ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, May 21, 2022

CHUO CHA RUAHA CDTI CHAZINDUA DAWATI LA JINSIA.

 

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na wanafunzi na wadau mbalimbali waliofika chuo cha maendeleo ya jamii Ruaha CDTI wakati wa uzinduzi wa dawati la jinsia.

Mkuu wa chuo cha CDTI Godfrey Mafungu akiongea na wanafunzi na wadau mbalimbali waliofika chuo cha maendeleo ya jamii Ruaha CDTI wakati wa uzinduzi wa dawati la jinsia.
Na Fredy Mgunda,Iringa.

 

 

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amezindua kitengo cha dawati la jinsia katika chuo cha maendeleo ya Jamii Ruaha CDTI kilichoanzishwa rasmi ili kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi chuoni hapo

 

Akizunguma wakati wa uzinduzi kitengo hicho, mkuu wa wilaya ya Iringa alisema kuwa uwepo wa dawati hilo utachangia maendeleo ya usawa wa kijinsia na kupunguza vitendo vya ukatili ikiwemo rushwa ya ngono inayotajwa kukithiri katika vyuo mbalimbali na kuchafua taswira ya elimu ya kati na ya juu nchini.

 

Moyo alisema kuwa uwepo wa kitengo hicho cha dawati la jinsia katika chuo hicho kutachochoe usawa wa haki kwa wanafunzi wa chuo hicho cha Ruaha.

 

Alisema kuwa Iringa kumeibuka wimbi kubwa kwa wanaume kuanza kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wanaume wameanza kutoa malalamiko yao kwenye vyombo husika hivyo wanafunzi wa kiume kutoona aibu kulitumia dawati hilo pindi wanapotendewa ukatili

 

“kitengo hicho siyo kwa ajili ya wanafunzi wa kike pekee, huku akiwahimiza wanafunzi wa kiume kutoona aibu kulitumia dawati hilo pindi wanapotendewa ukatili” alisema Moyo.

 

Kiongozi huyo amepongeza hatua ya uanzishwaji wa dawati hilo Chuoni hapo na kutoa mwito kwa taasisi mbalimbali kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia chuoni hapo.

 

Moyo alizitaka mamlaka nyingine kama vile jeshi la Polisi,TAKUKURU,ofisi ya mashtaka na taasisi zisiszo za kiserikalina za serikali kuendelea kuunga mkono juhudi zilizofanywa na chuo hicho kwa kutoa ushirikiano unatakiwa.

 

Kwa upande wake mratibu wa dawati la jinsia katika chuo hicho cha maendeleo ya jamii CDTI Asha Nyoni alisema kuwa Unzishwaji wa dawati hilo la jinsia umetokana na uwepo wa taarifa za matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya juu na ya kati.

 

Nyoni alisema kuwa maswala ya ukatili wa kijinsia ni mtambuka hivyo ni kuangalia kwa namna gani ya kuweka mfumo rafiki ya kuona namna gani wanakomesha au kuondoa kabisa vitendo vya ukatilii wa kijinsia.

 

 

Alisema kuwa ukatilii wa kijinsia umekuwa ukitokeza maeneo mengi ya elimu ya juu na kati ndio maana wizara ikaamua kuanzisha dawati la ukatilii wa kijinsia.

 

 

 Awali mkuu wa chuo cha CDTI Godfrey Mafungu ameeleza jitihada zilizoanzishwa na chuo hicho katika kuwawezesha wanafunzi kujitambua na kuepukana na vitendo hatarishi


Mafungu alisema kuwa umefika wakati kwa wanafunzi kujitambua kuhusu maswala ya ukatili wa kijinsia kwa ajili ya maendeleo ya elimu wanayoipata chuoni hapo.

 

Alisema kuwa imekuwa vigumu mno kwa vijana wengi kujitambua wawapo chuoni hivyo jambo la kujitambua linatakiwa kupigiwa kelele sana ili vijana waweze kujitambua.

 

Mafungu alisema kuwa ukatili wa kijinsia umekuwa unarudisha nyuma juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo wanafunzi wa chuo wakiwa na elimu ya ukatilii wa kijinsia basi wataifikisha kwa jamii husika juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia.

 

Hatua hii ni utekelezwaji wa maelekezo ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa  wakati akilihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano ambapo alielekeza Taasisi za Umma na Binafsi kuhakikisha zinaweka utaratibu unaofaa wa kutokomeza Ukatili kwa wanawake, wasichana wavulana na watoto.

HALIMA KOPWE MISS TANZANIA , RAIS SAMIA KUJENGA UKUMBI WA KIMATAIFA JIJINI DAR

 


Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Mhe. Rais Samia imedhamiria kuinua kuinua kiwango cha mashindano ya urembo nchini  ikiwa ni pamoja na kujenga ukumbi wa kimataifa  katika jiji la Dar es Salaam.


Akizungumza usiku wa kuamkia leo Mei 21, 2022 kwenye kilele cha mashindano ya kumtafuta  Miss Tanzania 2022 ambapo Halima Kopwe toka Mtwara ametwaa taji hilo, Mhe . Mchengerwa amesema ukumbi huo  licha ya kufanyiwa kazi mbalimbali za Sanaa na burudani pia utatumika kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na shindano la Miss Tanzania.

 "Ukumbi huo unatarajiwa kuongoza kwa ubora na ukubwa barani Afrika ambapo utachukua takribani watu elfu ishirini" amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwashika mkono washindi wote na kufafanua kuwa washiriki wote walioshiriki shindano hili hadi kufika fainali ni washindi.

Amewapongeza waandaji wa shindano hilo kwa uratibu mzuri  ambapo ameongeza kuwa washiriki  wamefanya kazi nzuri ya ubunifu na Sanaa.

Pia amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo Wizara pekee inayowapa furaha na faraja watanzania wengi.

Pia Mhe. Mchengerwa amesema Filamu ya Royal Tour imesaidia kufungua milango na kuitangaza Tanzania  duniani na kuwataka wasanii kutumia fursa hiyo kutengeneza ajira na vipato.

Miss Tanzania kwa mwaka huu; Halima Kopwe amejishindia gari  dogo aina ya Benzi lenye thamani ya shilingi milioni 30 na  fedha taslimu shilingi milioni kumi.


Shindano hilo limefanyika jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na mamia ya washabiki wa urembo.

SERIKALI IMETOA ZAIDI YA BILIONI 3 UKARABATI VYUO VYA SITA VYA WATOTO WENYE ULEMAVU -KATAMBI

 

Naibu Waziri toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi akizungumza jambo Mwenyekiti  wa Watu Wenye ulemavu  toka Korogwe Vijijini Shaban Shekihiyo wakati wa ghafla ya ufunguzi wa chuo cha walemvu
Naibu Waziri toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi akizungumza jambo Mwenyekiti  wa Watu Wenye ulemavu  toka Korogwe Vijijini Shaban Shekihiyo wakati wa ghafla ya ufunguzi wa chuo cha walemvu
Naibu Waziri toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi kulia akicheza mziki na wanafunzi walemavu toka kituo cha YDCP kwenye ghafla ya ufunguzi wa Chuo cha walemavu


NA OSCAR ASSENGA,TANGA
 
SERIKALI ya awamu ya Sita inaoongozwa na Rais Samia Suluhu imetenga zaidi ya Shs bil 3 kwa ajili ya ukarabati wa vyuo Sita vya watoto wenye ulemavu nchini


Kauli hiyo imetolewa Jijini Tanga  na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kazi,vijana,ajira na wenye ulemavu Patrobas Katambi wakati wa ufunguzi wa Chuo cha Ufundi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu

Katambi alisema Serikali inatambua umuhimu wa kundi hilo na ilitoa maelekezo ya kufanyiwa ukarabati wa vyuo hivyo ili kutoa fursa kwa jamii hiyo kupata elimu itakayowasaidia kujifunza ufundi utakao wanufaisha katika maisha yao.


Aidha aliitaja mikoa ambayo ina vyuo hivyo ni pamoja na Daresalaam,Tanga,Tabora,Mtwara,Singida na Mwanza ambapo alisema kuwa kama vyuo hivyo vitatumika vizuri idadi kubwa ya watoto walemavu inaweza kujitegemea na kuingia katika ajira kwa maslahi ya maisha yao na familia zinazowazunguka.
 
Katambi aliongeza kuwa Mh:Rais Samia Suluhu ameziagiza Wizara zote zihakikishe zinatoa ajira kwa asilimia 3 kwa kundi hilo la walemavu ili kuwaondolea dhana ya kuwa wategemezi na watu wasioweza kujiajiri ama kuajiriwa.


"Lazima haki ya elimu,afya na ajira zitekelezwe kwa mujibu wa sheria za Nchi yetu,unafikiri bila ya kuliwezesha kundi hili kielimu na ufundi,utawaajiri wapi,nazima tuwaandae na tunaweza kupata watumishi bora"Alisema Katambi.


Hata hivyo amemuagiza Katibu Tawala Mkoa kuhakikisha wanapata eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho ambapo kitakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi walemavu toka Kanda nzima ya Kaskazini.


Kwa upande wa katibu Tawala Mkoa Tanga Pili Mnyema alisema wapo walemavu elfu tatu ambapo Mkoa inawatambua na Serikali imeweka mazingira rafiki ili kuweza kuwawezesha.


Mnyema alisema kwa mwaka huu wa fedha tayari  Halmashauri imetoa Shs Mil 121 ambayo ni asilimia 2 ya Shs Mil 600 kwa ajili ya kuwawezesha walemavu.
 
Nae Mkuu wa Chuo hicho Joharia Msuya alisema changamoto ya chuo ni pamoja na kuwa na walimu 3 wa kuajiriwa jambo ambalo linazorotesha ufanisi wa majukumu ya kila siku.


Msuya alisema mbali ya walimu na wafanyakazi wasiokuwa walimu pia eneo la chuo hicho ni dogo ungilinganisha na idadi ya wanafunzi inayotakiwq kuhudumiwa ambapo wanatoka mikoa 3.

Thursday, May 19, 2022

KUMBE' BUGANDO INATIBU FISTULA BURE.

 MAADHIMISHO ya Siku ya Kutokomeza Fistula Duniani, Kitaifa nchini Tanzania yatafanyika jijini Mwanza katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikitajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya akinamama wenye changamoto hiyo. Jembe Fm imepata nafasi ya kuzungumza na Dr. Elieza Chibwe ambaye ni Daktari Bigwa wa Magonjwa ya Afya, Uzazi, pia ni Mratibu wa Huduma za Fistula toka Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza, hapa akitanabaisha kuwa matibabu ya Fistula yanatolewa BURE kutoka hospitali hiyo. Tarehe 23 Mei ya kila mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula ya uzazi. Huu ni Mwakani wa tisa tangu tulipoanza kuungana na mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hii. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula kwa mwaka 2022 ni: “Tokemeza Fistula, Wekeza, Imarisha Ubora wa Huduma za Afya na Wezesha Jamii” (End Fistula, Invest in Quality Health Care, Empower Communities) Ujumbe huu unaelekeza kila mtu na serikali kuhakikisha ugonjwa wa Fistula unatokomezwa na wanawake wanaopata matatizo haya hawatakiwi kunyanyasika kwenye jamii zao na wana haki za kupata huduma bora. Serikali kupitia Wizara ya Afya ikishirikiana na wadau wa maendeleo wanatakiwa kuwekeza zaidi kwenye huduma bora za Fistula nchini. Aidha, ujumbe unasisitiza wahudumu wa afya kuzingatia utoaji wa huduma bora za Fistula kwa kuzingatia usawa. Hivyo basi, ni wajibu wetu kuangalia tulipotoka, tulipo na kufikiri namna gani tutalimaliza tatizo la Fistula Tanzania.

Wednesday, May 18, 2022

MABALOZI WA SENSA MWANZA WAPANIA KUIFANYA SENZA 2022 KUWA YA KIHISTORIA

ZAIDI ya vijana 100 mkoani Mwanza, wameunda umoja wa mabalozi wa Sensa wa kujitolea kwaajili ya kusaidia tukio la Sensa lipate matokeo chanya.

Wakitangaza mikakati yao jijini Mwanza Mei 17, 2022 Mwenyekiti wa umoja huo Mansour Jumanne amesema wameguswa na umuhimu wa Sensa, kwani ina faida kubwa kwa maendeleo ya Taifa. Mwenyekiti huyo aliitaka jamii ihamasike na kutoa ushirikiano mkubwa kwa suala la Sensa ili taifa liweze kupata takwimu ya idadi ya watu na kupanga mipango ya maendeleo. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Cahama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana, Boniphace, amesema wamehamasika kwaajili ya umuhimu wake kwa taifa, akisema wanataka kusaidia kusukuma mbele juhudi za serikali kufanikisha kazi hiyo. Umoja huo unaundwa na kada ya vijana tofauti wakiwemo waandishi wa habari, wanafunzi wa vyuo vikuu, wasanii, wanasheria, wakulima, wafanyabiiashara wadogo (machinga), wavuvi, waganga na wauguzi.

SERIKALI KUPITIA UPYA MKATABA WA SONGAS

 


Dodoma. Serikali imesema itapitia upya mkataba wa mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Songas ili kuhakikisha kuwa haitakuwa na mkataba wenye dosari.

Mkataba wa sasa kati ya Serikali na Kampuni ya Songas utaisha muda wake Julai, 2024.

Hayo yamesemwa leo Mei 18,2022 na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maluum Jesca Kishoa.

Kishoa amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha inaingia mkataba mpya usiokuwa na dosari kwa manufaa ya wananchi kwa mwaka 2024.

Akijibu swali hilo Byabato amesema kuwa Serikali na Songas watakaa na kujadili mkataba mpya.

“Baadaye Serikali itajadili mkataba mpya na iwapo pande zote zitakubaliana, mkataba mpya wenye tija kwa Taifa na usio kuwa na dosari utasainiwa,”amesema

Amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) imeunda timu ya kupitia masuala ya msingi ya kuzingatiwa kwenye mkataba mpya kwa ajili ya maslahi kwa Taifa.

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya amehoji ni lini Serikali itapitia mikataba yote ili isipate hasara ikiwemo mkataba wa bwawa la uzalishaji umeme la Mwalimu Nyerere.

Akijibu swali hilo, Byabato amesema kwa niaba ya Serikali anachukua mawazo na maoni yaliyotolewa na wataendelea kushirikiana ya kufikia mikataba yenye tija kwa watu wote.

“ile ambayo imekwisha tutahakikisha tunafanya mikataba bora zaidi kwa nyakati zilizopo na ile inayoendelea tutaangalia namna ya kuifanya vizuri zaidi kwa manufaa ya wote,”amesema.

Tuesday, May 17, 2022

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUFUNGUA MAONESHO YA SABA YA WIKI YA UTAFITI NA UBUNIFU - UDSM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kufungua Maonesho ya Saba ya wiki ya Utafiti na Ubunifu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Akizungumza na Wanahabari jijini Dar es Salaam, Naibu Makamu Mkuu wa wa Chuo (Utafiti) UDSM, Profesa Bernadetha Killian amewaalika watu wote kuweza kuhudhuria maonesho hayo ya siku mbili ambayo yatakuwa ya kipekee kwa mwaka huu.

Maonesho ya Saba ya Wiki Ya Utafiti na Ubunifu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam yatakayofanyika rasmi Tarehe 24 hadi 26 Mei 2022, Katika Maktaba Mpya Ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Profesa Killian amesema kuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kimejipanga vyema kufanya maonyesho hayo kuwa ya kipekee na mwaka 2022 wanaadhimisha miaka saba tokea kuanzishwa kwa maonesho hayo.

RAIS SAMIA AMETOA BILIONI 500 UNUNUZI WA VIFAA VYA KUHUDUMIA MIZIGO BANDARI YA DAR KUONGEZA UFANISI

 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) Erick Hamisi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wa bandari kilichofanyika leo Jijini Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza wakati wa kikao hicho
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Captain Mussa Mandia akizungumza wakati wa kikao hicho
 
Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini (TRC) Masanja Kadogosa akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa meli nchini (TASAC) Kaimu Abdi Mkeyenge akiuzungumza mara baada ya kumalizika kikao hicho.

Sehemu ya Washiriki kwenye kikao hicho
Wadau wa kikao hicho

NA OSCAR ASSENGA,TANGA

SERIKALI ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imetoa sh.Bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo ili kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) Erick Hamisi wakati wa mkutano wa wadau wa bandari unaofanyika Jijini Tanga ambapo alisema uwekezaji huo unaokwenda kufanyika katika bandari hiyo ni mkubwa ambao utafungua fursa kwa nchi na maziwa makuu kwa matumizi ya bandari hiyo.

Alisema kuwa kuna mradi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwara ambapo watapeleka mizigo ya nje katika nchi za Maziwa makuu (Transit) baada ya serikali kuwekeza fedha hizo ambapo pia zitatumika kununulia vifaa ili kuwezesha ufanisi huo.

“Tutakuwa na ujenzi wa bandari ya nchi kavu ya kwara, isitoshe serikali ya awamu ya sita imewekeza kiasi cha shilingi Bilioni 500 kwa mara moja uwekezaji ambao hauajwahi kufanyika kwa mara moja hii inaonesha mhe Rais amedhamiria kuifanya bandari yetu ifanye kazi kwa ufanisi,” alisema Hamissi.

Mkurugenzi huyo alisema uwekezaji unaofanyika kwasasa katika miundombinu ya reli, Bandari na kwenye maziwa inaoensha kwamba nchi zote zinazotuzunguka hazitakuwa na chaguo lingine bali kutumia bandari ya Dar es salaam karibu watu milioni 700 za nchi hizo.

Mkurugenzi huyo alisema mkutano unaofanyika mjini Tanga kuwakutanisha wadau wa bandari haujawahi kufanyika hivyo utatoa fursa kwa wadau kujadili vikwazo na fursa zilizopo katika kuongeza ufanisi zaidi ya bandari zilizopo hapa nchini.

Awali akiungumza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa meli nchini (TASAC) Kaimu Abdi Mkeyenge alisema kwamba wadau wamekutanishwa pamoja ili kutazama changamoto wanazokutana nazo kasha waweze kuzipatia majawabu ya mapendekezo ya kuyafanyia kazi kwa pamoja.

Alisema warsha hiyo itatazama changamoto mbalimbali ambazo zinaipata bandari ya Dare s salaam na fursa zilizopo na kutoa mapendekezo ya kuboresha ikiwemo bandari ya Tanga.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini (TRC) Masanja Kadogosa, alisema mkutano huo wa wadau utasaidia kuongeza fursa za usafirishaji mizigo utakaofanywa na shirika hilo ambalo limefanya ukarabati wa reli yake ili kuweza kuhudumai nchi za maziwa makuu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wasafirishaji nchini (TAT), Ashraf Khan alisema wao kama wasafirishaji wanaiomba bandari iwasaidie maroli yao yanayobeba mizigo bandarini yaweze kutoka kwa wepesi ili meli zinazoingia bandarini zichukue muda mfupi kukaa bandarini.

Awali akifungua warsa hiyo ya siku mbili Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima, aliwataka wajumbe wa mkutano huo ikiwemo uongozi wa Bandari kutazama changamoto hizo na kuzipatia majawabu ili bandari ya Dar es salaam iweze kushindana na bandari nyingine zilzopo katika ukanda huu.

Alisema wanapofikiria kuondoa changamoto katika bandari ya Dar es salaam wafuate maelekezo yanayotolewa na rais ili waweze kuongeza tija lakini pia kushindana na bandari za Beira nchini Msumbiji pamoja na ile ya Mombasa nchini Kenya.

“Kuweni mfano wa kile ambacho Rais wetu anachohubiri kuitaka bandari ifanye kazi kwa ufanisi, tusiwe watu wa kuiangusha bandari tufanye ifanye vizuri kushindana na bandari nyingine,” alisema Mkuu wa mkoa huyo.

TAFIRI NA OMAN KUFANYA UTAFITI WA SAMAKI BAHARI YA HINDI

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye mazungumzo ya awali na uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA), ukiwa umeambatana na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi katika ofisi za Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutia saini hati ya makubaliano ya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. (12.05.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini hati ya makubaliano ya utafiti katika Sekta ya Uvuvi kwa Ukanda wa Bahari ya Hindi baina ya Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ana matumaini na uhakika kazi itafanyika vizuri na kuleta matokeo ambayo nchi ina matarajio makubwa katika kukuza Sekta ya Uvuvi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama wa pili kutoka wa kulia) na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania (aliyesimama wa tatu kutoka kushoto) Dkt. Salim Al-Harbi, wakishuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano baina ya Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) katika ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi, wakibadilishana nyaraka mara baada ya utiaji saini hati ya makubaliano baina ya OIA na TAFIRI kwa ajili ya kufanya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari wa Hindi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi na watafiti kutoka Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, mara baada ya hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi baina ya TAFIRI na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA). (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Na. Edward Kondela

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetia saini hati ya makubaliano na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) ili kufanya utafiti utakaosaidia kutathimini kiwango cha samaki kinachoweza kupatikana kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi hivyo kusaidia ongezeko la wawekezaji katika Sekta ya Uvuvi.

Utiliaji saini wa makubaliano hayo yamefanyika leo (12.05.2022) jijini Dar es salaam baina ya Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei na Mkurugenzi Mtendaji wa OIA katika Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi, ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki mara baada ya kushuhudia makubaliano hayo amesema yana lengo la kutathimini kiwango cha samaki kinachoweza kupatikana katika eneo la bahari na itakuwa ni mara ya kwanza kufanyika hapa nchini.

Waziri Ndaki amefafanua kuwa kazi ya kutathimini kiwango cha samaki kilichopo katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ina gharama kubwa na kwamba inahitaji fedha nyingi na rasilimali zingine ili kuweza kufanya kazi yenye matokeo mazuri.

“Tuna matumaini na uhakika kazi itafanyika vizuri na kuleta matokeo ambayo sisi kama nchi tuna matarajio makubwa sana.” Amesema Mhe. Ndaki.

Waziri Ndaki ameongeza kuwa bado sekta ya uvuvi inachangia pato dogo kwa taifa hivyo utafiti huo utasaidia nchi kuwa na mipango ya uhakika juu ya uvunaji wa rasilimali za uvuvi na kushawishi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei akafafanua juu ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kubainisha kuwa utafiti huo utafanyika kwa kushirikisha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI) ili kutimiza malengo ya sekta ya uvuvi Tanzania Bara na Visiwani.

Dkt. Kimirei amesema makubaliano hayo yatawezesha muda wowote kuwasili kwa meli ya kufanya utafiti ili kuiwezesha nchi kupata takwimu ya aina, wingi na mtawanyiko wa samaki katika ukanda wa bahari ili nchi iweze kupata taarifa sahihi ya uwepo wa samaki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi amesema utafiti huo utasaidia kuongeza thamani ya biashara katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kwa Tanzania na kwamba wanatarajia huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano baina ya Tanzania na Oman katika shughuli mbalimbali zinazohusu Sekta ya Uvuvi.

Zoezi la utiaji saini wa hati ya makubalino baina ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) kwa ajili ya kufanya utafiti wa samaki katika ukanda wa Bahari ya Hindi limeshuhudiwa pia na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi.