CHAMA CHA WAFANYAKAZI MIGODINI (NUMET),CHAISHAURI
SERIKALI IWACHUNGUZE WAGENI.
NA PETER FABIAN.
MWANZA.
KUMEKUWEPO Makampuni ya Kitapeli na kinyonyaji yaliyoibuka kama Uyoga nayotumiwa na waajiri Migodini, kuajiri wafanyakazi na kuwapeleka kufanya kazi katika baadhi ya Migodi ya Dhahabu, Almasi, Tanzanaite na Madini mengine ikiwemo Makaa ya Mawe, Mafuta na Gesi asilia kwa ujira mdogo, ikidaiwa kuwa chini ya kima cha chini cha ujira wa Migodini hapa nchini.
Imebainika Pia, bado kumekuwepo baadhi ya wageni wasiokuwa na ujuzi (kutoka nje ya nchi), kuendelea kufurika kwe migodi mbalimbali hapa nchini wakifanya kazi za kawaida zinazopaswa kufanywa na wananchi wazalendo ambao wanazosifa na uwezo wa kufanyakazi kwenye migodi hiyo lakini hawapewi nafasi na zaidi kumekuwa na urasimu wa Menejimenti za watu wa mataifa ya nje wanaoendesha migodi.
Taarifa ya risala iliyosomwa wakati wa uzinduzi wa Chama cha Wafanyakazi wa Nishati na Madini (NUMET) juma lililopita kwenye Uwanja wa mkongwe wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Akisoma risara ya NUMET kwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye hakuwepo kwenye uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Nicomedes Kajungu, alisema kwamba serikali inapoteza mapato mengi kutokana na ‘michezo michafu’ inayofanywa migodini na wafanyakazi wanaochangia baadhi yao kukosa au kupoteza haki zao.
Katibu Kajungu (NUMET) alisema moja ya changamoto inayoikabili Chama chake ni kuibuka kwa Mawakala katika sekta ya ajira katika Migodi mbalimbali hapa nchini (Third part employment agent) ambayo yanatumiwa na waajiri migodini kuajiri wafanyakazi na kuwapeleka kufanya kazi kwa ujira mdogo wa chini ya kima cha chini cha ujira wa migodini, taratibu na kisheria.
Baadhi ya Mawakala hao ambao ni baadhi ya Makampuni (ambayo hata hivyo hakuyataja) yasiyokuwa na mitaji ya kulipa ujira, lakini yenyewe yamekuwa yanalipwa fedha nyingi na wenye migodi huku yenyewe yakilipa ujira mdogo wafanyakazi hao na hivyo kunufaika na asilimia ya fedha yanazookoa kutokana na kuwapunja wafanyakazi wao.
“Waajiri kwa kufanya hivi wanakwepa wajibu wao wa kuwapa haki zao kama vile likizo na marupurupu mengine pia wafanyakazi wanashindwa kujua ni yupi mwajiri waoa halisi maana makampuni hayo ya kinyonyaji hayana mitaji ya kulipa ujira.” Alisema na kulalamika.
“Serikali imekuwa inapoteza Mapato mengi ya Kodi kwa mchezo huo na wafanyakazi kuajiriwa kwa Mikataba mifupi ili wasidai maslahi yao na kuvifanya vyama vya wafanyakazi vikose fursa ya kujadili nyongeza ya mishara, hili ni janga linalohitaji juhudi za pamoja baina ya wafanyakazi , wanachama na serikali kuliangamiza.”
Aidha aliidai kuwa , janga kubwa jingine lililopo migodini ni kufurika kwa wageni wasiokuwa na ujuzi toka nje ya nchi ambao wanafanya kazi za kawaida, wageni hao wengi hawana vibali vya kufanyakazi nchini au vibali vyao vimekwisha lakini bado wapo.
“Maeneo yetu ya kazi kuna tofauti kubwa ya ajira, wafanyakazi wazalendo bila kujali uzoefu wala weredi wao, wamekuwa wakiambulia kazi za mitulinga tu (ya kutumia nguvu nyingi sana)na kuwaachia wageni kazi za kitaalamu za maofisini na zinginezo.” Alieleza.
Aliongeza kwamba “Mtanzania mwenye shahada ya kwanza ya Uhandisi wa Miamba akipewa kazi ya kitaalamu, analipwa ujira usiozidi Dola za Kimarekani 800 kwa mwezi wakati mfanyakazi kama huyo wa kigeni analipwa ujira usiopungua dola za kimarekani 8,000 yaani mara kumi zaidi japo wanafanya kazi sawa.”alisisitiza kwa kuhoji hapa usawa uko wapi.
Alieleza kwamba pengo hilo la kipato kwa hali yoyote ni kubwa sana na ni changamoto kwa wafanyakazi, waajiri, vyama vya wafanyakazi na taifa kwa ujumla kwani madhara yake ni pamoja na kuwepo matabaka mahala pa kazi, migogoro na kuikosesha mapato makubwa serikali iwapo viwango hivyo havitarekebishwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza aliyekuwa amuwakilishe Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muongo, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Wambura Sabora alisema kuwa ni ajabu wageni wenye ujuzi sawa na wazawa (watanzania) kupata mishahara mikubwa mara kumi zaidi ya wazalendo hivyo atahakikisha atalifikisha suala hilo serikalini.
Mhandisi Sibora alisema kufatia risala hii iliyosomwa na Katibu, ambayo imeeleza mambo mengi nami niwahakikishie NUMET na kuwashukuru na kuikumbusha na kuiamsha serikali pale inapoonekana imelala hivyo ijikite katika misingi ya uanzishwaji wake na kuwa suluhisho la wanachama wake bila kuwa chanzo cha migogoro katika sekta ya Nishati na Madini kwenye migodi iliyopo hapa nchini.