ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 25, 2022

WALICHOKIFANYA MDEE, WENZAKE 18 BAADA YA KESI YAO KUTUPWA.


halimadeepic
Dar es Salaam. Siku moja baada ya maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama  wa Chadema kutupwa na Mahakama Kuu, wamerejea tena  mahakamani kupigania uanachama na ubunge wao.

Awali, Mdee na wenzake walifungua maombi Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiomba ridhaa ya mahakama kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wao.

Hata hivyo maombi hayo yalitupiliwa mbali Jumatano Juni 22, 2022 na Jaji John Mgetta kutokana na kasoro za kisheria, baada ya kukubaliana na hoja mbili kati ya sita za pingamizi zilzioibuliwa na Chadema kupitia jopo la mawakili wake lililoongozwa na wakili Peter Kibatala.

Lakini, Alhamisi Juni 23, 2022 walirudi mahakamani hapo na kufungua upya maombi hayo chini ya hati ya dharura  baada ya kurekebisha kasoro zilizoainishwa na mahakama.

Mawakili wao, Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya na Edson Kilatu wameieleza Mwananchi Digital leo  Ijumaa Juni 24,2022 kuwa shauri hilo jipya la ridhaa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama (kupinga uamuzi wa Chasema kuwavua uanachama, limesajiliwa kama shauri namba 27 la mwaka 2022.

Wasema kuwa sambamba na shauri hilo la msingi (maombi ya ridhaa) pia wamefungua shauri la maombi wakiomba amri ya mahakama kudumisha hali ilivyo kwa sasa (kulinda hadhi ya ubunge wa wateja wao), ambalo limepewa usajili wa namba 16 la mwaka 2022.


Mawakili hao wamelieleza Mwananchi Digital  kuwa wamefanikiwa kufungua tena shauri hilo mapema kiasi hicho kwa kuwa walikuwa wamejiandaa na kuwaandaaa wateja wao kwa uamuzi wowote wa mahakama.

“Tulikuwa tumejiandaa kwa uamuzi wowote na tulikuwa tumewaandaa wateja wetu kwamba lolote linaweza kutokea hivyo wanapaswa kuwa mahali pamoja ili mahakama vyovyote ambavyo mahakama ingeamuru tuweze kufanya marekebisho," amesema wakili Panya.

Amefafanua kwamba baada ya kutoka mahakamani tu kusikiliza uamuzi walirejea ofisini wakafanya marekebisho ya kasoro zilizoainishwa na mahakama na kwamba baada ya saa tatu walikuwa wamekamilisha kisha akasafiri usiku huo kuwafuata wateja wake kwa ajili ya kusaini nyaraka hizo.

“Baada ya wateja wetu kusaini, jana asubuhi tuka-file (wakawasilisha nyaraka mahakamani) na mpaka saa moja tulikuwa tumaliza ku-upload (kupakia nyaraka) maana siku hizi tuna-file online (kufungua kupitia mtandao)," amesema Panya na kuongeza,

“Mahakama baada ya kuzifanya nyaraka zetu assessment tulikwenda tukalipia kisha tukapewa namba. Kwa hiyo mpaka saa mbili tulikuwa tumeshapata na namna na tukawajulisha wateja wetu wamwandikie Spika kumjulisha kuwa tayari wameshafungua tena shauri na namba ni hiyo.”

Wakili Mwamanenge amesema licha ya kukamilisha mapema kufungua shauri hilo  hawakutaka kuweka wazi wakisubiri kwanza wapate hati ya wito kwa wajibu maombi ambayo ndio itaonesha tarehe ya kutajwa na hata Jaji atakayelisikiliza.

Amesema kuwa mpaka jioni bado walikuwa hawajapata hati hiyo ya wito na kwamba wanaendelea kuisubiri kwa ajili ya kuwapelekea Chadema.

Kina Mdee wamekwama aisee!

Wakili Kilatu amesema  ingawa walikuwa wanasoma taarifa nyingi na zisizo sahihi kwenye mitandao kuhusu uamuzi na hatima ya wateja wao lakini waliamua kutulia tu kwa kuwa walikuwa wanajua wanachokifanya.
CHANZO: MWANANCHI.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.