ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 21, 2019

KERO YA MIAKA 59 YA MAJI KITUO CHA AFYA NASSA YATATULIWA

 Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Sibtain Meghjee akitoaa taarifa ya mradi wa maji utakaohudumia Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa wilayani Busega jana.
 Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassani Kabeke akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi kisima cha maji wilayani Busega katika Kijiji cha Bukabile jana, ukiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W kwa imani ya dini ya Kiislamu.
 Diwani wa Kata ya Nyashimo (CCM), Mickness Mayela, akizungumza na wananchi wakiwemo wadau wa maendeleo kabla ya kupokea mradi wa kisima cha maji kilivhojengwa kwa gharama ya sh. milioni 20 na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation jana.
 Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwela akitoa shukurani za serikali kabla ya kupokea mradi wa kisima cha maji kilichojengwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa.
 mmoja akina mama wenye umri zaidi ya miaka 60 Ngunya Luja akipokea kitambulisho cha bima ya afya kati ya 800 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwela, vilivyotolewa an taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF).kulia anayeshuhudia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Alhaji Sibtain Meghjee.
 Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TDCF) Alhaji Sibtain Meghjee, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera (kulia) wakipeana mikono ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya kisima cha maji kitakachohudumia Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa jana.
 Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, akifungua koki ya bomba la maji lililounganishwa kutoka kwenye kisima cha maji kilichojengwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDFC) kwa ajili ya Kituo cha Afya Nassa na wananchi wa kijiji cha Bukabile.Kushoto ni mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Sibtain Meghjee na kulia ni Diwani wa Kata ya Nyashimo (CCM) Mickeness Mayela.
 Mkazi wa Kijiji  ha Bukabile, Specioza Mahondola akitwishwa ndoo ya maji na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera baada ya kupokea mradi kisima cha maji uliojengwa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF).Kushoto anayehushudima ni mwenyekiti wa taasisi hiyo Sibtain Meghjee.
 Mkuu wa Wilaya Tano Mwera (kushoto) akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake kwa jamii, Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TDCF) Sibtain Meghjee (kulia) muda mfupi kabla ya kuikabidhi serikali kisima cha maji safi na salama.
Mjane Leokadia Lyande wa kijiji cha Bukabile akipokea mtambo wa umemejua kwa ajili ya mwanga kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera (mwenye gauni la maua maua).Msaada huo wa mtambo pamoja na vyakula anuwai, mashuka na chandarua vilitolewa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF) jana.Kushoto ni mwenyekiti wa taasisi hiyo Alhaji Sibtain Meghjee.


 NA BALTAZAR MASHAKA, BUSEGA
TAASISI ya  The Desk & Chair Foundation imetumia sh.milioni 20 kutatua kero ya  maji  iliyodumu kwa miaka 59 ikiwakabili wananchi wa Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa wilayani Busega katika Mkoa wa Simiyu.

Kisima hicho kirefu cha maji  kitatumiwa na wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo wajawazito, wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa kwenye kituo hicho cha afya  huku  taasisi hiyo ikitoa sh. 800,000 kugharamia vitambulisho vya wazee 800  vitakavyowatambulisha  kupata matibabu.

Mwenyekiti wa TDFC, Sibtain Meghjee, akikabidhi mradi huo kwa serikali, alisema  kisima hicho kirefu cha maji kimegharimu sh. milioni 20 na kimefungiwa pampu ya kusukuma maji  inayotumia nguvu ya umeme jua na hivyo kukiwezesha kituo cha Afya Nassa na wananchi kupata maji ya uhakika muda wote.

“Tumeridhishwa na mfumo wa mitambo iliyofungwa kisimani hapo kuwa inasukuma maji vizuri hadi kituoni baada ya majribio kufanyika.Kwa niaba ya wafadhili na uongozi wa The Desk & Cair Foundation, tunaikabidhi serikali mradi  huu, hatutakuwa na mamlaka nao isipokuwa kwa matengenezo ya mitambo itakapoharibika,”alisema.

Meghjee alisema taasisi hiyo imetekeleza miradi mbalimbali ya kijamii mkoani Simiyu ikiwa ni pamoja na kuboresha visima vifupi 11 vya maji na kuchimba vipya 12, kufunga mitambo ya umeme jua kwenye Kituo cha Afya Nassa, mradi wa maji safi na salama Lamadi, baiskeli 5 kwa walemavu wa viungo na moja ya kawaida.

Mingine ni mradi wa nyumba 10 za nyasi vijijini kufungiwa mfumo wa umeme jua,vyoo kwenye shule ya Malayele,vibebeo 300 kwa wajasiriamali na vitambulisho vya afya kwa wazee 800 huku miradi kama hiyo ikifanyika pia kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati.

“Naishukuru serikali kwa kutoa vibali na ushirikiano wa dhatiwakati tunapotekeleza shughuli zetu kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi,kama ilivyo kauli mbiu yetu ya Tupo pamoja Iwe Dhiki Iwe Faraja:Huduma kwa Jamii Bila Kuchagua Bila Kubagua,”alisema Meghjee.

Aidha, baadhi ya akinamama wa Kijiji cha Bukabile ambao ni wanufaika wa mradi huo, Nadhifa Yusuf, Specioza Mahondola naWinfrida Masalu,walisema utainufaisha jamii na umewakomboa na adha ya kufuata maji  umbali mrefu,ambapo wakati wa kujifungua walipata shida ya kwenda na maji .

Walieleza kuwa wameteseka miaka mingi kufuata maji umbali wa km 4 kutokana na kijiji hicho kuwa mbali na Ziwa Victoria, walikuwa wakinunua maji sh.1000 kwa ndoo tano ama kuyateka kwenye madimbwi hivyo kwa sasa wataweza kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Kwa upande wa vitambulisho vya bima kwa wazee, mmoja wa wanufaika hao Kitula Kubangwa (71) aliishukuru The Desk & Chair Foundation kuwaondolea changamoto ya vitambulisho vya matibabu na kuishauri serikali iendelee kuwatizama kwa jicho la huruma.

Akipokea mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Busega,Tano Mwera, alisema The Desk & Chair Foundation ni wadau wakubwa wa maendeleo kutokana na misaada yao kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma mbalimbali kwa jamii.
Alisema mradi huo wa maji utabadilisha maisha ya wananchi na wagonjwa wanaotibiwa kwenye kituo cha afya Nassa kwani lengo la serikali ni kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani.

“Maji ni muhimu, mradi huu unaunga mkono juhudi za serikali za kuhudumia wananchi na kuwaletea maendeleo lakini pia sasa watayapata maji karibu na akinamama watatumia muda wao mwingi kufanya shughuli za maendeleo,”alisema Mwera.  

Awali Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nassa, Fred Mruma, alisema changamoto ya maji tangu kujengwa kwa kituo hicho mwaka 1960 imekwisha ingawa bado wana tatizo la nishati ya umeme kwenye chumba cha upasuaji, mashine ya kufua nguo za wagonjwa na mashine ya kupima damu (Full Blood picture machine).

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.