ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 24, 2026

SIMBA WALEEEE NUSU FAINALI KOMBE LA MUUNGANO 2026

 


TIMU ya Simba SC imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Muungano baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mafunzo usiku wa tarehe 23 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Bao pekee la Simba SC katika mchezo huo limefungwa na mshambuliaji wake tegemeo kwa sasa, Suleiman Abdallah Mwalimu ‘Gomez’ dakika ya 54.

Simba SC sasa itakutana na Mlandege FC katika Nusu Fainali Jumapili, baada ya mabingwa watetezi, Yanga kucheza na Azam FC katika Nusu Fainali ya kwanza Jumamosi, mechi zote zikianza kuanzia Saa 2:15 usiku hapo hapo Uwanja wa New Amaan Complex 

Mlandege FC imetinga Nusu Fainali baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars mchezo uliocheza jioni ya tarehe 23 April 2026 hapo hapo Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mabao ya Mlandege yamefungwa na Omar Juma’Samatta’ dakika ya 28 na Mussan Hassan ‘Mbappe’ dakika ya 45’+1, baada ya Mishamo Daudi kuanza kuifungia Singida Black Stars dakika ya tisa.

Wakati Yanga iliitoa Muembe Makumbi City FC kwa kuichapa mabao 4-0 juzi, Azam FC iliitupa nje KVZ FC KWA kuichapa mabao 2-0 hapo hapo Amaan Complex.

BETIKA WAZINDUA JEZI YA MSIMU WA 10 WA TULIA MARATHON MBEYA

 


KAMPUNI ya ubashiri, Betika Tanzania ikishirikiana na Taasisi ya Tulia trust kupitia Betika Mbeya Tulia Marathon imezindua rasmi jezi ambayo itatumika Msimu wa 10 wa Mashindano Jijini Mbeya mwaka huu.

Akizungumza na Wanahabari  Jijini Dar es Salaam Meneja Mkuu wa Betika Tanzania Samuel Mcheru amesema Betika inathamini sana michezo na itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kupitia Taasisi ya Tulia trust Kuhakikisha mbio hizo za Betika Mbeya Tulia Marathon zinafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa mashirikiano hayo yanalenga kuwaweka wananchi karibu na kushiriki michezo ili kuweka miili yao imara zaidi,kurudisha tabasamu kwa jamii na kutoa fursa za kibiashara kwa Wananchi wa Jiji hilo.

Mcheru ametoa wito kwa Makampuni mengine yawe yenye tija katika jamii kwani uwepo wa Betika Tulia Marathon ni kiashiria tosha kuwepo kwa ongezeko la kipato kila inapofanyika kutokana na jamii kukusanyika eneo moja hivyo inawapa fursa betika pia kujitangaza zaidi na Wafanyabiashara kuendesha shughuli zao.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya na Spika wa Bunge Mstaafu Dkt.Tulia Ackson amesema Kampuni ya Betika imekuwa na mchango mkubwa wa kuhakikisha mbio hizo zinafanyika kwa ufanisi mkubwa hasa kwa mchango wao wa vifaa vya kushiriki mbio hizo pamoja na miundombinu mbalimbali pindi linapokuja shindano hilo kutokana na kuweka udhamini wao kwa zaidi ya Miaka mitatu.

Ackson amesema kwa mwaka huu shindano hilo linatimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kwa mwaka huu wanategemea kukusanya kiasi cha fedha shilingi milioni 300 ili kugusa Maeneo ya Kijamii mbalimbali ikiwemo Kuboresha makazi ya Wahitaji, eneo la Afya hususani kujenga baadhi ya wodi hitajika, vifaa pamoja na eneo la Elimu Mashuleni.

Hata hivyo amesema Mbio hizo za kipekee zilizopewa chachu na hali ya hewa ya jiji hilo itatimua vumbi Mei 15 na 16 zikiambatana na burudani mbalimbali.

Aidha amevipongeza vyombo vya habari kwa kuendelea kutoa habari juu ya Taasisi ya hiyo ambayo kutokana na michango ya wadau mbalimbali katika kujikita kusaidia jamii.

Pia ametoa wito kwa Watanzania kujiandikisha kushiriki katika mbio hizo kupitia Ofisi zilizopo Jijini Mbeya pamoja na kujisajili mtandao kwenye kurasa za Taasisi hiyo.

Nae Afisa Habari wa Kampuni ya Betika Juvenalius Rugambwa aliongeza kuwa Jezi hiyo iliozinduliwa itatumika rasmi kwenye mbio hizo huku akisherehesha kuwa jezi hizo zimepambwa na rangi zenye mvuto zaidi zenye michoro ya vivutio vilivyopo Tanzania ikiwemo bendera ya Taifa.

Thursday, April 23, 2026

SAKATA LA MAHANDAKI MWANZA: MFANYABIASHARA AKAMATWA KWA UJENZI USIOFUATA SHERIA.

 news

Katika tukio linalozua maswali ya kiusalama na ufuatiliaji wa shughuli za ujenzi, mfanyabiashara Evance Bisesagu (47), mkazi wa Bupumula, Kata ya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuchimba mahandaki sita kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, mtuhumiwa huyo alikamatwa jioni ya Aprili 22, 2026, kufuatia taarifa za wananchi waliokuwa na hofu juu ya uwepo wa mahandaki hayo karibu na makazi yao. Wananchi hao walieleza kuwa shughuli hizo zilikuwa zikifanyika kwa siri na bila maelezo ya wazi, jambo lililozua wasiwasi mkubwa wa usalama.

Uchunguzi wa Polisi Wabaini Ukiukwaji wa Sheria

Akizungumza Aprili 23, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa ujenzi huo ulikuwa unafanyika bila vibali halali kutoka mamlaka husika.

Mbali na mmiliki wa eneo hilo, watu wengine wawili Ngasa Kasuka na Hamad Kashinje pia wanashikiliwa wakidaiwa kuwa walikuwa wakifanya kazi kama vibarua katika mradi huo.

 “Msako unaendelea kuwatafuta mafundi na watu wengine wote waliohusika katika shughuli hizi,” alieleza Kamanda Mutafungwa.


Hofu ya Usalama kwa Wananchi

Tukio hili limeibua mjadala mpana kuhusu usalama wa makazi ya wananchi, hasa pale shughuli za ujenzi zinapofanyika bila uwazi na ufuatiliaji wa karibu. Mahandaki kama hayo yanaweza kusababisha hatari kubwa, ikiwemo kuporomoka kwa ardhi au majengo, pamoja na uwezekano wa kutumika kwa shughuli zisizo halali.

Wito kwa Viongozi na Mamlaka

Jeshi la Polisi limetoa rai kwa viongozi wa serikali za mitaa na mamlaka za ujenzi kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu shughuli zote za maendeleo katika maeneo yao.

Kamanda Mutafungwa alisisitiza kuwa ni lazima kila ujenzi ufuate taratibu zote za kisheria, ikiwa ni pamoja na kupata vibali vinavyohitajika kabla ya kuanza kazi yoyote.

 “Hatutavumilia ujenzi holela. Kila anayekiuka sheria atachukuliwa hatua kali,” alionya.


Wednesday, April 22, 2026

ALIYEMUUA MUMEWE BAADA YA FUMANIZI AHUKUMIWA KIFUNGO CHA NJE.

 Mahakama

ELIZABETH Sylvester maarufu kama Sosomo, mkazi wa Kijiji cha Chudeko, Wilaya ya Songwe, amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi 18, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mumewe, Ally Masanja, bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songwe, imemhukumu Katika kesi hiyo namba 7304/2026, mshitakiwa alikiri kosa la kuua bila kukusudia kinyume na vifungu vya  195 na 198 vya kanuni ya adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Elbariki Mpinga, tukio hilo lilitokea Januari 3, 2026 katika Kijiji cha Chudeko, wilayani Songwe, ambapo mshitakiwa alimchoma mumewe kisu ubavuni wakati wa ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi.

Ilielezwa kuwa ugomvi huo ulizuka baada ya mshitakiwa kumkuta mumewe akiwa  nyumbani kwa mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi. 

Hali  hiyo  iliyoibua ugomvi kati yao watatu hao, hadi kufikia  kwenye shambulio hilo lililosababbisha mauti ya mwanaume huyo. 

Akisoma hukumu Aprili 21, 2026, Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Jaji Gabriel Malata, amesema mahakama imezingatia mazingira ya tukio, ikiwemo hali ya mshtakiwa kabla, wakati na baada ya tukio pamoja na ungamo lake.

Alisema mahakama ilimtia hatiani kwa kosa hilo na kuamua kumpa adhabu hiyo ya kifungo cha nje cha miezi 18 kwa kuzingatia masharti ya kisheria.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mshitakiwa hataruhusiwa kutenda kosa lolote la jinai katika kipindi hicho, na endapo atakiuka masharti hayo atalazimika kutumikia kifungo hicho gerezani.

Kesi hiyo ni miongoni mwa kesi tatu za mwanzo kutolewa hukumu na Mahakama Kuu Kanda ya Songwe tangu kuanza rasmi kwa shughuli zake za kimahakama Machi 30, 2026.

Awali, Wakili wa utetezi, Moses Mwampashi, aliomba mahakama imuonee huruma mshitakiwa, akieleza kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na halikupangwa bali lilitokana na mazingira ya tukio.

Aliongeza kuwa mshitakiwa ana watoto wanne aliowazaa na mumewe,ambao kwa sasa  ndiye mtu wa kuwalea na wanamtegemea, hivyo kuiomba mahakama izingatie maslahi yao katika utoaji wa hukumu.

KONGAMANO LA WANAUME (MEN AT WORK) KUFANYIKA MWANZA

 

Men at Work ni jukwaa maalum linalowakutanisha wanaume kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kujifunza, kujadili na kujengeana uwezo katika safari ya maisha. 

Kupitia kongamano hili, washiriki hupata fursa ya kuimarika katika nyanja muhimu kama uchumi, ndoa na mahusiano pamoja na kukuza nidhamu binafsi na uwajibikaji katika nafasi zao kama wanaume ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, Men at Work imeendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa wanaume wengi, ikiwa imefanikiwa kuandaa makongamano yenye tija ndani na nje ya Mwanza. 

Athari yake imekuwa kubwa kiasi cha kuibua majukwaa mengine yenye mwelekeo sawa, ikiwemo "Kikao cha Wanaume", lakini chimbuko lake ni Men at Work. 

Ushuhuda wa mafanikio na mabadiliko ya maisha ya washiriki ni mwingi na unaendelea kuongezeka kila mwaka na unatarajiwa kutolewa katika kongamano la wanaume jijini Mwanza.

Kongamano hilo la wanaume (Men at Work) linatarakiwa kufanyika jumamosi tarehe 26 Aprili 2026 katika ukumbi wa Chuo cha BOT, Capripoint jijini Mwanza kuanzia saa mbili asubuhi.

Mwandaaji wa kongamano hilo, Maxwell Chaila amesema jukwaa hilo ni linatoa fursa kwa wanaume kufahamiana na kujifunza safari ya mabadiliko chanya katika maisha yao.

Men at Work- Mwanaume Bora, Jamii Imara.