ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, May 6, 2022

SABAYA NA WENZAKE SASA HURU.


Mahakama Kuu imemuachia huru aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili baada ya kubaini kulikuwa na mapungufu katika mwenendo mzima wa kesi, pamoja na kutofautiana kwa mashahidi. 

 Sabaya na wenzake walikata rufaa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Mbali na Sabaya, wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura. 

 Hata hivyo, Sabaya ataendelea kukaa mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Wednesday, May 4, 2022

WASICHANA VYUO VIKUU WAONGOZA KUPIMA MAAMBUKIZI MAGONJWA YA KIZAZI.

 

wasichana pic

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahindi akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loleza Jijini Mbeya leo Jumatano Mei 2, 2022

Mbeya. Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mkoani Mbeya imesema wastani wa asilimia 21 ya wanafunzi 504 wa vyuo vikuu nchini waliopimwa wamebainika kuwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa huku wanaume wakiwa asilimia 14.

Mwanasayansi mtafiti  kutoka NIMR, Dk  Ruby Mcharo amesema hayo leo Jumatano Mei 4, 2022 wakati akitoa taarifa ya tafiti kwa Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi mara baada ya uzinduzi wa wimbo wa kuelimisha vijana na jamii kujikinga na magonjwa ya zinaa uliohusisha wanafunzi 63 katika shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza.

Amesema kuwa kumekuwepo na changamoto kubwa ya makundi ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 mpaka  21 kukutwa na magonjwa zinaa licha ya kuwepo kwa kampeni za utoaji elimu ya mara kwa mara  ili kunusuru kundi hilo inayotolewa na watafiti kutoka NIMR kwa kushirikiana na wataalam wa afya.

''Tafiti za maambukizi kwa wanavyuo ni kubwa na changamoto kubwa ni kufanya ngono na zinaa zisizo salama na wameona sasa kuwafikishia elimu kwa njia za wimbo kwa makundi mbalimbali ''amesema.

Dk Mcharo ameongeza kuwa awali kulikuwepo kwa kampeni mbalimbali za uelimishaji ambazo hazijafanya vizuri hivyo wamekuja na mbadala mwingine wa kutoa elimu kwa njia ya wimbo kwa kushirikisha wanafunzi wa shule za sekondari, vyuo vikuu  na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema kuwa kuna kila sababu kwa NIMR kuendelea kutoa elimu kwa jamii na wanafunzi mashuleni kuhusiana na kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na VVU hususan athari za mimba shuleni.

''Ninyi wanafunzi wa Loleza msikubali kufanya ngono zisizo salama na kuepuka kufanya umri wao bado wanahitaji kupata elimu na wakati wa kuyafanya hayo utafika huku akilaani kitendo cha baadhi ya wanafunzi katika Shule hiyo kuacha masomo kutokana na mimba za utotoni''amesema.

Amesema kuwa kupitia programu hiyo ni vizuri kushirikisha walengwa na makundi maalumu kwa mlengo wa kufikia malengo makubwa ya tafiti za magonjwa ya zinaa na VVU na kwamba Taasisi yake ya Maryprisca Women Empowerment Fund itaona namna ya kuwafikia.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua amesema kuwa Loleza imekuwa ikifanya vizuri sana katika masuala ya afya hivyo ni wakati sasa Taasisi hiyo kuongeza weledi kwa kutoa elimu bora ya kujikinga na magonjwa ya zinaa.

Mwanafunzi wa kodato cha sita ambao wako kwenye mradi huo, Catherine Mwajebele ameomuomba Naibu Waziri kuendelea kuwakumbuka na kuwashika mkono kupitia Taasisi yake ya Maryprisca Women Empowerment Fund.

WATOTO WANNE WAFA BAADA YA NYUMBA KUUNGUA SIMANJIRO.

New Content Item

Eneo ambako nyumba imeungua na kusababisha vifo vya watoto wanne katika Kijiji cha Ngage Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara. 


Watoto wanne wamefariki dunia baada ya nyumba kuungua moto wakiwa ndani katika Kijiji cha Ngage Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara. 

 Akizungumza leo Jumatano Mei 4, 2022, Diwani wa Kata ya Loiborsoit, Siria Kiduya amesema tukio hilo limetokea jana mchana. Kiduya amesema ajali hiyo pia imejeruhi mtu mmoja ambaye ni bibi wa watoto hao waliofariki. 

 Amesema kuwa watoto watatu walifariki papo hapo huku mmoja akifariki baada ya kupelekwa hospitalini. "Watoto watatu walifariki dunia papo hapo na bibi akajeruhiwa na mtoto mwingine walipelekwa hospitali ya KCMC ya Moshi Mkoani Kilimanjaro," amesema Kiduya. 

 Amesema chanzo cha ajali hiyo ni bibi huyo, Anna Kipututu kutumia petroli ili kuwaua kunguni waliokuwa kwenye kitanda chao. Amesema baada ya bibi wa watoto hao kumwagia petroli katika kitanda aliwasha moto ili kuwaua kunguni na moto ukaunguza nyumba wakiwa ndani. 

 Mkuu wa wilaya ya Simanijiro, Dk Suleiman Serera amethibitisha vifo hivyo na kutoa pole kwa wananchi wa kijiji hicho.

KOKA APANIA KUJENGA OFISI YA BAKWATA KIBAHA AANZA NA MIFUKO 100 YA SARUJI.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akizungumza wa Baraza hilo la Eidy Wilayani Kibaha.


Sheikh mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa akitoa maelezo wakati wa baraza hilo la Eidy  lilifanyika Wilayani Kibaha.
 Baadhi ya wazee maarufu wa dini ya kiislamu pamoja na waamini wengine wakiwa katika Baraza hilo wakifuatilia.

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ameungana kwa pamoja  na waamini wa dini ya kiislamu katika Baraza la sikukuu ya Eid ambapo ameahidi kuchangia  mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Bakwata Wilaya ya Kibaha.


 Koka ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe za Baraza hilo ambalo limefanyika katika shule ya msingi iliyopo kata ya Visiga Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani ambapo limehudhuliwa na viongozi mbali mbali wa dini na serikali. 

Alisema kwamba ofisi yake imekuwa bega kwa bega katika kushirikiana na Bakwata Wilaya tangu mwaka 2017 katika kuandaa Mabaraza hayo ya Eid lengo ikiwa ni kuweza kukutana kwa pamoja baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

  "Mimi ofisi yangu imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha mahusiano mazuri na wenzetu wa Bakwata bila kujali itikadi zozote za kidini kwa hivyo nimeamua kuchangia mifuko 100 ya saruji ambayo nina Imani itaweza kuleta mwanzo mzuri katika kuanza ujenzi,"alisema Koka

  Aidha ameongeza kuwa pamoja na Mambo mengine ataendelea kushirikiana na viongozi mbali mbali wa dini katika kuchochea zaidi kasi ya maendeleo kwa wananchi wa Jimbo lake la Kibaha mji ikiwemo miundombinu ya barabara maji,umeme,afya pamoja na Mambo mengine. 

 "Nampongeza Sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo tangu aingie madaraka ameweza kutoa fedha nyingine ambazo zimesaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa,zahanati,vituo vya afya pamoja na Mambo mengine mbali mbali,"alisema

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Hamis Mtupa aliwataka waamini wa kiislamu kutumia fursa mbali mbali walizonazo katika kuwasaidia watu wenye mahitaji wakiwemo wajane pamoja na watoto yatima.

Sheikh Mtupa aliongeza kuwa waislamu wanatakiwa kuwa wakarimu katika kipindi chote na sio mpaka uje mfungo wa mwenzi mtukufu wa Ramadhani na wanapaswa kuwa upendo ili kupata baraka kwa mwenyezi Mungu. 

 Pia alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini kwa upendo na moyo wake wa kujitolea katika kushirikiana katika Mambo mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kuungana na waislamu katika mambo mbali mbali.

 Katika hatua nyingine aliziomba kamati za ulinzi na usalama kuendelea kuweka ulinzi madhubuti ili kudumisha hali ya ulinzi na usalama na kuepuka vita na machafuko Kama nchi nyingine.

 Naye Sheikh wa Wilaya ya Kibaha Said Mtunda alitumia fursa hiyo kimshukuru Mbunge kwa mchango wake na kuwataka waislamu kuepuka kabisa na vitendo vya kufanya fujo na badala yake wajikite zaidi katika kutenda Mambo mema. 

Tuesday, May 3, 2022

𝐒𝐀𝐋𝐀𝐌𝐔 𝐙𝐀 𝐄𝐈𝐃 𝐊𝐔𝐓𝐎𝐊𝐀 𝐉𝐄𝐌𝐁𝐄 𝐌𝐄𝐃𝐈𝐀 𝐋𝐓𝐃

𝐒𝐀𝐋𝐀𝐌𝐔 𝐙𝐀 𝐄𝐈𝐃 𝐊𝐔𝐓𝐎𝐊𝐀 𝐉𝐄𝐌𝐁𝐄 𝐌𝐄𝐃𝐈𝐀 𝐋𝐓𝐃

Kando kando ya Magharibi, iliyojaa imani. Mwezi umebeba ujumbe na vimondo vinavyo tabasamu ndani ya Dunia.

Assallam aleykum Makka na Madina. Amani na iwe nanyi Makkarramah! Hamjambo! Na, karibuni Sevelim nyumbani kwa Sultan Ahmed mjini Istanbul.


Mahali hapa sote, tutakula, kunywa na kufurahi na kuusahau uchovu wa jangwani, kule anakoishi Ngamia mmoja mwenye maajabu yasiyogawanyika kwa mbili, haya ni maajabu Tisa!


Jembe Media inawatakia Eid Al fitr Madina, idd Mubarak Makka, iddi Mubarak Tanzania na Assallam Aleykum maskani ya Ahmed mjini Istanbul!...!!!


#eidmubarak

#jembemoney

#chezajembemoney

#jembefmupdates


 

RC SENDIGA :MARUFUKU KUPANDISHA BEI ZA BIDHAA KIHOLElA MKOANI IRINGA.

 

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen sendiga akiwa katika ziara kuangalia ongezeko la bei kwa wafanyabiashara mkoani humo na kuongea na wafanyabiashara wa soko kuu kuhusiana na kupanda bei kwa bidhaa kama matunda,vyakula ,lakini baadhi ya wafanyabiashara kama  wauzaji wa mbolea wamesema mfumuko wa bei upo kawaida.

  Na Fredy Mgunda,Iringa.

MKUU wa mkoa wa Iringa amepiga marufuku kwa wafanyabiashara kupandisha bei kiholela kwa ajili ya kupata faida hivyo wanatakiwa kupandisha bei kwa kufuata sheria za nchi ili kuondolea maumivu wananchi wa kawaida ambao ndio wanunuaji wa bidhaa hizo.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kuangalia kuagalia namna gani bidhaa zilivyopanda bei mkoani Iringa,Mkuu wa mkoa Queen Sendiga alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wanatumia kigezo cha kupanda bei kwa mafuta nao ndio wanapandisha bei.

Sendiga alisema kuwa wafanyabiashara wakipandisha bei kiholela wanawaumiza wanunuzi na wananchi wa kipato cha nchi hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kupandisha bei kwa kufuata sheria na tamko rasmi kutoka serikalini.

Akiwa katika ziara hiyo mkuu wa mkoa wa Iringa alibaini kuwa vituo vyote vya mafuta ya Petroli na Dizel vinauza mafuta hayo kwa kufuata sheria za nchi na muongozi ulitolewa na mamlaka husika hivyo aliwapongeza wamiliki wa vituo hivyo vya mafuta.

Sendiga alisema kuwa wafanyabisha wengi wamepandisha bei kwenye vyakula,matunda na bidhaa nyingine ambazo zinazalishwa kwenye viwanda ambavyo vipo nje ya mkoa wa Iringa jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi kwa mamlaka nyingine zinazohusika.

Alisema kuwa ikibaini kuna mfanyabisha amepandisha bei kiholela atachukuliwa hatua kali za kisheria na hakutakuwa na msamaa kwa mfanyabiashara huyo.

Sendiga alizitaka mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini (LATRA) na wakala wa vipimo (WMA) kufanya kazi zao kwa weredi kwa kuwa wameoneka kuwa wameshindwa kudhibiti vipimo  vya mizani pamoja na baadhi ya mabasi kupandisha bei nauli kinyume na sheria.

Kwa upande wa baadhi ya wafanyabishara wa mkoa wa Iringa walisema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ya magari kumesababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji na uzalishaji wa bidhaa za viwandani hivyo kusababisha nao kupandisha bei.

Walisema kuwa wanalazimika kupandisha bei za bidhaa mbalimbali ambapo inaonekana kama mzigo wote huo unamuangukia mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hizo.

Aidha wafanyabiashara hao walimuomba mkuu wa mkoa wa Iringa kufikisha kilio chao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan juu ya mfumko wa bei ambao unaendelea maeneo yote nchini.

TANESCO KUNUNUA NGUZO ZA UMEME NCHINI,WAZIRI ATANGAZA MASHARTI YAKE.

 

Waziri wa nishati January Makamba akiongea na wadau wa nguzo za umeme mkoani Iringa akiwaondolea sitofaumu iliyokuwepo ya kutonunua nguzo zao
Waziri wa nishati January Makamba akiwasikiliza wadau wa nguzo za umeme mkoani Iringa akiwaondolea sitofaumu iliyokuwepo ya kutonunua nguzo zaoWaziri wa nishati January Makambaakiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga wakati wa majadiliano ya kuondoa sitofaumu iliyokuwepo ya kutonunua nguzo zao

 

Na Fredy Mgunda,Iringa.

WAZIRI wa nishati January Makamba ameliagiza shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kuingia zabuni za ununuzi wa nguzo za kusambaza umeme kwa wakandarasi wanaokidhi vigezo,ikiwemo kuthibitisha baadhi ya nguzo zimetoka kwa wazalishaji wadogo wa ndani.

Waziri Makamba alisema kuwa TANESCO inatakiwa kushirikiana na taasisi zinazosimamia ubora wa bidhaa,ikiwepo shirika la viwango nchini (TBS) ili kuhakikisha nguzo zinazonunuliwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa na shirika hilo.

Makamba alisema kuwa ili kuondoa changamoto kwa wadau wa nguzo na serikali ataunda kamati y wadau wa nguzo watakaokuwa wanafuatilia namna ya utengenezaji wa nguzo bora za umeme ambao utasaidia kuuza nje ya nchi ambavyo wadau wanguzo nchi nyingine wanafanya kwa ubora unaotakiwa.

“Sasa ipo mifano ya mfumo huu wa uwekezaji wa viwanda vya nguzo,nchi kama Afrika Kusini inamfumo mzuri sana na serikali yenu ipo tayari kuwachukua watu kadhaa kwenye kila wadau na kuwapeleka na kuwalipia mkajifunze kuhusu mfumo wa kudhibiti na kuhusu ubora” alisema makamba

Aidha aliwatoa hofu wadau wa nguzo za Miti za Umeme nchini kwa kuwahakikishia soko la kuuza nguzo zenye ubora kwa Shirika la Umeme nchini( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), hapa nchini.

Makamba alisema kuwa mkutano ulilenga kuondoa sintofahamu pamoja na minong’ono inayoendelea kwa baadhi ya watu wanaopotosha kuwa Serikali haitanunua nguzo za Umeme za ndani na badala yake zitaagizwa kutoka nje ya Nchi.

Katika mazungumzo yake na Wadau hao, Makamba alisema kuwa, Serikali itaendelea kununua nguzo za miti za Umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani ili kulinda viwanda vya ndani kwa kuzingatia ubora wa nguzo uliowekwa.

“Tutakapo toa zabuni ili ufanikiwe kupata zabuni hiyo lazima angalau asilimia Fulani ya nguzo hizo utakazouza ziwe zimetoka ka watu wadogo wadogo na katika nyaraka yako ya kuomba zabuni iwepo ili ufanikiwa angalau asilimia 20 au 10 ya nguzo iwe inatoka kwa wadau wadogo na wawe wamepewa mikataba inayoeleweka” alisema Makamba

Makamba amewataka Wadau hao kuunda chama Cha wazalishaji wa nguzo ili kiweze kudhibiti ubora unaotakiwa na hata kutoa adhabu kali kwa atakayebainika kuzalisha chini ya Kiwango pamoja na kuandaa sheria zitakazoongoza chama hicho.“Lengo la Serikali ni kukuza uchumi wa wananchi wake kwa kuboresha bidhaa zao kwa kuwasimamia katika kuzalisha kwa vigezo na ubora uliowekwa, ili wananchi hao waweze kunufaika na kukuza uchumi wao na pato la Taifa kwa ujumla” Alisema Makamba.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharagwe Change, aliwataka Wadau hao kuwa waaminifu pale nguzo zao zinapotakiwa kupelekwa katika maeneo ya miradi kwa kuweka nguzo halisi zilizokaguliwa na siyo kufanya udanganyifu wa kuweka zisizokuwa na ubora.

Amesema kumekuwa na changamoto ya nguzo kuharibika baada ya muda mfupi kutumika kutokana na kuwa chini ya kiwango na ubora unaotakiwa, huku nguzo hizo zikiwa tayari zimekaguliwa na kuonekana zina ubora unaotakiwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said, amewahakikishia Wadau hao kuwa soko la nguzo lipo la kutosha kwani bado miradi mingi ya usambazaji wa Umeme vijijini inaendelea na nguzo nyingi zinahitajika.

Akitoa mfano Mkoa wa Iringa kuwa kuna Mradi wa Ujazilizi ambao unatarajia kuanza hivi karibuni katika Mkoa huo na mikoa mingine.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga amewapongeza wabunge wa Mkoa wa Iringa Kwa kuwa wamoja Katika kutetea ajenda za kimaendeleo zinazohusu Mkoa wa Iringa. 

Alisema kuwa umoja ambao wameonesha kwenye kupigania suala la nguzo za Umeme kuendelea  kununuliwa hapa hapa Nchini wamefanya Jambo la kizalendo sana kwani linaenda kuongeza mapato kwa serikali na Wananchi kwa ujumla. Vivyo hivyo amewataka kuendelea  kufanya hivyo kwenye ajenda nyingine za ki mkoa .

Sendiga Alisema kuwa  Mkoa wa Iringa na Njombe ndio ambao wameuza nguzo zaidi ya asilimia 90 zilizotumika kusambaza Umeme nchini na walishangazwa kusikia hoja ya kuwa nguzo za ndani sio bora wakati tayari nguzo nyingi zimesimikwa Vijijini na zipo imara

"Tukushukuru Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa kufanya maamuzi haya ambayo yana Afya kubwa Kwa uchumi wa mikoa hii miwili na Taifa"

Amewataka Wadau hao kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika na kuwa wasikivu kwa kile watakachokuwa wakielezwa kwa lengo la kupata bidhaa Bora kwa manufaa yao na taifa kwa jumla.

Sendiga alisema kuwa baada ya suala la nguzo kumalizika wabunge hao wana wajibu wa kuendelea kusukuma ajenda ya Mkoa wa Iringa ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha Lami toka Iringa hadi Ruaha Kwa ajili ya kuchochea kasi ya utalii ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha
 

Sunday, May 1, 2022

KIONGOZI WA KIJESHI WA GUINEA ATANGAZA KIPINDI CHA MPITO CHA MIEZI 39

 


Mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Guinea, Kanali Mamady Doumbouya, ametangaza kipindi cha miezi 39 ya utawala wa mpito kabla ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika kurejea kwenye utawala wa kiraia.


 Akihutubia taifa usiku wa kuamkia leo, Kanali Doumbouya amesema baraza la taifa la kipindi cha mpito litawasilisha mapendekezo yake bungeni. Tangazo hili limekuja baada ya kuundwa kile kiitwacho "mfumo shirikishi wa mashauriano" mnamo mwezi Aprili. 


Hata hivyo, mkutano uliopitisha chombo hicho ulisusiwa na makundi kadhaa mashuhuri ya upinzani. Siku ya Ijumaa, serikali ya kijeshi ilikuwa imetangaza kuwa mkutano huo ulipendekeza kipindi cha mpito kiwe baina ya miezi 18 na 52. 


Lakini kwenye hotuba yake ya usiku wa jana, Kanali Doumbouya alisema ameamuwa kuchukuwa njia ya kati kati. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) iliiweka Jumatatu iliyopita kuwa muda wa mwisho kwa utawala wa kijeshi wa Guinea kutoa ratiba inayokubalika ya kurejesha utawala wa kiraia, ama ukabiliane na vikwazo cha kiuchumi na kifedha.

ROYAL TOUR NI PONGEZI KILA KONA

 


RAIS ya Jumuiya wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu(TAHLISO), Frank Nkinda amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha uzinduzi wa filamu ya Royal Tour na kusisitiza kuwa Watanzania wote wapo nyuma ya jitihada anazozifanya kuitangaza Tanzania kimataifa.


Akizungumza ikiwa ni siku mbili tangu kuzinduliwa filamu hiyo uliofanyika jijini Arusha, Nkinda amesema kufanikisha hatua hiyo, Rais Samia anazidi kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuiletea maendeleo Tanzania kupitia sekta ya utalii.


Amesema kuzinduliwa filamu hiyo inayoonesha vivutio mbalimbali vya utalii na kiutamaduni, kutazidi kuongeza idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini kwa lengo la kuja kuvitazama, hatua ambayo itasaidia kukuza pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni.


Amewataka Watanzania wote kwa umoja wao kuendelea kumuunga mkono Rais Samia, ili aweze kutimiza malengo yake ya kuiletea nchi maendeleo, jambo ambalo pia litawezesha kuongezeka kwa kipato cha mtu mmoja mmoja.


Awali kabla ya kuzinduliwa kwa filamu hiyo Arusha juzi, Rais Samia alikuwa nchini Marekani aliposhiriki uzinduzi wa filamu hiyo ya Royal Tour katika Majiji mawili ya New York na Los Angeles.


Mtu mwingine mashuhuri aliyehudhuria ukiondoa mabilionea na wamiliki wa makampuni makubwa duniani ikiwemo watangazaji


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo juzi, Rais Samia alisema matarajio mara baada ya kuzinduliwa, idadi ya watalii nchini itaongezeka mara mbili zaidi ya ilivyo sasa na kuliongezea Taifa mapato yatokanayo na sekta ya utalii.


Baada ya uzinduzi huo mkoani Arusha ulioudhuriwa na watu takribani 5000, Mei 7  filamu hiyo ya Royal Tour   itazinduliwa Zanzibar na Mei 8 uzinduzi rasmi utafanyika Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere