Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akipata ufafanuzi kutoka kwa Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Y&P Architect inayosimamia Mradi wa Ujenzi wa Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kituo cha Dar es Salaam, Anna Shayo alipotembelea mradi huo Kunduchi Dar es Salaam. Picha na Mpiga Picha Wetu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiangalia ramani ya mradi wa jengo la Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Kituo cha Dar es Salaam baada ya kutembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo na kuunda tume kuchunguza mradi huo. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dk. Ismael Kimerei . Picha na Mpiga Picha Wetu.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesimamisha malipo yote kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Petra Construction co. Limited inayojenga maabara ya kisasa ya Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kituo cha Dar es Salaam hadi uhakiki wa gharama halisi za mradi huo utakapokamilika baada ya kubaini kuwepo matumizi mabaya ya fedha za umma kiasi cha shilingi bilioni 2.6
Hivyo Waziri Mpina ameunda tume ya kiuchunguzi itakayofanya kazi kwa siku saba na kuwahusisha wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kubaini ukweli wa gharama halisi za mradi huo.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, Waziri Mpina alisema amebaini mradi unaojengwa miundombinu yake ni midogo ikilinganishwa na mkataba ulioridhiwa wa sh. bilioni 2.6 na kwamba taarifa ya uhakiki ya mradi huo itawasilishwa wizarani ikiwa na mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya wizi huo wa fedha za umma.
Waziri Mpina alisema thamani halisi ya mradi huo hailingani na fedha zilizotolewa na Serikali huku akitolea mfano baadhi ya miradi ya ujenzi wa majengo mbalimbali ikiwemo vituo vya afya na hospitali za wilaya zinazojengwa maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo wakati wa mjadala ukiendelea wa kuhoji matumizi ya fedha hizo kwenye mradi huo, mmoja wa wakandarasi wanaojenga majengo hayo alimweleza Waziri Mpina kuwa hadi mradi utakapomika kutabaki ‘chenji’ kiasi cha shilingi milioni 500 jambo lililotilia mashaka na kuibua maswali mengi juu ya gharama halisi za mradi huo.
Kufuatia mkanganyiko huo wa maelezo ya mkandarasi na hali halisi iliyoonekana kwenye mradi huo ndipo Waziri Mpina akalazimika kutangaza uamuzi huo wa kuundwa tume hiyo ili iweze kufanya tathmini ya gharama ya mradi iliyofanywa na Mshauri mwelezi wa mradi, namna zabuni ya kumpata mkandarasi ilivyotangazwa na namna mshauri mwelekezi alivyopatikana na hali ya ujenzi unavyoendelea kwa sasa ili kujua dosari ilisababishwa na nani.
Hivyo Waziri Mpina akabainisha kuwa baada ya kazi hiyo ya uhakiki kukamilika ndani ya siku saba ukweli utajulikana na hatua zote zilizopitiwa katika mradi huo ili kubaini kama Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2004 ilikiukwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wote watakaohusika na ubadhirifu huo wa fedha za umma.
“Sikubaliani na hizi gharama za mradi majengo na miundombinu ni midogo ikilinganishwa na mkataba wa bilioni 2.6, BOQ ilihakikiwa na wahandisi wa wizara, washauri waelekezi walijiridhisha kwamba iko sawa na ujenzi ukaenda hadi bilioni 2.6 mtu yeyote akija anakataa” alihoji Waziri Mpina
Hivyo Waziri Mpina ameagiza ujenzi wa mradi huo uendelee bila kusimama na ukamilike ifikapo Aprili 20 mwaka huu kama mkataba unavyoeleeza na baada ya jengo litazinduliwa ikiwa ni sehemu ya kuleta mageuzi makubwa ya sekta ya uvuvi kupitia eneo hilo muhimu la utafiti.
“Nitaleta timu ya ukaguzi itakayofanya uhakiki wa thamani ya fedha katika ujenzi wa jengo hili, kuanzia kwenye kutangaza tenda yenyewe, thamani ya mradi, kumpata mkandarasi mwenyewe, cost estimates zilizofanywa na wizara na baadae watafanya uhakiki wa kinachoendelea kujengwa hapa na kujua thamani halisi inayotakiwa na kwanini mradi huu upitishwe hadi kusainiwa”alihoji Waziri Mpina.
Meneja wa Mradi wa Swiofish, Flora Luhanga alisema mradi huo wa ujenzi wa Jengo la Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi ulianza Juni 10, 2019 kwa gharama ya shilingi bilioni 2, 609,491,754 unajengwa na Mkandarasi Kampuni ya Petra Construction Limited na kusimamiwa na Kampuni ya YP Architect.
Luhanga alisema mradi huo unajumuisha pia ujenzi wa uzio, ofisi ya walinzi, kuchimba kisima cha maji, ujenzi wa tenki la maji ya mvua na kujenga mnara wa maji.
Mkandarasi wa Mradi huo, Nicholaus Mlayi alisema hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 70 na tayari ameshalipwa shilingi milioni 963 na unatarajia kukamilika mwezi Aprili.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Uvuvi, Magese Bulayi alimhakikishia Waziri Mpina kuwa maagizo yote aliyoyatoa atayasimamia kikamilifu hasa katika kuangalia thamani ya fedha ‘value for money’ katika mradi huo na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika katika mchakato huo.