Mkuu wa wilaya ya Bariadi Bw. Erasto Sima akisoma Hotuba katika makabidhiano ya msaada wa vitabu vya masomo ya sayansi kwa shule ya sekondari Bariadi uliotolewa na kampuni ya Airtel Tanzania |
AIRTEL YATOA VITABU VYA SAYANSI SHULE YA SEKONDARI BARIADI SIMIYU.
· Airtel yaahidi kukabidhi vitabu mikoa ya Kilimanjaro na Arusha mwezi huu
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imepiga jeki jitihada za serikali za kuhamasisha masomo ya sayansi kwa kutoa msaada wa vitabu vya sayansi kwa shule ya sekondari ya Bariadi iliyopo Mkoani Simiyu.
Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 6 unahusisha vitabu vya fizikia, hisabati, baiolojia na kemia kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma masomo hayo shuleni hapo.
Akipokea msaada huo mkuu wa wilaya ya Bariadi Bw. Erasto Sima amesema shule nyingi wilayani humo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitabu vya masomo ya sayansi licha ya kwamba kuna uhaba pia wa walimu wa masomo hayo.
“Ni kweli kwamba uhaba wa vitabu unakwamisha kwa kiasi kikubwa wanafunzi kujifunza kwa ufasaha masomo ya Sayansi wilayani Bariadi hali inayorudisha nyuma ukuaji wa elimu ya sayansi wilayani hapa”. Alisema Bwana Sima.
“uhaba wa vitabu ni moja ya changamoto, lakini uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi ni kikwazo kikubwa kwa utoaji wa elimu ya sayansi kwa wanafunzi wetu hapa Bariadi” aliongeza Bwana Sima.
Aidha Bw. Sima ameishukuru kampuni ya simu ya airtel kwa kuona umuhimu wa kuboresha masomo ya sayansi ambayo ufaulu wake umekuwa mdogo hali ambayo inayotoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa umakini zaidi.
“Msaada huu utaongeza hamasa kwa wanafunzi wetu kujifunza masomo ya sayansi hivyo tunawashukuru sana Airtel kwa kuona umuhimu wa kusaidia shule hii na hasa vitabu vya sayansi” alimalizia Bwana Sima.
Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari Bariadi Bw. Pawa Lutema akipokea vitabu hivyo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utatuzi wa changamoto ya vitabu vya sayansi na kisha kuahidi kuvitunza ili viwe msaada kwa wanafunzi watakaosoma shuleni hapo.
Awali meneja wa Airtel Mkoani Simiyu Bw. Ezekiel Nungwi akikabidhi msaada huo wa vitabu amesema kuwa kampuni yake inaendelea tena katika mwaka huu wa 2015 na mpango wake wa kutoa msaada wa vitabu kwenye shule mbalimbali nchini kwa lengo la kusaidia ukuaji wa elimu nchini.
Msaada huo wa vitabu vya masomo ya hisabati,kemia,fizikia na Bailojia utasaidia kupunguza uhaba wa vitabu vya sayansi kwenye shule hiyo.
Airtel pia kupitia mfuko wake huo wa Airtel Shule yetu mwezi huu imejipanga kukabidhi vitabu katika mikoa mingine miwili ikiwemo Kilimanjaro na Arusha ambapo inatarajiwa kuzifikia zaidi ya shule zingine sita.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.