ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, November 23, 2019

RC MONGELLA AIPONGEZA REA “WAHISANI WAAHIDI USHIRIKIANO ZAIDI”


Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella (katikati) ameupongeza mpango wa Serikali ya Tanzania wa usambazaji nishati vijijini kupitia REA na kubainisha kwamba ni miongoni mwa mipango bora ya uwezeshaji wananchi kiuchumi barani Afrika.

Mongella alitoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye mkutano wa majumuisho baina ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wabia mbalimbali wa Maendeleo baada ya kutembelea miradi ya nishati vijijini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa uliofanyika Novemba 22, 2019 jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Julius Kalolo akabainisha kwamba wabia wa maendeleo USAID, SIDA, Benki ya Dunia, Benki ya Afrika pamoja na Nchi za Nordic wameridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali kusambaza nishati vijijini na hivyo kuahidi ushirikiano zaidi.

Friday, November 22, 2019

WAZIRI MKUU KASIMU MAJALIWA MGENI RASMI MAADHIMISHO SIKU YA UKIMWI DUNIANI KITAIFA MWANZA


Suala la maambukizi ya virusi vya HIV vinavyosababisa ugonjwa wa Ukimwi bado linaendelea kuwakosesha usingizi wataalamu wa afya kote duniani.

Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO) hadi sasa ugonjwa huo umewaangamiza zaidi ya watu milioni 35, hii ni taarifa mbaya kuliko zote. 

Jeh Kipi cha kujifunza toka kwa waathirika wa virusi vya Ukimwi?
Jeh Jamii inawachukulia vipi waathirika wa virusi vya Ukimwi?
Jeh Vita dhidi ya unyanyapaa bado inapiganiwa na wana jamii?
Jeh Waathirika wa VVU wanawezajie kupata haki zao za msingi?

Majibu ya maswali haya yatajibiwa kupitia wiki ya Maonyesho ya Siku ya ukimwi Duniani, yanayo taraji kuanza tarehe 25 Novemba 2019, nacho kilele kuwa Disemba Mosi 2019 viwanja vya Rock City Mall Mwanza.

John Mongella ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, hapa anafunguka zaidi. 

SERIKALI YAMPA SIKU 14 MKANDARASI KUKAMILISHA MRADI WA MAJI MAGU

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akijadiliana jambo na Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga wakari wa ziara ya kukaga ujenzi wa mradi wa maji wa Mji wa Magu.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akimsikiliza Msimamizi wa ujenzi wa mradi wa maji mji wa Magu, Mhandisi Wilbert Bujiku akielezea hatua zilizofikiwa za ujenzi wake.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akitoa maelekezo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji Magu. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga na kulia ni Msimamizi wa ujenzi wa mradi, Mhandisi Wilbert Bujiku.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akitoa maelekezo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji Magu. 
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na ujumbe aliyoambatana nao wakimsikiliza msimamizi wa mradi, Mhandisi Wilbert Bujiku (hayupo pichani) akiuelezea mradi.
Eneo la chanzo cha maji cha mradi wa Mji wa Magu ambapo kuna mitambo ya kuvutia maji yanayotoka ziwani.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa muda wa siku 14 kwa Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji Mji wa Magu.

Ametoa agizo hilo Novemba 22, 2019 alipofanya ziara kwenye mradi huo Wilayani Magu, Mkoani Mwanza ili kujionea hatua ya ujenzi iliyofikiwa sambamba na kuzungumza na Mkandarasi.

Mara baada ya kutembelea eneo la chanzo cha maji na kituo cha tiba ya maji cha mradi, Mhandisi Sanga alibainisha kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi na kwamba tayari wananchi wameanza kupata huduma ya maji lakini yapo maeneo machache ambayo bado hayajakamilika inavyopasa na hivyo kumtaka Mkandarasi kuhakikisha anayakamilisha kwa muda aliyopangiwa.

“Mradi unaridhisha umejengwa vizuri ila tu shida ninayoiona hapa kuna maeneo machache bado hayajakamilishwa vizuri ambayo kitaalam tunaita 'snags' kama kuna pipe imechomoka, koki, kurudishia rangi,  na vingine vidogo vidogo.  Maelekezo yangu ni kwamba ndani ya wiki mbili kuanzia leo maeneo haya yakamilike,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Aliongeza kuwa Mkandarasi amekwishafanya kazi kubwa na kwamba hizo chache zilizobaki ahakikishe anazikamilisha haraka na kwamba baada ya siku hizo 14 awe amekabidhi mradi kwa Mamlaka ya Maji Mji wa Magu na awe ameondoka kwenye eneo la mradi ili kuondokana na gharama mbalimbali za usimamizi wake.

“Hata kama hatumlipi mkandarasi kwa hizi kazi zilizobakia lakini gharama bado zitakuwepo tu ikiwa ni pamoja na kulipa watendaji wetu ambao ni wasimamizi wa mradi fedha za kujikimu na gharama zingine zikiwemo za usafiri wa kuja kukagua kazi mara kwa mara na hivyo kutumia mafuta,” alisema Mhandisi Sanga.

Aliongeza kuwa fedha za ujenzi wa mradi ni za wananchi kwani zilitolewa na wadau wa maendeleo ambao aliwataja kuwa ni Benki ya Maendeleo ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kama mkopo wa masharti nafuu ambao Serikali inapaswa kulipa.

Alitahadharisha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli haipo tayari kushuhudia matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na kwamba haitowavumilia wakandarasi wanaochelewesha miradi kote nchini bila sababu za msingi.

“Namshukuru sana Mhe. Rais ambaye kimsingi ndio mtoaji wa fedha, tunasema fedha imetolewa na wafadhili lakini ni mkopo wa masharti nafuu na hivyo zitalipwa kwa kodi za wananchi, kwa hiyo tutahakikisha hata shilingi ya mwisho inatumika vizuri na hatuwezi kumtazama Mkandarasi afanye anavyojisikia yeye wakati wa kukamilisha mradi,” alisema Mhandisi Sanga.

Akizungumzia maeneo ambayo hayajafikiwa na mradi na uhitaji upo, Mhandisi Sanga alielekeza Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Magu (MAUWASA) pamoja na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wayafanyie kazi na kwamba kwa maeneo yatakayokuwa nje ya uwezo wao wayawasilishe wizarani ili wananchi wote waliokusudiwa waweze kunufaika na mradi huo. 

Aidha, alishukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Magu kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Magu, kwa ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa mradi na kwa uhamasishaji walioufanya kwa wananchi waliokuwa wakidai fidia.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa wa maji ambao aliuelezea kuwa ni mwarobaini wa kero ya muda mrefu ya upatikanajni wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wake.

Naye msimamizi wa mradi kutoka MWAUWASA, Mhandisi Wilbert Bujiku aliahidi kusimamia vyema utekelezaji wa maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu na kwa wakati kama ilivyoelekezwa.

Aidha, akiwasilisha taarifa ya mradi kwa ujumla, Mhandisi Bujiku alisema mradi utanufaisha zaidi ya wananchi 120,000 na kwamba hadi hivi sasa jumla ya kaya 4,911 tayari zimeunganishwa na wanapata huduma ya maji na kwamba vituo 21 vya kuchotea maji pia vimejengwa maeneo mbalimbali kulingana na idadi ya wakazi wa maeneo husika.

Aliongeza kuwa mradi umehusisha ujenzi wa tenki la lita milioni mbili za maji, ulazaji wa bomba kuu kutoka ziwani hadi kwenye tenki umbali wa kilomita 10.9 na bomba za usambazaji kwa wananchi umbali wa kilomita 67 na kwamba umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 16.


MAGOLI | YANGA SC 3-2 JKT TANZANIA (VPL - 22/11/2019)


Mabingwa wa Kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC wamechukua pointi tatu nyingine msimu huu kwa kuifunga JKT Tanzania mabao 3-2, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Magoli ya Yanga yamefungwa na Patrick Sibomana dakika ya 11, Juma Balinya dakika ya 22 na David Molinga dakika ya 35 huku mabao ya JKT yakifungwa na Adam Adam dakika ya 13 na Danny Lyanga dakika ya 45.

Thursday, November 21, 2019

MAHAFALI YA KUMI CHUO KIKUU CHA DODOMA (UDOM).


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli atunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

MASAUNI ATEMBELEA KITUO CHAKAVU CHA POLISI IKUNGI NA KUKAGUA UJENZI WA KITUO KIPYA

 Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Edward Mpogolo wakiongozana kuingia katika kituo chakavu cha polisi , leo wilayani Ikungi mkoani Singida. Serikali iko mbioni kujenga kituo kipya ikiwa ni moja kati ya hatua ya kuhamisha kituo hicho pichani ambacho ni chakavu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,akimuongoza  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(watatu)kutoka nje ya  Kituo cha Polisi Ikungi , leo wilayani Ikungi mkoani Singida. Serikali iko mbioni kujenga kituo kipya ikiwa ni moja kati ya hatua ya kuhamisha kituo hicho pichani ambacho ni chakavu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu pamoja na viongozi wengine wilayani Ikungi, wakitoka kukagua Mradi wa Makao Makuu ya Polis wilayani hapo(pichani), leo ikiwa ni harakati za kujenga kituo kipya wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi wakikagua Ujenzi wa Makao  wakitoka kukagua Mradi wa Makao Makuu ya Polisi wilayani hapo, leo ikiwa ni harakati za kujenga kituo kipya wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kutuma timu ya wataalamu kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kufika wilayani Ikungi Mkoani Singida, kutathmini maendeleo ya Ujenzi wa Ofisi na Kituo kipya cha Polisi baada ya kituo cha awali kuchakaa hali inayopelekea askari na mahabusu kukaa sehemu isiyo salama.
Ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kutembelea Wilayani Ikungi ikiwa ni kuitikia wito wa Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, aliyetaka kauli ya Serikali juu ya uchakavu wa Ofisi, kituo cha polisi Ikungi na hali mbaya ya chumba cha mahabusu wakati wa kipindi cha maswali katika kikao cha Bunge kilichoisha hivi karibuni.
“Nimefika hapa nimeona mazingira wanayofanyia kazi hayaridhishi, serikali ilishaanza Ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya lakini ujenzi umesimama kwa miaka mitano sasa, namuagiza IGP Sirro alete wataalamu waje wafanye tathmini juu ya gharama za umalizwaji ujenzi huu na baada ya kujua basi hatua za haraka zifanyike ili ujenzi huu ukamilike” alisema Masauni
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amesema hali ya kituo cha polisi hicho ni mbaya huku mahabusu wakikaa sehemu chafu ambayo si salama kwa afya ya binadamu.

“Mheshimiwa Naibu Waziri kama nilivyokueleza bungeni wakati nikiuliza swali la nyongeza nadhani sasa umejionea hali ilivyo mbaya, humo ndani umesikia harufu katika chumba cha mahabusu,wanajisaidia humo lakini pia umeona askari wanavyofanya kazi kwenye mazingira mabovu, naomba sasa serikali muangalie uwezekano wa kuharakisha kituo kile kipya hata mkianza na sehemu tu itasaidia adha hii wanayopata wananchi wa wilaya hii” alisema Mbunge Mtaturu
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogoro amesema uwepo wa kituo hicho kipya kikikamilika kitaimarisha Ulinzi na Usalama wilayani hapo ambapo kumekua na changamoto za kiusalama kwasababu ya upya wa wilaya hiyo ambayo imeanza.

NMB YAUNGA MKONO SAFARI KUELEKEA WIKI YA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI KITAIFA MWANZA


"Kama unavyojua NMB ni mdau mkubwa wa shughuli za kijamii, tumekuwa tukisapoti majukumu mbalimbali kama vile vitanda mahospitalini, madawati mashuleni, ujenzi wa madarasa lakini pia harakati mbalimbali za mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kusaidia wasiojiweza"    Alisema Amos David Mwabusi ambaye ni mwakilishi wa Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa katika makabidhiano ya T Shirt 400 zitakazotumika kama sare kupamba maadhimisho hayo ambayo kitaifa kwa mwaka huu 2019 yanafanyika mkoani Mwanza.

Siku ya Ukimwi Duniani inaadhimishwa kila tarehe 1 Desemba kama siku maalumu ya kupanua ufahamu kuhusu maafa yanayoletwa na ugonjwa wa Ukimwi.

Desemba mosi ilichaguliwa kuwa siku ya Ukimwi kutokana na tarehe hiyo kuwa ndiyo siku ambayo virusi cha Ukimwi kilitambulika rasmi mwaka 1981. Toka mwaka 1981 hadi 2007 watu zaidi ya milioni 25 wameshafariki kutokana na Ukimwi. Mwaka 2007 peke yake walifariki milioni 2, kati yao watoto 270,000.

Siku hiyo ilichaguliwa rasmi mwaka 1988 wakati wa Mkutano wa Dunia wa Mawaziri wa Afya Kuhusu Mpango wa Kuzuia Ukimwi. Kuanzia hapo siku hiyo imekuwa ikikumbukwa rasmi na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wanaharakati.

Toka mwaka 1988 hadi 2004, Siku ya Ukimwi Duniani ilikuwa ikiratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Ukimwi (UNAIDS). Mwaka 2005 UNAIDS ililipa shirika lisilo la kiserikali la Kampeni ya Ukimwi Duniani (the World AIDS Campaign) wajibu wa kuratibu siku hiyo.

Kila mwaka siku hiyo hufanyika kwa ujumbe maalumu ambapo Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Jamii ni Chachu ya mabadiliko, tuungane kupunguza maambukizi, mapya ya VVU"

KERO YA MIAKA 59 YA MAJI KITUO CHA AFYA NASSA YATATULIWA

 Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Sibtain Meghjee akitoaa taarifa ya mradi wa maji utakaohudumia Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa wilayani Busega jana.
 Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassani Kabeke akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi kisima cha maji wilayani Busega katika Kijiji cha Bukabile jana, ukiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W kwa imani ya dini ya Kiislamu.
 Diwani wa Kata ya Nyashimo (CCM), Mickness Mayela, akizungumza na wananchi wakiwemo wadau wa maendeleo kabla ya kupokea mradi wa kisima cha maji kilivhojengwa kwa gharama ya sh. milioni 20 na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation jana.
 Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwela akitoa shukurani za serikali kabla ya kupokea mradi wa kisima cha maji kilichojengwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa.
 mmoja akina mama wenye umri zaidi ya miaka 60 Ngunya Luja akipokea kitambulisho cha bima ya afya kati ya 800 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwela, vilivyotolewa an taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF).kulia anayeshuhudia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Alhaji Sibtain Meghjee.
 Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TDCF) Alhaji Sibtain Meghjee, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera (kulia) wakipeana mikono ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya kisima cha maji kitakachohudumia Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa jana.
 Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, akifungua koki ya bomba la maji lililounganishwa kutoka kwenye kisima cha maji kilichojengwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDFC) kwa ajili ya Kituo cha Afya Nassa na wananchi wa kijiji cha Bukabile.Kushoto ni mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Sibtain Meghjee na kulia ni Diwani wa Kata ya Nyashimo (CCM) Mickeness Mayela.
 Mkazi wa Kijiji  ha Bukabile, Specioza Mahondola akitwishwa ndoo ya maji na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera baada ya kupokea mradi kisima cha maji uliojengwa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF).Kushoto anayehushudima ni mwenyekiti wa taasisi hiyo Sibtain Meghjee.
 Mkuu wa Wilaya Tano Mwera (kushoto) akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake kwa jamii, Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TDCF) Sibtain Meghjee (kulia) muda mfupi kabla ya kuikabidhi serikali kisima cha maji safi na salama.
Mjane Leokadia Lyande wa kijiji cha Bukabile akipokea mtambo wa umemejua kwa ajili ya mwanga kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera (mwenye gauni la maua maua).Msaada huo wa mtambo pamoja na vyakula anuwai, mashuka na chandarua vilitolewa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF) jana.Kushoto ni mwenyekiti wa taasisi hiyo Alhaji Sibtain Meghjee.


 NA BALTAZAR MASHAKA, BUSEGA
TAASISI ya  The Desk & Chair Foundation imetumia sh.milioni 20 kutatua kero ya  maji  iliyodumu kwa miaka 59 ikiwakabili wananchi wa Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa wilayani Busega katika Mkoa wa Simiyu.

Kisima hicho kirefu cha maji  kitatumiwa na wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo wajawazito, wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa kwenye kituo hicho cha afya  huku  taasisi hiyo ikitoa sh. 800,000 kugharamia vitambulisho vya wazee 800  vitakavyowatambulisha  kupata matibabu.

Mwenyekiti wa TDFC, Sibtain Meghjee, akikabidhi mradi huo kwa serikali, alisema  kisima hicho kirefu cha maji kimegharimu sh. milioni 20 na kimefungiwa pampu ya kusukuma maji  inayotumia nguvu ya umeme jua na hivyo kukiwezesha kituo cha Afya Nassa na wananchi kupata maji ya uhakika muda wote.

“Tumeridhishwa na mfumo wa mitambo iliyofungwa kisimani hapo kuwa inasukuma maji vizuri hadi kituoni baada ya majribio kufanyika.Kwa niaba ya wafadhili na uongozi wa The Desk & Cair Foundation, tunaikabidhi serikali mradi  huu, hatutakuwa na mamlaka nao isipokuwa kwa matengenezo ya mitambo itakapoharibika,”alisema.

Meghjee alisema taasisi hiyo imetekeleza miradi mbalimbali ya kijamii mkoani Simiyu ikiwa ni pamoja na kuboresha visima vifupi 11 vya maji na kuchimba vipya 12, kufunga mitambo ya umeme jua kwenye Kituo cha Afya Nassa, mradi wa maji safi na salama Lamadi, baiskeli 5 kwa walemavu wa viungo na moja ya kawaida.

Mingine ni mradi wa nyumba 10 za nyasi vijijini kufungiwa mfumo wa umeme jua,vyoo kwenye shule ya Malayele,vibebeo 300 kwa wajasiriamali na vitambulisho vya afya kwa wazee 800 huku miradi kama hiyo ikifanyika pia kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati.

“Naishukuru serikali kwa kutoa vibali na ushirikiano wa dhatiwakati tunapotekeleza shughuli zetu kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi,kama ilivyo kauli mbiu yetu ya Tupo pamoja Iwe Dhiki Iwe Faraja:Huduma kwa Jamii Bila Kuchagua Bila Kubagua,”alisema Meghjee.

Aidha, baadhi ya akinamama wa Kijiji cha Bukabile ambao ni wanufaika wa mradi huo, Nadhifa Yusuf, Specioza Mahondola naWinfrida Masalu,walisema utainufaisha jamii na umewakomboa na adha ya kufuata maji  umbali mrefu,ambapo wakati wa kujifungua walipata shida ya kwenda na maji .

Walieleza kuwa wameteseka miaka mingi kufuata maji umbali wa km 4 kutokana na kijiji hicho kuwa mbali na Ziwa Victoria, walikuwa wakinunua maji sh.1000 kwa ndoo tano ama kuyateka kwenye madimbwi hivyo kwa sasa wataweza kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Kwa upande wa vitambulisho vya bima kwa wazee, mmoja wa wanufaika hao Kitula Kubangwa (71) aliishukuru The Desk & Chair Foundation kuwaondolea changamoto ya vitambulisho vya matibabu na kuishauri serikali iendelee kuwatizama kwa jicho la huruma.

Akipokea mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Busega,Tano Mwera, alisema The Desk & Chair Foundation ni wadau wakubwa wa maendeleo kutokana na misaada yao kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma mbalimbali kwa jamii.
Alisema mradi huo wa maji utabadilisha maisha ya wananchi na wagonjwa wanaotibiwa kwenye kituo cha afya Nassa kwani lengo la serikali ni kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani.

“Maji ni muhimu, mradi huu unaunga mkono juhudi za serikali za kuhudumia wananchi na kuwaletea maendeleo lakini pia sasa watayapata maji karibu na akinamama watatumia muda wao mwingi kufanya shughuli za maendeleo,”alisema Mwera.  

Awali Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nassa, Fred Mruma, alisema changamoto ya maji tangu kujengwa kwa kituo hicho mwaka 1960 imekwisha ingawa bado wana tatizo la nishati ya umeme kwenye chumba cha upasuaji, mashine ya kufua nguo za wagonjwa na mashine ya kupima damu (Full Blood picture machine).

Wednesday, November 20, 2019

BAADA YA KANISA LA MFALME ZUMARIDI KUFUNGIWA, MAASKOFU WATOA TAMKO.


Viongozi wa Umoja wa Makanisa (UMJM), jijini Mwanza, unaoundwa na Mabaraza matatu ya TEC, CCT na CPCT, umeitaka Serikali kuyapitia upya Makanisa mengine ambayo usajili wake haueleweki, ili kuondoa sintofahamu kwa waumini wa madhehebu hayo. 
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya ya Nyamagana, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Dkt. Philis Nyimbi, kufungia Kanisa la Mfalme Zumaridi lililopo eneo la Iseni jijini humo ambalo linadaiwa kuendesha Ibada zake kinyume cha sheria na Katiba ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, Mwenyekiti wa umoja huo, Askofu Philipo Mafuja amesema hatua hiyo iliyofanywa na viongozi wa Serikali kuyafungia Makanisa yanayoendeshwa kinyume cha sheria yanabaraka hata kwa Mungu.
"Maandiko matakatifu yanasema tuilinde imani na kulinda imani ni hii kuyachukulia hatua baadhi ya Makanisa ambayo yanafanya kazi kinyume na utaratibu" amesema Askofu Philipo Mafuja
Novemba 18, 2019 Uongozi wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza umepiga marufuku ibada zinazoendeshwa na kiongozi wa kanisa la Mfalme Zumaridi hadi hapo Serikali itakapojiridhisha kuwa ibada hazikinzani na sheria za nchi.

MAHOJIANO YA KWANZA YA JOSE MOURINHO BAADA YA KUJIUNGA TOTTENHAM


Mapema leo klabu ya Soka ya Tottenham imemtangaza Kocha raia wa Ureno, Jose Mourinho kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo baada yakumtimua aliyekuwa Kocha wake, raia wa Argentina Mauricio Pochettino.

Mara baada ya kukabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi cha  Tottenham inayoshiriki Ligi kuu ya Soka ya Uingereza (EPL), kocha Jose Mourinho amefunguka kupitia Sky Sports mtandao wa kijamii wa Twitter na kusema;

“Nina furaha ya kujiunga na club hii yenye historia nzuri na mashabiki wenye moyo na timu yao. Ubora wa kikosi na mfumo wa kukuza vipaji wa club hii unanifurahisha sana. Kwenda kufanya kazi na wachezaji ambao wananivutia inapa hamasa zaidi” amesema.


Tottenham inakuwa timu ya tatu ya Uingereza kufundishwa na Kocha Mourinho baada ya awali kuzifundisha Manchester United na Chelsea.

Mourinho ametajwa kuwa Kocha wa Tottenham akichukua mikoba iliyoachwa na Kocha Mauricio Pochettino kwa kusaini kandarasi hadi mwisho wa msimu wa 2022-23.

Mourinho akiwa Kocha nchini Uingereza alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu Soka nchini humo, Kombe la FA mara mbili akiwa na Chelsea, pia alishinda Europa League na Carabao Cup akiwa na Manchester United.RAIS MAGUFULI KUFANYA ZIARA YA KWANZA DODOMA.Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Binilith Mahenge (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais Dk. John Magufuli ambayo inataraji kuanza kesho Novemba 21 hadi 25 mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi.

Miongoni mwa shughuli atakazofanya ni kesho kuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 10 ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Ijumaa atatembelea na kuweka jiwe l msingi kwemye mradi wa Hospitali ya Uhuru Wilayani Chamwino, ujenzi wa Nyumba za Askari 118, Ujenzi wa Stendi Kuu ya mabasi na Soko Kuu la Dodoma zilizopo Nzuguni nankuzungumza na wananchi.

Jumatatu Novemba 25, Rais ataweka mawe ya msingi kwemye ujenzi wa miradi ya Makao Makuu ya JWTZ Kikombo, Ujenzinwa Ofisi za Uhamiaji na Jengo la Makandarasi.

Hii itakua ni ziara ya kwanza tangu ahamia rasmi Dodoma tangu atangaze kuhamia Oktoba 12,2019.

RAIS DKT. MAGUFULI AKIWA NJIANI KUELEKEA JIJINI DODOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wananchi mbalimbali waliomsubiri njiani akilekea Mako makuu ya Nchi Jijini Dodoma .

Meya wa Arusha Kalisti Lazaro aikimbia CHADEMA na kujiunga na CCM

Wakati kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zikiendelea nchini, aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha Kalisti Lazaro amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa na Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.

Ndugu Kalisti Lazaro aliyefika katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam ameeleza amefikia uamuzi huo baada ya kupitia wakati mgumu akiwa katika Wadhifa wake wa Meya wa Jiji la Arusha.

Ndugu Kalisti amesema amepokea barua za maonyo mara kadhaa kutoka Uongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambazo zilimtaka kutokutoa ushirikiano na Viongozi wa Serikali ambao anatakiwa kufanya nao kazi ngazi ya Mkoa na Wilaya na kutompongeza hadharani Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo ameifanya Nchini ikiwamo katika Mkoa wa Arusha.

Vitisho vya mara kwa mara ikiwamo dhidi ya uhai wake ndio vimepelekea kujivua nafasi zake zote katika Chadema na kujiunga na CCM, Chama ambacho kinashughulika na utatuzi wa kero za wananchi. Ndg. Lazaro pia amechukizwa na Chama chake kujitoa katika uchaguzi huku akiita kitendo hicho uvunjaji wa demokrasia ambacho ndani ya masaa mawili uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema iliwanyima mamilioni ya wapenda demokrasia haki ya kushiriki katika Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.

Ndg. Kalisti Lazaro amesema sasa yuko tayari kuchapa kazi ya wananchi akiwa ndani ya Chama ya Mapinduzi na kwamba yuko tayari kwa maelekezo ya kazi kutoka Uongozi wa CCM.

Ndg. Kalisti kwa kujiunga na CCM amejiuzuru nafasi ya Udiwani, Umeya wa Jiji la Arusha, Uenyekiti wa Mameya na Madiwani wote wa Chadema Nchini na Ujumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Ndugu Kalisti Lazaro atapokelewa rasmi na wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha katika tarehe itakayopangwa hivi karibuni.

Monday, November 18, 2019

BREAKING NEWS; SERIKALI YALIPIGA STOP KANISA LA 'MFALME ZUMARIDI'


Serikali kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya Nyamagana LEO Novemba 18, 2019 imesitisha shughuli za ibada nyumbani na katika Kanisa la Mfalme Zumaridi lililopo jijini Mwanza kutokana na kuendeshwa kinyume na taratibu. Uamuzi huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Dkt. Philis Nyimbi.


Aidha Dr. Nyimbi amemuomba msajili wa vyama vya kijamii wizara ya mambo ya ndani ya nchi kujiridhisha na utendaji wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (PCCT) kama unazingatia katiba yake iliyosajiliwa mwaka 1997.
MAREKANI: PELOSI AMTOLEA MWITO TRUM KWENDA KUJIELEZA BUNGENI.

Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi, amemtaka rais wa nchi hiyo Donald Trump kuenda katika baraza hilo na kueleza ukweli wake mbele ya kamati inayofanya uchunguzi dhidi ya rais huyo. 
Seneta mwingine Chuck Schumer ambaye kama Pelosi anatoka chama cha Democratic, ameunga mkono wito huo, akisema ikiwa Trump hakubaliani na yanayosemwa katika mchakato wa kumchunguza, badala ya kutuma ujumbe wa twitter anapaswa kujieleza mbele ya kamati ya uchunguzi, tena chini ya kiapo. 
Kupitia mtandao huo huo wa twitter, hivi punde Rais Trump amesema anafikiria kuitikia wito wa Pelosi na kujieleza mbele ya kamati inayomchunguza. 
Haya yanajiri wakati mchakato wa uchunguzi unaoweza kufungua njia ya kumshitaki Rais Trump ukiingia katika wiki ya pili, ukitarajiwa kumkaribisha mtu anayechukuliwa kama shahidi muhimu kuliko wote, ambaye ni balozi wa rais Trump katika Umoja wa Ulaya, Gordon Sondland.

VIONGOZI WA DINI MKOA WA DAR ES SALAAM WAAZIMIA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS MAGUFULI.

Viongozi wa Dini wakiwemo Maaskofu, Mashekhe, Wachungaji,Manabii, Maimamu na Wainjilisti Mkoa wa Dar es salaam leo November 18 wametoka na azimio la pamoja la kumuunga Mkono Rais Dkt. John Magufuli katika jitiada zake za kuleta maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kumaliza kero za Wananchi.

Hatua ya Viongozi hao wa dini imekuja baada ya Kuvutiwa na taarifa iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda dhidi ya Miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Mkoa huo chini uongozi thabiti wa Rais Dkt. John Magufuli jambo lililowakosha Viongozi wa Dini na Kuamua kuja na tamko hilo.

Katika mkutano huo RC Makonda amewasilisha kwa Uhalisia wa Video taarifa ya miradi iliyotekelezwa na serikali katika sekta zote muhimu ikiwemo Afya, Barabara, Maji, Umeme, Elimu, Viwanda, Usafirishaji na sekta anyinginezo jambo lilikowagusa viongozi wa dini.

Pamoja na hayo Viongozi hao wa Dini wamesema wataendelea kumuombea Rais Dkt. John Magufuli azidi kuwa na Nguvu na uwezo wa kuwatumikia wananchi.

WAZIRI MAJALIWA ATOA MAAGIZO KWA DC MTATIRO KUFUATILIA WALIOKULA FEDHA ZA KOROSHO.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Julius Mtatiro ahakikishe anaondoka na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho hadi Tunduru ili wakahakiki ni kwa nini wakulima hawajalipwa.

“Nimefurahi kusikia minada ya korosho inakwenda vizuri. Lakini sijafurahia habari ya Tunduru. Mheshimiwa Rais aliagiza sh. milioni 40 zipelekwe kwa wakulima. Na ninajua kwamba zimeshalipwa. Sasa ni kwa nini wakulima bado wanadai?, alihoji.

“Ukitoka hapa kwenye mkutano nenda pale jengo la Bodi ya Korosho. Ondoka na Mtendaji Mkuu wake, mwende Tunduru akafuatilie ni kwa nini malipo ya mwaka jana hayajalipwa hadi sasa.” Bw. Mtatiro ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru.

“Nataka afuatilie fedha zimekwama kwa nani. Kaimu Mkuu wa Mkoa ukigundua wanaokwamisha ni viongozi wa ushirika, shughulika nao hukohuko kama ambavyo umekuwa ukifanya,” amesisitiza.

Ametoa agizo hilo leo mchana wakati akifungua kongamano la siku moja la Wakandarasi na Wazabuni wa mikoa ya Kusini lilioandaliwa na benki ya CRBD kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mtwara.

Akizungumzia kuhusu kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni “Pamoja nawe kukuza uchumi”, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi hao baada ya kupata elimu kidogo kuhusu shughuli za benki hiyo, anataraji kuwa wataenda kwenye Halmashauri zao na kutafuta ……..

“Serikali inajenga miradi mikubwa kama vile bwawa la kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji la Mwalimu Nyerere, bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga na miradi ya maendeleo kama ile ya barabara, reli, ujenzi wa  hospitali, madarasa na nyumba za walimu. Miradi yote hii inawatarajia ninyi wakandarasi mkaijenge.”

Alisema Serikali imeendelea kuimarisha na kusogeza karibu kwa wananchi huduma za jamii ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu. “Katika kipindi cha Januari hadi Juni 2019, kwa shule za msingi, Serikali imejenga madarasa 473, matundu ya vyoo 1,405, nyumba za walimu 24 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,760. Kwa shule za sekondari, Serikali ilijenga madarasa 465, matundu ya vyoo 736, nyumba za walimu 23 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,392,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hii kutoa wito kwa viongozi na watendaji wazingatie utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutenga zabuni zenye thamani ya chini ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya wazabuni Watanzania ili kuwajengea uwezo na kushiriki katika zabuni. Alisema Serikali kwa upande wake itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa CRDB kwa kubuni programu hiyo ya tofauto ambayo imelenga kuwainua wakandarasi wadogo na wa kati.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki qa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,  Bw. Gelasius Byakanwa alisema hadi sasa jumla ya tani 67,000 za korosho zimeuzwa mkoani humo kupitia minada mitatu.

Oktoba 30, mnada wa kwanza ulipofanyika bei ilikuwa sh. 2,468/- kwa kilo na mnada wa tarehe 15 Novemba, ulishihudia bei ikipanda na kufikia sh. 2,890/- kwa kilo, alisema.

Alisema katika msimu huu, korosho zimeingiza sh. Bilioni 1.75  ambapo kati ya hizo, sh. Bilioni 1.20 zimeshaingizwa kwenye akaunti na kupelekwa kwa wakulima.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa benki ya CRDB, Bw. Abdulmajjid Nsekela alisema bei hiyo inamsaidia mteja kwa kutoa ushauri, kumwezesha na  kushirikiana naye kuijenga nchi.

“Leo tuko Mtwara,  lakini tumeshaendesha makongamano kama haya katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza. Na hapa Mtwara tumejumuisha pia mikoa ya Lindi na Ruvuma,” alisema.

Alisema benki hiyo ina hisa trilioni 6.3 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya hisa za mabenki yote na kwa upande wa amana, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema amana za benki hiyo zinafikia trilioni 4.9 ambazo ni sawa na asilimia 23 ya amana za benki zote nchini.