiwamo kukosekana kwa mazingira sawa ya ushindani.


“Vyama vya upinzani havikufanya vizuri katika uchaguzi uliopita na pia uwanja wa ushindani haukuwa linganifu, haukuwa sawa, kwa hiyo kwa kiasi fulani iliathiri ushindani na ushiriki wa vyama vya upinzani,” alisema Profesa Mukandala.


Profesa Mukandala alisema ushindani unategemea nyezo au rasilimali za kuwezesha kushindana, hivyo katika uchaguzi uliopita, vyama vya upinzani havikuwa na rasilimali za kutosha.


“Katika uchaguzi wa mwaka 2015, kulikuwa na mabango ya wagombea wa vyama vingine, Lowassa alikuwepo, Dk Magufuli pia…walikuwa wanakwenda sambamba lakini kwa uchaguzi wa mwaka jana kulikuwa hakuna mabango ya wagombea wa upinzani.


“Hii ni kwa sababu ya rasilimali ndiyo ilikuwa kikwazo, hawakuwa na uwezo wa fedha za kuweka hayo mabango ili yaonekane, kuwa na vipeperushi. Wagombea wengi hawakufanya mikutano ya kampeni, walikuwa wanasubiri siku za mwisho au wakati mgombea urais anapita,” alisema.


Mwenyekiti huyo wa Redet alisema huko zilichukuliwa hatua kadhaa za kuhakikisha kwamba vyama vinapata ruzuku ambayo inaviwezesha kuzitumia katika uchaguzi, lakini katika uchaguzi uliopita, hilo halikuzaa matunda.


Alisema watu wengi walijitokeza kujiandikisha kupiga kura lakini siku ya uchaguzi, watu wengi hawakwenda kupiga kura. Alisema sababu za watu kutokwenda kupiga kura zinatakiwa zifanyiwe tafiti zaidi kujua kilichosababisha.


Profesa Mukandala alibainisha kwamba katika hatua mbalimbali za kupiga kura, vitendo vya rushwa vilishamiri, hasa katika kupata wagombea ndani ya vyama, alishauri vyama vihakikishe kwamba mchakato wao wa kupata wagombea unakuwa huru na wa haki.


Kuhusu suala la wagombea kuenguliwa kwa kukosea kujaza fomu za uchaguzi, Profesa Mukandala alisema jambo hilo ni tata kwa sababu kwa mujibu wa Katiba, kigezo kikuu cha mtu kugombea nafasi yoyote ni awe raia wa Tanzania.


“Vitu vingine kwamba aliweka ‘a’ badala ya ‘e’ iwe ndiyo sababu ya kumuengua, kwa kweli hiyo inatia shaka na huko katika chaguzi zote zilizopita hayo yalikuwepo…huko mbele tunakokwenda, watu wasienguliwe kwa sababu tu kakosea tarehe, tufuate katiba inavyosema,” alisema.


Awali akifungua mkutano huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Utafiti, Profesa Bernadetha Kilian alisema vyuo vikuu ni wadau muhimu wa kufuatilia kinachoendelea katika jamii, hivyo walishiriki katika kuangalia uchaguzi huo kama ilivyo utamaduni wao.


Alisema chuo kiliiwezesha Redet kutekeleza majukumu yake ya msingi katika uchaguzi huo na kwamba majukumu yake hayakuishia hapo, bali kuwawezesha wanawake pia kushiriki kwenye demokrasia kwa kuwapatia mafunzo maalumu.


“Ripoti za Redet na Temco zinawapatia wanafunzi ujuzi na rejea za kusoma wakati wa masomo yao. Tunazishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ZEC kwa ushirikiano wao,” alisema Profesa Kilian.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo alisema ni muhimu kwa vyama vya siasa navyo kushirikishwa katika uandaaji wa ripoti hiyo ili vifahamu kilichokuwa kikiendelea majimboni na kupokea ushauri.


“Ningefurahi kuona kwamba hata sisi wadau wa siasa tunashirikishwa katika uandaaji wa ripoti hii na kupata ushauri wa moja kwa moja,” alisema Lyimo. Hata hivyo, Profesa Mukandala alimweleza kwamba hawawezi kuvishirikisha vyama vya siasa kwa sababu ripoti hiyo ni ya uangalizi wao.


Naye Mhadhiri wa Udsm, Dk Audax Kweyamba alisema ripoti imebainisha mambo ya msingi ambayo yanaonekana katika uchaguzi uliopita na jitihada zinahitajika kuhakikisha kwamba mapendekezo yaliyotolewa yanafanyiwa kazi ili uchaguzi ujao uwe bora zaidi.


Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa, Athuman Ismail alisema ripoti hiyo ya Redet itaongeza mjadala kwenye jamii na watu wanaweza kuzungumza kwa uwazi zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.


“Wengi wetu tunajua kuwa wapinzani walibanwa mbavu na mabavu yalitumika, hivyo leo hii huwezi kusema uchaguzi ulikuwa huru na haki,” alisema.


Itakumbukwa pia mgombea wa urais wa Chadema, Tundu Lissu alipinga matokeo yaliyompa ushindi hayati Magufuli, akidai yaligubikwa na udanganyifu.

JICHO LA WIZARA YA AFYA KUDHIBITI UKATILI DHIDI YA WATOTO.

 


Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ameiomba jamii kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wote wanaosaidia kupambana na ukatili dhidi ya watoto likiwemo Jeshi la Polisi,  Mahakama na Taasisi zinazojihusisha na uboreshaji wa huduma za  Madawati ya Jinsia kwa kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wadogo.


Amebainisha hayo leo Tarehe 02, Desemba 2021 katika ufunguzi wa Kituo cha Kulea Watoto cha pamoja cha huduma ya mkono kwa mkono kwa watoto waliofanyiwa ukatili kilichopo Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT, Jordan kilichopo Morogoro kitakacho hudumia wananchi wa kata 15 katika manispaa ya Morogoro. Lengo ni kumuwekea kinga mtoto dhidi ya ukatili na kumpa huduma zote pindi anapofanyiwa ukatili.

Dkt.Gwajima amesema kuwa jamii ikitambua umuhimu wa kulea watoto kutapunguza ukatili dhidi ya watoto. Kwa takwimu za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huduma dhidi ya ukatili kwa watoto imeendelea kutoa huduma katika vituo 17 vya mkono kwa mkono hapa nchini na katika kipindi cha Julai 2020 hadi juni 2021 kulikuwa na waathirika 1,857 wa kufanyiwa ukatili wa kijinsia na kati yao watoto 1,072 walihudumiwa" amesema Dkt.Gwajima

"Tatizo la ukatili linaathiri maendeleo ya Taifa kwa kuwa na watoto watakaojifunza ukatili hali inayo ongeza mzigo kwa jeshi la polisi ambalo linafanya kazi kubwa ya kuanzisha madawati ya kijinsia kwa lengo la kuelimisha jamii itambue umuhimu wa kuzingatia maadili na malezi bora kwa watoto ili kuandaa taifa la vijana wazalendo kwa manufaa ya Taifa.


Dkt Gwajima amevipongeza vvyombo vyote vya sheria vinavyoshughulikia masuala ya ukatili na ametoa rai kwa vyombo hivyo  vikiwemo polisi na mahakama kuongeza kasi ya kudhibiti kufanyia kazi mashauri ya ukatili ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kwa wakati kwa wale wote wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. 

Awali Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela akimkaribisha waziri wa Afya Dkt Gwajima amesema kuwa Mkoa wa morogoro unakabiliwa na changamoto ya uwepo wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo Jeshi la Polisi kwa Julai hadi Septemba 2021 limepokea taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima 200 kati yao wanaume wapo 41 na wanawake 159 huku taarifa za watoto 275 zikitajwa kati yao 64 ni wavulana na watoto 136 watoto wa kike hali inayoonyesha watoto wa kike na wakina mama kuwa kwenye mazingira magumu kiasi cha kuhitaji kuimarisha kamati ya ulinzi na usalama ziweze kuweka mikakati madhubuti ili kukabiliana na hali hiyo.

Mkuu wa Chuo Kishiriki cha Jordan Prof.Bertram Mapunda amesema kuwa chuo kimebaini morogoro ukatili upo kwa kiwango cha asilimia 60 ambapo kila watoto 10 sita hufanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ulawiti,Ubakaki,Vipigo,Kuunguzwa kwa maji na moto watoto pindi wanapokosea,kuwafanyisha kazi ngumu,Kuwanyima Chakula,Haki ya kupata elimu,Matibabu na malezi Bora kutokana na ugomvi wa wazazi,Ulevi uliopindukia na msongo wa mawazo hali inayohatarisha maisha ya watoto wadogo

Wednesday, December 1, 2021

MIILI 9 YAPATIKANA BAADA YA TUKIO LA KUZAMA KWA BOTI NIGERIA.

 

 Maafisa wa Nigeria wamethibitisha kuwa miili tisa zaidi ya mkasa wa ajali ya boti ya Jumanne imepatikana Jumatano asubuhi.


Hii inafanya idadi ya waliofariki kufikia 29 kufikia sasa.


Shughuli ya utafutaji na uokoaji inaendelea ikihusisha polisi, zima moto na wanachama wa Kikosi cha Usalama na Ulinzi wa Raia wa Nigeria pamoja na waliojitolea.



Polisi katika eneo hilo wameiambia BBC kwamba idadi ya manusura waliookolewa kufikia sasa bado ni saba.

Manusura wa ajali ya boti walikuwa wengi wanafunzi wa shule ya Kiislamu - wenye umri wa kati ya miaka sita na 12 - waliokuwa wakisafiri kwenda kwenye sherehe za kidini katika mji wa Bagwai.

Tuesday, November 30, 2021

KESI INAYOMKABILI MKE WA BILIONEA MSUYA YAANZA KWA PINGAMIZI.

 


Upande wa utetezi katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella umepinga kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza.


Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kumuua kwa kusudia Aneth Msuya,  dada wa marehemu Msuya Mei 25, 2016 katia eneo la Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.


Maombi hayo yametolewa na mawakili wa utetezi Omary Msemo na Nehemia Nkoko baada ya shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, WP 4707 Sajenti Mwajuma (42) kuomba maelezo yake yapokewe kama kielelezo.


Akitoa sababu za kupinga maelezo hayo Wakili Msemo amedai maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda kinyume na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 kinachotaka mtuhumiwa kumchukulia maelezo ndani ya saa 4 tangu alipokamatwa.


Amedai mshtakiwa alikamatwa Agosti 5, 2016 na maelezo kumchukulia Agosti 7, 2016 ambapo kifungu cha 51 kinataka muda wa nyongeza kuongezwa endapo maelezo hayajakamilika.


Wakili Msemo alidai sababu ya pili ya kutaka maelezo hayo yasipokelewe ni kutokana na mshtakiwa kudai maelezo hayo yalichukuliwa baada ya kuteswa.


"Suala hili lilianzia mahakama ya Kisutu hata mshtakiwa alisema kuna baadhi ya sehemu zake za mwili zilikuwa na makovu,” alisema.


Sababu nyingine ya upande wa utetezi kupinga maelezo hayo, wakati mshtakiwa anachukuliwe maelezo hakupewa haki zake kisheria kinyume na kifungu cha 53(c) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.


"Haki hizo ni pamoja na kuwa na mwanasheria, ndugu au rafiki, hivyo kwa kuwa mshtakiwa hakupewa haki hii tunapinga kupokelewa kama ushahidi katika kesi hii.


Hata hivyo Wakili Nkoko naye alidai mpelelezi ni lazima wakati anamuhoji mtuhumiwa ajue amekamatwa lini ili kujua kama maelezo ya nachukulia ndani ya muda na kama yatakuja nje ya muda, ipo haja ya kupeleka maombi mahakamani ili kuongeza muda.


Alidai sababu nyingine ya kuomba mahakama isipokee maelezo hayo wakati shahidi anatoa ushahidi wake hakueleza maelezo hayo yalichukuliwa kituo gani.


Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Gloria Mwenda alidai hoja zilizotolewa na Wakili Msemo ni za kisheria hivyo anaomba Mahakama isikilize kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.


"Pingamizi 1, 2 na 3 ni ya kisheria ya nahitaji mashadi wengine kudhibitisha, hivyo tunaomba mahakama yako kufanya kesi ndogo ndani ya kesi hii," amesema Wakili Mwenda.


Jaji anayesikiliza kesi hii, Edwin Kakolanya amesema kutokana na pande zote mbili kupingana kuchukuliwa kuhusu kuchukuliwa maelezo hayo, mahakama imeona umuhimu wa kufanya kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.

AMCHOMA MTOTO SEHEMU ZA SIRI NA MOTO WA SIGARA.

 


Jeshi la Polisi mkoani hapa,linamshikilia Apolikarp Mushi kwa tuhuma za kumuunguza sehemu za siri kwa moto wa sigara, mjukuu wake wa kiume pamoja na kumtegua nyonga kwa kutumia kitu kizito.


Mushi anayeishi kijiji cha Uru Kyaseni wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kumfanyia vitendo hivyo mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita anayeishi naye baada ya kutelekezwa na mama yake mzazi.


Anadaiwa kumfanyia ukatili huo kwa muda mrefu sasa ikiwemo vipigo vilivyopelekea mifupa ya nyonga kutenguka na kuchomwa na sigara sehemu za uume wake na kumsababishiavidonda.


Jana, Mwananchi lilishuhudia sehemu za mwili wa mtoto huyo ikiwamo miguuni, mapajani, makalioni na usoni zikiwa na majeraha huku akionekana kuwa na maumivu makali.


Katika mwili wa mtoto huyo kuna majeraha mengine ya mouda mrefu.


Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani hapa,Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa unyama huo.


Maigwa alisema wanamshikiliza babu wa mtoto huyo na wameshaandaa jalada kwa ajili ya kulipeleka kwa Mwanasheria wa Serikali kwa hatua zaidi.


“Tunalifahamu tukio hilo, hatua zaidi zinaendelea, mtuhumiwa yupo mahabusu kwa ajili ya taratibu za kisheria,”alisema Maigwa.


Akizungumzia hali ya Mtoto huyo,baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, Dk Tumaini Mtui, “Mtoto alipofikishwa hapa alikuwa hawezi kutembea na alikuwa amevimba sana mwili , tulimfanyia vipimo tulibaini alivunjika nyonga za upande wa kulia na kushoto na zilikuwa na mpasuko unaonekana umetokana na kipigo.Tumempa dawa, anatakiwa kupumzika ndani ya mwezi mmoja na kuhudhuria klinki ya mifupa”alisema Dk Mtui.


Kwa upande wa bibi mlezi wa mtoto huyo,Maria Masao alisema “Mara nyingi nimekuwa nikitoka asubuhi kwenda kwenye shughuli zangu na kurudi jioni,sasa juzi niliporudi nikamkuta yupo vibaya, yaani amevimba na mwili wake una majeraha kila mahali,ilinibidi niombe msaada kwa majirani ambapo nilipata msaada wa polisi,”alisema Masao na kuongeza.


“Nikimuuliza ananitishia kunipiga na panga na anasema atampiga hadi amuue, yaani hata hapa nyumbani hakuna jirani anayethubutu kuja kutokana na ukorofi wa huyu baba,”alisema mama huyo.


Mmoja wa majirani wa mtoto huyo,Gaudence Njau alisema , “Kwa kweli huyu mtoto ananyanyasika sana na amefanyiwa ukatili wa kila namna baada ya kuona unazidi ilibidi sisi wenyewetuingilie kati maana mtoto bado ni mdogo na anachofanyiwa hakiendani naye,”alisema jirani huyo.

UJERUMANI YAFIKIRIA KUCHUKUWA HATUA KALI KUKABILIANA NA WIMBI JIPYA LA CORONA.

 


Kansela wa Ujerumani anayemaliza muda wake, Angela Merkel, na mrithi wake, Olaf Scholz, wanatazamiwa hivi leo kufanya mkutano na mawaziri wakuu wa majimbo kujadiliana juu ya wimbi jipya la virusi vya corona, huku kukiwa na miito ya hatua kali zaidi kuchukuliwa dhidi ya aina mpya ya kirusi kinachosambaa kwa kasi ulimwenguni. 


Msemaji wa chama cha Walinzi wa Mazingira, Janosch Dahmen, ameliambia shirika la habari la dpa kwamba kuna haja ya kufungwa baadhi ya shughuli za kawaida kwenye majimbo mengi ya nchi. 


Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria kutokea chama cha CSU, Markus Soeder, ametowa wito wa ushirikiano na hatua kali zaidi. 


Hayo yanakuja wakati Mahakama Kuu ya Kikatiba ikiwa leo imetoa hukumu yake ya kwanza ambapo imesema kuweka zuio la shughuli za maisha na uhuru wa watu katika kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona kulikuwa halali.

TANZANIA IMEJIPANGA HIVI KUKABILIANA NA TISHIO LA WIMBI LA NNE LA UVIKO 19

 


Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi mbalimbali Duniani zilizojiandaa kukabiliana na tishio la wimbi la nne  la UVIKO 19 ambapo hivi sasa pia katika baadhi ya nchi duniani imegundulika kuwepo kwa anuwai mpya ya kirusi kinachotambulika kwa jina la OMICRON.


Ametoa tamko la serikali dhidi ya mwenendo wa UVIKO 19 na Tishio la wimbi la nne la ugonjwa huo baada ya taarifa kuenea kutoka nchi mbalimbali Duniani ambazo zimeanza kuripoti ongezeko la visa vipya vya UVIKO 19 huku ikiripotiwa kuwepo kwa Tishio la kirusi kipya cha Omicron hali inayohitaji jamii kuchukia tahadhari zaidi.

Dkt Gwajima amesema kuwa takwimu zinaonyesha hadi kufikia tarehe 29 Novemba 2021 jumla ya waliothibitika kuwa na maambukizi Duniani watu 260,867,011 kati yao vifo 5,200,267 ambapo takwimu za zaTanzania zinaonyesha hadi kufikia 28 Novemba 2021 jumla ya watu waliothibitika kuwa na maambukizi ni 26,273 na vifo vilivyotoke ni 731 ambavyo vimetolewa taarifa.


Amesema kuwa jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote ni la kila mwananchi ambapo Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wadau wake kwa pamoja wanasimamia utekelezaji wa afua mbalimbali ili kuwezesha jamii kujikinga na UVIKO 19 wakati serikali ikiwezesha upatikanaji wa chanjo hadi sasa dozi za chanjo 4,305,750 zimepatikana kwa ajili ya kuchanja wananchi 2,766,575 amesema Dkt Gwajima.


Aidha Dkt Gwajima amesema kuwa serikali imepokea chanjo ya Jansen dozi 1,227,400,Sinopharm dozi 2,578,400 na chanjo aina Pfizer hadi kufikia 28 Novemba 2021 jumla ya wananchi waliopata chanjo 1,520,275 sawa na asilimia 2.7 ya watanzania Wote.

KAZI INAENDELEA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA NYASAKA KAZI

 


#NYASAKA

Mheshimiwa Diwani KATA NYASAKA comrade ABDULRAHMAN RASHID SIMBA akifuatilia Kwa ukaribu Ujenzi wa vyumba vya madarasa sita (6) kata ya Nyasaka huku yakiwa yamefikia hatua ya upauaji.





KAZI IENDELEE 🇹🇿

WAZIRI AWESO AKEMEA VITENDO VYA UBAKAJI, ULAWITI PANGANI ATAKA VIKOMESHWE

 

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso katikati akitoa  tuzo kwa mmoja wa wawakilishi wa Kijiji bora Kimanga wilayani Pangani Mkoani Tanga vilivyofanya vizuri kwenye mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 
WAZIRI wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso  katikati akizinduzi wa Igizo la Radio lenye lengo la kuyawezesha makundi ya waendesha pikipiki maarufu Bodaboda kushiriki kwenye mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wenza.
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso kushoto akikabidhi zawadi mbalimbali 
WAZIRI wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso akizungumza wakati wa halfa hiyo

MKUU wa wilaya ya Pangani Ghalibu Ringo akizungumza wakati wa halfa hiyo


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Pangani Akida Bohorera akizungumza 


Mkurugenzi wa Uzikwasa Novatus Urassa akizungumza wakati wa halfa hiyo


Mwakilishi Hakimu Mkazi Mfawidhi ,Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Pangani  Fransisca Magwiza 

Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wilayani Pangani (Takururu)  akizungumza 

Wasanii wilayani Pangani wakitoa burudani


OSCAR ASSENGA, PANGANI.


WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema kasi ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia wilayani Pangani yanatakiwa kuongezwa nguvu kwa sababu hawataki kusikia vitendo vya ubakaji na ulawiti vikiendelea.

Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Igizo la Radio lenye lengo la kuyawezesha makundi ya waendesha pikipiki maarufu Bodaboda kushiriki kwenye mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wenza.

Igizo lilikwenda sambamba na Kampeni ya Mapambano dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa jinsia lilioandaliwa na Shirika la Uzikwasa lenye makazi yake wilayani Pangani Mkoani Tanga ikiwemo kutoa zawadi kwa vijiji bora vilivyofanya vizuri kwenye mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Alisema hawataki kusikia watu wanabakwa huku akilitaka Shirika la Uzikwasa watoke na kwenda kuwaelimisha fursa zinazowazunguka wilaya ya Pangani kutokana na uwepo wa maji yanayotiririka baharini wakati hawana hata shamba la kulimia mchicha.

“Ndugu yangu Akida wewe ni Mwenyekiti wa Halmashauri tutakuwa wasaliti wakubwa kama hatutakuwa tumetenda haki kwa wananchi kama tutakuwa sehemu ya kuwapigia Maocd mahakami kwamba aliyefanya tukio hilo ni mwenzetu tumsamehe”Alisema Waziri Aweso

Alisema yeye hawakuwa tayari ya kuwaombea msahama watu wanaofanya vitendo vya namna hiyo badala yake nitahakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo kwa jamii.

“Uchungu wa u mwana aujuaye ni mzazi hebu fikiria wewe mama umezaa mtoto wa kiume ambaye atakuja kusaidia jamii yake anashindwa kufikia malengo kwa sababu ameharibiwa hii sio sawa kabisa lazima tuchukue hatua “Alisema

“Wakati mwengine unasikia mtu anabakwa mpaka anafikia hatua ya kufa na kushindwa kufikia malengo yake nani aje aseme hapo niwaombe wazazi wangu na wananchi mtu yoyote ambaye atataka kutuharibia jamii yetu ya Pangani lazima tumnyooshee vidole na achukuliwa hatua tunasema uzikwasa tupo tayari kushirikiana nanyi”Alisema

Awali akizungumza wakati wa tamasha hilo Mkuu wa wilaya ya Pangani Ghaibu Lingo alisema ukatili wa kijinsia kwa sisi watu wa Pangani wazazi ndio wanaanza kwa kuwakatili watoto na wakina mama.

Alisema wamewakatili wakiiamini kuwa ni tamaduni waziache huku akieleza kwamba sasa ameanzisha taratibu kwamba taarifa ya ukatili ikikingia kwenye mikono yake akisikia imefika mahakamani na watu hawajaenda kutoa ushahidi atawashughulikia.

“Kwa sababu haiweziekani mtu ameharibika na unashindwa kutoa ushaidi mahakamani na ndio maana ukatili unaongezeka sasa kama DC ndio mimi mwenyewe nikisikia taarifa ya ukatili na mtu akijaribu kuiharibu walahi tutawashughulikia”Alisema

Naye kwa upande wake Mwenyekiti Halmashauri Akida Bahorera alilipongeza Shirika la Uzikwasa kwa jinsi wanavyofanya kazi nzuri na kubwa ya kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia.

Alisema wanafanya kazi kubwa ya kuelimisha wakina mama wamepata elimu kubwa ya kupambana na ukati wa kijinsia na wamewaunganisha wana vijiji na matunda yake yameonakana kwani ripoti inayotolewa na vijiji kuita vikao na kusaidia maendelea ya jamii.

Hata hivyo alisema Shirika la Uzikwasa limetusaidia kwenye eneo la mguso maana yake watu wa bodaboda wakati hawajapata elimu ilikuwa ni eneo hatarishi kwa vijana lakini kutokana na elimu hiyo imewabadilisha na kuondokana na vitendo hivyo huku akieleza halamshauri haitutakuwa vikwazo badala yake watashirikiana nayo.