Lwakatare alikamatwa juzi makao makuu ya
chama hicho na kupelekwa katika Makao Makuu ya Polisi kwa mahojiano.
Bakari Kiango na Nuzulack Dausen, MWANANCHI
Polisi wamezidi kumbana Mkuu wa Usalama
wa Chadema, Wilfred Lwakatare baada ya kupekua nyumbani kwake kwa siku ya pili
mfululizo.
Lwakatare, ambaye ni mbunge wa zamani wa
Jimbo la Bukoba Mjini kupitia CUF, alikamatwa juzi mchana kwa kutuhumiwa kwa
kufanya uchochezi wa uvunjifu wa amani baada ya kunaswa kwenye picha ya video
iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii.
Upekuzi wa pili
Nyaronyo Kicheere, ambaye ni Mwanasheria
wa Lwakatare, aliliambia gazeti hili jana kuwa mteja wake, ambaye anashikiliwa
na polisi hao, alipelekwa nyumbani kwake Kimara-King’ong’o jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya upekuzi huo.
Ilikuwa mara ya pili kwa Lwakatare
kupekuliwa kwani mara ya kwanza ilikuwa juzi jioni baada ya kuhojiwa Makao
Makuu ya Jeshi la Polisi. Lwakatare, ambaye alitolewa Kituo cha Kati cha
Polisi, alipelekwa jana kwa msafara wa magari mawili ya polisi chini ya ulinzi
mkali.
Nyaronyo alisema kuwa msafara huo
uliondoka saa 10.00 jioni kwa ajili ya safari hiyo ya Kimara wakitokea katikati
ya Jiji la Dar es Salaam kilipo Kituo cha Kati cha Polisi. Alisema kuwa uamuzi
huo ulifikiwa baada ya kikao kizito kati ya maofisa wa Idara ya Upelelezi (DCI)
na wale wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).
“Hawa watu walikuwa na kikao kirefu siku
nzima ya leo (jana) nadhani walikuwa wanaangalia kama kuna uwezekano wa
kumshtaki au la mteja wangu.Walipomaliza kikao waliamua turudi tena nyumbani
kwa Lwakatare ili kuendelea na upekuzi,” alieleza Kicheere.
Kama ilivyokuwa juzi, upekuzi kwa
Lwakatare uliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Obadia Jonas.
Polisi wanasemaje
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema
kuwa bado wanaendelea kumshikilia Lwakatare huku wakiendelea na uchunguzi wa
suala hilo. “Kama kukiwa na taarifa za ziada nitawajulisha msiwe na wasiwasi,”
alisema Senso na kukata simu.
Lwakatare alikamatwa juzi saa saba
mchana katika makao makuu ya chama hicho na kupelekwa katika Makao Makuu ya
Polisi kwa mahojiano.
Juzi siku nzima mitandao ya kijamii
ilikuwa imetawala na habari picha ya video ikimwonyesha Lwakatare akidaiwa
kupanga mikakati ya kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky kwa
madai kuwa anashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, kutengeneza
migogoro.
Pia, Lwakatare alionekana akitoa
maelekezo kwa watu , ambao sura zao hazikuonekana, akiwataka kufuatilia nyendo
za Msacky.
Chadema wapinga
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa alisema mkanda wa video unaoonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii
ukimwonyesha Lwakatare akipanga njama za uhalifu hauna uhalisia na kwamba huo
ni uzushi ulioratibiwa na kufanikishwa na vyombo vya dola.
Pia Dk Slaa alidai kuna mpango mwingine
kabambe unaofanywa na idara za dola kuhakikisha kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa anakamatwa kutokana na sumu anazotema bungeni na
kwingineko dhidi ya Serikali.
Dk Slaa alisema kuwa taarifa za kuwapo
njama za kukichafua chama chake kupitia mkanda huo wa video alizipata kutoka
ndani ya Serikali Jumatatu iliyopita hata hivyo, wakati akiendelea kupanga
mkakati wa kushughulikia tayari ulikuwa umeshaingizwa katika mitandao ya
kijamii.