NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Ofisi ya Wilaya ya Kibaha kwa kushirikiana na Umoja wa vijana (UVCCM) Kibaha mjini katika kutekeleza agizo la serikali la kufanya usafi wa mazingira ifikapo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi imeamua kutambulisha rasmi Club ya Jogging pamoja na kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga afya zao na ili kuweza kujikinga na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Utambulisho huo wa Jogging inayotambulika kwa jina la Kibaha Fitness Club umekwenda sambamba na zoezi la ufanyaji wa usafi katika kituo cha afya Mkoani kilichopo Wilaya ya Kibaha pamoja na uchangiaji wa damu kwa ajili ya kuweza kuwasaidia wagonjwa mbali mbali wenye uhitaji hususan wakinamama wajawazito.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magogwa amesema kwamba wameamua kuungana na vijana wa UVCCM kufanya usafi wa mazingira ikiwa ikiwa ni moja ya utekelezaji wa agizo la serikali la kufanya usafi ifikapo kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.
"Sisi kama serikali ya Wilaya ya Kibaha tumeamua kushirikiana na vijana wetu wa UVCCM, katika kufanya utambulisho wa Club ya Jogging ambayo pia imeambatana na suala la usafi wa mazingira na nipo hapa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha na kwamba tumeweza kusafisha maeneo mbali mbali ya kituo cha afya Mkoani pamoja na uchangiaji wa damu,"alisema.
Aidha Katibu Tawala huyo aliwapongeza kwa dhati vijana hao wa UVCCM Wilaya ya Kibaha mji kwa maamuzi yao kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uchangiaji wa wa damu,kufanya usafi wa mazingira pamoja na kuweza kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali katika wodi ya wazazi katika kituo hicho cha afya Mkoani.
Katika hatua nyingine Katibu huyo alibaisha kwamba lengo lao kubwa kama Wilaya ya Kibaha ni kuendelea kutekeleza kwa hali na mali agizo la serikali katika kuendelea kufanya mazoezi ya mara kwa mara ikiwa pamoja na kuanzisha Club za Jogging ambazo zitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa vijana (UVCCM) Wilaya ya Kibaha mjini Ramadhani Kazembe amesema kwamba wao kama vijana wameungana na Ofisi ya Wilaya ya Kibaha na kufanya mazoezi ya pamoja ambayo pia yameambatana na uchangiaji wa damu, pamoja na kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali katika wodi ya wazazi.
"Tumeamua kuungana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha katika kuunga mkono juhudi za serikali katika jambo zima la usafi wa mazingira na tumefanya mazoezi ambayo pia yameambatana na uchangiaji wa damu ikiwa sambamba na utoaji wa mahitaji mbali mbali ambayo yatawasaidia wakinamama wajawazito,"alisema Kazembe.
Kadhalika Kazembe alimpongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ya viwanda ikiwa pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, maji,pamoja na huduma ya afya.
Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mjini Catherine Saguti ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na vijana wa UVCCM kwa kwenda kutoa msaada wa kuchangia damu na kuwatembelewa wakinamama waliojifungua na kuwapatia mahitaji mbali mbali ikiwemo sabuni za kufulia.
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa kushirikiana na umoja wa vijana (UVCCM) Wilaya ya Kibaha mjini imeweza kutambulisha Club ya Jogging na kufanya mazoezi ambayo yamekwenda sambamba na uchangiaji wa damu, kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali ikiwa sambamba na kufanya usafi wa mazingira katika katika kituo cha afya.