ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 26, 2025

WAPANDA MLIMA KILIMANJARO KUTOA UJUMBE MZITO WA TAHADHARI DHIDI YA MAAMBUKIZI YA VVU.

 NA ALBERT G.SENGO

Katika kuhakikisha jitihada za kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (HIV), kuondoa unyanyapaa, na kupunguza vifo kufikia mwaka 2030, jamii imetakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuacha ngono zisizo salama na kutumia kinga ili kuepukana na ugonjwa huo. Akiongea wakati wa kukabidhi vyeti vya pongezi kwa mashujaa wa kampeni ya GGML Kili Challenge waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa miguu na baiskeli kupitia njia ya Machame inayofadhiliwa kwa pamoja na mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw.Nurdin Babu ameikumbusha jamii kuwa ugonjwa huo bado upo. #mountkilimanjaro #samiasuluhuhassan #habari

Friday, July 25, 2025

Rais Dkt. Samia] Ashiriki Maadhimisho ya Mashujaa Kitaifa katika viwanja vya Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma

 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ana ule wa Afrika Mashariki ukiimbwa katika Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025.
















 Matukio mbalimbali kwenye Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mtumba Jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025.

JAMII YATAKIWA KUENDELEA KUCHUKUWA TAHADHARI DHIDI YA UKIMWI


Katika kuhakikisha jitihada za kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (HIV), kuondoa unyanyapaa, na kupunguza vifo kufikia mwaka 2030, jamii imetakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuacha ngono zisizo salama na kutumia kinga ili kuepukana na ugonjwa huo. 

Akiongea wakati wa kukabidhi vyeti vya pongezi kwa mashujaa wa kampeni ya GGML Kili Challenge waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa miguu na baiskeli kupitia njia ya Machame inayofadhiliwa kwa pamoja na mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw.Nurdin Babu ameikumbusha jamii kuwa ugonjwa huo bado upo.

“Kuweni makini na kuchukua tahadhari, ugonjwa wa Ukimwi bado upo,” amesema Mkuu wa Mkoa, akisisitiza umuhimu wa elimu endelevu na tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.

Alisema jamii likiwemo kundi kubwa la vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30 — linahitaji elimu zaidi kuhusu Virusi vya Ukimwi na jinsi ya kujikinga na kuwalinda wengine.
Sehemu ya wapanda mlima Kilimanjaro baada ya kupokelewa waliposhuka katika Kili Challenge kwa ajili ya kuchangia watu wenye Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Bw. Ashraf Suryaningrat, ameweka bayana kuwa mgodi huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya Virusi vya Ukimwi ili kufanikisha malengo ya Sifuri Tatu (yaani hakuna maambukizi, hakuna unyanyapaa, na hakuna vifo kufikia mwaka 2030).

“Mgodi wa GGML sio tu unajihusisha na uchimbaji madini wenye uwajibikaji, bali pia unachangia maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo afya — ambayo ni msingi mkuu wa maendeleo,” amesema. 
Ameongeza kuwa upandaji wa Mlima Kilimanjaro haukuwa tu kielelezo cha utalii, bali pia ulikuwa kielezo cha na uzalendo ambapo waliopanda mlima huo, wakiwemo watoto yatima wawili wenye umri wa miaka 13 walijitolea kwa jasho na maumivu kwa ajili ya kuonesha uzalendo huo na upendo kwa jamii.

Akiongea mapema asubuhi wakati wa kuwapokea mashujaa hao, Pia Simon Shayo, Makamu wa Rais wa Uendelevu na Mahusiano, Africa, AngloGold Ashanti, kampuni mama ya GGML amesema katika kuadhimisha miaka 25 ya mgodi huo hapa nchini, wanaona fahari kampeni hiyo ikiendelea kufanyika kila mwaka kwa kipindi cha miaka 23 mfululizo, kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali na kuleta matokeo chanya katika jamii.

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kupitia kampeni hii katika miaka ijayo ili kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema Bw.Shayo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa, ameeleza kuwa mbali na upandaji wa Mlima Kilimanjaro, kampeni hiyo pia ilihusisha upimaji wa hiari wa UKIMWI na utoaji wa elimu ya kujikinga, ambapo jumla ya watu 1,632 walipimwa, nusu yao wakiwa wanawake, na kondomu 54,728 zilisambazwa.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita (Bw. Martin Shigela) uliopo mgodi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Bi. Sakina Mohamed, ameongeza kuwa mgodi huo umechangia miradi mbalimbali ya kijamii mkoani humo — ikiwemo maji, ujenzi wa barabara na kulea kituo cha watoto yatima — kama sehemu ya kuunga mikono juhudi za Serikali.
Sehemu ya wapanda mlima Kilimanjaro baada ya kupokelewa waliposhuka katika Kili Challenge kwa ajili ya kuchangia watu wenye Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.


Wakati wa makabidhiano hayo ya vyeti kwa washiriki, kampeni hiyo pia ilikabidhi zaidi ya milioni 130 kwa asasi tano za kiraia wakati wa sherehe hizo zilizofanyika Moshi Club mkoani humo.
Taasisi zilizokabidhiwa fedha ni pamoja na Mtandao wa Vijana wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ( Network For Young People Living with HIV, ambao wamekabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 29.

Taasisi nyingine ni Pata Maendeleo ya Rukwa iliyokabidhiwa milioni 20, Kikundi cha Wanawake cha Kupambana na Ukimwi cha Kilimanjaro (KiwakkukiI kilichokabidhiwa milioni 29 , Jali Afya Yako, Epuka Maambukizi kilichokabidhiwa milioni 30 na Kongwa Arusha DC kilichokabidhiwa kiasi hicho hicho cha fedha.
Kampeni ya GGM Kili Challenge iliyoanza miaka 23 iliyopita, imekuwa ikikusanya fedha kwa ajili ya kusaidia katika mapambano ya janga hilo kupitia taasisi mbalimbali zilizojikita katika mapambano hayo na kutoa misaada katika hospitali, vituo vya afya na kulelea watoto yatima.

WATAALAMU WA AFYA MUHIMBILI MLOGANZILA WATAKIWA KUZINGATIA KWA WELEDI MATUMIZI YA VIFAA TIBA

 


NA VICTOR MASANGU 

Wataalam Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wametakiwa kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa tiba ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kupunguza gharama za kukarabati vifaa hivyo pale vinapoharibika.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Tiba MNH-Mloganzila Dkt. Elineema Meda wakati wa kongamano la kitaaluma lilokutanisha wataalam wa kada mbalimbali wa hospitali hiyo.

Dkt. Meda ameongeza kuwa matumizi sahihi ya vifaa tiba yataendelea kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwakuwa wagonjwa watakuwa na uhakika wa kupata huduma wakati wowote bila kikwazo chochote kinachotokana na ubovu wa vifaa tiba.

Akitoa mada katika kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Vifaa Tiba Mhandisi Chacha Saidi amesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2024/2025 idara yake imefanya matengenezo ya vifaa tiba 250, utambuzi wa vifaa tiba vilivyoharibika 286, ukaguzi wa vifaa 180 na utekelezaji wa matengenezo kinga kwa vifaa 60.

Aidha, Mhandisi Chacha ameongeza kuwa idara yake imeendelea kutoa mafunzo kwa watumiaji, kufunga vifaa tiba 18 na utatuzi wa changamoto mbalimbali 102 hatua iliyoboresha utendaji kazi na kuendelea kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Wednesday, July 23, 2025

JIBRIL SILLAH WA AZAM FC AJIUNGA NA ES SETIF YA ALGERIA

 

ALIYEKUWA winga wa Azam FC ya Dar es Salaam, Gibril Sillah raia wa Gambia amejiunga na ES Setif ya Algeria.


Setif ilipost juzi kumtambulisha na kumkaribisha mchezaji huyo aliyeondoka Azam FC baada ya kumaliza mkataba wake.


Sillah aliwasili Azam FC katika dirisha dogo Januari 7, mwaka 2023 akitokea Raja Casablanca ya Morocco baada ya awali kuchezea timu nyingine nchini humo, JS Soualem.


Alijiunga na Raja Agosti 27 mwaka 2021 akitokea Teungueth ya Senegal, lakini Januari 24 mwaka 2022 akapelekwa kwa mkopo JS Soualem alikocheza hadi anasajiliwa Azam FC.


Kabla ya kwenda Teungueth Julai 1, mwaka 2017 alichezea Samger FC na Fortune FC za kwao, Gambia.

YANGA SC YAMSAJILI CASEMIRO WA ZENJI, ABDULNASIR MOHAMED ABDALLAH

 KLABU ya Yanga imemtambulisha kiungo chipukizi, Abdulnasir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’ (20) kuwa mchezaji wake mpya akijiiunga na mabingwa hao wa Tanzania kutoka Mlandege ya Zanzibar.

Huyo anakuwa mchezaji mpya wa tatu Yanga kuelekea msimu ujao – baada ya kiungo raia wa Guinea, Balla Mousa Conte kutoka Sfaxien ya Tunisia na winga mzawa, Offen Francis Chikola kutoka Tabora United.

Casemiro ni mchezaji ambaye amekipambanua vyema kipaji chake ndani ya misimu michache ya kucheza soka ya Zanzibar kiasi cha kuwa tegemeo kwenye klabu yake na timu ya taifa ya visiwani humo.


Mshindi huyo wa Tuzo Mwanasoka Bora kijana msimu wa 2024-25 katika tuzo za Farafa Zanzibar – aliiwezesha Mlandege kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya PBZ Zanzibar na kuiwezesha pia Zanzibar Heroes kutwa Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu.

INEC YAWANOA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MKUU WA MIKOA YA MWANZA,MARA YAWATAKA KUZINGATIA SHERIA NA TARATIBU

Jaji wa Mahakama Kuu na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Asina Omari akizungumza kwenye mafunzo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi Hidaya Gwando akielezea lengo la mafunzo.

…………….

Na Hellen Mtereko, Mwanza

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa mafunzo kuhusu Sheria,kanuni,maelekezo mchakato na taratibu za uchaguzi kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa,wasimamizi wa uchaguzi,wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo,maafisa uchaguzi na maafisa ununuzi 110 kutoka mikoa ya Mwanza na Mara.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Benki Kuu Jijini Mwanza.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Hidaya Gwando amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa na uwezo wakusimamia shughuli za uchaguzi watendaji wa uchaguzi walioteuliwa ili waweze kuifanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Mafunzo haya yanafanyika katika awamu mbili awamu ya kwanza yakifanyika Julai 15 hadi 17 julai 2025 katika vituo saba vya mikoa ya Dodoma,Geita,Iringa,Kagera,Kasikazini unguja,Kigoma,Kilimanjaro,Kusini Unguja,Lindi,mjini Magharibi,Morogoro,Mtwala,Njombe,Ruvuma,Singida,Tabora na Tanga”, Amesema Gwando.

Aidha, kwa sasa Tume ipo katika awamu ya pili ambapo katika awamu hiyo mafunzo yameanza leo Julai 21 na yatamalizika Julai 23 mwaka huu.

“Awamu hii itahusisha Mikoa ya Arusha, Dar es salaam,Kasikazini Pemba,Katavi,Kusini Pemba,Mara,Mbeya,Pwani,Rukwa,Shinyanga,Simiyu,Songwe na Mkoa wa Mwanza”

Awali akifungua mafunzo hayo Jaji wa Mahakama Kuu na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Asina Omari ametoa maelekezo nane kwa watendaji hao akiwataka kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea na wazingatie kuwa baadhi ya mambo yamekuwa yakibadilika mathalani kumekuwa na mabadiliko makubwa ya sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

“Vishirikisheni vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote zenye kuzingatia matakwa ya sheria na katiba ya tume,”amesema Jaji Asina

Jaji huyo pia amewataka kushirikisha wadau wa uchaguzi hususani katika maeneo ambayo kwa mujibu wa Katiba,sheria,kanuni miongozo na maelekezo yatakayotolewa na tume yanatakiwa kushirikishwa huku pia wakitakiwa kufanya utambuzi mapema wa vituo vya kupigia kura na kuhakikisha kunampangilio mzuri na unazozingatia watu wenye ulemavu.

Wanchoke Chinchibera ni msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ukerewe amesema tofauti na zamani katika awamu hii, majina ya wasimamizi wa majimbo yamechapishwa kwenye mfumo na gazeti la serikali hali itakayoondoa malalamiko yaliyokuwa yanatokea kipindi cha nyuma na hivyo kuufanya uchaguzi kuwa huru na haki.

“Tumeaminiwa na sisi tunaporudi kwenye majimbo yetu tunaenda kutenda haki na kutoleta migogoro miongoni mwa vyama na wadau wa siasa walioko kwenye maeneo yetu kwakuwa sisi tunakuwa sehemu ya utekelezaji wa sheria mpya ya uchaguzi na sio kusababisha migogoro,” amesema Chinchibela.

Kwa upande wake Mohamed Chande, Msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Magu amesema baada ya mafunzo hayo wataenda kusimamia haki ya makundi mbalimbali na kukahakikisha kwamba uchaguzi unakuwa huru na waki.

Tuesday, July 22, 2025

DED HALMASHAURI WILAYA YA MBEYA KUCHELE ASHUSHA NONDO BABU KUBWA KWA WATUMISHI WAPYA 119

 


Na Mwandishi wetu,Mbeya


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Erica E. Yegella, amewataka  watumishi ambao wamepata ajira mpya  kuhakikisha wakwenda kufanya kazi kwa weledi na maarifa kwa kuzingatia sheria na taratibu za  utumishi wa umma. 

 Yegella ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wapya wa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kuwataka  kufanya kazi na  kuwaheshimu viongozi wengine kwenye maeneo wanayokwenda wakiwemo viongozi wa dini na wale viongozi wa dini. 

Aidha mkurugenzi huyo amewataka kwenda kuwa kioo kwa jamii na wenye kutunza maadili ikiwemo kwenye eneo la mavazi akiwaasa kuzingatia mavazi ya utumishi wa umma hususani wanapokuwa katika utendaji wao.

 Erica amesisitiza kufanya kazi kwa bidii na kutokuwa na makundi yasiyo faa kazini na katika jamii kwa ujumla.

Pamoja na maonyo, maelekezo na ushauri wake pia mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Mbeya amewataka kuwa na ushirikiano na wakuu wao wa kazi na viongozi watakaokuwa wakifanya kazi pamoja na jamii inayowazunguka ili kudumisha umoja na kuendeleza shughuli za maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji amehitimisha hafla hiyo fupi na watumishi hao kwa kuwaapisha kiapo cha uadilifu na utii pamoja na kutunza siri za utumishi wa umma.

RAIS DKT. SAMIA KUZINDUA RASMI MRADI WA BANDARI KAVU YA KWALA JULAI 31 KIBAHA PWANI

 


Na Victor Masangu,Pwani 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara mkoani Pwani Julai 31,2025 hususani katika Kata ya Kwala Halmashauri ya Kibaha Vijijini ambapo pamoja na mambo mengine Rais Samia atazindua Kongani ya viwanda ya Kwala yenye viwanda 250.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa kauli hiyo Julai 22 ,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika mkutano uliofanyika katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani lililopo Manispaa ya Kibaha.

Kunenge amesema kuwa,Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan atafanya ziara katika eneo la Kwala sehemu ambayo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa ambapo akiwa katika eneo hilo atafanya mambo mbalimbali makubwa.

Amesema Rais akiwa katika eneo la Kwala miongoni mwa shughuli atakazozifanya ni pamoja na  kuzindua safari rasmi ya treni ya Mwendokasi (SGR) ya kubeba Makasha na kupeleka Dodoma.

Ameongeza kuwa ,shughuli nyingine atakayoifanya Rais ni kuzindua bandari Kavu ya Kwala yenye uwezo wa kuhudumia Makasha 823 kwa siku na Makasha 30,000 kwa mwaka.

Kunenge amesema bandari Kavu ya Kwala itaongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ambapo kimsingi bandari Kavu hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa Makasha katika bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 30.

Aidha ,Rais Dkt.Samia akiwa katika eneo hilo la Kwala pia atazindua maeneo ya ujenzi wa bandari Kavu kwa ajili ya nchi za Kongo, Zambia,Burundi,Malawi, Zimbabwe na Uganda ambapo pia alisema Sudan na Somalia nao tayari wameonyesha nia ya kujenga bandari Kavu katika eneo hilo.

Amesema siku hiyo itakuwa fursa kwa Rais Samia kupokea Mabehewa 160 ya Reli ya Kati ambapo kati ya hayo Mabehewa 20 yamekarabatiwa na Mabehewa 100 yamenunuliwa mapya na Serikali na mengine 40 yamekarabatiwa na Shirika la Chakula Duniani pamoja na Wakala wa Ushoroba wa Kati.

Kunenge amesema pamoja na mambo mengine lakini pia Rais Samia ataweka jiwe la msingi kwenye Kongani ya Viwanda ya Kwala yenye viwanda 250 Kongani ambayo ni kubwa katika nchi ya Tanzania.

MUDATHIR YAHYA AJITIA KITANZI YANGA SC HADI 2027


 KIUNGO wa Kimataifa wa Tanzania, Mudathir Yahya Abbas (29) amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.

Yanga wameposti video ya Mudathir akiwa anasaini na kuambatanisha a maelezo kwamba mchezaji huyo ni mali yao hadi mwaka 2027.
Mudathir Yahya Abbas aliyezaliwa Mei 6, 1996 huko Jang’ombe, visiwani Zanzibar alijiunga na Yanga Januari mwaka 2023 akitokea Azam FC na katika misimu miwili na nusu ya kuwa wana Jangwani hao amejijengea heshima kubwa kwa uhodari wake kwenye eneo la kiungo.

Kisoka Muda aliibukia katika akademi ya Azam FC mwaka 2012 kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa chini ya Kocha Muingereza, Stewart John Hall na kufanikiwa kuwa mchezaji muhimu.

Hata hivyo, mara mbili Muda alikwenda kucheza Singida Black Stars baada ya kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC na mar azote alirejeshwa baada ya kufanya vizuri, kabla ya kuhamia Yanga Januari 2023.

DC CHIRUKILE AZINDUA MAFUNZO YA MAAFA SUMBAWANGA ASISITIZA UTAYARI MAPEMA

 

 

*Na Mwandishi wetu- RUKWA

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya, Mhe. Nyakia Ally Chirukile, amezindua rasmi mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa wajumbe wa kamati za wilaya hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuwa tayari kabla ya majanga kutokea.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, yaliyofanyika  tarehe 21 Julai, 2025 kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Menejimenti ya Maafa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Mhe. Chirukile amesema kuwa maafa kama maporomoko ya ardhi, mlipuko wa kipindupindu, radi na ajali za majini yameathiri jamii na uchumi wa wilaya hiyo.

> “Kuchukua hatua kabla ya majanga ni nafuu zaidi kuliko kushughulika na athari. Mafunzo haya ni nyenzo ya kuongeza ufanisi wetu katika kuzuia na kukabili majanga,” alisema Mhe. Chirukile.

Kwa upande wake, Kanali Selestine Masalamado kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Maafa, amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, na yana lengo la kuwawezesha viongozi wa serikali za mitaa kuwa mstari wa mbele wakati wa dharura.

 Naye mwakilishi wa UNDP, Bi. Clara Peter Maliwa, amepongeza Wilaya ya Sumbawanga kwa kujitoa kikamilifu kushiriki mafunzo hayo na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo ya kukabili majanga nchini.

Mafunzo haya yamewaleta pamoja wajumbe wa Kamati Elekezi ya Maafa ya Wilaya na Kamati ya Wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, wakiwa na lengo la kujifunza mbinu bora za kupanga, kukabili, na kurejesha hali baada ya majanga.


AWAMU YA PILI YA MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHIMINI (M&E) KWA WATUMISHI WA UMMA YAFUNGULIWA JIJINI DODOMA

Na mwandishi wetu Dodoma


Awamu ya Pili ya Mafunzo ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa Watumishi wa Umma, yamefunguliwa leo tarehe 21 julai, 2025 na Bi. Sakina Mwinyimkuu — Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini ili kujenga utamaduni wa uwajibikaji na utendaji unaotegemea matokeo katika Serikali yetu.

Mafunzo haya, yanayofanyika jijini Dodoma, yamewakutanisha washiriki kutoka wizara, idara na taasisi mbalimbali za Serikali, kwa lengo la kuongeza uwezo wao katika usimamizi wa matokeo, matumizi ya taarifa na takwimu, pamoja na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango.

RC BALOZI,DKT BATILDA BURIAN ATOA AGIZO KWA WAKANDARASI MRADI WA UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI TANGA WA HATIFUNGANI YA KIJANI

 


Na Oscar Assenga,TANGA


MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt Batilda Burian amewataka wakandarasi watakaohusika katika utekelezaji wa mradi wa hatifungani ya kijani kwa ajili  kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Tanga kuhakikisha wanautekeleza kwa ufanisi mkubwa na ukamilike kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma lengwa.



RC Batilda aliyasema hayo Jumatatu ya Tarehe 21 July 2025 wakati akipokea vifaa ambayo vinakwenda kuboresha huduma za maji katika mkoa wa Tanga na wilaya ya Tanga na Jiji la Tanga ambavyo ni mabomba na viungo yenye urefu wa kilomita 55 na kati ya mabomba yenye urefu wa kilomita 170 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa h
ati fungaji ya kijani.


Vifaa hivyo vinakwenda kutumika katika kutekeleza na kuendelea mradi wa uboreshaji wa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Tanga katika awamu ya tatu unaogharimu kiasi cha zaidi ya Bilioni 6 ambao utaongeza wigo na fursa ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Maeneo yanayokwenda kutumika na vifaa hivyo katika uboreshaji wa Maji ni Muheza,Pangani na Mkinga ambapo alisema huo ni ubunifu ambao sio mamalaka nyingi za maji mjini zinaweza kwenda wilaya karibia tatu hivyo aliwapongeza kwa kuwa mamlaka ya mfano Tanzania nzima.

“Tunawapongeza sana na tumetayarisha nishani tuwapatie kwa kuendelea kutuheshimisha mkoa wa Tanga katika tasnia ya maji najua mlipewa zawadi siku ya maji katika bara la afrika kama mnatambulika Kimataifa na Afrika na wao kama mkoa watakuwa watu wa ajabu wasipotambuaa mchango wao naa jutihada”Alisema

Alisema kwamba lazima wakandarasi ambao watakaotekeleza mradi huo kuhakikisha wanafanya kazi kwa waledi mkubwa ambao utakuwa chachu ya kukamilika kwa wakati na hivyo wananchi kuweza kunufaika na huduma hiyo muhimu jambo ambalo linawezesha kuondokana na changamoto walizokuwa wanakumbana nazo awali

“Leo hii ni siku muhimu tunapokea mabomba haya na viungio vyake hivyo niwatake wakandarasi wote ambao wanahosuka kwenye utekeleza wa mradi kuhakikisha mradi unatekeleza kwa ufanisi mkubwa na unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma lengwa”Alisema RC huyo.

Aliongeza kwamba fedha hizo zimetokana na ubunifu mkubwa uliofanywa na  Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) katika kupata hati fungani ya gharamai ya Bilioni 53.12 ambayo imewezea shughuli hizo kuweza kufanyika na kuleta tija kubwa katika utekelezaji wa miradi.

Aidha alitumia fursa hiyo kuhimiza ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo kutokana na upekee wake kwenye bara la ulimwengu kutokana na kwamba uwekezaji wake na waliowekeza hisa kwa sasa wameshaanza kupewa gawio kila kota wanapata gawio.

“Huu ulikuwa ni ubunifu mkubwa na mafanikio yanaonekana kwa mtu mmojammoja  na mkoa umekuwa salama kuwa sababu kukosekana kwa maji ni jambo la kiusalama hivyo tuendeee kuhakikisha maeneo yenye uvujaji wa maji mnaendelea kuyazibiti ili kupunguza upotevu wa maji “Alisema RC Balozi Batilda.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza Tanga Uwasa kwa jitihada zao kubwa za kuongeza upatikanaji na ubora wa maji na kuangalia vyanzo vya maji na mipango na mikakakti ya kupanda miti mingi kwa kuwashirikisha wananchi waliopo kwenye vyanzo vya maji ikiwemo kuendelea kutoa vifaa lakini kuwasaidia katika shughui zao mbalimbali ili waendelea kuwa walinzi wazuri na wajue kwamba vyanzo hivyo vinathamani na wanathamni mchango wao katika kuvilimda.

Aliongeza kwamba mkoa huo unathamani mchango  unaofanywa na Wizaraa ya maji chini ya Waziri Jumaa Aweso na ameendelea kufanya makubwa Kitaifa na kimkoa ndio maana hata watendaji wa Maji mkoa ikiwemo mameneja hawajamuangusha ndio wamesimama kidete kuelezea umma ilani ya CCM imetekelezwa kwa asilimia 100 na katika miji yetu asilimia 95 ya maji imewezeka kufikiwa.

Awali akizungumza katika halfa hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanga Uwasa Dkt Ally Fungo alisema kutokana mradi huo anaona mamlaka ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa asilimia 100 kwa muda mfupi ujao hivi sasa wapo asilimia 95 na kukamilika kwa mradi huo asilimia hiyo wameuvuka na mradi huo wanatarajia mpaka utakapofika mwezi Octoba mwaka huu utakuwa umekamilika kama mambo yote yatakwenda sawa.

Alisema kwamba hakuna sababu kwanini yasiende sawasawa kwa leo wamepokea mabomba kontena 11 bado 8 na vitafika kwa muda ambao umewekwa hivyo wanaiona Tanga Uwasa ikitatua shida ya maji katika wilaya hizo nne ambazo ni wilaya ya Tanga,Muheza,Mkinga na Pangani na hawaoni kama kuna shida na wapo wapi tayari hata wakiambiwa wasogee wilaya nyengine ikiwemo Korogwe uwezo wanao kutokana na utalaamu walionao

Aidha alisema kwamba hiyo ni awamu ya nne ya mradi huo na awamu ya kwanza walipanua mtambo wa kusafisha maji  na awamu nyengine kusogeza maji kwenye wilaya ambazo wameongezewa na awamu ya tatu ni mkopo kutoka benki ya TIB wakatanua zaidi huduma zao katika awamu tofauti tofauti ikiwemo kurekebisha mitambo ambayo ni ya muda mrefu eneo la usafishaji Maji Mowe na awamu ya nne ni kusambaza huduma ya maji katika maeneo ya miji.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Geofrey Hilly  alisema wana jambo kubwa la kupokea baadhi ya mabomba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa hati fungaji ya kijani ambayo kwa sasa yana kilomita 55 na lengo la mabomba yote yana kilomita 170 ni thamani ya zaidi Bilioni 6.3 .

Alisema mradi huo unalengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya Maji katika wilaya ya Tanga, Mkinga Muheza na Pangani utakapokamilika wananchi 555,000 watanufaika kwa namna mbalimbali wapo ambayo hawajafikiwa na maji watafikiwa na wale ambao miundombinu ulikuwa chakavu itaboresha.

Aidha alisema wanategemea mwisho wa mradi huo hali ya upatikanaji wa maji itakuwa ni nzuri sana lakini pia watajenga miundombinu mikubwa na wanaongeza chanzo cha maji kutoka uwezo wa lita Milioni 42 kwenda Lita Milioni 72 lakini na mtambo wa kusafisha maji kutoka lita milioni 45 hadi Lita Milioni 60 kwa hiyo maji hayo yatasaidia kwenda kwenye hizo wilaya bila shaka yoyote.

Mwisho.