ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 6, 2025

TAKUKURU TANGA YAOKOA FEDHA ZA SERIKALI MILIONI 76,048,459.1

 


Na Oscar Assenga,TANGA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefanikiwa kuokoa kiasi cha Milioni 76,048,459.1 baada ya kuwafikisha mahakamani waliokuwa watumishi wa umma kwa tuhuma za ubadhirifu na ufujaji wa Fedha za Umma katika wilaya za Kilindi, Korogwe na Tanga Jiji.

Tuhuma ambazo zilikuwa zinawakabili ni kutokuwasilisha fedha ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS na kuzitumia kwa manufaa yao pasipo kuwasilishwa sehemu husika kwa taratibu zilizowekwa.

Hayo yalisemwa leo na  Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Ramadhani Ndwatah wakati akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia mwezi Octoba hadi Desemba mwaka 2024.

Ambapo alisema kwamba baada ya kufikishwa mahakamani Jamhuri ilishinda kesi hiyo ambapo waliamriwa na mahakama kurejesha fedha kiasi hicho kwa mchanganuo mbalimbali.
Aidha alisema kwa wilaya ya Kilindi katika ufuatiliaji wa Jamhuri kushinda kesi za hujumu uchumi  namba 13,2023,11/2023 na 06/2024 dhidi ya watumishi ambao walishtakiwa kwa ubadhirifu kufuatia kutokuwasilisha fedha ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS na kuzitumia kwa manufaa yao pasipo kuwasilishwa sehemu husika kwa taratibu zilizowekwa.

“Fedha kiasi cha Sh Milioni 58,678,780.00 zilirejeshwa na watumishi hao kwa amri ya mahakama sambamba na adhabu nyengine “Alisema

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa alitaja wilaya nyengine kuwa wilaya ya Korogwe ambapo kiasi cha Milioni 9,198,045.31 ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS zilirejeshwa kwa amri ya mahakama kufuatia Jamhuri kushinda kesi za uhujumu Uchumi namba 09/2023 na 10/2023 dhidi ya watuhumiwa.

“Katika Jiji la Tanga Jamhuri ilishinda kesi za uhujumu uchumi namba 16558/2025 na 7/2023 ambapo Jumla ya Sh.Milioni 3,171,633.9 zilizofanyiwa ubadhirifu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya Elimu huku Milioni 5,000,000 ya mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu”Alisema.

Hata hivyo alisema kwamba fedha hizo zilirejeshwa na watuhumiwa kwa amri ya mahakama sambamba na adhabu nyengine .

“Tunatoa onyo kali kwa watu wote wanaofikiria kufanya hujuma ya aina yoyote katika matumizi ya rasilimali za umma  na tunawaasa waache tabia na fikra hizo mara moja na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya utendaji katika utumishi wa umma vyenginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”Alisema


Wednesday, February 5, 2025

UTENDAJI KAZI KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA TANESCO WAMKWAZA DKT. BITEKO

 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kutoridhishwa kwake na Kituo cha Huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kusema huduma duni zinasababisha malalamiko kutoka kwa wateja.

Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati wa Kikao cha Tatu cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2024 ikiwa ni utaratibu aliouanzisha kwa lengo la wa kujipima katika kila baada ya miezi mitatu ili kuboresha utendaji wa kazi wa Wizara na Taasisi zake.

“Pamoja na kazi zote nzuri mnazozifanya lakini eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni utoaji wa huduma kwa wateja, juzi nilitembelea kituo hiki nikawaambia sifurahishwi na utendaji kazi wa kituo,  mimi nafahamu changamoto za kituo hiki si kwa kuota bali wananchi wananipa mrejesho pamoja na viongozi wanaonisimamia, hivi tumefanya kazi yote hii ya kuwa na umeme wa ziada, tunajenga laini za umeme, lakini mtu  mmoja ambaye kazi yake ni kumsikiliza mteja na kumpa majibu sahihi anatupaint wote vibaya tunaonekana hatufai, majibu yapo lakini wataalam wanageuka kuwa wababe kwa wateja, hii hakubaliki.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ametolea mfano lalamiko la mwananchi la kupiga simu TANESCO kisha akapewa tiketi namba ya lalamiko lakini baada ya muda tiketi namba hiyo ilifutwa kwa madai kwamba lalamiko husika limeshashughulikiwa huku ikiwa sikweli, hata hivyo baada ya mteja kuuliza kwa nini lalamiko lake limefutwa aliishia kufokewa.

Kutokana na hilo, Dkt.Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuchukua hatua kwa mtaalam aliyehusika na suala hilo na endapo TANESCO haitachukua hatua ifikapo ijumaa wiki hii, atachukua hatua huku akisisitiza kwamba heshima kwa wananchi lazima iwepo na Wataalam wa Kituo cha Huduma kwa wateja wanapaswa kuwapa majibu stahiki na ya staha wananchi na wawe ni sehemu ya kutatua shida za wananchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameziagiza Taasisi zote chini ya Wizara ya Nishati kuupa kipaumbele Mpango wa Mahsusi wa Nishati (Energy Compact) ambao ulisainiwa katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika tarehe 28 Januari 20225 ambao pamoja na masuala mengine ya nishati, umelenga kusambaza umeme kwa watanzania milioni 8.3 ifikapo 2030.

“Kila mmoja kwa nafasi yake ajipange atatekeleza vipi hii Energy Compact, fedha hizi mlizosikia zimetolewa na wadau wa maendeleo kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika zinahusu Bara lote la Afrika, hazitakuja Tanzania pekee hivyo lazima tujipange jinsi ya kupata hizi fedha ili kutekeleza miradi tuliyopanga kuifanya na tumheshimishe Rais, Dkt. Samia kwa kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji Mpango huu mahsusi ambao ni muhimu katika Sekta yetu ya Nishati.” Amesema Dkt. Biteko

Aidha, ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kwamba kazi ya usambazaji wa  nishati safi ya kupikia vijijini inaenda sambamba na  tathmini ya idadi ya watu wanaohama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi na Taasisi ijipange kuhakikisha kwamba ifikapo  mwaka 2030 asilimia 75 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Katika Kikao hicho cha Tathmini, Dkt. Biteko pamoja na Wizara ya Nishati walitoa zawadi kwa Taasisi zilizoshika nafasi za juu katika utendaji kazi ambazo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) iliyoshika nafasi ya kwanza, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulioshika nafasi ya Pili na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ulioshika nafasi ya Tatu. 

Pia ametoa zawadi kwa mikoa ya Kitanesco iliyofanya vizuri katika utendaji kazi ambayo ni Kilimanjaro (I), Kinondoni Kusini (II) na Kinondoni Kaskazini (III).

Kwa upande wake,, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameeleza kuwa  vikao vya tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake ambavyo muasisi wake ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati vimeleta matokeo chanya kwa kuleta mabadiliko ya utendaji kazi kwa Wizara na Taasisi zake.

Amepongeza Watendaji wa Wizara na Taasisi zake kwa kazi kubwa inayofanyika na inayoonekana katika macho ya wananchi ikiwemo uwepo wa nishati.

Mhe. Kapinga amewaasa watendaji na watumishi wa Wizara na Taasisi zake kufanya kazi kwa umoja na kwa kujitoa ili kuendelea kumheshimisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pamoja na Sekta ya Nishati kwa ujumla.

Taasisi zilizoshiriki Kikao cha Tatu cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Wizara na Taasisi zake ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja ( PBPA),  Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania

( TGDC).


Viongozi wa Wizara walioshiriki Mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio pamoja na Menejimenti ya Wizara.



KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI MAWASILIANO, ARDHI NA NISHATI ZANZIBAR YAIPONGEZA TASAC.

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar, imelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa utendaji kazi madhubuti katika usimamizi wa sheria na kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira wa usafiri majini.


Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahya Rashid Abdulla, leo tarehe 03 Februari 2025, walipotembelea Ofisi za TASAC mkoani Tanga na kufanya kikao na watumishi wa TASAC pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).

"Tumefurahishwa na utendaji kazi mzuri wa TASAC katika udhibiti na usimamizi wa safari kwa njia ya maji hasa katika Bandari hii ya Tanga ambayo kwa kiasi kikubwa imerahisisha usafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani kwa eneo hili la mwambao ambalo lilikua na changamoto kubwa ya usafiri kwa njia ya maji,” amesema Mhe. Abdulla.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, Meneja Mafunzo na Utoaji vyeti Mha. Lameck Sondo ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendeleza weledi, ufanisi na mashirikiano katika kudhibiti shughuli za usafiri majini kwa maslahi mapana ya Taifa.


Mha. Sondo ameongeza kuwa TASAC inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria ambao ni mradi wa ushirikishwaji wa nchi za Uganda na Tanzania katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na ujenzi wa kituo kikuu cha uratibu wa masuala ya Utafutaji na Uokozi (MRCC) katika Ziwa Victoria.


Aidha, ameelezea kufanikiwa katika ukaguzi wa meli za kigeni, pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya kuwajengea uwezo watumishi wake katika kutekeleza majukumu hayo ya kiudhibiti.


Kamati hiyo inafanya ziara hiyo lengo la kujifunza utendaji kazi pamoja na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAC na TPA mkoani Tanga ikiwemo Bandari za Tanga, Pangani na Kipumbwi.
Picha ya pamoja.
Kamati hiyo inafanya ziara hiyo lengo la kujifunza utendaji kazi pamoja na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAC na TPA mkoani Tanga ikiwemo Bandari za Tanga, Pangani na Kipumbwi.

Monday, February 3, 2025

MNEC HAMOUD AIKOMBOA JUMUIYA YA WAZAZI KIBAHA MJI KWA MIFUKO 100 YA SARUJI

 
NA VICTOR MASANGU, PWANI

Mjumbe wa Halmashauri kuu  ya Chama cha mapinduzi (CCM) Taifa Taifa Hamoud Juma (MNEC) kupitia wazazi katika juhudi za kukiimarisha chama ameahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa jumuiya wa wazazi Wilaya ya Kibaha mjini.
 
Juma  ametoa ahadi hiyo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika kufunga rasmi kikao cha baraza la jumuiya ya wazazi Wilaya ya Kibaha  mjini kilichohudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama cha mapinduzi (CCM)  pamoja na jumuiya zake sambamba kwa  lengo la kuweza  kubadilishana mawazo na kuweza kuweka mikakati  kabambe ya kuimarisha na kuijenga jumuiya hiyo kuanzia ngazi za chini.
Alisema kwamba lengo lake lake kubwa ni kuhakikisha kwamba anashirikiana bega kwa bega na jumuiya ya wazazi ndio maana ameamua kuchangia mifuko 100 ya saruji ambayo itaweza  kusaidia kwa kiasi  kikubwa katika ujenzi wa nyumba ya mtumishi na kwamba ataendelea kuwapa sapoti katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo.

"Kwa upande wangu mimi nimefarijika sana kuweza kunialika katika kikao cha baraza  kuna mambo mengi ambayo mmeyasema na mimi kwa kushirikian na wenzangu tutaona namna ya kufanya ili lakini mimi katika kuwaunga mono nitachangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mtumishi kwani hii ni moja ya hatua kubwa katika kuimarisha jumuiya yetu ya mtumishi kuwa na nyumba ikiwa saambamba na kuitangaza jumuiya yetu,"alisema Juma.

Pia alimpongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuweza kuteuliwa na mkutano mkuu maalumu kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Urais pamoja na mgombea mwenza  Dkt. Emmanuel Nchimbi kwani wajumbe wamemekuwa na imani nao kubwa katika  katika uchaguzi mkuuu wa mwaka wa 2025.

Aidha Juma ameitaka jumuiya ya wazazi kuhakikisha kwamba wanakuwa na umoja na mshikamano sapoti ya kutosha viongozi waliopo madarakani wakiwemo madiwani, pamoja na wabunge wafanya kazi zao katika kutekeleza ilani ya chama mpaka hapo muda wao utakapofika na sio kuanza kuwaingilia katika majukumu yao.

Katika hatua nyingine  katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 amewahimiza wagombea wote katika nafasi  za udiwani na ubunge kuhakikisha kwamba wanaheshimu kauli ya Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukemea vikali vitendo vya kufanya kampeni za chini chini kabla ya muda wake kwani ni kinyume kabisa na utaratibu wa chama cha mapinduzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Kibaha mjini Yahaya Mtonda ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ambayo wamepatiwa na kwamba atahakikisha wanajipanga imara kuanzia ngazi za chini kwa ajili ya kumpa sapoti kubwa Rais Samia Suluhu pamoja na mgombea mwenza ili waweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025.

NACHINGWEA WATOA ZAIDI YA MILIONI 800 MIKOPO YA ASILIMIA 10 ZA MAPATO YA NDANI

 

Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo akimkabidhi funguo ya Trekta katibu wa kikundi cha wanawake Khadija Said Ng'ombo walilopewa na Halmashauri ya Nachingwea kutokana na mkopo wa asilimia 10 uliotengwa na Halmashauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo akiwa analiwasha Trekta lilitolewa na Halmashauri ya Nachingwea kutokana na mkopo wa asilimia 10 uliotengwa na Halmashauri hiyo

Na Fredy Mgunda, Nachingwea Lindi 

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, ameongoza hafla ya utoaji mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, ambapo zaidi ya shilingi milioni 800 zimetolewa kwa vikundi 60 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Lengo kuu la mikopo hii ni kuwasaidia wananchi wa kundi hili kujikwamua kiuchumi na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hafla hiyo, Moyo alisisitiza umuhimu wa kufuata kanuni za utoaji mikopo kwa kuhakikisha usawa, haki na ufanisi katika usambazaji wa fedha hizi. Alionya dhidi ya kurejesha mikopo kupitia njia zisizo rasmi kama vile ofisi za kata au maafisa maendeleo ya jamii, akisema kuwa mchakato wa kurejesha utahakikisha uwazi na utaratibu wa kisheria.

Mikopo hii imetolewa kwa awamu ya kwanza chini ya kaulimbiu "Pochi la Mama Limefunguka", ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kufanyika marekebisho kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka 2023 kama vile vikundi hewa na kushindwa kwa baadhi ya vikundi kurejesha mikopo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea, ndugu Joshua Mnyang’ali, alielezea kuwa vikundi 33 vya wanawake vimepata Shilingi Milioni 365, vikundi 22 vya vijana vimepata Milioni 375, na vikundi 5 vya walemavu vimepata Milioni 60. Alisema kwamba usimamizi mzuri wa mikopo ni muhimu ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati na faida inapatikana kwa wote.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Adinan Mpyagila, alikumbusha wanufaika kutimiza majukumu yao kwa kutumia mikopo kwa malengo yaliyoainishwa na kurejesha kwa wakati ili kuwezesha wanufaika wa awamu zijazo kupata mikopo hiyo kwa urahisi.

Wanufaika wa mikopo hiyo walishukuru Serikali kwa msaada huo na walieleza kujitolea kwao kurejesha mikopo kwa wakati ili wafaidi wengine. 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Halmashauri, wanufaika, na wadau wa maendeleo ya jamii.

Sunday, February 2, 2025