ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, November 24, 2024

SABA WAFARIKI AJALI YA BAJAJI NA ROLI.

 Saba wafariki ajali ya bajaji na lori

WATU saba wamefariki dunia baada ya bajaji waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori eneo la Mpemba, Tunduma wilayani Momba, mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Augustine Senga, alisema jana ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:15 usiku, wakati dereva wa bajaji yenye namba za usajili MC 783 DUF akijaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake.

Alisema dereva wa bajaji hiyo, Emmanuel Hakimu, ambaye ni mmoja wa watu saba waliofariki dunia katika ajali hiyo, alikuwa akitokea eneo la Mpemba kwenda  mjini Tunduma.

Alisema bajaji hiyo iligongana na lori aina ya Scania lenye namba T 958 BCS na kwamba watu watano walifariki dunia papo hapo na wengine wawili, akiwamo mtoto wa miaka miwili, Isack Mambwe, walifariki dunia wakati  wakipatiwa matibabu.

Kamanda Senga aliwataja wengine waliofariki dunia kuwa ni Rehema Christopher (25) mkazi wa Msongwa, Festo Mambwe (57) mkazi wa Mbeya, Rosemary Njema (44) mkazi wa Ipito mjini Tunduma na Milembe Siyantemi (36) mkazi wa Kapele, wilayani Momba.

Kamanda Senga alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku wakiendelea kumtafuta dereva wa lori ambaye alitoweka baada ya tukio hilo.

“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Tunduma. Chanzo cha ajali hii bado tunakichunguza ikiwa ni pamoja na kumsaka dereva wa Scania," alisema.

Kamanda Senga aliwataka madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kujenga tabia ya kukagua vyombo vyao kabla ya kuanza safari na kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wote ili kuzuia ajali zinazoepukika.

TEF YAMPONGEZA WAZIRI KUUNDA BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI


Na Mwandishi Wetu, JAB.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amempongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa kwa kuunda Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari mapema mara baada ya kuteuliwa.

Balile amesema hiyo ni hatua kubwa kwani imechukua miaka Nane tangu kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 inayotamka uundwaji wa bodi hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Novemba, 2024 wakati akiwasilisha hoja za jukwaa hilo mbele ya Waziri kwenye Kikao cha kwanza cha kufahamiana na Wajumbe wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) kilichofanyika Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa kwa sababu imechukua miaka Nane tangu Sheria imepita 2016 na Bodi ilikuwa haijawahi kuundwa na leo tumesikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi Bw. Patrick Kipangula, siyo mgeni sana kwetu lakini leo tumemsikia kwa cheo kipya, tunashukuru sana na tunampongeza sana,” amesema Balile akionesha kuridhishwa na Hatua hiyo ya Waziri Silaa kuunda Bodi ya Ithibati.

Waziri Silaa aliiteua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Septemba 18 na kumteua Mwandishi wa Habari Nguli Tido Mhando kuwa Mwenyekiti wa Kwanza na wajumbe wengine sita kutoka Taasisi za Habari kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Huduma za Habari.

Wajumbe wa Bodi hiyo ni Bw. Thobias Makoba, Mgaya Kingoba, Dkt. Rose Reuben Mchomvu, Dkt Egbert Mkoko na Laslaus Komanya.



Akizungumza na Wadau wa Habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, tarehe 19 Novemba, Waziri Silaa alibainisha kuwa uzinduzi rasmi wa bodi hiyo muhimu utafanyika mapema mwezi Disemba, 2024 na kwamba itafungua njia ya safari ya kuanzisha Baraza Huru la Habari na pia Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari na tathimini ya hali ya uchumi kwa vyombo vya habari.

Katika hoja yake Balile alimuomba Waziri kuwa na kikao kazi kitakachogusia Sera ya Habari, Sheria na mfuko wa mafunzo ili kupata uelewa wa pamoja wa namna ya kuiboresha tasnia ya Habari na Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Ombi kama hilo pia liliwasilishwa na Mwenyekiti wa CoRI, Ernest Sungura aliyemuomba Waziri katika vikao vijavyo kuwa na majadiliano ya namna Baraza Huru la Habari lililoundwa na Sheria ya Huduma za Habari litakavyoendesha majukumu yake ili kujitofautisha na Baraza la Habari Tanzania (MCT) ili kuondoa mgongano.



Picha ya pamoja

KOKA AFANYA KWELI KWA WAGOMBEA WA KATA YA KONGOWE AWAAHIDI MAKUBWA

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA

 
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka amewahimiza  wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi  wote kwa ujuma kuhakikisha kwa hawafanyi makosa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuhakikisha wanakwenda kuwachagua wagombea wote wa  CCM  lengo ikiwa ni kushinda kwa kishindo katika mitaa yote 73.

Koka ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kampuni za chama cha mapinduzi (CCM) Kata ya Kongowe zilizofanyika katika eneo la Bamba na kuhudhuliwa na wanachama wa chama hicho pamoja na  wakiwemo wananchi pamoja naa viongozi mbali mbali wa chama pamoja na jumuiya zake.

Koka amesema kwamba wakichaguliwa viongozi wote wa CCM inatoa urahisi wa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kupanga mambo ya maendeleo kwa pamoja tofauti na kuchanganya na vyama vingine.

"Ndugu zangu mimi Mbunge wenu leo nimekuja kwa ajili ya kuwazindulia rasmi kampeni hizi za uchaguzi na mimi kitu kikubwaambacho ninawaomba ni kunichagulia wagombea wote wa chama cha mapinduzi ambao na mimi nitafanyanao kazi begaa kwa bega na hii ni katika kumsaidia Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutimiza wajibu wake wa kuwaletea maendeleo wananchi,"alisema Koka.

Amesema kwamba kwa sasa Jimbo la Kibaha limeweza kuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ambayo yameatokana naa juhudi zake kwa kushirikiana na wenyeviti ambao wamemaliza muda wao lakini ana imani katika uchaguzi huu wagombea wote ambao wameeteuliwa wataweza kuendelea kuwahudumia wananchi ikiwemo kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Koka amemshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi ambazo zimeweza kusaidia katika kutekeleza miradi mbali mbali ya kimkakati sambambaa na   kuweza kujenga shule mpya katika jimbo lake ambazo zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha ufaulu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kongowe Hamis Shomari amesema kwamba wagombea ambao wameteuliwa kwa ajili ya kuipeperusha bendera ya chama wanamatarajio makubwa ya kuibuka naa ushindi katika uchaguzi huo kutokana na kuwa na uwezo na sifa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Diwani huyo amesema kwamba kutokana na chama cha mapinduzi kilivyojipanga kuanzia ngazi zote watahakikisha kwamba wanashinda katika mitaa yote na kuwapata viongozi ambao atakwenda kufanya nao kazi ya pamoja katika suala zima la kuwaletea maendeleo ikiwemo sektaa yaa elimu, afya,  maji pamoja na miundombinu ya barabara, sambamba na huduma nyingine za kijamii.
 
Nao baadhi ya wagombea katika nafasi ya uenyekiti akiwemo Nuru Awadhi amesema kuwa wamejiandaa vema katika uchaguzi huo na kuahidi endapo wakichaguliwa katika uchaguzi huo wataweza kushirikiana na wananchi katika kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi na kuwaletea maendeleo.