ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 4, 2021

RAIA WA KENYA AHUKUMIWA MIAKA 27 JELA

 


Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, imemhukumu raia wa Kenya, Samwel Murwa (25) kutumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kosa la kupatikana na mafurushi saba ya kilo 259 za Mirungi.


Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Jaji Imaculeti Banzi baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi watano na vielelezo saba vya upande wa mashitaka, ambao alisema ulikuwa ni ushahidi mzito na haukuacha mashaka yoyote.


Awali mawakili wa upande wa mashitaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Sabitina Mcharo na Grace Kabu waliieleza mahakama mshitakiwa alikamatwa na mirungi hiyo Agosti 19,2018 katika kijiji cha Mnoa wilaya ya Mwanga.


Siku hiyo ya tukio, mshitakiwa alikamatwa porini akiwa amekalia mfuko wa Sandarusi ukiwa na mirungi na pembeni yake kulikuwa na mifuko mingine sita yote ikiwa imesheni mirungi ambayo huingizwa nchi kutoka  Kenya.


Katika utetezi wake ambao mahakama iliukataa, raia huyo wa Kenya alijitetea kuwa siku hiyo alikamatwa na polisi kwa kuingia nchini bila kibali lakini alivyofikishwa katika gari ya polisi ndio akakuta magunia hayo saba ya Mirungi.


Akisoma hukumu yake, Jaji Banzi alisema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka ulijitosheleza na haukuacha mashaka na kwamba utetezi wake hauna mashiko kwani hakuwadodosa mashahidi juu ya hicho alichojitetea nacho.


Hukumu hiyo ni mfululizo wa hukumu za vifungo dhidi ya wanaojihusisha na biashara ya Mirungi ambapo wiki hii pia mzee wa miaka 71, Patrick Malya alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na kilo 83 za Mirungi.


Adhabu hizo imetolewa wakati mkoa wa Kilimanjaro hasa wilaya za Rombo, Moshi, Hai, na Mwanga zikitikiswa kwa biashara ya mirungi inayoingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya, kupitia njia za panya zilizopo mpakani katika wilaya hizo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.