ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, May 14, 2016

SWAHILI FOOD FESTIVAL NI LEO MWANZA.

Swahili Food Festival
Kama ni burudani kutoka WCB team Wasafi Raymond atakuwa pale eneo la tukio Rock City Mall Mwanza. Wasanii wengine ni Mirror Rhymes, Edu Boy na wengine wakali kibao.

Mziki mzuri toka Jembe Djz, na Mc wa mpango mzima ni Mbaba Vc na Bonz Balaa.
Kama ni misosi....Misosi yote inahusika toka bara hadi pwani.....

MWIGULU NCHEMBA KUWAKABIDHI YANGA KOMBE LEO TAIFA.

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba Madelu leo Jumamosi Mei 14, 201 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda na Young Africans katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya Nchemba ambaye atakabidhi Kombe kwa Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16, wageni wengi maalumu watakaokuwa kwenye mchezo huo ni Mkurugenzi wa Vodacom, Ian Ferrao sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ya Kuu Tanzania Bara (TBLB).

Mchezo huo utafanyika kwa baraka za TPLB baada ya maombi ya Young Africans kukubaliwa na Ndanda ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni.

Mara baada ya mchezo huo, Mabingwa Young Africans watapewa Kombe la ubingwa, medali na fedha Sh 81,345,723; Mshindi wa Pili Sh 40,672,861; Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 na Mshindi wa Nne atazawadiwa Sh 23,241,635.

Mcehzaji Bora atapewa Sh 5,742,940 sawa na Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom, Bia ya Kilimanjaro, Azam, Startimes na NHIF. Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 saw na Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.

Young Africans ndiyo iliyoomba kwa Ndanda kadhalika TPLB kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa kusafiri kwa ndege Jumapili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola utakaofanyika ama Mei 17 au 18, mwaka huu.

Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF imesema kwamba Young Africans watatumia mchezo huo ambao Ndanda itakuwa mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara litakalotolewa na Nchemba ambaye mara nyingi anaonekna uwanjani.

Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu, timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi, utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,” inasehemu kanuni hiyo. Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za yanga ambazo Ndanda na Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es Salaam.

Tayari Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameipongeza timu ya soka ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.

Hii ni mara ya 26 kwa Young Africans ambayo kwa sasa inacheza mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutwaa taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.

“Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa. Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,” amesema Rais Malinzi baada ya Young Africans kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.

RAIS MAGUFULI AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA UWANJA WA NDEGE DAR ES SALAAM.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One) Dar es salaam.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Mei, 2016 alipofanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo na kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maafisa wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere waliokuwa wakitoa maelezo juu ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo, walikuwa wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi, hali iliyosababisha Dkt. Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja.

“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa huwezi ukajiuliza? eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi miwili."Dkt. Magufuli aliwahoji Maafisa wa uwanja wa ndege.

“Kwa hiyo mizigo inayoingia humu huwa hamuikagui kwa namna yoyote ile, kwa hiyo mtu nikiamua kuja na madawa yangu ya kulevya, nikaja na dhahabu zangu, na almasi zangu na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu” Rais Magufuli aliendelea kuwabana maafisa hao wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara hii ya kushtukiza mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akitokea Jijini Kampala nchini Uganda ambako jana alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.



UPDATES ZA MSIBA WA MTOTO WA ANKAL: MWILI UMESHAWASILI DAR ES SALAAM, MAZISHI LEO JUMAMOSI SAA 10 ALASIRI MAKABURI YA KISUTU

Assalaam Aleikhum,
Updates za familia ya Ankal Issa Michuzi iliyopatwa na msiba wa kuondokewa na Mtoto wa Ankal, Maggid Muhidin (18),  aliyefariki Jumapili Mei 8, 2016 huko Durban, Afrika Kusini:

Mwili wa Marehemu umeshawsili  nchini jana Ijumaa Mei 13, 2016 majira ya saa tisa  mchana kwa  ndege ya shirika la Emirates kupitia Dubai (kwa kukosekana kwa  ndege za moja kwa moja kuja nchini kutoka Durban). Mwili wa kijana wetu umepokelewa na ndugu, jamaa, majirani na marafiki katika   uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius  Nyerere eneo la Cargo la Swissport, Jijini Dar es salaam.
Mazishi yamepangwa  kufanyika leo  Jumamosi saa 10  alasiri katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam. Taratibu  za kuandaa mazishi zitaanza  saa 4 asubuhi leo  Jumamosi, nyumbani  kwa mama wa marehemu kota za Wazo Hill, Tegeta, ulipo msiba.
 Jeneza lenye mwili wa marehemu Maggid baada ya kuwasili Dar es salaam jana Ijumaa
Ankal akiwa na ndugu, jamaa na  marafiki mara baada ya kuwasili na mwili wa marehemu katika msikiti wa Maamur, Upanga, Dar es salaam, ambako unahifadhiwa hadi baadae leo kabla ya kupelekwa Wazo Hill saa nne kwa dua na baadaye kurudi hapo msikitini kuswaliwa na hatimaye kupelekwa makaburi ya Kisutu kwa mazishi saa 10 Alasiri.


Ankal akiwa na ndugu, jamaa na  marafiki mara baada ya kuwasili katika msikiti wa Maamur, Upanga, Dar es salaam


Ankal akiwa msibani Wazo Hill na wanahabari wenzie usiku huu. Kutoka kushoto ni Faraja Mugwabati, Maggid Mjengwa na Sufiani Mafoto.

NAMNA YA KUFIKA MSIBANI
Ukitokea Tegeta Kibaoni kama unaelekea Kiwanda cha Cement cha Wazo Hill, mbele mkono wako wa kulia kuna Kanisa la KKKT na ukienda mbele tena kidogo, utaona Bar yenye uzio wa rangi ya njano ambao umeandikwa "Twiga Cement",  hapo pana bango linaloelekeza njia karibu na kituo cha Bajaji nje. Unaingia upande huo wa kulia mita 250 mbele unakata tena kulia, mita 70 mbele utakuta maturubai, ndipo msibani.
Innalillah wa inna ilayhi raajiun
-AMIN.

MAGAZETI YA LEO:> RAIS MAGUFULI ATUA DAR, AIBUA MADUDU. KUBENEA ABANWA BUNGENI. LIPUMBA AMVAA RAIS MAGUFULI. MAPATO HOSPITALI YANUKA UFISADI.


Rais Magufuli atua Dar, aibua madudu. Kubenea abanwa bungeni. Lipumba amvaa rais Magufuli. Mapato hospitali yanuka ufisadi;  


Nape: Mchakato sheria ya habari mbioni kukamilika. Sukari ya viwandani yafurika . Zitto, Mdee ,Heche washtakiwa kwa fujo.

SERIKALI YASITISHA AJIRA ZA MAJESHI.

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesitisha kwa muda ajira zote kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vilivyomo ndani ya wizara hiyo, ikiwemo Jeshi la Polisi ili kupitia upya utaratibu wa kutoa ajira na kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), aliyetaka kufahamu ni kwa nini Serikali inasitisha ajira katika Jeshi la Polisi, wakati bado nchi inakabiliwa na uhaba wa askari ndani ya jeshi hilo wakiwemo askari wa kike.

“Tumesitisha kutoa ajira ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza na kupata ajira ndani ya vyombo vilivyo chini ya wizara hiyo,” alisisitiza.

Miongoni mwa vyombo hivyo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mbali na Jeshi la Polisi ni Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uhamiaji. Mbali na Komu, Mbunge mwingine ambaye ni wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema), alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha askari wasio na sifa wanachukuliwa hatua, ambapo pia alitaka kufahamu utaratibu wa uhakiki vyeti vya askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi umefikia wapi.

Akizungumzia Jeshi la Polisi, Masauni alisema Jeshi la Polisi limo kwenye utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria askari wachache, wanaochafua taswira na kazi nzuri inayofanywa na Polisi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwa kujihusisha na vitendo vinavyokinzana na maadili.

Kuhusu uhakiki wa vyeti, waziri huyo alielezea kuwa, uhakiki huo unahusu askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi unaendelea na mpaka sasa, askari 19 wamechukuliwa hatua za kisheria baada ya kugundulika kuwa walipata ajira kwa njia zisizokubalika.

Kuhusu uhaba wa askari wa kike, Waziri huyo alikiri kuwa kuna uhaba wa askari wa kike katika Jeshi la Polisi na kutoa mwito kwa wanawake wahamasike zaidi kujiunga na vyombo vya usalama.

Mwaka jana Idara ya Uhamiaji iliyokuwa chini ya Wizara hiyo, ililazimika kufuta ajira mpya 200 za makonstebo na makoplo, baada ya kubaini upatikanaji wa ajira hizo, ulifanyika kwa upendeleo.

Friday, May 13, 2016

JHIZI NDIZO HATUA ZILICHUKULIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MWANZA JUU YA MAUAJI YA WATU 7 WILAYANI SENGEREMA.

Kwamba tarehe 11.05.2016 siku ya jumatano majira ya saa 03:45hrs usiku katika Kijiji na Kata ya Sima Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza, watu wawili wasiofahamika majina wakiwa na mapanga walivunja mlango na kuingia kwenye nyumba ya Mama Eugenia Philipo miaka 60, akiwa amelala na familia yake na  kuwakata mapanga sehemu mbalimbali za miili yao hadi kufariki papo hapo, Mama mwenye Kaya Bi Eugeni, Mdogo wake, Watoto, pamoja na watu wengine wawili waliokua wakifanya kazi hapo nyumbani kwao wakitokea Ngara Mkoani Kagera.

Waliouawa 1. Eugenia Philipo miaka 60 Mama mwenye Kaya, 2. Maria Philipo miaka 50, mdogo wa Mama Mwenye Kaya 3.Mabula Makeleja miaka 20 mwanafunzi wa kidato cha nne, 4. Mkiwa Philipo mika 12, mwanafunzi shule ya msingi 5. Leonard Aloyce miaka 13 mwanafunzi shule ya msingi sima wote wa familia moja na 6. Donald miaka 40, pamoja na 7. Samson miaka 23 wakazi wa Ngara waliokuwa wakifanyakazi hapo nyumbani kwa Bi Eugeni.

Aidha katika utekelezaji wa mauaji hayo watu hao walianza kuingia kwenye nyumba walipokuwa wamelala watoto wa familia hiyo pamoja na wafanyakazi, na baada ya kuwakata mapanga hadi kuwaua waliingia kwenye nyumba ya jirani alipokuwa amelala Mama mwenye Kaya na mdogo wake Bi Maria na kuwaua vivyo hivyo, kisha wakaondoka eneo la tukio na kwenda kusiko julikana. Huku watoto wengine wanne wakinusurika kwenye mauaji hayo baada ya kujificha chini ya uvungu wa kitanda.

Jeshi la Polisi linawashikilia watu nane kwa mahojiano dhidi ya mauaji hayo na msako mkali wa kuwasaka wahusika wengine waliohusika kwa namna yeyote katika mauaji hayo bado unaendelea. 

Chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana, uchunguzi bado unaendelea. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawaomba wananchi wenye mapenzi mema na nchi yao watusaidie kutupa taarifa za wahusika wa  mauaji hayo ili tuweze kuwakamata.

Imetolewa na:

SACP: AHMED MSANGI                         
KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA

MAGAZETI YA LEO.


Jipu la sukari laibua mazito, JPM walioua familia moja wakamatwe haraka,  Serikali yajipanga kuzika matibabu ya kwenda India.  

Kilo milioni 6 za sukari zanaswa Dar, Chadema waungana na CUF kutomtambua Dk shein, Wabubge wanawake upinzani wajitoa TWPG. Rais Magufuli awavutia Waganda, Kanisa lalaani waficha sukari, Mdee akomalia “u baby”. Bunge laungana vifo vya akina mama. 

Thursday, May 12, 2016

RAIS YOWERI MUSEVENI AAPISHWA

Yoweri Museveni leo ametawazwa rasmi kuwa Rais mpya wa Uganda kwa muhula wa tano mfululizo.Tayari Rais Museveni amekwisha tawala miaka 30. Kutawazwa kwake leo, ambako kunashuhudiwa na viongozi wa mataifa 14 kutoka Afrika na wageni wengine mashuhuri, kuna fuata ushindi uliojaa ubishani katika uchaguzi wa Februari 18.
Yoweri museveni amkaribisha rais wa Zimbabwe,Omar el bashir wa Sudan.
Miongoni mwa marais wanaohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na rais wa Sudan Omar el Bashir anayeswaka na mahakama ya uhailifu wa kivita ICC kwa madai ya kutekeleza uhalifu katika eneo la Darfur na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.
Jeshi la Uganda latoa heshima zao kwa rais Museveni hivi sasa.
Leo rasmi imetangazwa kuwa siku ya mapumziko ili watu watokeze kwa wingi kwa sherehe hizo. Ingawaje bado kuna hali ya wasiwasi kwa vile chama cha upinzani na FDC na mgombea urais wa zamani Dk Kizza Besigye bado wanakana ushindi wa Museveni.
Rais Yoweri Museveni kuapishwa kuwa rais kwa muhula wa saba mfululizo nchini Uganda
Museveni kumkabidhi madaraka Museveni si jipya kwa Waganda. nani Rais ambaye alilaumu mwaka 1986, viongozi wa Afrika kukaa madarakani kwa muda mrefu sana.
CHANZO: BBC SWAHILI.

SHIRIKA LA NDEGE LA ETHIOPIA AIRLINES KUSAFIRISHA ABIRIA WAENDAO TAMASHA LA ZIFF.

???????????????????????????????????? Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha la ZIFF, Profesa Martin Mhando (Wa pili kutoka kushoto) akitia saini makubaliano baina ya ZIFF na shirika la ndege la Ethiopia. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mkuu wa Shirika la ndege la Ethiopia Tanzania na Comoro, Bi Milat Mekonen. Wengine wanaoshuhudia ni viongozi wa viongozi wa ZIFF na Ethiopia Airlines.???????????????????????????????????? Meneja wa Tamasha la ZIFF, Dean Nyalusi (kushoto) na Afisa Masoko mwandamizi wa shirika hilo la Ethiopia, Bi. D'Silva wakiisaini mkataba huo wa ushirikiano.???????????????????????????????????? Meneja wa Tamasha la ZIFF, Dean Nyalusi (kushoto) na Afisa Masoko mwandamizi wa shirika hilo la Ethiopia, Bi. D'Silva wakiisaini mkataba huo wa ushirikiano 2Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha la ZIFF, Profesa Martin Mhando na Meneja Mkuu wa Shirika la ndege la Ethiopia kwa Tanzania na Comoro, Bi Milat Mekonen wakikabidhiana nyaraka baada ya kumaliza kutiliana saini za makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, mapema leo Mei 12.2016. Wengine wanaoshuhudia ni viongozi wa viongozi wa ZIFF na Ethiopia Airlines ???????????????????????????????????? Meneja Mkuu wa Shirika la ndege la Ethiopia kwa Tanzania na Comoro, Bi Milat Mekonen akielezea machache wakati wa hafla hiyo leo jijini Dar es Salaam. DSC_3104Tukiohilo likiendelea leo Jijini Dar es Salaam . (Picha zote na Andrew Chale,Modewjiblog).

Shirika la ndege la Ethiopia Ethiopia Airlines limeingia mkataba wa kusafirisha abiria waendao katika tamasha la filamu la Kimataifa la Zanzibar maarufu kama (ZIFF) ndani ya mwezi Julai mwaka huu.

Uongozi wa juu ya ZIFF na Shirika hilo la ndege, mapema leo Jijiji Dar es Salaam, wamesema kuwa, usafiri wa ndege utakuwa rahisi baada ya shirika la ndege la Ethiopia kutoa punguzo la bei kwa wasafiri wote waendao kwenye tamasha hilo huko Zanzibar.

Akizungumza katika hafla za kutia saini makubaliano rasmi kati ya ZIFF na Ethiopian, Meneja Mkuu wa Ethiopian mjini Dar es Salaam, Bi Milat Mekonen, alisema kuwa shirika lake litatoa tiketi 5 kwa wageni mashuhuri wa ZIFF mwaka huu.

“Shirika liliamuwa kuwa mdhamini wa tamasha ili kuongeza kasi ya ukuwaji wa tasnia ya filamu Tanzania, na Afrika, na kuzidisha huduma zake na kujitangaza kwa wateja.

ZIFF ndio tamasha kubwa kuliko yote hapa Afrika ya Kati na ya Mashariki likiwafikia wadau zaidi ya 100,000 na kuwavutia watalii wasiopungua 6000 kila mwaka. Tamasha ni kivutio kikubwa cha watalii toka nje na ndani likichangia uchumi wa Zanzibar ambao unaotegema sana utalii. Kwa sababu hiyo kudhamini tamasha kunatoa fursa kubwa kwa mashirika kujitangaza na kutambulisha biashara zao.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa tamasha Profesa Martin Mhando alisema, “Udhamini huu ni muhimu kwa ZIFF maana misaada ya kifedha kwenye shughuli za kitamaduni imepungua sana kwa hiyo mashirika ya kibiashara yanaweza kutumia fursa za matamasha kama ZIFF kukuza biashara zao. Alisema hilo ni jambo la kawaida sana duniani na tunawashukuru Ethiopian kwa kuwa mfano kwa mashirika mengineyo”.


Tamasha litakuwepo kati ya tarehe 9 na 17 Julai Visiwani Zanzibar na filamu na muziki unatarajiwa kupamba. Pia ni miongoni mwa matamasha makubwa kwa ukanda huu wa Afrika na Duniani kwa ujumla ambapo watu mbalimbali kutoka Duniani kote ukusanyika visiwani humo.

WATANO WAINGIA FAINALI ZA AIRTEL TRACE MUSIC STARS.

Afisa Uhusiano wa Airtel Bi Jane Matinde (wa pili kulia) akimpongeza  Nandi Charles mmoja ya  kati ya washiriki waliochaguliwa kuingia katika tano bora katika fainali ya  shindano la Airtel Trace Music Stars zitakazofanyika tarehe 20 mei 2016 hapa jijini Dar es Saalam. Pichani ni washiriki wengine walioingia tano bora  ambao ni (kulia) Benny Sule akifatiwa na  Melisa Elina John (kushoto) ni Salim Mlindila akifatiwa na Nicole Grey.
Mkufunzi na Mwalimu wa Sauti Tony Joett akitoa mafunzo ya sauti kwa washiriki waliochaguliwa kuingia tano bora katika fainali za  shindano la Airtel Trace Music Stars zilizopangwa kufanyika tarehe 20 mei 2016 hapa jijini Dar es Saalam. . Mshindi ataondoka na zawadi ya shilingi milioni 50 na kupata nafasi ya kuiwakisha Tanzania katika mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Nigeria
Afisa Uhusiano wa Airtel Bi Jane Matinde (wa pili kulia) wakijipongeza kwa pamoja na washiriki waliochaguliwa kuingia tano bora katika  shindano la Airtel Trace Music Stars ambapo fainali zake zitakafanyika tarehe 20 mei 2016 hapa jijini Dar es Saalam. Mshindi ataondoka na zawadi ya shilingi milioni 50 na kupata nafasi ya kuiwakisha Tanzania katika mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Nigeria
washiriki waliochaguliwa kuingia tano bora katika  shindano la Airtel Trace Music Stars wakifurahia ushindi huo uliowapa tiketi ya kuingia katika fainali zitakafanyika tarehe 20 mei 2016 hapa jijini Dar es Saalam. Mshindi ataondoka na zawadi ya shilingi milioni 50 na kupata nafasi ya kuiwakisha Tanzania katika mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Nigeria.  Kutoka kushoto ni Benny Sule, Nicole Grey, Salim Mlindila,  Nandi Charles na Melisa Elina John

Press Release
Watano waingia kwenye fainali za Airtel Trace Music Stars
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel leo imetangaza washiriki waliongia kwenye tano bora katika shindano kubwa Afrika la kusaka vipaji vya muziki lijulikanalo kama Airtel Trace Music Stars.

Ikiwa ni miezi mitatu tangu kuanza kwa msimu wa pili wa shindano la Airtel Trace Music Stars na kushirikisha  maelfu ya vijana wa kitanzania, Airtel imetangaza majina ya washiriki wa tano bora walioingia kwenye fainali za kitaifa ambao ni pamoja na Benny Sule, Nicole Grey, Nandi Charles, Melisa Elina John na Salim Mlindila.

Washiriki hawa walichaguliwa na jopo la majaji  mahiri akiwemo mtangazaji wa TV mahiri, Mwanamuzi, Mwigizaji na msanii aliyejikita katika maeneo mengi, Jokate Urban Mwegelo,  mtunzi wa nyimbo na mwalimu wa sauti Tony Joett pamoja na mtengenezaji wa Muziki na mfanyabiashara Luciano Gadie Tsere.
   
Akitangaza walioingia tano bora, Afisa Uhusiano wa Airtel , Jane Matinde  aliwapongeza washiriki hao kwa kufika katika hatua ya fainali na kusema “ msimu wa pili wa shindano la Airtel Trace Music Stars umekuwa ni wa mafanikio makubwa na leo tunayo furaha kutangaza majina ya washiriki waliofanya vizuri zaidi na kuwa kwenye nafasi ya kushinda na  kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Airtel Trace Music Stars ya Afrika”.

“Tunaamini Airtel Trace Music Stars ni  Fursa muhimu ya kuwainua wanamuziki chipikizi kuweza kuonyesha vipaji vyao na hatimae kuzifikia ndoto zao. Airtel itaendelea kuwawezesha vijana wa kitanzania kutambua uwezo wao na kuishi ndoto zao na shindano hili la Airtel Trace Music Stars ni kielelezo tosha cha dhamira hii”. Aliongeza Matinde

Kwa upande wake mmoja ya washiriki waliotinga tano bora , Benny Sule alionyesha furaha yake ya kufika katika finali na kusema “ mashindano haya yamenipa Fursa kubwa kiasi ambacho nashindwa kuelezea. Nimejipanga vyema kushiriki katika fainali zinazofanyika wiki ijayo na natumaini kushinda na kuiwakilisha vyema nchi yangu

Aliongeza kwa kusema “Huu ni mwanzo mzuri wa safari yangu ya kuwa mwanamuziki nyota ndani na nje ya nchi. Nawashukuru sana Airtel kwa mpango huu ambao umewawezesha vijana wengi barani Afrika  kuonyesha vipaji vyao na kuzifikia ndoto zao.”

Washiriki waliongia tano bora wanategemea kushindana katika kinyanganyiro cha mshindi wa Airtel Trace Music Stars wa Tanzania katika finali zitakazofanyika tarehe 20 Mei 2016.  Mshindi ataondoka na zawadi ya shilingi milioni 50 na kupata nafasi ya kuiwakisha Tanzania katika mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Nigeria ambapo atapata nafasi ya kushinda na kusaini mkataba wa  mafunzo.

Tunatoa wito kwa watanzania kuwapiigia kura washiriki ili kupata mshindi atakayetuwakalisha vyema  katika mashindano ya Afrika, ili kupiga kura weka jina la fumbo (nickname) ya mshiriki kisha tuma kwenda namba 15594 .  zifuatazo ni jina la fumbo (nickname ) za washiriki  Beny  Sulle “Ben”, Nicole Grey “Nic, Nandi Charles”Nan”,Melissa John “Mel”na Salim Mlindila “Sal”.

AIR MAURITIUS YAZINDUA SAFARI ZAKE NCHINI

Marubani wa Air Mauritius na Mabalozi wa Air Mauritius Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi maalumu wa ndege hiyo ilipowasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Julius Nyerere Dar esSalaam. Ndege hiyo itakuwa ikifanya safari zake kila ijumaa ikitokea Mauritius kuja Dar nakurudi.
Marubani wa Air Mauritius na Mabalozi wa Air Mauritius Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi maalumu wa ndege hiyo ilipowasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Julius Nyerere Dar esSalaam. Ndege hiyo itakuwa ikifanya safari zake kila ijumaa ikitokea Mauritius kuja Dar nakurudi.
Marubani wa  Air Mauritius, Wafanyakazi wa Air Mauritius na Mabalozi wa Air Mauritius Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi maalumu wa  ndege hiyo ilipowasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam. Ndege hiyo itakuwa ikifanya safari zake kila ijumaa ikitokea Mauritius kuja Dar nakurudi.
Marubani wa  Air Mauritius, Wafanyakazi wa Air Mauritius na Mabalozi wa Air Mauritius Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi maalumu wa  ndege hiyo ilipowasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam. Ndege hiyo itakuwa ikifanya safari zake kila ijumaa ikitokea Mauritius kuja Dar nakurudi.

MIJADALA BUNGENI LEO:-


Hii hapa randama ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya habari, tamaduni, sanaa na michezo kwa waka wa fedha 2016/2017. 


Mhe. Suleiman Jafo atoa majibu ya namna serikali ilivyojipanga kutatua tatizo la maji kwa wananchi wa vijijini. 


Mbunge wa Chamwino Mhe. Joel Mwaka aitaka serikali kutoa hatma ya ujenzi wa madaraja mawili yaliyopo kati ya barabara ya Chamwino kuelekea kaskazini. 


Je shirika la ndege la Tanzania ATCL ni shirika la pamoja kati ya Tanganyika na Zanzibar, Zanzibar ina asilimia ngapi  katika shirika hilo? 


 Je ni lini serikali italeta marekebisho ya sheria ya NECTA ili kuondoa nguvu ya waziri kutoa maelekezo bila kuhoji? Mhe. Waitara aihoji. 


Hii hapa mikakati wa serikali juu ya kuanzisha benki ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili kuwawezesha wajasiliamali kupata huduma bora. 

UPDATES: MSIBA WA MTOTO WA ANKAL ISSA MICHUZI

Assalaam aleikum,

Familia ya Ankal Issa Michuzi iliyopatwa na msiba wa kuondokewa na Mtoto wa Ankal, Maggid Muhidin aliefariki Jumapili Mei 8, 2016 huko Durban, Afrika Kusini.

 Taarifa ya sasa ni kwamba, Ndugu zetu kule Durban wanakamilisha taratibu za kusafirisha mwili, hivyo sote tupo standby kwa hilo na naomba tufanye subira kwani hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na mwili ukiwasili ratiba rasmi ya mazishi itatolewa.

Msiba uko Tegeta Wazo Hill, Nyumbani kwa Mama Mzazi wa Marehemu (likiwa ni ombi maalum la Mama), na taratibu zote zinafanyika huko.

NAMNA YA KUFIKA MSIBANI
Ukitokea Tegeta Kibaoni kama unaelekea Kiwanda cha Cement Wazo, mbele mkono wako wa kulia utaona Kanisa la KKKT na ukienda mbele tena kidogo, utaona uzio wenye rangi ya njano umeandikwa Twiga Cement, unakatisha hapo upande huo huo wa kulia. ukikatisha tu utaona kuna mtaa mwingine unaingia upande wa kulia, uache na usogee mbele, utaona mtaa mwingine unaingia kulia, ingia nao huo na utakuwa umefika msibani.



Innalillah wa inna ilayhi raajiun
-AMIN.

MAGAZETI YA LEO: UTUMBUAJI MAJIPU WA MAGUFULI UMEKOSA DIRA. KASUSURA AACHIWA HURU. BUNGE LAANIKA MAJIPU MATANO WIZARA YA AFYA.


CHADEMA: Utumbuaji majipu wa Magufuli umekosa dira. Kasusura aachiwa huru. Bunge laanika majipu matano wizara ya afya.


Sukari ya bil.5 yakamatwa Dar. Magufuli avunja mwiko akitua Uganda. Saba wa familia moja wauawa kwa kukatwa mapanga; 


 Mazito yaibuka kamati ya Lugumi. Wazee watengewa kijiji kwa imani za ushirikina. Migogoro yaibuka walikohamishiwa machinga Dar; 

Tuesday, May 10, 2016

MGODI WA DHAHABU WA BULHANHLU WAINGIA MAKUBALIANO NA TAASISI YA BENJAMINI WILLIAM MKAPA YA KUBORESHA HUDUMA YA AFYA YA MAMA NA MTOTO KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA MSALALA MKOANI SHINYANGA.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu Graham Crew akibadilishana hati za makubaliano na Afisa Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa,Dkt Ellen Mkondya wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati hizo iliyofanyika wilayani Kahama.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu,Graham Crew pamoja na Afisa Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Dkt Ellen Mkondya wakitia saini katika hati za makubaliano ya kuboresha mradi wa huduma ya afya ,Zoezi la utiaji saini ulishuhudiwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Vita Kawawa(kulia) ,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala,Patrick Karangwa (nyuma ya mkuu wa wilaya) pamoja na viongozi wa Mgodi wa Bulyanhulu ,Elias Kasitila na Mganga Mkuu wa wilaya ya Msalala Dkt Hamad Nyembea.
Meneja wa Mgodi wa Bulyanhulu ,Graham Crew akizungumza mara baada ya kutiliana saini makubaliano ya kuboresha huduma za Afya na Taasisi ya Benjamini William Mkapa wakati wa hafla iliyofanyika katika mji wa Kahama.
Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Vita Kawawa akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu kwa michango ambao wameendelea kutoa kwa wilaya ya Kahama na Msalala.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii aliyeko Shinyanga.

MGODI wa dhahabu wa Bulyanhulu ulioko wilayani Kahama umetiliana saini hatii ya makubaliano ya Dola 200,000 sawa na shilingi Milioni 440 za Tanzania na Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF) kwa ajili ya mradi wa kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa mama na mtoto katika wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga

Mgodi  Bulyanhulu kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Acacia na Taasisi ya Benjamin W. Mkapa (BMF) wamesaini hati ya makubaliano ili kushirikiana katika kutekeleza mradi wa miaka miwili unaolenga kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto katika jamii .

Mgodi wa Bulyanhulu kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Acacia utatoa kiasi cha dola za Kimarekani 200,000 kusaidia awamu ya pili ya mradi wa BMF utakaosaidia kuboresha huduma ya vituo viwili vya afya wilayani humo, Kituo cha Afya cha Bugarama na Zahanati ya Kakola kupitia mradi huo.

Mradi huo katika vituo tajwa unatarajiwa kunufaisha wananchi 321,852 katika Halmashauri ya Msalala ambapo makubaliano hayo ya miaka miwili yanaanzia, 01 April 2016 hadi 30 Machi 2018.

“Mgodi wetu unaendesha shughuli zake katika halmashauri ya Msalala hapa mkoani Shinyanga na sehemu ya uwajibikaji wetu kwenye jamii, kupitia mkakati wa mipango endelevu kwenye jamii na kusaidia mikakati ya uboreshaji wa sekta ya afya kwa ajili ya jamii inayozunguka mgodi.”alisema Graham Crew.

“Ushirikiano huu na Taasisi ya BMF umekuja wakati muafaka ambapo BGML imewekeza katika miundombinu ya kuipandisha hadhi zahanati ya Bugarama kuwa kituo cha afya na pia kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Kakola.” Aliongeza meneja huyo mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew.

Awamu ya pili ya Mradi wa BMF inalenga kutekeleza mradi utakaoboresha huduma za HIV/AIDS, huduma za mama na mtoto kwa kuongeza upatikanaji wa wataalamu wa afya na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BMF Dk Ellen Mkondya Senkoro amesema; “Takwimu zinaonyesha kwamba mkoa wa Shinyanga una maambukizi kwa asilimia 7.4% ambapo kiwango kikubwa kipo katika halmashauri ya Msalala kutokana na shughuli za uchimbaji madini hasa uchimbaji mdogo mdogo.”

“Kiwango hiki kimeendelea kuwa hivyo tangu mwaka 2007/2008 hadi 2011/2012 ingawa kiwango cha maambukizi nchini kimepungua kutoka asilimia 5.7% hadi 5.1% hivyo sehemu hii inahitaji hatua maalumu. “alisema Dkt Mkondya.

Alishukuru Kampuni ya  ACACIA kwa msaada huo na kwamba utasaidia kwenye utekelezaji wa uboreshaji wa mifumo ya kukabiliana na tatizo la Virusi vya Ukimwi, huduma za uzazi na watoto kwa kuongeza rasilimali watu ya watalaamu wa afya, uendelezaji wa miundombinu na kujengea uwezo maeneo yanayohitaji ufanisi zaidi.

 Tangu mwaka 2013 Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF) imekuwa ikishirikiana na Acacia kupitia Mfuko wake wa Acacia Maendeleo Fund katika kutekeleza sehemu ya miradi ya awamu ya pili ya mfuko wa taasisi ya BMF katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na Halmashauri iliyokuwa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kuhusu Mfuko wa Maendeleo wa Acacia:
Mfuko wa Maendeleo wa Acacia maarufu kama Acacia Maendeleo Fund ulianzishwa mwaka 2011 kama sehemu ya dhamira katika kuboresha maendeleo endelevu katika jamii kwenye maeneo tunayofanya kazi. Hadi sasa tumefanikiwa kuwekeza dola za kimarekani milioni 35.0 katika miradi 150 kwenye maeneo mbalimbali.

Misaada kutoka kwenye mfuko huu hutoa kipaumbele kwa vitega uchumi vinavyosaidia maendeleo ya jamii, ujengaji wa uwezo, sekta ya afya, elimu, maji, mazingira katika maeneo tunakoendesha shughuli zetu.

Taasisi ya Benjamin W. Mkapa 
Taasisi ya Benjamin W. Mkapa ilianzishwa April 2006 na Rais Mtaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa, taasisi hii isiyo ya kiserikali ina dhamira ya kuboresha afya na hali za watanzania hasa katika maeneo yaliyoko vijijini kwa kutekeleza miradi yenye kutoa matokeo.

Mwisho.