ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, November 30, 2024

VYAMA VYA SIASA WILAYA YA TANGA VYAPONGEZA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.

 



Na Oscar Assenga,TANGA

Vyama vya Siasa vilivyoshiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba 27 mwaka huu katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, vimetoa tamko la pamoja na kupongeza mchakato wa Uchaguzi huo huku vikitaka dosari chache zilizojitokeza zifanyiwe kazi na Tamisemi.

Vyama hivyo ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM),Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ,vyama vyengine ni (ACT-Wazalendo) CUF, ADC,TLP na NCCR-Mageuzi.


Vyama hivyo vimetoa tamko la pamoja leo Novemba 29 mara baada ya matokeo ya jumla kutangazwa hapo Novemba 28 mwaka huu ambapo CCM katika Jiji la Tanga kimeibuka kidedea kwa kushinda viti vyote vya kuanzia wajumbe na wenyeviti wa mitaa yote.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa tamko la pamoja,Mussa Mbarouk ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Tanga alisema kwamba uchaguzi ulifanyika kwa njia ya amani japo kulikuwa na dosari ndogondogo ambazo wanaamini zitafanyiwe kazi,

"Mchakato wa Uchaguzi huu ulienda vizuri, tulikuwa tukishirikiana na Serikali ya Mkoa na Jiji, kulikuwa na dosari ndogondogo lakini hata sisi vyama vya siasa tunatakiwa tukae na tuungane ili yale maeneo yote yenye Wagombea wanaokubalika tumuunge mkono" Alisema Mbarouk


Mbarouk alisema kwamba chama chake pamoja na vyama vyote shiriki katika Uchaguzi huo vimesikitishwa na matokeo ya jumla ambapo hakuna chama cha upinzani kilichoshinda kiti hata kimoja.

" Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2019 tulipata walau viti 61,lakini safari hii haijawahi kutokea kiukweli ni lazima tujipange vizuri Uchaguzi Mkuu Ujao mwaka 2025" Alisisitiza Mbarouk

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Chadema Hemed Bakari alisema kuna umuhimu mkubwa kwa vyama vya siasa kuongeza nguvu ya ushawishi kwa wapiga kura,

Kwa upande wake Katibu wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tang Shaban Kalaghe alisema mchakato wa Uchaguzi huo ulienda vizuri na kuwashukuru watu wote waliojiandikisha na kupiga kura,

“Kwa kweli niwapongeze wasimamizi wa uchaguzi huu ulienda vizuri tulikuwa na wagombea kwenye mitaa yote na tumeshinda kwa asilimia 100 lakini pia tunawashukuru wenzetu wa vyama vingine kwakukubali matokeo ni jambo zuri na linaonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa”Alisema

Hata hivyo alisema kwamba uchaguzi huu umeisha na sasa wanakwenda kufanya kazi lakini pia kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.