ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, September 22, 2018

FUNDI ALIYEOKOLEWA HII HAPA SABABU YAKE KUBAKI HAI



GSENGOtV

Baada ya mamia kunasuliwa wakiwa tayari wameaga dunia, imekuwa faraja kwa maelfu ya watu waliofurika kwa wingi hii leo katika eneo la hospitali ya Bwisya, Ukara, ambao walijikuta wakilipuka kwa furaha, baada ya Fundi mkuu wa meli iliyopinduka na kuzamisha mamia ya watu, Alphonce Cherehani kupatikana akiwa hai na kuokolewa.

Imeelezwa kuwa Mhandisi Alphonce Charahani aliyeokolewa akiwa hai kwenye ajali ya MV Nyerere leo, alikuwa amejifungia kwenye chumba maalum na kujipaka oili mwilini ili maji yasipite kwenye vinyweleo vyake kuingia mwilini. (ZAIDI VIDEO)
Cherehani ameongeza idadi ya waliosalimika kuwa 41.

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere sasa imefikia 218.

Waliotambulika ni 172 na ambao hawajatambuliwa na ndugu zao ni 46

Kwamujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, amesema kwa sasa taratibu mbalimbali zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na jitihada za kukinyanyua kivuko hicho kazi ambayo itafanywa na timu ya waokoaji iliyonjiani kuingia eneo la ajali.

“Kesho kuanzia saa 2 asubuhi kamati itafanya maziko ya miili 47”, amesema Mongella.

SIKU YA TATU SASA KAZI YA UOKOZI WALIOZAMA NA MV NYERERE KISIWANI UKARA.



GSENGOtV

Shughuli za uopoaji miili ya ndugu waliozana na Mv Nyerere kisiwani Ukara zimeendelea tena huku idadi ikiendelea kuongezeka kadri saa zinavyoendelea kusonga. 

Shuhudia yale yaliyojiri hii leo tarehe 22 Septemba 2018 ikiwa kabla ya saa 10 jioni nayo ni  siku ya tatu mara baada ya ajali hiyo ya kutisha.

MAANDALIZI YA MAZISHI YA WALIOFARIKI AJALI MV NYERERE YAANZA.



Maandalizi ya maziko ya waathiriwa wa mkasa wa MV Nyerere hapo kesho yameanza karibu na eneo ambalo kivuko hicho kilizama.

Tayari jeshi la akiba nchini limeanza kuchimba makaburi ya pamoja ambapo waliofariki watazikwa siku ya Jumapili.

INASIKITISHA - KINACHOENDELEA SHUGHULI ZA UOKOAJI AJALI MBAYA YA MV NYERERE KATIKA PICHA

GSENGOtV

Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama juzi mchana Septemba 20, 2018 imefikia 209

Hayo yamebainisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe  leo jioni Jumamosi Septemba 22, 2018, alipozungumza na waandishi wa habari katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, Kamwelwe amesema watu waliopatikana wakiwa hai ni 41, baada ya mmoja kuongezeka leo ambaye ni mhandisi wa kivuko hicho, Alphonce Charahani.

Waziri Isack Kamwelwe amesema miili iliyotambuliwa ni 172, kati ya hiyo 112  tayari imeshachukuliwa na ndugu kwa ajili ya maziko.

“Miili 37 bado haijatambuliwa, nieleze tu kuwa ndugu wanaochukua miili kwa ajili ya maziko wanapatiwa ubani wa Sh500,000 kama ambavyo Serikali imeahidi,” amesema Kamwelwe.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  John Mongella amesema meli ya MV Nyehunge kutoka Mwanza inaelekea kisiwa cha Ukara ikiwa na vifaa maalum vitakavyotumika kukinyanyua kivuko hicho ili kurahisisha uokoaji na taratibu nyingine.

Kazi ya uokoaji ililejea tena mapema leo asubuhi majira ya saa 12:30
Maskauti pamoja na vijana toka JKT wamefanya kazi ya kipekee hapa Ukara.
Kikosi cha wazamiaji toka shule ya uokoaji Mwanza nacho kiko eneo la tukio.
Mazingitra na jiografia ya eneo la ajali.
Kutoka njia kuu ya kuingia ufukwe wa Bwisya hapa Ukara hii ndiyo jiografia.
Tayari miili kwa ndugu jamaa na marafiki wa marehemu waliowatambua imekwishaanza kuchukuliwa baada ya utambuzi kufanyika.
Uokoaji unaendelea kufanyika...ingawa ni zoezi gumu.
Kwa karibu zaidi....
Pilika pilika eneo la ajali.
Toka hospoitali ya Bwisya hapa Ukara hali halisi na mazingira, hakuna jinsi.
Vikosi kazi.

Mazingira barabara kuelekea Kituo cha afya Bwisya hapa Ukara.

IDADI YAONGEZEKA AJALI KIVUKO CHA MV NYERERE



GSENGOtV
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe amesema uokoaji wa miili ya waliofariki dunia baada ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere utakamilika leo Septemba 21, 2018 kabla ya saa 12 jioni. 

Kamwelwe ametoa kauli hiyo leo mchana wakati akiwa eneo la tukio Kisiwa cha Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza. 

Mpaka sasa miili zaidi ya 131, imepatikana huku waliookolewa wakiwa hai 38 ambao wamekimbizwa kituo cha afya Bwisya.


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella yuko wilayani hapa kuratibu zoezi zima.

Simanzi na huzuni ndizo zilizotawala  katika kisiwa cha Ukara  Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza kufuatia ajali mbaya ya kivuko cha Mv Nyerere kilichokuwa kinafanya safari zake kutoka Bugorora kwenda Kisiwa cha Ukara  kupinduka na kuzama ndani ya Ziwa Victoria mita 100 kabla ya kufika kisiwani hapo.
Siku ya pili sasa Zoezi la uokoaji wa miili ya marehemu linaendelea ambapo hadi sasa zaidi ya miili 100 imeokolewa huku juhudi za utambuzi wa miili hiyo nazo zikiendelea.
Mkuu wa jeshi la Polisi nchini Saimoni Sirro anaeleza juhudi za uokoaji zinazoendelea na kuwatoa hofu wananchi kuhusu miili iliyosalia.

Thursday, September 20, 2018

HILI HAPA GOLI PEKEE LA MBAO LILILOIANGAMIZA SIMBA



NA ZEPHANIA MANDIA/GSENGOtV

Bao la Mbao FC limefungwa na kiungo Said Khamis Said dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti, kufuatia mshambuliaji Pastory Athanas kuangushwa na kipa Aishi Salum Manula wakati anakwenda kufunga.















MBAO MOJA TU YATOSHA KUTENGENEZA JENEZA LA SIMBA MAZISHI CCM KIRUMBA MWANZA.



NA ZEPHANIA MANDIA/GSENGOtV

MABINGWA watetezi, Simba SC leo wamepoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Kwa ushindi huo, Mbao FC wanapanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, wakifikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi tano, wakiwazidi kwa pointi moja Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi tatu. 

Simba SC wanabaki na pointi zao saba baada ya kucheza mechi nne, wakishinda mbili dhidi ya timu za Mbeya, Tanzania Prisons 1-0 na Mbeya City 2-0, sare moja 0-0 na Ndanda FC na kipigo cha leo cha Mbao FC. 

Bao la Mbao FC limefungwa na kiungo Said Khamis Said dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti, kufuatia mshambuliaji Pastory Athanas kuangushwa na kipa Aishi Salum Manula wakati anakwenda kufunga.

Simba SC ilikuja juu baada ya bao hilo na kucheza kwa kushambulia mfululizo kujaribu kutafuta bao la kusawazisha, lakini sifa zimuendee kipa Hashimu Mussa aliyeokoa vizuri hatari zote.


Kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems aliiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwa kumuingiza Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere akimpumzisha kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.


Lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuisaidia Simba SC kupata bao zaidi tu ya kuendelea kulitia misukosuko lango la Mbao FC.


Amri Said ‘Stam’, kocha wa Mbao FC na beki wa zamani wa Simba SC aliyeanzia ukocha timu ya vijana ya Wekundu hao wa Msimbazi, alimpumzisha Rajetsh Kotecha kipindi cha pili baada ya kazi nzuri kipindi cha kwanza na kumuingiza Evarist Mjwahuki kuongeza kasi ya mashambulizi.


Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Hashim Mussa, Vincent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Peter Mwangosi, Ally Mussa, Said Khamis, Hussein Suleiman/Rolland Msonjo dk76, Rajesh Kotecha/Evarist Mjwahuki dk58, Pastory Athanas na Abubakar Mfaume/Hamim Abdulkarim dk90. 


Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Rashid Juma dk74, Cletus Chama, John Bocco, Emmanuel Okwi na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Meddie Kagere dk55. 

BREAKING NEWS:- KIVUKO CHA MV NYERERE CHAZAMA

 GSENGOtV

Breaking news saa kadhaa zilizopita Kivuko cha MV Nyerere kinachotoa huduma ya usafiri majini ndani ya Ziwa Victoria kati ya Bugolola Kisiwa kikubwa na Bwisha Kisiwa cha Ukara kinazama kikiwa na abiria (idadi haijajulikana bado) hivyo jitiada zinaendelea kuokoa abiria waliokuwemo.


Tayari mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama,  Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella tayari kafika eneo la tukio,  zaidi waandishi wetu wako eneo la tukio na habari kamili kuwajia hivi punde.
Kwa Updates zaidi Sikiliza @jembefm #JembeHabari 
@gsengotv

MUENDELEZO.

KIVUKO cha MV. Nyerere kinachofanya safari zake kati ya Bugorora na Ukara katika wilaya ya  Ukerewe mkoani Mwanza kimezama ziwa Victoria.

Inadaiwa kwamba kivuko hicho kimezama kikiwa na abiria ambapo hata hivyo bado haijafahamika idadi ya abiria waliokuwemo ingawa taarifa za awali zinadai kilikuwa na abiria zaidi ya 90.

Kwa mujibu wa baadhi ya waliozungumzia kivuko hicho wamedai kilikuwa kinatokea Bugorora kwenda Ukara kati ya saa 6 na saa 7.30 mchana na kilizama dakika kama 5 kabla ya kufika kwenye ghati ya Ukara.

Kwa mujibu wa mashuhuda wamedai kuwa ghafla kilianza kutitia kwenye maji kwa nyuma kulikokuwa na mzigo na kuwezesha abiria waliokuwa mbele kurukia majini na kuogelea na mitumbwi iliyokuwa pale kufanya kazi ya kuwaokoa abiria waliorukia majini.

Pia inadaiwa abiria wengi waliokuwa ndani ya Mv Nyerere hawakuweza kutoka na kuwa wamezama.

Mmoja ya waliozungumzia kuzama kwa kivuko hicho amedai idadi ya abiria waliopanda haijulikani ingawa uwezo wa kivuko ni kubeba abiria 150.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa kwani simu yake haikuwa hewani.

Hivyo tutaendelea kuwajuza kinachoendelea na idadi kamili au abiria waliokuwamo kwenye kivuko hicho.



WAZIRI KALEMANI AWASHA UMEME KIJIJI CHA SANGA WILAYANI KWIMBA




NA ZEPHANIA MANDIA/GSENGOtV
Zaidi ya wakazi laki moja na elfu tano katika vijiji thelathini na tano wilayani Kwimaba mkoani Mwanza, wanatarajia kuondokana na tatizo la ukosefu wa nishati ya Umeme, baada ya kukamulika mradi wa Nishati ya Umeme vijijini REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza

CCM YAZOA 21 NA MBILI TU ZA HABANA UCHAGUZI NAIBU MEYA HALMASHAURI YA JIJI LA MWANZA



Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji Mwanza Jumatano ya Sep 19, limefanya uchaguzi wa kumpata Naibu Meya ambapo Bhiku Kotecha CCM amerejea kwenye nafasi hiyo, ambayo amekuwako tangu uchaguzi wa kwanza wa baraza hili mwaka 2015.

KATIBU MKUU UVCCM AONGOZA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA JOHN GUNINITA IFAKARA WILAYANI KOLOMBELO LEO.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala akimpa pole mdogo wa marehemu John Guninita Ndg Gerald John Guninita alipowasili nyumbani kwao Ifakara Wilaya ya kilombero.
 Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala wakati akiwasili nyumbani kwao marehemu pamoja na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Ndg  Innocent Karogelesi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala akizungumza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Ndg Innocent Karogelesi
Waombolezaji wakiandamana kutangulia mbele wakati mwili wa Marehemu John Guninita ulipokuwa ukipelekwa eneo la kusaliwa wakati wa mazishi hayo
Muombolezaji Wakilia kwa uchungu wakati wa mazishi ya marehemu John Guninita



Vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM wakibeba jeneza lenye mwili wa marehemu John Guninita kulipeleka kwenye eneo la kusaliwa wakati wa mazishi hayo
Mwili wa Marehemu ukiwa umepakizwa kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa eneo la ibada
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala akitoa mkono wa pole kwa mdogo wa marehemu John Guninita Ndg Gerald John Guninita alipowasili nyumbani kwao Ifakara Wilaya ya kilombero.
Jeneza Lililobeba Mwili wa Marehemu Ndg John Guninita likiwekwa ndani ya Kaburi na Waombolezaji |(Picha Zote Na Fahadi Siraji Wa UVCCM)

Wednesday, September 19, 2018

MTOTO WA MFALME PRINCE WILLIAM KUKUTANA NA RAIS MAGUFULI.




Mwanamfalme William wa Uingereza anapangiwa kukutana na rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki ijayo wakati wa ziara yake ya siku saba Afrika.

Anatarajiwa kuzuru pia Kenya na Namibia katika ziara hiyo ambayo si ya kikazi. Ziara hiyo itafanyika kuanzia 24 Septemba hadi 30 Septemba.

Lengo kuu la mwanamfalme huyo litakuwa kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama.

Atafanya ziara hiyo katika wadhifa wake kama rais wa mashirika yanayotetea uhifadhi wa wanyama ya United for Wildlife na Tusk Trust.

Amekuwa pia mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili.

Akiwa ziarani Tanzania, Mtawala huyo wa Cambridge, atafanya mashauriano na Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo katika kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama pori kwa mujibu wa shirika la habari la Press Association.

Kadhalika, atazuru bandari ya Dar es Salaam kujifahamisha zaidi kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama.

Mwaka 2013, mwezi Oktoba, ilizindua Operation Tokomeza Ujangili ingawa ilisitishwa takriban mwezi mmoja baadaye, huku watetezi wa haki wakiwalaumu waliokuwa wanaendesha operesheni hiyo kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Tanzania ilikuwa na tembo 110,000 mwaka 2009 lakini idadi hiyo imeporomoka hadi kufikia tembo 43,000 kutokana na ujangili.

Moja ya malengo ya ziara ya Mwanamfalme William Afrika ni kupigia debe mkutano mkuu wa kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori ambao utaandaliwa jijini London kati ya 11-12 Oktoba.

Mkutano huo ambao kwa kirefu unafahamika kama Illegal Wildlife Trade Conference, unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori, kwa kuangazia mambo matatu makuu: ulanguzi wa wanyama, wadudu na mimea kama uhalifu, kujenga ushirikiano na kufunga masoko yanayotumiwa na wahalifu kulangua wanyamapori.

Taarifa ya Kensington Palace inasema ingawa atakuwa katika ziara ya kibinafsi, ameombwa na Malkia kutekeleza shughuli kadha rasmi kwa niaba yake.

Akiwa nchini Kenya, Mwanamfalme William atatembelea kikosi cha wanajeshi wa Uingereza cha 1st Battalion cha Irish Guards Battlegroup.

William huwa na cheo cha kanali wa jeshi la Ireland, na anatarajiwa kujifahamisha ni jinsi gani wanajeshi wa Uingereza na Kenya wanafanya kazi kwa pamoja kuimarisha shughuli zao.

Kikosi hicho cha Irish Guards Battlegroup hujumuisha wanajeshi wa Ireland na kundi la wanajeshi wa kenya ambao wamekuwa wakipokea mafunzo kutoka kwa kikosi cha jeshi la Uingereza.

Nchini Namibia, mtawala huyo anatarajiwa kukutana na makamu wa rais Nangolo Mbumba na pia ahudhurie hafla ya kusherehekea ushirikiano kati ya Uingereza na Namibia katika makazi ya balozi wa Uingereza nchini humo Kate Airey.

TAWLA TANGA YAENDESHA MDAHALO WA WADAU WA MASUALA YA ARDHI MKOANI TANGA



Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania Mkoani Tanga TAWLA Latifa Ayoub akisisitiza jambo wakati wa mdahalo wa wadau wa masuala la ardhi mkoani Tanga leo mjini Tanga kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake kwenye kumiliki ardhi uliofanyika leo kwenye ukumbi wa YDC Jijini Tanga ukihusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ulioandaliwa na chama hicho
 Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania Mkoani Tanga TAWLA Latifa Ayoub kulia akisisitiza jambo wakati wa mdahalo wa wadau wa masuala la ardhi mkoani Tanga leo mjini Tanga
kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake kwenye kumiliki ardhi kushoto ni Mwanasheria wa TAWLA Mkoani Tanga Mwanaidi Kombo ambapo mdahalo huo uliandaliwa na chama hicho
Mwanasheria wa TAWLA Mkoani Tanga Mwanaidi Kombo akisisitiza jambo kwenye mdahalo huo
 Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Tanga Doris Wilson Mangwe akizungumza katika mdahalo huo
 MWANASHERIA wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza mkoani Tanga katika Sigisbert Akwilini akiwa na wadau wengine wakifuatilia mdahalo huo ambao uliandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) mkoani Tanga 
Madiwani wa Kata za Chumbangeni Saida Gadafi CCM) kushoto akiwa na Diwani wa Kata ya Majengo (CUF) Suleimani Mbaruku wakifuatilia mdahalo huo
 MWANASHERIA wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza mkoani Tanga Sigisbert Akwilini akichangia kwenye mdahalo huo
 Afisa Mipango wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga Rehema Akida akizungumza katika mdahalo huo
 Afisa Mtendaji wa Kata ya Mabokweni Salim Mdoe akizungumza katika mdahalo huo
 Afisa Mtendaji wa Kata ya Masiwani Jijini Tanga Sheria Salame akizungumza katika mdahalo huo

 Baadhi ya wadau wa mdahalo huo wakizungumza
 Mwansiti Bashiru kutoka kata ya Mbaramo wilayani Muheza akizungumza katika mdahalo huo

Diwani wa Kata ya Majengo (CUF) Suleimani Mbaruku