THT kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, tarehe
31/1/2015, Escape 1
·
Kufungua kampuni ya
ushonaji na ubunifu wa mavazi
Kituo cha kuzalisha
na kukuza vipaji, Tanzania House of Talent, kinatarajia kuadhimisha miaka kumi
toka kuanzishwa kwake hapo tarehe 31/1/2015 Escape 1 jijini Dar es Salaam.
THT ilianzishwa
mwishoni mwa mwaka 2005 kwa lengo la kuwasaidia vijana wenye vipaji, lakini
wasio na uwezo wa kujiendeleza wenyewe, kwenye sekta ya sanaa hapa nchini, na
toka wakati huo kituo kimekuwa na mafanikio makubwa na mchango wa pekee kwenye
kukuza sanaa ya muziki nchini.
Akizungumza wakati
wa kuzindua maadhimisho hayo ambayo yatakuwa kwa mwaka mzima, Meneja Mkuu wa
Kituo hicho, Mwita Mwaikenda alisema ni heshima kubwa kuweza kusherehekea miaka
kumi toka imeanzishwa kwani wameweza kufanikisha mambo mengi makubwa.
‘Tulianzisha kituo
hiki miaka kumi iliyopita kwa hakika tukiwa hatuna chochote zaidi ya imani yetu
kwenye vipaji vya vijana, na tulianza hatuna hata sehemu ya maana, lakini leo
miaka kumi baadaye vijana zaidi ya 3000 wamefaidika na kituo hiki kwa namna
moja au nyingine na wameweza kumudu maisha yao na familia zao kutokea kuwa
watoto wa mitaani’ alisema Mwita.
THT ikiwa
imeanzishwa kama kituo cha kusaidia watoto wa mtaani wenye vipaji, imeweza kukua
kwa kipindi cha miaka kumi, na sasa sio tu inazalisha na kukuza vipaji bali
imekuwa ikitoa huduma zote kuanzia kuratibu matamasha, kuandaa mpangilio wa
burudani, kutengeneza matangazo ya radio na televisheni pamoja na makala na
vipindi vya televisheni.
‘THT imeweza
kuratibu burudani ya matamasha mbalimbali kama FIESTA, Mkutano wa Smart
Partnership, Sensa ya mwaka 2013, Sherehe za miaka 50 ya Muungano pamoja na
mikutano na matamasha kadha wa kadha’ alisema Meneja Masoko wa THT, Michael
Nkya.
THT imeendelea kukua
kwa kuweza kuanzisha studio yake ambayo imeweza kurekodi matangazo, nyimbo za
wasanii wote wa THT pamoja na wengine wengi kama Mdogomdogo na Number One Remix
ya Diamond, Me and You ya Ommy Dimpoz, Prokoto ya Victoria Kimani na nyingine
nyingi.
Kwa sasa THT
inatengeneza vipindi mbalimbali vya televisheni kama 69 Records, na vingine
vingi vinavyorushwa chaneli za nje huku pia ikijivunia kuwa na maktaba ya
nyimbo kubwa zaidi nchini.
‘Shukrani zetu za
dhati kwa kweli ni kwa serikali, hasa hasa Mheshimiwa Rais Kikwete, ambaye toka
mwanzo alikubali wazo na akaamini mziki unahitaji elimu ya peke yake, lakini
pia makampuni mbalimbali ambayo wamekuwa wakitupa kazi pamoja na vyombo vyote
vya habari kwa kutuunga mkono siku zote’ alisema Bwana Nkya.
Akielezea kuhusu
mwelekeo wa kituo baada ya miaka kumi, Mwita alisema anaamini kituo kimefanya
kazi yake tayari kwa kuweza kuchagiza sanaa ya muziki nchini, na sasa ni wakati
wa kuendelea kusaidia wadau au vituo vingine kama Mkubwa na Wanawe kufika THT
ilipofika.
‘Kimsingi mwaka huu
ndio mwaka wa mwisho kuendela kupokea wanafunzi wapya wa kuimba, na mpango wetu
ni kuendelea kukuza kituo kwa kuanzisha kampuni ya ushonaji na ubunifu wa nguo
kwa kutumia kitenge ambao tunaamini utatoa ajira kwa vijana wengi zaidi hapa
nchini’ alisisitiza Mwita.
Kampuni ya ubunifu
na ushonaji kwa kutumia vitenge, tayari ishaanza mchakato wake kwa kuhusisha
wadau wa biashara ya vitenge, na mbunifu mahiri Ally Remtullah, mwanamitindo
Flaviana Matata wakiwa ndio walezi na wasimamizi wa mradi ambao utaanza na
wabunifu wanaochipukia Neyonce pamoja na Adam Mchovu.
‘Kwa kuanza mradi
utapeleka wabunifu nchini China ili wakajifunze zaidi juu ya ubunifu na
kuongeza ubora kwenye kazi zao, wakirudi tunaamini wataweza kuwafundisha vijana
wengi zaidi, na kutimiza lengo letu la kuwasaidia vijana kujiajiri’ alimaliza
Mwita.