Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.Nikson Saimon akizungumza na madiwani wa halmashauri ya Kibaha mji katika kikao hicho.Na Victor Masangu,Kibaha
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson Saimon katika kuhakikisha anachochea zaidi chachu ya kufanya kazi kwa bidii na kuwaletea matokeo chanya ya kimaendeleo wananchi ameamua kuanzisha mpango wa kuwapa motisha watumishi na madiwani ambao wanatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa maslahi ya jamii.
Kwa kulitambua hilo Mkuu wa Wilaya hiyo ameamua kutumia kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya Kibaha mji kuwaeleza kwamba atakuwa anatoa zawadi na motisha mbali mbali kwa wafanyakazi ambao watakuwa mstari wa mbele katika kuwatumikia wananchi na kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo.
Katika kikao hicho cha Baraza la madiwani cha robo ya nne aliweza kutumia fursa ya kumtangaza Diwani wa kata ya mail moja Ramadhani Lutambi kuchaguliwa kuwa mshindi kutokana na kuonyesha juhudi zake katika Mambo mbali mbali ambapo amemzawadia kiasi cha shilingi laki tano kama zawadi kwake.
"Kwa sasa nimeweka utaratibu wangu wa kuwa natoa motisha na zawadi mbali mbali na leo hii nimeanza na madiwani na nitafanya hata kwa watumishi na watendaji wengine kwa hiyo diwani Lutambi nampatia zawadi hii ya shilingi laki tano kwa kuwa ndio amechagulia na jopo la watu mbali mbali,"alisema Mkuu huyo.
Aidha alifafanua kwamba kuchaguliwa kwa diwani huyo ni mwanzo tu na kwamba utaratibu huo utaendelea kufanyika na kwamba mpaka jina lake limeweza kupatikana sio Mimi pekee bali kuna jopo la watu wengi ambao wameweza kushiriki katika mchakato mzima wa ziezi hili la kumpata diwani Bora.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliwahimiza madiwani wote kuiga mfano wa diwani aliyeshinda na kuwataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ikiwa sambamba na kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo ili iwe endelevu zaidi kwa maslahi ya wananchi wote.
Pia hakusita kuwakumbusha madiwani kuhakikisha wanakuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato ikiwa sambamba na kuweka na kutunga sheria ndogo ndogo ambazo zitakuwa ni rafiki na sio kandamizi kwa wafanyabiashara.
Kwa Upande wake diwani huyo wa kata ya maili moja Ramadhani Lutambi alimshukuru kwa dhati mkuu huyo wa Wilaya kwa kutambua mchango wake katika kutimiza wajibu wa kuwatumikia wananchi na mpaka kumpatia motisha ya laki tano.
Lutambi pia aliahidi kuendelea kushirikiana na madiwani wenzake na kwamba hata zawadi ambayo amepatiwa ni kwa ajili ya heshima kubwa ya madiwani wenzake ambao wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo.
Nao baadhi ya wananchi ambao walihudhulia katika kikao hicho walimpomgeza diwani huyo kwa kuibuka na ushindi pamoja na kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa kuanzisha utaratibu huo ambao utasaidia zaidi watumishi na madiwani kutimiza majukumu yao kwa bidii.
MWISHO