ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, April 8, 2023

LINDI YAPAA UFAULU WA ELIMU KWA MIAKA MITATU MFULULIZO.

 

Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck akiwakabidhi mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo, mwenyekiti wa Halmashauri ya Nachingwea Adinani Mpyagila na afisa elimu sekondari Endrew Muhulo wakati siku ya utoaji tuzo kwa waliofanya vizuri kwenye sekta ya elimu
Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck akiwakabidhi mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo, mwenyekiti wa Halmashauri ya Nachingwea Adinani Mpyagila na afisa elimu sekondari Endrew Muhulo wakati siku ya utoaji tuzo kwa waliofanya vizuri kwenye sekta ya elimu


Na Fredy Mgunda, Lindi.

MKOA wa Lindi umeendelea kufanya vizuri kwenye sekta ya elimu kwa kufaulisha wanafunzi kwa miaka mitatu mfululizo kwa asilimia 100 na kuongeza ufaulu wa kimadaraja jambo ambalo linasaidia watoto wengi kupata elimu.


Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa elimu, uzinduzi wa mpango mkakati wa elimu 2023 na sherehe za utoaji wa tuzo za ufaulu wa mitihani na pimaji za mwaka 2022/2023, Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck alisema kuwa ufaulu wa kidato cha nne katika kipindi cha miaka miwili mfululizo (2021-2022), mkoa wetu umeendelea kufaulisha wanafunzi wake wote kwa 100%. Kwa upande wa ufaulu kimadaraja, mkoa umeongeza idadi ya Wanafunzi wanaopata daraja la kwanza kutoka 426 mwaka 2021hadi 645 mwaka 2022 (sawa na ongezeko la 33.95%), Daraja -l kutoka wanafunzi 1,055 mwaka 2021 hadi 1,283 mwaka 2022 (sawa na ongezeko la 17.77%) na kupunguza daraja la IV kutoka wanafunzi 4 mwaka hadi 1 mwaka 2022 (sawa na punguzo la 75%). 

Taleck alisema kuwa katika mtihani wa kidato cha sita mkoa huo umeendelea kupandisha ufaulu kutoka 92.51l% mwaka 2021 hadi 95.52% mwka 2022 ikiwa ni ongezeko 3.02%. 

Kwa upande wa madaraja ya ufaulu mkoa wa Lindi umeongeza Wanafunzi wanaopata Daraja la |-|| kutoka 2,352 mwaka 2021 hadi 2,612 mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la 11.05% na kupunguza daraja la sifuri kutoka wanafunzi 539 mwaka 2021 hadi 334 mwaka 2022 sawa na punguz0 la 
38.03%. 

Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck alisema kuwa Halmashauri ya Liwale imefanikiwa kupunguza wanafunzi wanaopata daraja sifuri kutoka Wanafunzi 14 (2021) hadi wanafunzi 2 (2022) tu ndani ya wilaya. 

Aidha Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck aliwataka wazazi kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi waweze kupata chakula wakiwa shuleni kwa lengo la kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule zote za mkoa wa Lindi.

Alisema kuwa wanafunzi wasipotapa chakula shuleni hawawezi kufanya vizuri kimasoma kutokana na kila wakati kukabiliana na njaa wawapo darasani na kuwaondolea umakini wa kufuatilia masomo darasani.

Taleck aliwataka viongozi,walimu na wazazi kukemea kwa dhati vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa jamii ili kuwawezesha wanafunzi kusoma na kupata wananchi wengi ambao wamesoma katika mkoa wa Lindi.

Mkoa wa Lindi umeendelea kupandisha ufaulu kutoka 86.32% mwaka 2021 hadi 86.42% mwaka hii ikiwa ni ongezeko la 0.10% huku Baraza la Mitihani la Tanzania iliyotolewa kwa mwaka 2020 na 2021, imeutaja Mkoa wa Lindi Kuwa miongoni mwa Mikoa mitatu iliyofanikiwa kupandisha ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo. 

Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, afisa elimu mkoa wa Lindi Joseph Mabeyo alisema kuwa kufikia 31 Januari, 2023, Mkoa ulikuwa na Walimu wa Shule za Msingi 3,500 kati ya Walimu 5,450 wanaohitajika na upungufu wa walimu 1,950 sawa na asilimia 35.78 na kwa upande sekondari mkoa una walimu 1,701 kati ya walimu 1,950 wanaohitajika na upungufu wa walimu 249 sawa na asilimia 12.77.

KAMPUNI YA KYEM YAWAFUTA MACHOZI WATOTO YATIMA KITUO CHA BULOMA KIBAHA.

 


Na Victor Masangu,Kibaha 

KAMPUNI ya Kyem General Supplies  Limited ya Kibaha Mailimoja inayojishughulisha na masuala ya  uuzaji na usambazaji  wa vyuma chakavu  pamoja na vifaa vya ujenzi imetoa msaada wa vyakula mbalimbali kwa watoto yatima wa kituo cha Buloma Foundation kilichopo Kata ya Sofu katika Halmashauri ya Mji Kibaha.


Msaada uliotolewa ni pamoja na mchele kilo 100,unga kilo 100, sukari ,mafuta ya kupikia,sabuni na Mbuzi mmoja ambapo lengo la msaada huo ni kusaidia watoto hao katika Sikukuu ya Pasaka.


Mkurugenzi wa kampuni hiyo Josephu Mwakasyuka ,amekabidhi msaada huo leo katika hafla fupi iliyofanyika katika kituo hicho huku akisema kampuni itaendelea kutoa misaada hiyo katika makundi mbalimbali ya jamii inayoishi katika mazingira magumu.

Mwakasyuka, amesema kuwa kampuni ya Kyem inatambua kuwa watoto yatima ni jamii inayopaswa kuishi kama binadamu wengine hivyo lazima wasaidiwe katika mahitaji yao ya kila siku.

"Leo tumeona tuje kuwaona watoto yatima wa kituo hiki cha Buloma na tumewaletea vyakula mbalimbali kama vile mchele,unga,sukari,sabuni na Mbuzi mmoja ili kwa pamoja viwasaidie katika sikukuu ya Pasaka ", amesema Mwakasyuka.
Aidha, Mwakasyuka amesema kampuni imeweka mipango endelevu ya kusaidia yatima pamoja na jamii inayoishi katika mazingira magumu kama vile wajane,Walemavu na wazee bila kuangalia kabila wala dini.

Hatahivyo, Mwakasyuka amewaomba wadau wengine kujitokeza katika kusaidia watoto yatima waliopo katika kituo hicho na hata  jamii nyingine inayoishi katika mazingira magumu kwakuwa na wao wanamahitaji sawa na binadamu wengine.

Kwa upande wake msimamizi wa kituo hicho Baraka Peter, ameishukuru kampuni ya Kyem General Supplies kwa msaada huo kwani kiwango cha msaada walichotoa ni kikubwa na kitaweza kuwasaidia mwezi mzima.

Peter,amesema kituo hicho kwasasa kina watoto 46 ambapo kati yao wakiume ni 24 na wakike 22 nakusema wengi wao wanasoma Shule ya awali, Msingi , Sekondari na watoto watatu wanasoma vyuo vikuu.

"Ninatumia fursa hii kuishukuru kampuni hii kwa msaada huu mkubwa maana inawezekana mkaona ni kidogo lakini kwa moyo wa dhati mlichotoa ni kikubwa Sana na kitawasaidia watoto hawa kupata chakula cha mwezi mzima", amesema Peter

Hatahivyo , baadhi ya watoto yatima wa kituo hicho akiwemo Lilian Masawe na Yohana Almasi wameishukuru kampuni hiyo kwa hatua kubwa ya kuwakumbuka katika sikukuu ya Pasaka na kuomba wasichoke kuisaidia kwakuwa changamoto zao ni nyingi.

FATHER MAZIKU AIGUSA RIPOTI YA CAG KWA FIMBO YA PASAKA

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Yesu aliubeba msalaba, ingawa ulikuwa mzito na ulimchosha alipambana nao mpaka mwisho na kuishinda mauti na hata leo hii ndiye mkombozi wetu. Tutoke kwenye msalaba wa Goligota twende kwenye msalaba wa kijamii, tunapotafuta shortcut/njia za mkato kujinufaisha tukaingia kwenye ufisadi na dhuluma, tumeukwepa msalaba/majukumu tuliyo kabidhiwa. - Ukiwa na nidhamu ya kuamka mapema na kuwahi kazini, umeamua kuubeba msalaba, - Kama wewe ni baba au mama ukiishi kwa kutimiza majukumu yako, kwa watoto kupata elimu, chakula na malazi safi na salama, umeamua kuubeba msalaba. - Kama wewe ni mwanasheria, daktari au muuguzi na umeamua kufanya kazi kwa misingi ya taaluma yako kuwaokoa wagonjwa na wenye tabu na shida, umeamua kuubeba msalaba. - Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa siku za hivi karibuni amekuwa akipokea ripoti ya CAG yenye hati nyingi chafu, humo ndani watu wamepiga hela nyingi mabilioni kwa mabilioni ya fedha, mpaka rais anatumia lugha kali yenye ukakasi, yote yamesababishwa na watendaji aliowaamini na kuwapa majukumu kusimamia anachokipambania kwa maslahi ya taifa lakini wao wameamua kumwangusha kwa kufanya kwa njia zao, kwa maslahi yao, kwa ufupi wameukwepa msalaba. Yesu amefanya kitu ambacho sayansi haiwezi kufanya. - Yeye alivunja miiko ya sayansi. Ni sehemu ya ufafanuzi kwa swali, nililomuuliza Padre Leons Maziku, Muhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agustino Mwanza Tanzania (SAUT) swali likiwa - Kuna lipi la kujifunza kwa jamii yetu kupitia Pasaka na mateso ya Bwana Yesu Kristu pale msalabani?

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA AMWAGA NEEMA KWA MADEREVA BAJAJI

 

Mwenyekiti wanchama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Daud Yassin akiongea na madereva bajaji wa mkoa wa Iringa umuhimu wa kusomea udereva na kupata cheti cha udereva


Na Fredy Mgunda, Iringa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa,Daud Yasin amemwaga neema kwa madereva bajaj watakao kubali kuingia darasani kupata mafunzo ya udereva na usalama barabarani.


Amesema kwa wale 100 wa kwanza kupata mafunzo hayo atawalipia leseni na lengo kubwa kwake ni kupunguza makosa ambayo huchangia ajali za barabarani.


Ndugu Yassin alikuwa akiongea kwenye mkutano wa madereva bajaj uliofanyika kwenye ukumbi wa CCM Mkoa wa Iringa pia, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, *Ndugu Halima Dendego* alitumia nafasi yake kuwafunda watii sheria bila shuruti.


"Wale 100 wa kwanza watakao jifunza vizuri na kuelewa nitawalipia leseni, lakini muhimu kufuata sheria," amesema *Ndugu Yasin*


Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Iringa aliwaambia kazi ya chama hicho ni kuisimamia Serikali lakini, madereva hawana budi kutii sheria bila shuruti.


Alitumia nafasi hiyo kutoa salamu za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan akiwasihi vijana hao kuendelea kumuunga mkono.

Friday, April 7, 2023

SHEIKH KABEKE 'JUMAMOSI HII 8APR2023 UWANJA WA FURAHISHA JAMBO KUBWA KWA WATU WA DINI ZOTE MWANZA'

 Ikiwa ni siku moja kabla ya tukio la kusanyiko kubwa la Jihad Badri Day, lililopagwa kufanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Sheikh wa mkoa huo Al-Haji Hassan Kabeke hii leo kazungumza na Jembe Fm kutoa maelezo na utaratibu jinsi utakavyokuwa kwa tukio husika.

#mwanza #ShkHassanKabeke #Bakwata #JembeUpdates #ShkHassanKabeke #Bakwata #JembeTv #Mwanza

RIPOTI YA CAG YABAINI MAGARI 21 YAMELIPIWA Sh4 BILIONI HAYAJAPOKELEWA.

 


Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imebaini kuwa taasisi tisa zilinunua magari 21 kupitia kwa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) magari hayo hayajakabidhiwa kwa taasisi ambazo zimenunua.

Ripoti hiyo ya CAG, Charles Kichere iliyowasilishwa jana Alhamisi Aprili 6, 2023 jijini Dodoma ilisema magari yaliyolipiwa Sh4.06 bilioni lakini hayajakabidhiwa kwa wamiliki husika.

“Kanuni ya 242 (i) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013 iliyorekebishwa mwaka 2016, inaeleza kuwa ambapo upokeaji wa bidhaa unacheleweshwa au unaonekana utacheleweshwa zaidi ya wakati uliowekwa katika mkataba, taasisi nunuzi lazima ipate ripoti na maelezo kutoka kwa wauzaji au mawakala wao. Pia, inaweza kuweka adhabu ya kikomo kama ilivyoelezwa katika mkataba.

“Maoni yangu ni kuwa, kuchelewa kukabidhi magari yaliyonunuliwa, kunakwamisha kufikiwa kwa malengo yaliyotarajiwa, hivyo kuathiri shughuli za usimamizi na ufuatiliaji. Napendekeza menejimenti za taasisi husika zifanye ufuatiliaji wa karibu kwa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) ili kuhakikisha magari yanafikishwa kwa taasisi nunuzi,” imeeleza Ripoti ya CAG.

Thursday, April 6, 2023

MAAFISA TEHAMA HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO WAPEWA MAFUNZO YA UBORESHAJI WA MAZINGIRA YA MTOA HUDUMA

 

 

Mkuu wa Idara ya Udhibiti Ubora wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga  (Bombo ) Joseph Nzige akitoa mafunzo ya uboreshaji wa mazingira ya mtoa huduma kwa dhana ya 5S-KAIZEN kwa Maafisa Tehama wa Hospitali hiyo,Picha na Hospitali ya Rufaa ya Bombo   

Mkuu wa Idara ya Tehama wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo William Masika  wa kwanza kulia akiwa na maafisa tehama wengine wakifuatilia mafunzo hayo
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini 
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini 
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini 


BWANA HARUSI AANGAMIA BAADA YA KULIPULIWA NA BOMU LILILOTEGWA KWENYE ZAWADI


Mwanaume mmoja amefariki baada ya mfumo wa ukumbi wa michezo nyumbani aliyopokea hivi majuzi kama zawadi ya harusi kulipuka.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, bomu hilo lilikuwa limetegwa kwenye zawadi hiyo ambalo lililipuka muda tu ilipowekwa katika umeme.

Bwana harusi huyo ambaye alikuwa pamoja na kaka yake, alifariki papo hapo huku kaka yake akifariki kutokana na majeraha alipokuwa akipokea matibabu.

Wakati huo huo watu wengine wanne, akiwemo mvulana wa miezi 18, walijeruhiwa katika mlipuko huo, ambao ulifanyika Jumatatu, Aprili 3, nyumbani kwa bwana harusi katika wilaya ya Kabirdham katika jimbo la kati la India la Chhattisgarh

Polisi wamesema mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kuta na paa la chumba hicho zilianguka kutokana na athari zake.

Bomu hilo lilidaiwa kutegwa na mpenzi wa zamani wa bibi harusi ambaye alikuwa na machungu dhidi yake kwa kuolewa na mwanamume mwingine.

Mshukiwa kwa jina Sarju Markam kutoka jimbo jirani la Madhya Pradesh alikamatwa Jumanne, Aprili 4.

Markam, 33, alikuwa na uhusiano na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29 na alikuwa akisisitiza kuwa awe mke wake wa pili.

Lakini familia ya mwanamke huyo ilikataa na kupanga ndoa yake mahali pengine.

Bwana harusi amtema bibi harusi madhabauni

Baada ya kugundua swala la kuhuzunisha kuhusu mke wake siku ya harusi yake, bwana harusi amefutilia mbali mipango ya ndoa.

Mwanaume  huyo aligundua kwamba mrembo wake tayari alikuwa na watoto wawili na mwanamume mwingine.

Bwana harusi huyo ameelezea uchungu wake alipofuta mipango ya harusi na kuvua viatu vyake vya harusi na suti.

Licha ya juhudi kadhaa ya walioshuhudia kumtuliza, bwana harusi aliyekuwa amepandwa na mori alikataa kuendelea na harusi.

Pia alidai kurejeshewa mahari aliyolipa.

MGANGA WA KIENYEJI INDONESIA ASHUTUMIWA KWA KUUA TAKRIBAN WATU 12


Polisi
nchini Indonesia wamemkamata mganga mmoja wa kijiji anayedaiwa kuwaua takriban watu 12 baada ya miili kadhaa kupatikana ikiwa imezikwa kwenye bustani ya mtu huyo.

Slamet Tohari, 45, alikiri kwa polisi kwamba makumi ya wahasiriwa walizikwa kwenye ardhi yake.

Ameshtakiwa kwa mauaji ya kukusudia ya wateja nyumbani kwake huko Banjarnegara katika Java ya Kati.

Polisi wamesema aliahidi kuzidisha pesa zao kwa njia za kichawi na wateja walipotaka kurejeshewa pesa zao, aliwapa sumu.

Alikamatwa wiki moja hii baada ya mtoto wa kiume wa anayedaiwa kuwa mwathiriwa hivi majuzi kuwaambia polisi kwamba nyumba ya Tohari palikuwa mahali pa mwisho pa babake kwenda .

Familia ya Paryanto haikuweza kuwasiliana naye tangu machi 24

Alimweleza mwanawe eneo lake kupitia ujumbe wa WhatsApp na kumtaka awaarifu polisi ikiwa hatarudi kufikia machi 26.

Ripoti ya polisi ilitolewa siku iliyofuata.

Polisi kisha walikwenda nyumbani kwa Tohari katika kijiji cha Desa Balun, wilaya ya Wanayasa siku ya Jumatatu, ambapo waligundua makaburi kadhaa ya kina kifupi katika eneo la karibu.

Baadhi ya makaburi yalikuwa na wahasiriwa wawili hadi watatu waliozikwa pamoja.Chupa ya maji ya madini pia ilipatikana katika kila kaburi.

Polisi wanasema wahasiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 50, na wengine walikuwa wamezikwa kwa miezi sita.

Miili yao haikuonyesha dalili zozote kuuawa kwa kutumia nguvu .

Haijulikani ikiwa miili hiyo imetambuliwa.Polisi hawakutoa taarifa iwapo kumekuwa na uchunguzi kuhusu kesi hizo.

Tohari hajakanusha mauaji hayo.Hapo awali alifungwa 2019 kwa uhalifu wa pesa ghushi na anakabiliwa na hukumu ya kifo kwa mashtaka ya sasa.

Polisi walisema alijifanya kuwa mganga, (Babu Slamet), ambaye angeweza kuzidisha pesa utakayompatia

Waliamini kuwa Tohari amekuwa akiwaua wahasiriwa wake tangu 2020.

JUMUIYA YA WAZAZI KIBAHA MJI YAWAKUMBUKA KWA MSAADA WAKINAMAMA KITUO CHA AFYA MKOANI.



Na  Victor Masangu,Kibaha 

Jumuiya ya wazazi ya chama Cha mapinduzi (CCM) Wilaya Kibaha mji katika kuboresha afya ya mama na mtoto imeamua kufanya ziara katika kituo cha afya mkoani kilichopo Wilaya ya Kibaha na kufanya  matendo ya huruma katika wodi ya wazazi kwa kugawa msaada wa vifaa mbali mbali na mahitaji muhimu.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo Mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya wazazi Yahaya  Mtonda amesema kwamba wameamua kufanya ziara hiyo ya kutembelea kituo hicho cha afya ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya wazazi hivyo wakaona kuna umuhimu kufanya matukio ya kuisaidia jamii.
 





Mwenyekiti huyo ya wazazi ambaye aliambatana na viongozi mbali mbali wa jumuiya hiyo wakiwemo wajumbe wa kamati ya utekelezaji sambamba na baadhi ya madiwani ambapo walipokelewa kwa furaha  na kuweza kupata fursa ya kuwatembelea wazazi waliojifungua kwa ajili ya kuwajulia hali na kuwapatia mahitaji yao muhimu wanayostahili.

Mtonda alisema kwamba jumuiya yao ya wazazi imeona kuna changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili wakinamama wajawazito pindi wanapojifungua wanahitaji mahitaji mbali mbali ili kuweza kuwasaidia pindi wanapokuwa wodini wao pamoja na watoto ambao wamezaliwa.


"Tupo katika kipindi cha  maadhimisho wiki ya wazazi ambapo kwa Upande wetu kama Wilaya ya Kibaha mji tumeamua kuchagua baadhi ya maeneo kwa ajili ya kuyatembelea ikiwemo kituo Cha afya mkoani hususan katika wodi ya wazazi na tumetoa msaada wa vitu mbali mbali ikiwemo sabuni,pampasi za watoto pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya watoto na wakinamama.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kubadilika kwa kuhakikisha kwamba wanawalea na kuwatunza watoto wao kwa lengo la kuijenga nchi na kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazokikabili kituo hicho ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ili wagonjwa waweze kupata huduma nzuri.


Awali mganga mfawadhi wa kituo cha afya Mkoani Abdulkadri Sultan ameipongeza kwa dhati jumuiya hiyo ya wazazi kutokana na kuona umuhimu mkubwa wa kutumia wiki ya maadhimisho yao kwenda kutoa msaada katika wodi ya wazazi kwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mahitaji pindi wanapojifungua.

Sultan alisema kuwa licha ya jumuiya ya wazazi kwenda kutoa msaada lakini kwa Sasa bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kupokea idadi kubwa ya wagonjwa ukilinganisha na idadi ya wodi zilizopo ni chache hivyo kuiomba jumuiya hiyo iwasadie katika jambo hilo.

Naye diwani wa Kata ya Tumbi ambaye naye alishiriki katika ziara hiyo hakusita kuwashukuru kwa dhati uongozi mzima wa jumuiya ya wazazi Wiyala ya Kibaha mji kwa kuona umuhimu wa  kuwasapoti kwa hali na mali wakinama hao pamoja na watoto wao.



Nao baadhi wa wakinamama ambao walipata fursa ya kutembelewa na kupatiwa msaada wa vitu mbali mbali wamesema kitendo hicho kimeweza kuwafariji kwa kiasi kikubwa kwani hawakuweza kutegemea kama watapatiwa msaada huo kwani utawasaidi wao pamoja na watoto wao.


Katika hatua nyingine uongozi wa jumuiya hiyo uliweza kutoa salamu zao kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka pamoja na mke wa Mbunge Selina Koka kwa kuweza kusapoti kufanikisha zoezi hilo pamoja na wadau wengine wakiwemo baadhi ya madiwani wa halmashauri ya mji Kibaha.

ANUSURIKA KUFA BAADA YA KUJIKATA NYETI


Mwanaume aitwaye Anselumu Sebuka, miaka 42, Mkulima na mkazi wa Namagondo  wa kitongoji cha Kasuzu, kijiji na kata ya Namagondo, tarafa ya Mumulambo wilayani Ukerewe  alikutwa ndani ya chumba chake akiwa amejaribu kujiua kwa kukata uume wake kwa kutumia kisu chenye ncha kali.

Inadaiwa Ansele Sebuka alikuwa anatuhumiwa na ndugu zake kuiba mali mbalimbali za familia yake na za jamii inayomzunguka na kwenda kuziuza pamoja na ulevi uliokithili ambapo waliamua kumtenga kutokana na tabia zake.

Baada ya tuhuma hizo ndipo aliamua kujikata uume wake kwa kisu na kuacha unaning’inia kwa lengo la kujiua.

 Chanzo cha tukio hilo ni ugonvi wa kifamilia uliopelekea mhanga kupata msongo wa mawazo.

Ansele Sebuka alipelekwa katika Hospitali ya wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kufuata njia sahihi za kutatua matatizo yao hususani kuwaona wataalamu wa afya ya akili ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na msongo wa mawazo na kukosa uvumilivu wa migogoro mbalimbali katika jamii.

 Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake watumie njia sahihi katika kuhakikisha wanatatua matatizo yao bila kuleta madhara na usumbufu.

Wednesday, April 5, 2023

MUSONDA: MOTO UTAWAKA HAPO

 


Mshambuliaji wa Yanga, Kenedy Musonda amesisitiza kwamba kuna moto unakuja kimataifa.

.

“Nimecheza mechi nyingi za mashindano ya ndani na kimataifa nje ya Yanga lakini tangu nimetua hapa nimegundua utofauti mkubwa ni nchi ambayo mashabiki wanapenda sana mpira wapo na timu zao nyakati zote.

.

“Tuna timu nzuri wachezaji ni wapambanaji na wana uchu wa mafanikio ukimuangalia mchezaji mmoja mmoja unaona anapambana kutafuta nafasi ili kuonyesha kile alichonacho na benchi la ufundi limekuwa likitoa nafasi.” alisema.

.

Musonda alisema wao kama wachezaji baada ya kupambana na kufanikiwa kuongoza kundi sasa wanataka kuionyesha Afrika walichonacho.

MWANAFUNZI AUAWA AKIENDA KWENYE MIHADI YA MPENZIWE.

 


June Jerop, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kenyatta aliyekuwa akisomea shahada ya uzamili katika Utawala wa Biashara alipatikana akiwa amefariki saa chache baada ya kwenda kuchumbiana na jamaa anayeshukiwa kuwa mpenzi wake.

 

June Jerop, 36 alikaa siku nzima na marafiki zake mnamo Machi 18 kabla ya kujiondoa kwenda kwenye mtoko huo. Aliwaambia rafikize kuwa atakutana na rafiki wa kiume kwenye mgahawa mahali flani lakini hakufichua mengi kuhusu hilo.

Baada ya mtoko huo simu yake ilizima na familia yake na marafiki walijaribu kuwasiliana naye bila mafanikio.

 

Mwili wake uliripotiwa kutupwa karibu na Shule ya Msingi ya Jamhuri jijini Nairobi kabla ya polisi kuhamishia mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City. Kulingana na polisi, mwili wake ulipatikana ukiwa umevimba na ukiwa na damu.

UVCCM KIBAHA MJI YAPANIA KULETA MAGEUZI MAKUBWA KWA VIJANA

 


Na Victor Masangu,Kibaha 


Mwenyekiti  wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM)  Wilaya ya Kibaha mji Ramadhani Kazembe amewataka vijana wenzake  kuhakikisha wanashikamana kwa pamoja na kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuchapa kazi  kwa uzalendo ili kuleta chachu ya maendeleo.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake katika kata ya Tangini yenye lengo la kuweza kuzungumza na vijana pamoja na kutoa shukrani zake za dhati kwa kuweza kumchagua kushika nafasi hiyo ya Mwenyekiti.

Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa suala la uchaguzi limeshamalizika hivyo hakuna budi kuachana kabisa na makundi na kuelekeza nguvu zao zote katika kuweka misingi imara kuanzia ngazi za matawi hadi ngazi ya Wilaya ikiwa sambamba na kutenda haki.

Aidha katika hatua nyingine Mwenyekiti Kazembe amesema lengo lake kubwa ni kuendelea kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo kwa kushirikiana na vijana wenzake ili kuweza kuleta chachu ya  maendeleo katika jumuiya ya vijana.

Pia alifafanua kwamba ataendelea kuwatumikia na kuwaongoza kikamilifu vijana wenzake katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi  kwa kuzingatia kanuni ya umoja wa vijana Kama inavyoelekeza katika ibara ya saba na nane kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi.


Kwa upande wake Katibu wa Uvccm Kibaha mji Gamalu Makona amesema kwamba ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wenzake pamoja na vijana ili kuweza kuimarisha jumuiya ya umoja wa vijana.

Ziara ya Mwenyekiti wa Uvccm Wilaya ya Kibaha mjini katika kata ya Tangini imeweza kuleta tija zaidi kwa jumuiya hiyo kutokana na kujadili Mambo mbali mbali kwa maslahi mapana ya vijana pamoja na jamii kwa ujumla.

Tuesday, April 4, 2023

MFUKO WA JIMBO KIBAHA MJI WATOA MILIONI 20 KUCHOCHEA MIRADI YA MAENDELEO.

Picha za matukio mbali mbali zinazoonyesha ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini akiwa na viongozi wa chama pamoja na wajumbe wa mfuko wa Jimbo ikiwa ni pamoja na kupanda mti.

 Na Victor Masangu,Kibaha


Katika kuchagiza chachu ya kuleta  maendeleo kwa wananchi mfuko wa Jimbo kutoka ofisi ya Mbunge wa Kibaha mjini imeamua kutoa zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 20 katika kusaidia kuinua na kuchochea kasi ya maendeleo katika sekta mbali mbali.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvesty Koka wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuweza kukagua na kutembelea baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa kupitia fedha za mfuko wa Jimbo.

Ziara hiyo ambayo iliambatana na wajumbe mbali mbali wa mfuko wa Jimbo pamoja na viongozi wengine wa Chama Cha mapinduzi (CCM) ngazi za matawi,mashina,kata,pamoja na wilaya ili kuweza kujiridhisha kama miradi hiyo inafanyika kwa kiwango kinachotakiwa 

Akizungumza pindi alipokuwa katika miradi hiyo Koka alisema kwamba katika fedha hizo ambazo zilishatolewa ni kwa ajili ya kuchochea zaidi kasi ya maendeleo katika miradi mbali mbali ikiwemo,afya,elimu,miundombinu ya barabara maji na huduma nyingine za kijamii.

Aidha Mbunge huyo alifafanua kwamba katika fedha hizo zimeweza kusaidia mambo mbali mbali ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari,ununuzi wa madawati na viti katika shule mpya ya sekondari Misugusugu.



Pia aliongeza kuwa katika fedha hizo zimeweza kutumika katika kuanzisha mradi wa ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika kata ya Mbwawa kwa lengo la kuwasaidia wakinamama wajawazito kuondokana na changamoto ya kutwmbea umbari mrefu kufuata huduma ya kujifungulia.

Sambamba na hilo alifafanua kuwa dhamira yake kubwa ni kuwaletea wananchi maendeleo kwa pamoja na hususan atazipa kipaumbele kwa Hali na mali kata ambazo zipo pembezoni mwa mji.

"Mimi Kama Mbunge lazima niweke mipango madhubuti ya kushirikiana na wananchi na ndio maana nimeamua kutumia fedha hizi za mfuko wa Jimbo ili kuchochea kasi ya maendeleo na mieanza ziara yangu katika kata zipatazo sita na nitamalizia na nyingine kwani Jimbo langu lina kata 14,"alisema Koka.

Nao baadhi ya wananchi ambao wamenufaika miradi hiyo ambayo imetokana  na fedha za mfuko wa Jimbo wameishukuru serikali ya awamu ya sita pamoja na Mbunge Koka kwa kujikita zaidi katika kuwaletea maendeleo yenye tija kwa maslahi ya jamii kwa ujumla.

Fedha za mfuko wa jimbo zimekuwa zikitolewa kwa ajili ya kuweza kuchochea maendeleo kupitia miradi mbali mbali ikiwemo afya,elimu,maji,umeme,miundombinu ya barabara,pamoja na huduma nyingine za kijamii.


Ziara hiyo ya Mbunge wa Jimbo a Kibaha mjini ya kutembelea miradi yamaendeleo imefanyikakatika kata sita ikiwemo Mbwawa,Visiga,Misugusugu,Viziwaziwa,Kibaha ,pamoja na kata ya mkuza.