ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 18, 2016

POLISI WAPIGA STOP MAAFALI YA CHADEMA VYUO VIKUU - NGUVU YATUMIKA KUWATAWANYA.

 Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma  limewasambaratisha wanafunzi  wa vyuo vikuu  wanachama wa Chadema ( Chadema Students Organization -CHASO ) waliokuwa wakishiriki hafla ya mahafali katika  Ukumbi wa African Dreams  ulipo Area D mjini Dodoma.

Katika hafla hiyo mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambapo baadhi ya wanafunzi wamekamatwa baada ya kuwambiwa watawanyike na kurudi majumbani kwao.

Polisi wamesema mikusanyiko  yote ya kisiasa ilishapigwa marufuku, hivyo hata mahafali hiyo ilikuwa batili.

PICHA ZA MKUTANO WA CHADEMA DAR ES SALAAM.

RC MWANZA APOKEA GARI LA WAGONJWA.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, akizungumza na watumishi kabla yakupokea msaada wa gari la wagonjwa.
Mkuu wa mkoa akikata Utepe kuashiria uzinduzi wa mapokezi ya Gari la Wagonjwa kutoka Rafiki Surgical Mission.
Balozi, Issaya Chialo, alipokuwa akitoa maelezo mafupi juu ya msaada wa gari la wagonjwa walilo likabidhi kwa hospitali ya Mkoa wa Mwanza.
Watumishi katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza, wakimasikiliza kwa makini mkuu wa mkoa wa Mwanza hayupo pichani, wakati wa hafla fupi yakukabidhi gari hilo.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Subi, akitoa maelezo ya awali kuhusu huduma za afya katika mkoa wa Mwanza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.
Wananchi wanao hudumiwa katika hospitali hiyo ya mkoa nao hawakuwa nyuma katika hilo, hapo wakisiliza kwa makini maelezo ya mkuu wa mkoa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, Bi Maricella, akimkaribisha mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, akikabidhi cheti cha Shukrani kwa Balozi Issaya Chialo, kama sehemu ya shukrani kwa kutambua mchango wa Rafiki Surgical Mission, walio utoa kwa Mkoa huo wa Gari la Wagonjwa.(Habari na picha zote na Afisa habari wa mkoa wa Mwanza)
Hilo ndilo gari lililotolewa na Rafiki Surgical Mission.
Na. Atley Kuni RS Mwanza.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amepokea gari la Wagonjwa kutoka kwa Sargical Rafiki Mission kwaajili ya kuhudumia wananchi wa mkoa huo ambalo amelikabidhi kwa uongozi wa  hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekouture na kuwataka kuitunza kwa maslahi mapana ya wananchi wa mkoa huo.
Akizungumza kabla yakupokea gari hilo mkuu huyo wamkoa amesema, msaada walio upokea kutoka kwa Rafiki Mission ni masaada wakupigiwa mfano kwakuwa watu wengi wanabarikiwa vitu vingi lakini suala lakutoa misaada wameshindwa.
Mongella amesema kama mkoa ukipata marafiki wa aina ya Rafiki hawana budi kuwa ng’ang’ania wasiondoke kwenye himaya yao. “ Nafahamu hata sisi tunabarikiwa sana lakini hata siku moja hakuna mtu aliwahi kuleta hata mkasi, hivyo lazima tufahamu kutoa ni moyo na sio utajiri.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amesema, karibu asilimia tisini ya matatizo ya afya yanayo ikabili jamii ya kitanzania yamejikita katika suala la afya ya mama na mtoto ambayo kama taifa tukifanikiwa kuwekeza katika hili, basi matatizo mengine ya afya yataondoka yenyewe “ Najua suala la mama na mtoto ni tatizo mtambuka kwa taifa, hivyo tukiwekeza zaidi katika afya ya mama na mtoto tutakuwa tumekabili changamoto kubwa ya masuala ya afya na itawawezesha wananchi kujikita katika shughuli za maendeleo”, alisema Mongella
Awali akitoa salama za Rafiki Mission, Balozi Issaya Chialo, alisema wao kama Rafiki Mission, wanatambua matatizo yanayo ikabili jamii ya kitanzania hususan masuala ya afya,  na kwamba wao kama Rafiki Surgical mission, hawana ubaguzi katika utoaji wa misaada kwa jamii nzima ya kitanzania.
“ Mkuu wa mkoa sisi shughuli zetu zipo katika mkoa wa Mtwara tukijikita katika zaidi katika utafutaji wa mafuta na Gesi, lakini hiyo haituzuii sisi kupeleka misaada pembe zingine za nchi na ndio maana leo tupo katika mkoa wako wa  Mwanza” alisema Balozi Chialo nakuongeza kuwa, wanajisikia fahari katika hilo.
Chialo ameutaka uongozi wa Hospitali ya rufaa ya  mkoa wa Mwanza Seko’uture kulitunza gari hilo la wagonjwa lenye thamani ya Mil. 40, ambalo litasaidi katika kuwakimbiza wagonjwa wenye mahitaji maaluma sehemu mbali mbali za mkoa huo na mikoa ya jirani.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Subi, amesema hivi sasa hospitali ya mkoa huo inakabiliwa na changamoto ya chumba cha kutolea huduma ya upasuaji kwa akina mama, ambapo mkuu wa mkoa amemtaka Mganga huyo wa mkoa kutenga kiasi cha Mil. 5 kutoka katika makusanyo ya ndani ya hospitali ya mkoa huo  na Mkuu wa mkoa kupitia wadau wa maendeleo atahakikisaha kiasi kingine cha fedha kinacho salia  kinapatikana kwaajili ya ukarabati wa chumba hicho ambacho kinahitaji Mil.20 ili kiweze kufanya kazi ya upasuaji kwa akina mama.
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza  Seko’uture, imekuwa msaada kwa wagonjwa wa mkoa huo na mikoa ya jirani kutokana na huduma zake kuwa nzuri na madaktari mabingwa wanaopatikana katika mkoa huo.

Friday, June 17, 2016

HUU NI UCHAMBUZI WA HABARI ZA MAGAZETI YA LEO JUNE 17, 2016


Mjadala wa mikoa ya masikini yaligawa bunge, Majanga matano uzimaji simu feki na Askofu Gwajima sasa mkononi mwa Polisi na Manji aibeba Simba. Pata dondoo za magazeti ya leo hapa.


Polisi wapiga kambi ya saa 7 nyumbani kwa Gwajima. Seif asisitiza Serikali ya mapito Zanzibar, Lugumi kuwarejesha wapinzani Bungeni na Mangula aweka mambo hadharani.

Thursday, June 16, 2016

AIRTEL YAENDELEA KUWAPATIA WATANZANIA SIMU ZENYE UHALISI.

Maafisa wa Airtel watitoa maelekezo kwa Wateja kutokana na ofa kabambe za “simu za bure na halisi" zinazopatikana katika maduka Airtel, ambapo leo hii Airtel wapo maeneo ya mnazi mmoja katika ofisi za halmashauri ya manispaa ya Ilala, ambapo wiki ijayo wataendelea kuwepo katika ofisa za halmashauri ya manispaa ya Ilala na Kinondoni.

Airtel yaendelea kuwapatia watanzania simu zenye uhalisi.
• Simu za Bure katika maduka ya Airtel nchi nzima
• Vifurushi vinavyodumu kwa miezi minne na dakika zaidi ya 1000
Dar Es Salaam, 16 Juni 2016, Kufuatia tamko la serikali la kuzima simu zote bandia ifikapo tarehe 16 Juni 2016, Airtel Tanzania imeendelea kutoa ofa kabambe za “simu za bure na halisi" zinazopatikana katika maduka yote ya Airtel nchi nzima. Tangazo hilo limesema kwamba simu za Bure na halisi zinapataikana kwa wateja wote wenye simu bandia na  ambazo sio za viwango vinavyokubalika  katika soko la Tanzania  , kwa kununua kifurushi chenye dhamani  ya sh. 22,000 / = Tshs tu.   Simu hizi za bure na halisi zinazotolewa  na Airtel ikiwemo  ITEL 2090 na FERO 180, zikiwa na dakika  550  kwa kupiga mitandao yote, zenye ujumbe mfupi 3000 na 250 MB kwa muda wa miezi minne.

 Akitoa maoni yake juu ya ofa hii, mkuu wa kitengo cha  Internet Airtel Tanzania, Gaurav Dhingra alisema "kwakutambua kwamba baadhi ya wateja wetu  bado wanatumia simu ambazo hazina uhalisia, tumeendelea kufanya jitihada za kuwapatia simu halisi.Napenda kusisitiza kuanzia kesho kwa wale  wenye simu zitakazo zima leo usiku wasi hofu kwani laini zao hazitahadhirika na vifurushi na pesa ndani ya simu zao zitaweza kutumika pale watakapo nunua simu zenye kiwango kinachokubalika kwenye maduka yetu nchi nzima kwa kupata simu halisi, na vifurushi vitakavyo dumu kwa miezi mine

Le tupo maeneo ya mnazi mmoja katika ofisi za halmashauri ya manispaa ya Ilala, ambapo wiki ijayo wataendelea kuwepo katika ofisa za halmashauri ya manispaa ya Ilala na Kinondoni.  Dhingra aliendelea kufafanua kuwa, ili kuwapa wateja wetu uwezo wa kuchagua simu zinazokidhi mahitaji yao ,tumeongeza simu za aina mbalimbali ikiwemo Magnus Z11, Huawei Y3C na Techno W3  ambapo mteja akinunua anapata kifurushi chenye dakika zaidi ya 1000 . "Tunatoa wito kwa wateja wetu wa Airtel wenye simu bandia kufika kwenye duka letu lolote la Airtel na simu yake ili ajipatie  simu yenye kiwango kinachokubalika kwa gharama nafuu zaidi kwa kununua kifurushi cha Airtel na kupata simu bure. "alinukuliwa Dhingra

Wateja wa Airtel wanaweza kuhakikisha kama simu zao ni bandia au la, kwa kupiga *#06# au kutembelea mawakala katika maduka ya Airtel lililokaribu nae.

SIKU YA MTOTO WA AFRIKA NI MIAKA 40 SASA MACHOZI YASIYOFUTIKA KWA WANA WA AFRIKA KUSINI.

Mwanahabari/Blogger kutoka Jembe Fm Gsengo mbele ya kaburi la kijana Hector Pietersen.
Afrika Kusini inaadhimisha miaka 40 tangu maandamano ya wanafunzi wa Soweto, walipopinga ubaguzi wa rangi katika elimu kwa kulazimishwa kusomeshwa kwa lugha ya Ki-Afrikaan.
Afrikaans ni lugha inayotumika huko Magharibi mwa Ujerumani na kabila dogo la nchi hiyo na ilitambulishwa hapa Afrika na makaburu kwa makusudi ya kuwachanganya waafrika wakibaki kuwa watumwa ikasambaa sehemu za Afrika ya kusini na Namibia.

Lugha hiyo haikuwa na msaada kwa wahitimu zaidi ya kuwachanganya pindi wanapo hitaji kwenda kwenye masomo ya juu au pindi wanapo ajiriwa wakashindwa kupenya kwenye nafasi za juu za uongozi na kubakia kuwa watumwa.

Mamia ya wanafunzi walifariki katika vurugu zilizojiri wakati serikali ya ukoloni ya wazungu makaburu ilipotumia nguvu kupita kiasi, kujaribu kuzima maandamano hayo.
Maandamano hayo yalikuwa kama mwanzo wa kuelekea hatua za kumalizwa kwa utawala wa makaburu wa Afrika Kusini.
Luis ni mwelekezi anayejitolea kwa watalii wanaodhuru eneo hili la kaburi la Hector Pieterson anasimuliwa kilichotokea. BOFYA PLAY KUMSIKILIZA 
(SAUTI ITAWAJIA HIVI PUNDE)
Ujumbe aliouandika mama wa kijana aliyebeba mwili wa kijana Hector Pieterson katika harakati za kumuokoa baada ya kupigwa risasi na polisi. Ujumbe unasomeka "Mbuyisa ni au alikuwa kijana wangu (kwa sababu alitoweka baada ya tukio hilo na hajulikani aliko mpaka sasa) akiendelea kusema ...... "Lakini si Shujaa. Kwenye utamaduni wetu kumbeba Hector siyo tukio la kishujaa, lilikuwa ni jukumu lake kama kaka. Kama angemuacha pale chini na mtu mwingine angemshuhudia akiuruka au kuukanyaga mwili wa marehemu Hector, asingestahili kuishi hapa"  ujumbe wa Ma'Makhubu.
Kila kilichopo hapa kina maana yake:-  Ukuta wa mawe yaliyopangwa ukimaanisha umoja wa watoto walioungana kwenye maandamano hayo kupinga ubaguzi, maji yanayotiririka yanaashiria machozi ya huzuni yaliyomwagika siku ya tukio toka kwa wazazi, watoto na taifa kwa ujumla, urefu unaopishana wa mawe unamaanisha umri wa watoto waliouawa, mianya katikati ya mawe inamaanisha taarifa zilizo potea au kufichwa hadi leo na kubaki bila ufafanuzi kama nani aliyemuua Pieterson na kadhalika, sakafu nyekundu ni damu iliyo mwagika, mawe ndani ya maji yanaashiria silaha pekee walizotumia watoto kujilinda dhidi ya polisi siku ya tukio.
Gsengo mbele ya picha ya mwili wa kijana Hector Pieterson uliobebwa na mwanafunzi mwenzake aitwaye Mbuyisa baada ya kupigwa risasi na polisi. Hii ndiyo picha iliyoibua hamasa na hasira kubwa na kuufanya ulimwengu kulaani ukatili uliokuwa ukiendelezwa na utawala wa makaburu enzi za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Marehemu Hector Pieterson alizaliwa mnamo mwaka 1963 na June 1976 alikuwa ni mmoja kati ya mamia ya watoto waliouawa naye amewekwa kwenye historia kwani ni mmoja ya vijana wadogo waliouawa na makaburu na risasi ya kwanza ilimuua kijana huyo  akiwa na umri mdogo miaka 12 tu.
Pichani juu mwili wake ukiwa umebebwa na mwanafunzi mwenzake aitwaye Mbuyisa Makhubu baada ya kupigwa risasi huku dada yake akiwa naye anakimbia jirani kutafuta msaada.
Maji haya yanayotiririka mbele ya kaburi la Hector Pieterson yanaashiria machozi ya wazazi watoto na taifa juu ya tukio hilo la mauaji ya mamia ya watoto lililotokea mnamo tarehe 16 June 1976. 
Jiwe hili lilitumika ngao kujikinga na risasi za mitutu ya bunduki za polisi kwenye maandamano ya watoto mnamo mwaka 1976.
Barabara hii ndiyo iliyo tumika kwa maandamano ya mwaka 1976 ikiwa ndiyo kiunganishi cha maeneo ya mji wa Soweto nchini Afrika Kusini.
Pembeni hatua chache kutoka eneo lilipo kaburi kuna Jumba hili la makumbusho la Hector Peterson, Humo ndani kunavielelezo vyote vya yale yaliyotokea kwa njia ya picha, video na baadhi ya mabaki ya nguo, silaha na baadhi ya nyezo walizotumia watoto hao kujikinga wakati wa vurugu zilizotokea zilizotumika kwenye tukio hilo lenye kumbukumbu yenye simanzi.


The Hector Pieterson Museum is a large museum located in Orlando West, Soweto, South Africa, two blocks away from where Hector Pieterson was shot and killed. Jumba hili lilipewa jina la marehemu kijana huyo kama heshima kwake.

PANAFRICAN ENERGY TANZANIA YAKABIDHI MADAWATI 800 KWA WILAYA YA KILWA


Meneja wa Uwajibikaji na Huduma za kijamii wa Kampuni ya Uchimbaji gesi ya PanAfrican Energy (CSR Manager) Andrew Kashangaki akifafanua jambo wakati wa hafla ya makabidhiano ya madawati kwaajili ya watoto wa shule za msingi wilayani Kilwa

Baadhi ya madawati yaliyotolewa na Kampuni ya uchimbaji gesi ya PanAfrican Energy
Meneja wa Uwajibikaji na Huduma za kijamii wa Kampuni ya Uchimbaji gesi ya PanAfrican Energy (CSR Manager) Andrew Kashangaki(kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilay ya Kilwa Juma A. Njwayo madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi wilayani mwake. Wanaoshuhudia ni baadhi ya viongozi wa halmashauri ya Kilwa, viongozi kutoka PanAfrican Energy na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Masoko katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Kilwa Masoko.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mh. Juma Abdallah Njwayo akiwaasa wanafunzi wa shule ya Msingi Masoko ambao ni moja ya wanufaikaji wa madawati 800 kutoka PanAfrican Energy kuyatunza madawati waliyopewa na kusoma kwa bidii.

Meneja wa Uwajibikaji na Huduma za kijamii wa Kampuni ya Uchimbaji gesi ya PanAfrican Energy (CSR Manager) Andrew Kashangaki akitoa neno wakati akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mh. Juma A. Njwayo madawati 800 yatakayosaidia watoto 2400 na kupunguza tatizo la uhaba wa madawati.

Meneja wa Uwajibikaji na Huduma za kijamii wa Kampuni ya Uchimbaji gesi ya PanAfrican Energy (CSR Manager) Andrew Kashangaki akitoa neno wakati akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mh. Juma A. Njwayo madawati 800 yatakayosaidia watoto 2400 na kupunguza tatizo la uhaba wa madawati.

PANAFRICAN ENERGY TANZANIA YATOA MADAWATI 800 KWA WILAYA YA KILWA 

 Kapuni ya uchimbaji gesi asilia PanAfrican Energy jana imekabidhi madawati 800 kwa ajili ya shule za msingi wilayani Kilwa yenye thamani ya shilingi za kitanzania Milioni 104. Makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Masoko iliyopo wilayani humo katika hafla fupi iliyoandaliwa na Kampuni hiyo, huku ikishuhudiwa na wana habari, viongozi mbali mbali wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Juma Njwayo, walimu, wanafunzi na wananchi wa Kilwa Masoko. Msaada huo wa madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule za Msingi ni kuunga mkono Kampeni ya uchangiaji madawati iliyoanzishwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.

Akiongea wakati akipokea madawati hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mh. Juma Njwayo, ambaye alikua mgeni rasmi katika hafla hiyo aliwashukuru sana Kampuni ya PanAfrican Energy kwa msaada wao mkubwa wanaotoa kwa wilaya ya Kilwa. 
“Kwa niaba ya wana Kilwa naomba kutoa shukrani zetu za dhati kabisa kwa PanAfrican Energy kwa siku zote kutuangalia kwa jicho la tatu kwa mmekua mkijitoa kawa hali na mali kuwezesha huduma mbali mbali katika Wilaya yangu Ya Kilwa. Leo napokea madawati 800 ambayo yatasaidia kupunguza uhaba wa madawati mashuleni kwani yatasaidia watoto 2400 kutokukaa chini, hili si jambo dogo kabisa hivyo mnahitaji pongezi. 
Natoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huu walionesha PanAfrican Energy kwani bado tuna uhaba wa madawati katika shule zetu za msingi hapa Kilwa. Hapa katika Shule ya Msingi Masoko watapata madawati 145 ambayo yapo mbele yetu hapa na mengine 655 yaliyobakia yatagawiwa kwa shule zingine zenye uhaba huo. Tunategemea ifikapo katikati ya mwezi Julai tutakua tumemaliza tatizo la madawati katika shule za msingi wilayani humu. Pia alitoa wito kwa wanafunzi kutunza madawati hayo ili yaweze kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.”

“Mbali na kupata madawati pia tunawapongeza kwa kuwa na uzalendo na wilaya yetu kwani hata mzabuni aliyepata kazi ya kutengeneza madawati haya ni mwananchi wa Kilwa ambapo vijana kadhaa wamepata ajira kupitia kazi hiyo na kuongeza kipato chao. 
Ukiachilia mbali swala la elimu Kampuni hii imekua mstari wa mbele katika swala la afya pia ambapo katika kuupunguza vifo vya kina mama na watoto wanatujengea jengo la Mama Ngojea katika hospitali yetu ya Wilaya ambako kabla yam waka huu kuisha tutakua tumeshakabidhiwa jengo hilo pia wanakarabati kituo cha afya cha Kilwa Masoko.” Aliongeza Mh. Njwayo.

Naye Meneja wa Uwajibikaji na Huduma za jamii wa Kampuni ya Uchimbaji wa Gesi ya PanAfrican Energy Andrew Kashangaki alisema, “Ni furaha yetu kuona watoto wa kitanzania wanasoma kwa Amani bila kuwa na matatizo yeyote na ndomana tumesukumwa kuunga mkono sekta ya elimu nchini kwa kuanza na wilaya ya Kilwa. 
Leo tunakabidhi madawati 800 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa yatakayosaidia kupunguza tatizo la watoto wetu kukaa chini na wadawati haya yatagawanywa kwa shule za msingi mbalimbali kutokana na uhitaji wao. Sisi kama wadau wa Elimu tumefanya kile tulichoweza kufanya hivyo tunaamini kwa madawati haya tunawawezesha watoto wa kitanzania watakaosomea katika shule hizo kutoa ujinga na tunatengeneza Taifa la wasomi.

Aliongeza kwa kusema kuwa, “Tayari tuna programu ya kusomesha watoto kutoka kisiwa cha Songosongo ambako kila mwaka tunasomesha watoto 28, tumejenga mabweni kwaajili ya watoto wa kike kisiwani songosongo, pia ujenzi wa maabara za kisasa kwa ajili ya masomo ya sayansi kwa shule za Sekondari hiyo yote ni kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kusomea kwa watoto wetu.”

Wilaya ya Kilwa ilikua ina uhaba mkubwa wa madawati tangu mwaka jana lakini inaaminika kuwa ifikapo katikati ya mwezi Julai watakua wameshatatua tatizo hilo. Wamepata madawati kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Kampuni ya Uchimbaji gesi ya PanAfrican Energy iliyotoa madawati mengi zaidi yaw engine, huu ni mfano wa kuigwa kwa wadau wengine kwani mtoto wa mwenzako ni wako na kila mtoto ana haki ya kusoma katika mazingira rafiki.

MAGAZETI YA LEO:- MAALIM SEIF ASEMA CUF HAIWEKI UONGOZI JUU YA UONGOZI, MADUDU YAIBULIWA BODI YA MIKOPO, WALIOSUSIA BUNGE WAKOSA MILIONI 300


Maalim Seif: CUF haiweki uongozi juu ya uongozi. Madudu yaibuliwa bodi ya mkopo. Waliosusia bunge wakosa milioni 300.

AIRTEL FURSA YAWAFIKIA WATOTO 500 MSIMU WA RAMADHANI.

Airtel FURSA yawafikia watoto 500 msimu wa Ramadhan
  • Vijana wa Airtel FURSA kujitolea kazi zao
Kampuni ya za mkononi ya Airtel kupitia mpango wake wa huduma kwa jamii  chini ya mradi wa Airtel FURSA imeanza kutoa futari  katika kindi hichi cha Ramadhan kwa vituo vinavyolea watoto waliopo katika mazingira magumu nchini.
Airtel ikishirikiana na vijana wajasiriamali wa Airtel FURSA imetoa msaada wa vyakula vitakavyowasaidia watoto walio katika vituo mbalimbali nchini kufuturu wakati wote wa msimu huu wa ramadhani.
Akiongelea kuhusu “FUTARI na Airtel FURSA” Bi Dangio Kaniki, Afisa Mahusiano na Matukio wa Airtel Tanzania alisema, “Tumeweza  kuwafikia watoto walio katika vituo mbalimbali nchini, kama sehemu ya shughuli zetu za jamii. Leo tunatoa Tshs million 10 kwa ajili  ya watoto zaidi ya 500 katikamikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza, Zanzibar, Dodoma na Dar es saalam.  
“FUTARI na Airtel FURSA” kwa mwaka huu imeshirikisha vijana walio nufaika na Airtel FURSA kwa kutoa sehemu ya kazi zao kusaidia jamii.Kwa namna ya pekee tunawapongeza Vijana walionufaika na Airtel FURSA Kwa kutambua changamoto nyingi zinazozikumba jamii na kushiriki kutoa kidogo walichonacho. 

Lengo la Airtel kupitia Airtel FURSA ni kuhakikisha tunagusa mahitaji ya jamii kwa ujumla, husasani watoto kupitia vituo vinavyowatunza huku tukihakikisha tunarudisha faida tunayoipata kwa kuwafikia watanzania wengi kupitia shughuli zetu za huduma za kwa jamii kwa kila mwaka.


Vituo hivyo vitakavyopata msaada kutoka Airtel  ni pamoja na  Sarnaa Islamic Ophanage center Mwanza, Kiboa Islamic Center Arusha, Nuru Ophanage Center na Hope for the future Mbeya, Swadiq Development Foundation Dodoma, Maua Daftari Zanzibar na vituo vingene vitatu  kutoka katika wilaya ya Temeke, Ilala na Kinondoni  jijiji Dar es Saalam

Wednesday, June 15, 2016

RAIS MAGUFULI AONYA WANAOPANDISHA BEI ZA VYAKULA.

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli.
Rais Magufuli amewasihi Watanzania wote kuungana na Waislamu walio katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kuiombea Tanzania iendelee kuwa  nchi ya Amani, Utulivu, Umoja na Mshikamano ili iweze kutimiza malengo yake ya kimaendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo mbele ya Masheikh, Maimamu na viongozi wa dini ya Kiislamu na baadhi ya viongozi na waumini wa madhehebu mengine mbalimbali ya dini aliowaalika katika futari jana jioni tarehe 14 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.

"Kwa niaba ya serikali na mimi mwenyewe na watanzania kwa ujumla, napenda kutumia fursa hii adhimu kuwatakia waislamu wote nchini Tanzania mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, uwe mfungo wa amani na wenye baraka, lakini pia ninamuomba Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema azikubali funga zenu na kuwalipa malipo stahiki.

"Niwaombe ndugu zangu waislamu msisahau kuliombea taifa hili amani, palipo na amani ndipo palipo na maendeleo ya kweli, palipo na amani ndipo biashara itaenda vizuri, palipo na amani hata mahubiri mazuri kwa watu yatasikika vizuri, tulisimamie hili kwa manufaa ya Tanzania" Amesema Rais Magufuli.
FUT4
Pamoja na kuwaalika watanzania wote kuliombea taifa, Rais Magufuli pia amewahakikishia watanzania wote kuwa serikali yake ipo imara kuhakikisha inailinda na kuidumisha amani iliyopo.
Aidha, Dkt. John Pombe Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na umoja na ushirikiano wa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wanaounda kamati za amani za mikoa.

Pia amewataka wafanyabiashara wa vyakula waache kupandisha bei za vyakula hasa vinavyotumika wakati wa mfungo huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuwawezesha waliofunga kumudu kununua vyakula hivyo.

Katika futari hiyo Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wameungana na viongozi mbalimbali wa dini wakiwemo Kaimu Mufti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaji Hamid Masoud Jongo, Askofu Mkuu wa Anglikani wa Mkoa wa Dar es salaam Baba Askofu Valentino Mokiwa, na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa na Mwenyekiti wa Wanawake Waislamu Tanzania Hajjat Shamim Khan.

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA SERIKALI KUHUSU UKOMO WA MATUMIZI YA SIMU BANDIA NCHINI HAPO KESHO JUNI 16 2016


 1.0   UTANGULIZI

1.1. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kusimamia shughuli za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini. Kuwepo kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 na Kanuni za EPOCA (CEIR) za mwaka 2011 zimewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.


1.2. Mfumo huu wa kielektroniki ulizinduliwa rasmi tarehe 17 Desemba 2015 na unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi  (IMEI) kwa lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano. Namba tambulishi za vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo kesho tarehe 16 Juni 2016.

1.3. Kipindi cha mpito cha kuelimisha umma pamoja na zoezi la wateja kuhakiki simu walizo nazo au wakati wanataka kununua simu mpya lilianza mwezi Desemba 2015 wakati mfumo ulipozinduliwa na litamalizika kesho tarehe 16 Juni 2016. Hata hivyo, elimu kwa umma kuhusu simu bandia imekuwa ikitolewa nchini tangu mwezi Novemba 2011 baada ya Kanuni za CEIR kutoka, kufuatia kupitishwa na Bunge Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta tarehe 20 Juni 2010 ikielekeza kuwekwa kwa mfumo wa namba za utambulisho wa vifaa vya Mawasiliano vya kiganjani.

2.0    KAZI ZILIZOFANYIKA TANGU KUZINDULIWA KWA MFUMO

2.1 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendelea kusimamia kwa karibu makampuni ya simu hapa nchini katika uendeshaji wa kila siku wa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi. Hii imesaidia pamoja na mambo mengine kupata taarifa za namba tambulishi (IMEI) na kuzifanyia uchambuzi wa kina ili kupata mwelekeo halisi kabla ya kipindi cha mpito kuisha hapo tarehe 16 Juni, 2016.


2.2 Mamlaka ya Mawasiliano iliendelea pia na kampeni za kutoa elimu kwa umma kuhusu jinsi ya kuhakiki namba tambulishi (IMEI) za vifaa vya mkononi (mobile devices). Katika kampeni hizo wananchi walipata uelewa wa kutambua uhalisia wa simu zao ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu mpya. Makampuni yote ya simu hapa nchini kwa nyakati tofauti wameshiriki pia katika kuelimisha umma, ikiwa ni pamoja na kuwapelekea ujumbe mahususi moja kwa moja kwa watumiaji wote wa simu za mkononi. Hali kadhalika Shirika la Viwango Tanzania na Tume ya Ushindani nchini, wameshiriki moja kwa moja katika kutoa elimu kwa umma sambamba na Mamlaka ya Mawasiliano.


2.3     Kipindi cha kuanzia Desemba 2015 mpaka mwezi Mei 2016 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilitoa elimu kwa umma katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Dodoma, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera. Pia elimu kwa umma ilitolewa Zanzibar. Mamlaka imefanya pia elimu kwa umma katika miji ya, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara wiki iliyopita pamoja na wiki hii. Aidha kesho ambayo ndio siku ya ukomo wa matumizi ya simu bandia nchini, kutakua na mkutano wa wafanya biashara wa simu wa mkoa wa Dar es Salaam. Mkutano huo utawahusisha pia mafundi wa simu, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa. Pamoja na mikutano ya hadhara na mikutano ya barabarani (road shows), elimu imetolewa kwa wauzaji wa simu, Mafundi wa Simu na Maafisa Biashara pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za maeneo husika.


3.0     UCHAMBUZI WA NAMBA TAMBULISHI (IMEI)

Wakati mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi unazinduliwa mwezi Desemba 2015, idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zilikuwa sawa na 4% na zile ambazo zilikuwa zimenakiliwa (duplicates) zilikuwa ni sawa na 30%. Hii ikiwa na maana 66% ni sio simu bandia. Uchambuzi huu haukuhusisha taarifa za makampuni ya Viettel na Smile.

Kielelezo 1: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Disemba, 2015


Uchambuzi wa mwezi Februari 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 3%, vilevile idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 18%. Simu halisi zilikuwa sawa na 79%.


 Kielelezo 2. Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI)February 2016


Uchambuzi wa mwezi Machi 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 4%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 13%. 83% zikiwa simu halisi. Uchambuzi huu unahusisha taarifa za makampuni yote ya simu nchini.Kielelezo 3: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Machi, 2016


Uchambuzi wa mwezi Aprili 2016 unaonyesha hakuna mabadiliko yoyote ya idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) hivyo kubakia 4%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa ziliongezeka kutoka 13% na kufikia 14%. Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia ilipungua kutoka 83% mpaka 82% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo kifuatacho.
Kielelezo 4: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Aprili, 2016


Matokeo ya uchambuzi wa mwezi Aprili, 2016 umeonyesha namba tambulishi ambazo zilikua zimenakiliwa kuongezeka na kuleta taswira kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa wauzaji wa simu wasio waaminifu kupunguza bei za simu zao zenye namba tambulishi zilizonakiliwa na kuwafanya watumiaji wa simu katika maeneo husika ambayo elimu kwa umma ilikua bado haijawafikia kushawishika kununua simu hizo. Matokeo haya yalitoa msukumo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na wadau wote kuongeza nguvu zaidi kuelimisha wananchi katika maeneo yaliyobakia kuhusu umuhimu wa kuhakiki simu zao ikiwa ni pamoja na kuelewa zaidi utaratibu wa kufuata wakati mtu atakapo hitaji kununua simu mpya.


Kielelezo 5: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Mei, 2016


Uchambuzi wa mwezi Mei, 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 3%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 2% ambapo 95% zikiwa simu halisi. Uchambuzi huu unahusisha taarifa za makampuni yote ya simu nchini.


Matokeo haya mazuri yanaonyesha matokeo ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu hapa nchini pamoja na wadau wengine katika kuelimisha umma juu ya kuhakiki uhalisia wa simu walizo nazo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu mpya.


Kielelezo 6: Uchambuzi wa takwimu za namba tambulishi (IMEI) za Juni, 2016


Uchambuzi uliofanywa tarehe 14 Juni 2016 unaonyesha mabadiliko chanya ya idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) kupungua kutoka 3% hadi kufikia 2.96%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zikipungua kutoka 2% hadi kufikia 0.09%. Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia zimeongezeka kutoka 85% mpaka 96.95% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo 6 hapo juu.


Matokea haya yanaonyesha mwitikio mzuri wa wananchi juu ya uelewa wao katika suala zima la uzimaji wa simu ambazo hazikidhi viwango. Matokeo hayo yanatoa picha nzuri hasa tunapoelekea kuhitimisha zoezi la uzimaji wa simu bandia kesho tarehe 16 Juni 2016.


4.0     CHANGAMOTO

Pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Mamlaka pamoja na wadau wengine bado kuna changamoto ambazo zinahitajika kutatuliwa. Changamoto hizo ni pamoja na:


(i)  Uaminifu mdogo kwa baadhi waauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu;


(ii) Gharama zinazohitajika katika kuwafikia wananchi na kuelimisha ili waweze kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu zao; na


(iii) Uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi katika kuitikia wito wa kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito.


5.0     HITIMISHO


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inaendelea kumbusha watanzania wote kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa simu yake ni halisi na sio bandia kwani kuanzia kesho, hakuna simu bandia itakayoweza kufanya kazi nchini. Vilevile Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi kutambua kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi (mobile devices) kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka kumi (10) au faini isiyopungua TZS millioni 30 au vyote kwa pamoja.


Mamlaka inatoa wito kwa wale wote wote wanaofanya biashara za kuingingiza simu hapa nchini kutoka nje wahakikishe kuwa simu wanazoleta zinakidhi viwango, zimehakikiwa kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania. Aidha Mamlaka inawakumbusha kwa mara nyingine kuwa wanapaswa kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria. Hii pia ni kwa mafundi wote wa simu nchini, wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu.


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inayapongeza makampuni ya simu kwa ushirikiano mzuri wanaondelea kuuonesha katika kutekeleza agizo hili la Serikali kupitia Mamlaka. Hali kadhalika, jitihada zao za kushiriki elimu kwa umma kwa wateja wao pamoja na kuwapatia simu wateja waliokuwa wanatumia simu bandia, kumepelekea agizo hili kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu. Mafanikio ya jambo hili, kwa kiasi kikubwa yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali wa Mawasiliano, wakiwemo jeshi la Polisi, Tume ya Ushindani pamoja na Shirika la Viwango Tanzania.


Mhandisi James Kilaba

KAIMU MKURUGENZI MKUU

15 Juni, 2016


Maelezo ya ziada kwa Wahariri


FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI


Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:

Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi  na pia garantiii ya miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.

Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha Polisi  cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB. Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu iliyopotea (risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo).

Mtoa huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani ya saa 24.


Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.

JEMBE FM YAMSAKA SURA MBAYA NA MKALI WA DANADANA.

Mc wa mpango mzima wa kumsaka Sura mbaya na Mkali wa danadana, ambaye ni Mtangazaji wa Jembe Fm kipindi cha Hit Zone, Babajuti akiongoza mchakato wa kusaka vipaji kwa kutaja vigezo na masharti kwenye uwanja wa Stendi ya Igoma ulioko Nyamagana jijini Mwanza.
Ufundi wa kucheza na mpira kwa kutumia miguu yote ni moja ya vigezo vya kufaulu kuwakilisha kituo kwenye fainali zitakazopigwa tarehe tarehe 25 Juni 2016 pale Rock City Mall. Hewani ni mshindi toka Igoma Owasi Tiger akionesha maufundi katika kinyang'anyiro cha kumsaka Mkali wa danadana chini ya udhamini wa Tigo, StarTimes, na pikipiki za GSM.
Igoma kumekucha
Msemaji kutoka GSM akizungumza na wana Igoma kuhusu huduma wanazozitoa kupitia pikipiki zao mpya zenye ubora uliofanyiwa tafiti kulingana na soko na mazingira ya watumia barabara nchini Tanzania.
Muamko wa wana Igoma.
Ushindani katika Mkali wa Danadana ulikuwa mkubwa.
Maufundi hadi ndala zinakatika......balaaaaaaaa!!!
Ufundi na mautundu.
Alaaaaa......maufundi zaidi.
Ze area.
Mshiriki wa shindano la Sura Mbaya Igoma katika pozi la kucheka.
Wadau wa Igoma.
Pia mashabiki waliojitokeza viwanjani hapo walichomoka na zawadi mbalimbali kutoka kwa wadhamini hapa jamaa anaondoka na Tishirt ya StarTimes baada ya kujibu swali.
Mshindi mwingine katika maswali ya papo kwa hapo..
Kijana huyo aliigiza moja kati ya sauti za matangazo ya Jembe Fm ambapo alimuigiza Mhe. Magufuli na kujinyakulia kalamu toka kwa moja wa wadhamini wetu StarTimes.
Ze area.
Pozi la kushangaa mshiriki toka Igoma.
Kucheka jeh!!.
Washiriki wawili Stamin Chankaga (kushoto) na Elisha Ezekiel (kulia) ndiyo wawakilishi kwenye kinyang'anyiro cha kumsaka Sura Mbaya, wakiwakilisha kituo cha Igoma kwenye fainali itakayopigwa tarehe 25 Juni 2016 pale Rock City Mall ambapo mshindi atachomoka na zawadi ya pikipiki toka Kampuni ya GSM pamoja na zawadi nyingine kibao toka kwa wadhamini wa mchakato mzima ambao ni Tigo, StarTimes na Jembe Fm.
Wawakilishi wa shindano la Sura Mbaya kutoka Igoma katika picha na wadhamini.
Wawakilishi wa kumsaka mkali wa danadana igoma Owasi Tiger (wapili kutoka kulia) na Chuse Juma (wapili kutoka kushoto) wakiwa wamewekwa kati na wadhamini kwenye picha ya pamoja.
Maufundi ya Jembe Djz na Deejay Jacko.
Mzigo wa mshindi toka GSM.
Me inade area.
Next ni Pasiansi wilayani Ilemela jijini Mwanza