ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, December 2, 2024

MAAMBUKIZI YA VVU YAPUNGUA NCHINI TANZANIA-WAZIRI MHAGAMA

 

Leo ni tarehe 1 Desemba 2024, ambapo dunia inaadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani. Kitaifa, maadhimisho haya yamefanyika Mkoani Ruvuma yakiongozwa na mgeni rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dkt. Philip Mpango.

Akitoa taarifa yake, Waziri wa Afya nchini, Mheshimiwa Jenista Mhagama, ameeleza juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. 

Amesema, Serikali imeendelea kugharamia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), hatua inayosaidia wananchi wanaoishi na maambukizi ya virusi hivyo kuendelea na maisha ya kawaida.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, wananchi takriban milioni 1.7 wanaishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini. 

Serikali imetumia shilingi bilioni 750 kununua dawa za ARVs, ambapo gharama ya matibabu kwa kila mgonjwa mmoja ni takriban shilingi 400,000 kwa mwaka.

"Maadhimisho haya ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI na kupunguza unyanyapaa" amesema Mhe. Jenista

Pamoja na hayo  amehimiza jamii kuchukua hatua za kinga na matibabu kwa ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali. 

Kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuimarisha mshikamano wa kidunia katika kukomesha maambukizi mapya na kuboresha huduma kwa walioathirika.

MWENYEKITI JUNGULU AAHIDI KUSHIRIKIANA NA WENYEVITI WAPYA KULETA MAENDELEO

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA

 
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Kata ya picha ya ndege Grace Jungulu katika kuhakikisha anaendelea kukijenga na kukiimarisha chama ameahidi kushirikiana bega kwa bega na wenyeviti wote wa mitaa mitatu walioshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

Jungulu ameyasema hayo wakati wa kuzungumzia mikakati mbali mbali  ambayo amejiwekea mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo na kusema kuwa lengo lake kubwa ni kuendelea kukijenga chama cha mapinduzi kwa kushirikiana na wanachama wengine kuanzia ngazi za mashina na matawi.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba ana imani katika kata ya picha ya ndege ataweza kusikiliza kero na changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi kwa kushirikiana  kwa hali na mali  na wenyeviti wa serikali za mitaa ambao wameweza kuibuka na ushindi  kwa lengo la kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

"Lengo langu kubwa mimi kama mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) kata ya Picha ya ndege napendakuchukua fursa hii kuwashuru kwa dhati wana chama wote wa ccm ambao wameweza kuwa mstari wa mbele kujitokeza kwa wingi katika zoezi zima la upigaji wa kura na kuweza kushinda katika mitaa yote mitatu hii ni dalili nzuri ya ushirikiano mzuri uliopo katika ya viongozi na wanachama,"alisema Jungulu.

Aidha aliongeza kwamba katika kata ya picha ya ndege amejiwekea mikakati madhubuti ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika sekta mbali mbali ikiwemo, kuboresha miunombinu ya barabara, huduma ya maji safi na salama, afya, elimu, pamoja na huduma nyingine za msingi.

Katika hatua nyingine Jungulu aliwashukuru wanachama wote wa CCM Kata ya picha ya ndege pamoja na wananchi wote kwa ujumla kwa kuweza  kufanya maamuzi sahihi na kukiamini chama cha mapinduzi kwa kukipigia kura na kufanikiwa kuweza kushinda kwa kishindo katika mitaa yote mitaa.

Aidha Jungulu alimshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza  kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo ikiwa pamoja na kutenga fedha ambazo zimeweza kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kuwahudumia wananchi katika nyanja mbali mbali.
                             MWISHO.  

DKT.MPANGO -MKAKATI WA SERIKALI NI KUTOKOMEZA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI NCHINI

  Siku ya Ukimwi Duniani, Imeadhimishwa Kitaifa leo tarehe 01/12/2024, maadhimisho yamefanyika katika Uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma. 

Hafla hii imeongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ambaye amesisitiza azma ya serikali kuhakikisha inatokomeza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) nchini.

Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Mpango, ameonesha dhamira ya dhati ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupambana na maambukizi mapya ya VVU.

Takwimu zinaonesha kwamba vijana, hasa wa kike, wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, serikali imeweka mkazo mkubwa katika kutoa elimu kwa vijana ili kuwasaidia kujitambua, kuchukua hatua za kujikinga, na kwa wale wanaoishi na VVU, kuhakikisha wanafuata taratibu kwa kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi (ARVs).

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango ametoa wito kwa jamii nzima kushirikiana, kuhakikisha kwamba maambukizi mapya yanapungua, kwa kuelimisha vijana kuhusu umuhimu wa afya ya uzazi, matumizi sahihi ya kinga, na upimaji wa afya mara kwa mara.

BENKI YA CRDB YASHINDA TUZO YA CHAGUO NAMBA MOJA, BUNIFU KWA WATEJA.

 

Dar es Salaam. Tarehe 1 Desemba 2024: Baada ya kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa kwa mwaka mzima, Benki ya CRDB imeingia mwezi Desemba kwa kushinda tuzo mbili kutambua juhudi zake za kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kote nchini.

Tuzo hizo zilizotolewa na Consumer Choice Awards Africa (CCA) 2024, zimezingatia maoni ya wateja na wadau tofauti walioshirikishwa na kupiga kura kumchagua mtoa huduma bora.

Benki ya CRDB imenyakua tuzo ya benki chaguo namba moja ukanda wa mashariki mwa Afrika (the most preferred, convenient, and accessible bank in eastern Africa) kutokana na urahisi wa kufikika pamoja na tuzo ya benki yenye promosheni bunifu inayowanufaisha wateja wake (the most creative and innovative consumer benefiting campaign of the year).



Akikabidhi tuzo hizo mbili, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo amesema ushindi huo unatokana na juhudi makini za kulihudumia soko.

“Nawapongeza sana. Juhudi zenu zinaonekana kwa namna mnavyowahudumia wateja na kushirikiana na wadau tofauti kuongeza ubunifu wenye tija. Hongereni sana Benki ya CRDB,” amesema Waziri Nyongo.

Akipokea tuzo hizo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema ubunifu unaomzingatia mteja ndio msingi wa huduma za Benki ya CRDB kila siku hivyo ni furaha kuona jamii inalitambua hilo.
“Sisi ni benki inayomsikiliza mteja. Wateja wetu waliosambaa nchi nzima wana mahitaji tofauti ambayo tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kuyakabili. Kwa walio mbali na tawi, tunawasogezea na wale wanaohitaji huduma mahali popote walipo na wakati wowote tunawapa wanachokitaka. Tunaamini mteja akifurahi biashara yetu itakuwa endelevu,” amesema Raballa.

Kuhusu tuzo ya benki bora inayopendwa, inayopatikana popote na rahisi kufikika ukanda wa mashariki mwa Afrika (the most preferred, convenient, and accessible bank in eastern Africa), Raballa amesema Benki ya CRDB inaongoza kwa mtandao mpana wa matawi ambayo ni zaidi ya 260 yaliyopo katika halmashauri zote nchini pamoja na mawakala zaidi ya 25,000 wanaosaidia kutoa huduma.

“Mambo haya yote yanaonyesha ni kwa namna gani hatupati usingizi tusipomhudumia mteja wetu mahali popote alipo. Hakuna benki nyingine yenye ukubwa huo,” amesema Raballa.

Na kuhusu tuzo ya benki yenye promosheni bunifu inayowanufaisha wateja wake (the most creative and innovative consumer benefiting campaign of the year) ambayo imeitambua promosheni ya Benki ni SimBanking; miamala inalipa swahiba, Raballa amesema ni ukweli ulio wazi kwamba Programu ya SimBanking imeleta mapinduzi makubwa kwenye huduma za fedha nchini.

“Kupitia SimBanking mteja anaweza kupata huduma yoyote aitakayo kuanzia kufungua akaunti, kuomba mkopo, kufanya uwekezaji au kufahamu viwango vya kubadilisha fedha. Haya yote yanafanyika kupitia simu ya mkononi. Kwa mwaka mzima, tulikuwa na promosheni inayohamasisha kufanya miamala kidijitali na washindi waliopatikana tunawazawadia gari jipya aina ya Nissan Dualis, bajaji au pikipiki pamoja na zawadi nyingine kemkem,” amesema Raballa.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Consumer Choice Awards Africa, Diana Laizer amesema Benki ya CRDB ni mdau mkubwa wa tuzo hizo na imekuwa ikishiriki mara nyingine.

“Kila mwaka tunakuwa na Benki ya CRDB. Kura za wateja ndizo zinazoipa ushindi kutokana na jinsi wanavyoridhishwa na huduma inazozitoa,” amesema Diana.

Akieleza kuhusu namna ambavyo Benki ya CRDB haimwachi mteja wake njiani pindi akihitaji msaada, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo amesema kipo kituo cha huduma kwa huduma kwa wateja kinachofanya kazi muda wote.

“Tunamsikiliza mteja atakayepiga simu, kutuma baruapepe au barua hata yule atakayewasiliana nasi katika akaunti zetu za mitandao ya kijamii. Tunafanya hivi ili kuhakikisha changamoto yoyote inayomkabili mteja inatatuliwa kwa wakati,” amesema Yolanda.


CCM PWANI YAWEKA WAZI JINSI ILIVYOWABAMIZA WAPINZANI MITAA YOTE 146 BILA HURUMA

 


VICTOR MASANGU, PWANI


Chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani  kimesema kwamba kimeshinda kwa kishindo na kufanikiwa kuweza kuchukua mitaa yote 146 ndani ya Mkoa mzima katika uchaguzi wa serikali za mitaa  kutokana na kuwepo  kwa ushirikiano wa kutosha baina ya viongozi  pamoja na wanachama ikiwemo sambamba  kutoa hamasa kuanzia ngazi za chini kuhusiana na umuhimu wa kujitokeza kwa wingi  kwa ajili ya kupiga kura.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake  katika mahojiano maalumu kuhusiana na suala zima la kumalizika kwa  uchaguzi wa serikali Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Pwani   Dkt. David Mramba amesema kwamba wameweza kuibuka na ushindi wa kishindo kutokana na maandalizi  mazuri ambayo wameyafanya katika maeneo mbali mbali ili kuweza kushinda.

Dkt. Mramba amesema kwamba katika Mkoa mzima  wa Pwani kuna jumla ya kata zipatazo 133 na kwamba wameweza kushinda kwa kishindo kikubwa katika mitaa hiyo yote ambapo wagombea  wote waliogombea katika kuwania nafasi ya uenyeviti wa serikali  za mitaa  ushindi wote umekwenda kwa chama cha mapinduzi (CCM)

"Ndugu zangu waandishi wa habari nimeona niwajuze juu ya matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umemalizika Novemba 27 mwaka huu katika hali ya ulinzi na usalama na chama chetu ma mapinduiz (CCM) tumeweza kushinda kwa kishindo kikubwa sana na hii ni baada ya kunyakua mitaa yote ipatayo 146 ambayo ipo katika Mkoa wa Pwani na hii imetokana na hamasa kubwa ambayo tumeweza kuitoa kwa wanachama wetu  pamoja na  kuwahimiza wananchi kwa ujumla,"alifafanua Dkt. Mramba  

Aidha Dkt. Mramba amefafanua  kwamba  katika uchagzui huo mbali na kushinda katika mitaa yote  ya Mkoa wa Pwani pia katika vitongozi  vyote vipatavyo 2028 wameweza  kupoteza vitongoji tisa tu ambavyo vimechukuliwa na  vyama pinzani kutokana na kuwepo kwa sababu mbali mbali ambazo zilikuwepo katika baadhi ya maeneo.

Kadhalika Mramba meweza kusema kuwa katika ngazi ya vijiji CCM imeweza kushinda kwa kishindo na kuweza kufanikiwa kuibuka kidedea katika vijiji vipatavyo 416 kati ya vijiji 417 ambapo kijiji kimoja kimekwenda kwa chama pinzani na kwamba kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi  mwingine wa kuziba nafasi ambazo maeneo mengine haukuweza kufanyika kutokana na sababu mbali mbali.

Kadhalika Katibu Dkt. Mramba amesema kuwa Mkoa wa Pwanini moja kati ya mikoa ambayo imeweza kutenda haki zaidi ya kukiheshimisha  chama cha mapinduzi (CCM) kutokana na kufanya vizuri zaidi kuanzia hatua za awali kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika zoezi la uandikishaji wa daftari kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika hatua nyingine Dkt. Mramba amemshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa (CCM) Taifa ambaye pia ni Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo ikiwa sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi.