Raia wawili wa Uingereza, Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18) waliomwagiwa tindikali visiwani Zanzibar juzi na kulazwa Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, wamesafirishwa kwenda kwao kwa matibabu zaidi.
Aidha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza zawadi ya Sh10 milioni kwa mtu yeyote atakayesaidia kukamatwa wahalifu waliowamwagia tindikali raia hao wa Uingereza. Akizungumza na wanahabari mjini Zanzibar, Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii wa SMZ, Said Ali Mbarouk alisema wanafanya hilo kwa lengo la kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi ikiwa pia moja ya njia za kukomesha matendo hayo.
Taarifa zilizopatikana jana zilidai kuwa raia hao ambao walidhurika katika maeneo ya kifuani, usoni na mikononi baada ya kumwagiwa tindikali na vijana waliokuwa wakiendesha pikipiki, maeneo ya Shangani Zanzibar, walichukuliwa hospitalini hapo juzi saa 1 usiku.
Raia wa Uingereza waliomwagiwa tindikali wakiwa kisiwani Zanzibar |
Habari za uhakika kutoka Hospitali ya Aga Khan, zilithibitisha kuwa Katie na Kirstie walichukuliwa na kusafirishwa kwenda Uingereza kwa matibabu zaidi. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally alisema kuwa wizara hiyo haikuhusika kuwasafirisha na kwamba amepata taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa wameondoka nchini.
“Nilisikia tu kwenye vyombo vya habari kwamba wamekwenda kutibiwa nje, sisi hatukuhusika hiyo ni mipango yao,” alisema Ally.
Hata hivyo, gazeti la The Telegraph la Uingereza jana liliripoti kuwa raia hao walikuwa njiani kuelekea nchini humo na kwamba wazazi na ndugu wa vijana hao walipokea kwa mshituko taarifa za tukio hilo.
Taarifa iliyotolewa kwa niaba ya familia hizo ilisema kuwa wamesikitishwa na kilichotokea wakikitaja kitendo hicho kuwa ni tukio lisilotamkika kuwatokea mabinti zao waliokwenda Zanzibar kwa nia njema.