ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 25, 2022

WANAOKWENDA HIJJA KUCHANJWA TENA UVIKO-19

 


Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema waliochanjwa chanjo ya Uviko-19 mwaka mmoja au miaka miwili iliyopita hawataruhusiwa kwenda hijja hadi watakaporudia kuchanja chanjo hiyo.


Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Juni 25,2022 na Mkurugenzi wa Hija wa Bakwata, Haidary Kambwili, katika semina ya mahujaji inayofanyika ofisi za Makao Makuu ya Bakwata jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya wahusika kwenda nchini Saudi Arabia kuhiji.


Kwenda kuhiji katika mji Makka uliopo nchini Saudi Arabia kwa mwenye uwezo ni moja kati ya nguzo tano za uislamu.


Kambwili amesema miongoni mwa masharti wanayopaswa kuyafuata wanaotaka kwenda hija ni kuchanja saa 72 kabla ya kuanza safari.


Kambwili amesema utaratibu huo wameelekezwa na nchi ya Saud Arabia ikiwa ni mkakati endelevu wa nchi hiyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

WALICHOKIFANYA MDEE, WENZAKE 18 BAADA YA KESI YAO KUTUPWA.


halimadeepic
Dar es Salaam. Siku moja baada ya maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama  wa Chadema kutupwa na Mahakama Kuu, wamerejea tena  mahakamani kupigania uanachama na ubunge wao.

Awali, Mdee na wenzake walifungua maombi Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiomba ridhaa ya mahakama kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wao.

Hata hivyo maombi hayo yalitupiliwa mbali Jumatano Juni 22, 2022 na Jaji John Mgetta kutokana na kasoro za kisheria, baada ya kukubaliana na hoja mbili kati ya sita za pingamizi zilzioibuliwa na Chadema kupitia jopo la mawakili wake lililoongozwa na wakili Peter Kibatala.

Lakini, Alhamisi Juni 23, 2022 walirudi mahakamani hapo na kufungua upya maombi hayo chini ya hati ya dharura  baada ya kurekebisha kasoro zilizoainishwa na mahakama.

Mawakili wao, Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya na Edson Kilatu wameieleza Mwananchi Digital leo  Ijumaa Juni 24,2022 kuwa shauri hilo jipya la ridhaa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama (kupinga uamuzi wa Chasema kuwavua uanachama, limesajiliwa kama shauri namba 27 la mwaka 2022.

Wasema kuwa sambamba na shauri hilo la msingi (maombi ya ridhaa) pia wamefungua shauri la maombi wakiomba amri ya mahakama kudumisha hali ilivyo kwa sasa (kulinda hadhi ya ubunge wa wateja wao), ambalo limepewa usajili wa namba 16 la mwaka 2022.


Mawakili hao wamelieleza Mwananchi Digital  kuwa wamefanikiwa kufungua tena shauri hilo mapema kiasi hicho kwa kuwa walikuwa wamejiandaa na kuwaandaaa wateja wao kwa uamuzi wowote wa mahakama.

“Tulikuwa tumejiandaa kwa uamuzi wowote na tulikuwa tumewaandaa wateja wetu kwamba lolote linaweza kutokea hivyo wanapaswa kuwa mahali pamoja ili mahakama vyovyote ambavyo mahakama ingeamuru tuweze kufanya marekebisho," amesema wakili Panya.

Amefafanua kwamba baada ya kutoka mahakamani tu kusikiliza uamuzi walirejea ofisini wakafanya marekebisho ya kasoro zilizoainishwa na mahakama na kwamba baada ya saa tatu walikuwa wamekamilisha kisha akasafiri usiku huo kuwafuata wateja wake kwa ajili ya kusaini nyaraka hizo.

“Baada ya wateja wetu kusaini, jana asubuhi tuka-file (wakawasilisha nyaraka mahakamani) na mpaka saa moja tulikuwa tumaliza ku-upload (kupakia nyaraka) maana siku hizi tuna-file online (kufungua kupitia mtandao)," amesema Panya na kuongeza,

“Mahakama baada ya kuzifanya nyaraka zetu assessment tulikwenda tukalipia kisha tukapewa namba. Kwa hiyo mpaka saa mbili tulikuwa tumeshapata na namna na tukawajulisha wateja wetu wamwandikie Spika kumjulisha kuwa tayari wameshafungua tena shauri na namba ni hiyo.”

Wakili Mwamanenge amesema licha ya kukamilisha mapema kufungua shauri hilo  hawakutaka kuweka wazi wakisubiri kwanza wapate hati ya wito kwa wajibu maombi ambayo ndio itaonesha tarehe ya kutajwa na hata Jaji atakayelisikiliza.

Amesema kuwa mpaka jioni bado walikuwa hawajapata hati hiyo ya wito na kwamba wanaendelea kuisubiri kwa ajili ya kuwapelekea Chadema.

Kina Mdee wamekwama aisee!

Wakili Kilatu amesema  ingawa walikuwa wanasoma taarifa nyingi na zisizo sahihi kwenye mitandao kuhusu uamuzi na hatima ya wateja wao lakini waliamua kutulia tu kwa kuwa walikuwa wanajua wanachokifanya.
CHANZO: MWANANCHI.

MKANDARASI APEWA MIEZI MITANO KUKAMILISHA MRADI WA BWAWA KATAVI


  Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wapili kushoto) alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mlele. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Philbert Sanga.

 Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Philbert Sanga akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) wilayani humo.


Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akizungumza wakati wa ziara yake Wilayani Mlele. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Philbert Sanga na kulia ni Meneja RUWASA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Peter Ngunula.


Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) akimsikiliza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Gilbert Isack (kushoto) wakati wa ziara yake kwenye mradi wa ujenzi wa Bwawa la Maji la Nsekwa.


  Muonekano wa Bwawa la Maji la Nsekwa Wilayani Mlele

Na Mohamed Saif

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amemuelekeza Mkandarasi anayejenga mradi wa Bwawa la maji la Nsekwa Wilayani Mlele kampuni ya Hematec Investment Ltd ya Dar es Salaam awe amekamilisha ujenzi wake ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu. 

 

Mhandisi Sanga ametoa maelekezo hayo Wilayani Mlele Mkoani Katavi Juni 23, 2022 alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa hilo linalotarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 68,426 wa vijiji 16 kutoka Kata za Inyonga, Utende, Nsekwa, Ilela na Kamsisi.

 

Awali akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Philbert Sanga alimuelezea Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Sanga kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa bwawa pasi na sababu za msingi.

 

"Ninawapongeza sana Wizara ya Maji, kazi mnayofanya ni kubwa na sote ni mashahidi tunakiona mnachokitekeleza. Kabla ya ziara yako alitutembelea Mheshimiwa Waziri na alituahidi kwamba utakuja kufuatilia ujenzi wa miradi wilayani hapa na hili limetimia, hii inadhihirisha uchapakazi wenu," alisema Mhe. Mkuu wa Wilaya.

 

Akiwa katika eneo la mradi ili kushuhudia kinachoendelea, Mhandisi Sanga hakuridhishwa na hali ya utekelezwaji wake hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo umechukua muda mrefu kukamilika licha ya Mkandarasi kulipwa fedha zake kwa wakati.

 

"Kazi hairidhishi, nilitarajia kukuta Mkandarasi anaendelea na kazi lakini bahati mbaya sana hakuna kinachoendelea, tumeleta fedha za kutosha hapa sijaridhika na ninachokishuhudia," alisema Mhandisi Sanga.

 

Alisema Wizara ilikwamua miradi mingi ambayo ilikua ikisuasua maarufu kama miradi chechefu na hayupo tayari kushuhudia hali hiyo ikijirudia na kwamba anachohitaji ni kuona kazi ikiendelea kwa kasi ili kuwaondolea adha wananchi.

 

Katibu Mkuu Sanga alisisitiza kuwa Wizara ya Maji imekwishajipambanua mapema kuwa haitoendekeza wakandarasi wababaishaji kama ambavyo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyoelekeza.

 

"Mhesimiwa Rais Samia alikwishatupatia maelekezo na mara nyingi Waziri wangu amekuwa akiyarejea maelekezo haya kwa wataalam wetu na wakandarasi kila anapotembelea miradi; tunachokifanya sisi ni utekelezaji. Hatuwezi kurudi huko tulikotoka, kama suala ni fedha semeni, hatupo tayari kudanganywa kwa uzembe wa mkandarasi," alisisitiza Mhandisi Sanga.

 

Mhandisi Sanga alisema baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakijificha kwenye kisingizio cha fedha jambo ambalo alisema halina ukweli wowote kwani kwa utaratibu wa sasa wa Serikali kupitia Wizara ya Maji malipo yanatoka kwa wakati pindi Mkandarasi anapowasilisha hati ya madai.

 

Alimuelekeza mkandarasi kuhakikisha bwawa hilo linakamilika ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu ili msimu wa mvua unapochanganya ukute tayari bwawa limekamilika na alisisitiza kuwa ikitokea mkandarasi akachelewesha basi akatwe malipo yake.

 

"Maelekezo ya Wizara kwa Mkandarasi ni kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya Mwezi Desemba mwaka huu, mvua zinapoanza bwawa linakuwa liko tayari," alielekeza Mhandisi Sanga.

 

Naye mkandarasi kupitia mwakilishi wake, Elimring Molth alimuahidi Mhandisi Sanga kuwa bwawa hilo litakamilika kama alivyoelekeza na kwamba ifikapo Jumamosi ya tarehe 25 mwezi huu, timu ya wataalam wake itakuwa imewasili eneo la mradi na kuendelea na kazi.

 

Mhandisi Sanga aliiomba Kamati ya Ulinzi na Usalama kufika hapo siku hiyo ya Jumamosi ili kujiridhisha kama kazi inaendelea.

 

Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Gilbert Isack alisema mradi huo wa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2 ulianza kutekelezwa mwaka 2018 na ulipaswa kukamilika mwaka 2019.

 

Mhandisi Isack alisema kukamilika kwa mradi huo kutatosheleza mahitaji ya wananchi wa vijiji hivyo 16 kwani mahitaji kwa sasa ni takribani lita milioni 500 kwa mwaka wakati bwawa hilo uwezo wake ni kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 2 kwa mwaka.

IGP SIRRO AZINDUA OFISI USALAMA BARABARANI ILIYOJENGWA KWA ZAIDI YA SH MILIONI 100 IRINGA.

 

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro akizindua ofisi mpya ya kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa iliyojengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 100 kwa msaada wa kampuni ya Ivori Iringa.


Na Fredy Mgunda,Iringa.

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro amezindua ofisi mpya ya kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa katika kituo kikuu cha Polisi cha mjini.

 

Wakati ofisi ya kikosi cha usalama barabarani imejengwa kwa msaada wa kampuni ya Ivori Iringa ambayo inazalisha bidhaa za Ivori.

 

Akizindua jingo hilo IGP Sirro alimshukuru mkurugenzi wa kampuni yaIvori kwa michango wake mkubwa akisema inasaidia kuliongezea jeshi hilo ufanisi katika utendaji wake kazi.

 

“Nawashukuru Ivori Iringa kwa misaada yao kwa jeshi la Polisi. Wafanyabiashara wengine acheni ubahiri, kama hakuna ulinzi, hamuwezi kulala kwa raha kwani mtakuwa na hofu kubwa ya kuibiwa mali zenu. Nawaomba mjitokeze kulichangia jeshi la Polisi ili lifanye kazi yake sawasawa,” alisema.

 

Alisema Jeshi la Polisi ni mali ya wananchi na kwa muktadha huo wanatakiwa kulipa ushirikiano ukiwemo wa kusaidia kuboresha mazingira ya utendaji wake kazi.

 

Alizungumzia pia ulinzi shirikishi akisema Jeshi la Polisi haliwezi kuifanya kazi ya kulinda wananchi na mali zao pekee yake.

 

“Halmashauri zitunge sheria za ulinzi shirikishi ili katika maeneo yote kuwepo na vikundi vya kijamii vinavyofanya ulinzi mitaani kwa gharama za wananchi wenyewe, " alisema na kuwataka hata wale wananchi wenye walinzi wao binafsi au silaha kuchangia ulinzi shirikishi maarufu kama polisi jamii.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ivori Iringa, Suhail Esmail Thakore alisema waliamua kujenga jengo hilo la usalama barabarani kwa kuwa wanatambua kazi kubwa inayofanywa na kikosi hicho na jeshi la Polisi kwa ujumla wake katika kulinda wananchi na mali zao.

 

Takore alisema wameamua kujenga jengo hilo la usalama barabarani kwa kuwa wanatambua kazi kubwa inayofanywa na jeshi la polisi kwa ujumla.

 

“Tutaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kadri tutakavyopata fursa. Sisi ni wadau na tunaamini tunatakiwa kuwa sehemu ya usalama wa Taifa hili,”alisema.

 

Thakore alisema wataendelea kushirikiana na jeshi la Polisi katika nyanja mbalimbali ili kurahisisha utendaji kazi wake.

 

Aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kukabiliana na makosa ya usalama barabarani, na uharifu vikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia na ubakaji wa watoto.

 

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi alimueleza IGP Sirro kwamba vitendo vya uharifu mkoani Iringa vimeendelea kupungua kupitia mikakati mikubwa waliyonayo ya kukabiliana na vitendo hivyo.