Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akitoa taarifa ya ukusanyaji, Ukoboaji na uuzaji wa kahawa Mkoani Kagera katika msimu wa mwaka 2018/2019 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa kahawa katika ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba. (Picha Na Mathias Canal-WK)
Na Mathias Canal-WK,
Bukoba-Kagera
Imebainika kuwa pamoja na
changamoto zilizojitokeza katika msimu wa kahawa wa mwaka 2018/2019 lakini bado
mfumo wa uuzaji wa kahawa kupitia ushirika umekuwa wa manufaa kwa mkulima
kutokana na mkulima kupata uhakika wa kilo za kahawa alizozipeleka chamani
tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Manufaa hayo yamejili kutokana
na kuingia mikataba ya kuuza moja kwa moja, ambapo matarajio ya serikali ni
kuhakikisha kuwa mkulima analipwa malipo ya awali na kiasi kingine kubaki kwa
ajili ya kuendelea kukusanya kahawa na kufanya maandalizi ya malipo ya
pili.
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt
Charles Tizeba amebainisha hayo Leo tarehe 6 Octoba 2018 wakati akitoa taarifa
fupi ya ukusanyaji, Ukoboaji na uuzaji wa kahawa Mkoani Kagera katika msimu wa
mwaka 2018/2019 hadi kuishia tarehe 2 Octoba 2018 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa
kahawa.
Katika mkutano huo uliofanyika
kwenye Ukumbi ELCT Mjini Bukoba na kueleza kuwa ubora wa kahawa umeongezeka kwa
kiasi kikubwa tofauti na misimu iliyopita.
Waziri Tizeba alizitaja
changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika kwenye zao la kahawa kwa msimu wa
mwaka 2018/2019 kuwa ni pamoja na Bei za mnadani, Kahawa kununuliwa kwa kiwango
kidogo mnadani na wakati mwingine kutonunuliwa kabisa.
Kuwepo kwa taarifa za upotoshaji
kwa wakulima toka kwa Walanguzi za kuzuia wakulima kukusanya kahawa yao kupitia
Vyama vya Ushirika vya Msingi kuwa wao (Walanguzi) watanunua na kuwapatia
bei nzuri na Kuwepo kwa katizo la umeme mara kwa mara linalopelekea ukoboaji wa
kahawa kutofanyika kwa wakati (hususani Wilayani Ngara).
Aidha, aliutaja mkakati wa
kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuuza kahawa kupitia mnada wa
Moshi na mauzo ya moja kwa moja nje ya nchi “Direct Export” ambao umeonesha
kuwa na bei nzuri ukilinganisha na ile inayotolewa mnadani Moshi,
na Kuomba mkopo wa nyongeza toka TADB kwa ajili ya kuwalipa wakulima
malipo yao ya Awali.
Alisema Chama Cha Ushirika cha
Karagwe KCU wanatarajiwa kupata mkopo wa Tshs. 2,000,000,000/= kwa wiki hii na
kiasi cha Tshs. 2,000,000,000/= kinaendelea kushughulikiwa ili kiweze
kutolewa wiki ijayo ambapo wanatarajiwa kupata malipo ya mauzo ya kahawa
yao kwa wiki ijayo kiasi cha Tshs Bilioni 2.1
Mikakati mingine ya kukabiliana
na changamoto ya zao la kahawa ni pamoja na Vyama kuingia mikataba mbalimbali
ya kuuza kahawa moja kwa moja nje. KDCU Ltd wana mikataba ya mauzo nje yenye
thamani ya Tshs 20,819,815,820.66 ambapo malipo yake yanatarajiwa kulipwa
kuanzia wiki hii. Kwa KCU Ltd wana mkataba wa Tshs Bilioni 1.3 na wanatarajia
kuingia mikataba mingine na wanunuzi wengine kwa wiki ijayo.
Dambamba na jitihada za
kupatikana kwa umeme wa uhakika katika kiwanda kilichoko Wilayani Ngara
zinaendelea kufanyika kwa kushirikiana na mamlaka husika.
Katika hatua nyingine alieleza
kuwa mpaka sasa Kahawa iliyoko ghalani ni Kiasi cha Kilo 3,000,464 za kahawa
maganda ambayo ilikuwa bado kukobolewa huku Kilo 8,191,867 za kahawa safi
kilikuwa bado hakijauzwa na kilikuwepo kwenye maghala ya vyama.
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa
ameanza ziara ya kikazi Mkoani Kagera kuanzia Leo tarehe 6 mpaka tarehe 9
Octoba 2018 ambapo pamoja na mambo mengine lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua
Maendeleo ya zao la kahawa Mkoani humu.