Mbeya. Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mkoani Mbeya imesema wastani wa asilimia 21 ya wanafunzi 504 wa vyuo vikuu nchini waliopimwa wamebainika kuwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa huku wanaume wakiwa asilimia 14.
Mwanasayansi mtafiti kutoka NIMR, Dk Ruby Mcharo amesema hayo leo Jumatano Mei 4, 2022 wakati akitoa taarifa ya tafiti kwa Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi mara baada ya uzinduzi wa wimbo wa kuelimisha vijana na jamii kujikinga na magonjwa ya zinaa uliohusisha wanafunzi 63 katika shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza.
Amesema kuwa kumekuwepo na changamoto kubwa ya makundi ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 mpaka 21 kukutwa na magonjwa zinaa licha ya kuwepo kwa kampeni za utoaji elimu ya mara kwa mara ili kunusuru kundi hilo inayotolewa na watafiti kutoka NIMR kwa kushirikiana na wataalam wa afya.
''Tafiti za maambukizi kwa wanavyuo ni kubwa na changamoto kubwa ni kufanya ngono na zinaa zisizo salama na wameona sasa kuwafikishia elimu kwa njia za wimbo kwa makundi mbalimbali ''amesema.
Dk Mcharo ameongeza kuwa awali kulikuwepo kwa kampeni mbalimbali za uelimishaji ambazo hazijafanya vizuri hivyo wamekuja na mbadala mwingine wa kutoa elimu kwa njia ya wimbo kwa kushirikisha wanafunzi wa shule za sekondari, vyuo vikuu na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema kuwa kuna kila sababu kwa NIMR kuendelea kutoa elimu kwa jamii na wanafunzi mashuleni kuhusiana na kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na VVU hususan athari za mimba shuleni.
''Ninyi wanafunzi wa Loleza msikubali kufanya ngono zisizo salama na kuepuka kufanya umri wao bado wanahitaji kupata elimu na wakati wa kuyafanya hayo utafika huku akilaani kitendo cha baadhi ya wanafunzi katika Shule hiyo kuacha masomo kutokana na mimba za utotoni''amesema.
Amesema kuwa kupitia programu hiyo ni vizuri kushirikisha walengwa na makundi maalumu kwa mlengo wa kufikia malengo makubwa ya tafiti za magonjwa ya zinaa na VVU na kwamba Taasisi yake ya Maryprisca Women Empowerment Fund itaona namna ya kuwafikia.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua amesema kuwa Loleza imekuwa ikifanya vizuri sana katika masuala ya afya hivyo ni wakati sasa Taasisi hiyo kuongeza weledi kwa kutoa elimu bora ya kujikinga na magonjwa ya zinaa.
Mwanafunzi wa kodato cha sita ambao wako kwenye mradi huo, Catherine Mwajebele ameomuomba Naibu Waziri kuendelea kuwakumbuka na kuwashika mkono kupitia Taasisi yake ya Maryprisca Women Empowerment Fund.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.