ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, November 8, 2013

RAIS JK AELEZEA MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Tanzania haina mpango wa kujitoa ndani ya jumuiya ya Afrika mashariki kwa kuwa haijafanya lolote baya ndani ya nchi wanachama hivyo inasikitishwa na vitendo vya ubaguzi vinavyofanywa na baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo. CHANZO: ITV

ULIVYOKUWA USIKU WA USHINDI KWA WANAHABARI WA TZ

Mkurugenzi wa MOIL Aritaf Mansoor aka Dogo, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Usiku wa ushindi wa wanahabari wa Tanzania uliofanyika JB Belmonte jijini Mwanza akihutubia hadhara iliyohudhuria hafla hiyo ambayo ilifuata mara baada ya kufanyika kwa Tuzo ya Daudi Mwangosi siku ya jana.
Wadau wa habari kwa umakini wakifuatilia kwaumakini kilichokuwa kikijiri haflani.
Ni taswira za wadau shughulini hapa.
Kutoka kushoto ni Adam Lyoba, Meneja mdhibiti viwango MCT Pili Mtambalike na Mwenyeji wao Mwenyekiti wa Mwanza Press Club Mr. Deus.
"Wacha na burudani zitawale....." Hapa ni Mc Erica toka Radio Free Africa na Mc G. Sengo wa Clouds Fm wakitambulisha jambo ambapo yeyote aliyekuwa na kipaji cha burudani alikaribishwa kukionesha...mmmmh waandishi  ni balaaa!!!
Rais wa UTPC (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa MOIL (kulia).
Hapa kulikuwa na bo-bo-bonge la burudani sehemu ambapo tuligundua kipaji kingine kilichofichika cha Mtunukiwa wa Tuzo ya Daudi Mwangosi 2013-2014 Absolum Kibanda (wa kwanza kulia) wengine katika picha ni Fredrick Katulanda wa Mwananchi Communication na Erica Elias wa radio Free Africa.
Jaji alikuwa Fredrick Katulanda (mwenye kipaza sauti) ambapo kilichofuata mara baada ya hapo ebana--eeeeeeh...Duh Uspime...!! Video yake itauzwa ghali sana.
Kisha chakula....
Na mazungumzo ya hapa na pale.
Wakiwa deep sana kushoto ni Hamza Kasongo na kulia ni Mansoor Dogo.
Akipewa tafu na Jambo Stars Band, Aisha Hamadi aliutendea haki wimbo wa Mbilia Bell.
Muziki uliwakolea...
Watu walivunja makabati ...
Bass guitalist.
Mduala toka Tabora.
Vijana wa kazi wakiwa na Mkurugenzi wa MOIL Mr. Mansoor Dogo.
G. Sengo (L) akiwa na Mzee Hamza Kasongo(C) na Makamu wa rais wa UTPC (R).
Safi.

MGAMBO ISAIDIE OPARESHENI KIMBUNGA-DC

Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Erasto Sima, akikagua kikosi cha mgambo wakati akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya Mgambo katika Kijiji cha Ikungulyambeshi ‘A’ Kata ya Kilalo wilayani humo.
Kikosi kikipita kutoa heshima. 
"Heshimaaaa....Toaaa....!!"
kwa-kwa-kwa-kwaaa..!
Ukakamavu.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Erasto Sima, akihutubia wakati wa shughuli ya kuhitimisha awamu ya kwanza ya mafunzo ya Mgambo katika Kijiji cha Ikungulyambeshi ‘A’ Kata ya Kilalo wilayani humo.
Mshauri wa Mgambo wa wilaya hiyo Sajenti Ndasan Josephat akitoa nasaha zake.
"Ili muwe wakakamavu mwahitaji kuwa na afya na afya hujengwa kwa mazoezi" 
Picha ya pamoja.
Habari na Peter Fabian.
SERIKALI wilayani hapa, imewaagiza vijana waliohitimu mafunzo ya Mgambo wasaidie kukamata wahalifu mbalimbali, wakiwemo wahamiaji haramu waliokimbia opalesheni Kimbunga na kujificha wilayani humo.

Imewaonya baadhi ya wanasiasa wanaopinga mafunzo hayo na kuwaasa vijana hao wasitumie vibaya mafunzo waliyopata, yakiwemo ya siraha, kwa kujihusisha na vitendo vya ujambazi, ujangiri, uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya, vinginevyo watakiona cha mtema kuni.

Wito huo ulitolena na Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Erasto Sima, juzi katika Kijiji cha Ikungulyambeshi ‘A’ Kata ya Kilalo wilayani humo, wakati akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya Mgambo Katani humo.

Sima alisema kwamba, baadhi ya watu wakiwemo wana siasa walijaribu kukwamisha mafunzo hayo kwa kuwashawishi vijana wasishiriki lakini wananchi na viongozi wanaojali maslahi ya umma, walisimama kidete na kushirikiana na wakufunzi wa JWTZ, hatimaye mafunzo hayo yakafanyika kwa ufanisi.

“Baadhi waliona mafunzo haya ni jambo la kisiasa wakati sivyo, maafunzo haya ni kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi yetu hivyo mliopata mafunzo, msaidie opaleshen Kimbunga kwa kufichua wahamiaji haramu waliokimbilia kujificha huku.” Alisema Mkuu huyo.

Alieleza kuwa ni wajibu wao kulisaidia taifa kupambana na uhalifu mbalimbali ukiwemo dawa za kulevya, rushwa, majambazi, majangiri ambayo yanaisumbua nchi yetu na kujitolea katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa.

“Jeshi la Mgambo limeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 147, kifungu (1) na (2) kwa kuwa vijana ndiyo tegemeo la taifa, msikub ali kushawishiwa kukataa mafunzo ya mgambo, wanaowakataza ni maadui wa ndani wasioitakia mema Tanzania, ole wao watakao bainika.” Alionya Sima.

Mshauri wa Mgambo wa wilaya hiyo Sajenti Ndasan Josephat akiwapongeza vijana hao na wakufunzi wa JWTZ, alieleza kwamba, anayo furaha kubwa kupata walinzi 138 waliohitimu mafunzo ya ukakamavu, ujanja wa porini, mbinu za kivita na siraha ndogondogo kwa manufaa ya umaa.

Awali katika risara yao iliyosomwa na Hosea Peter, Mgambo hao walisema kwamba walioandikishwa katika mafunzo hayo walikuwa vijana 540 lakini waliohitimu ni 138 ( wanawake wakiwa sita) kutokana na wengine kukimbia mafunzo hayo kwa kushawishiwa na baadhi ya watu.

Vijana hao waliiomba serikali iwape kipaumbele katika nafasi mbalimbali za ulinzi zinazopatikana na kuahidi kufanya kazi za kujitolea kulinda usalama wa wananchi na mali zao pia kupambana na kila aina ya uhaifu katika maeneo yao.

HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA WATOTO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI 1 OCTOBA 2013

Ummy Jamaly Mwenyekiti wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA WATOTO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
1OCTOBA 2013

Ndugu watoto wenzangu,                                                                                                                
Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujaalia siku hii ya leo kuwa na afya njema kabisa. Kwa wale watoto wenzangu ambao hali zenu kiafya si njema nakuombeni sana kwa Mwenyezi aweze kuwajaalia afya njema “Amina.”

Ndugu watoto wenzangu,    
Kuanzia leo Alhamis ya tarehe 31/10/2013 nitakuwa nawahutubia ikiwa ni sehemu ya utaratibu wangu mpya wa kuzungumza nanyi watoto wenzangu. Nitajitahidi kila mwisho wa mwezi kutoa hotuba yangu katika sehemu tofauti tofauti kama vile shuleni, kwenye vituo vya watoto, mabaraza ya watoto na hata kwenye ofisi za mashirika ya watoto kama hii leo ambapo natoa hotuba yangu tokea ndani ya ofisi za shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza zilizoko Ghana hapa Jijini Mwanza nchini Tanzania. Shirika hili ndilo ambalo linatuwezesha sisi watoto kuweza kutoa hotuba kupitia program ya “Hotuba ya watoto” Tunashukuru sana shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza kwa kutujali watoto na kutuwezesha sauti zetu kusikika. Pia tunaomba waandishi wa habari muweze kuirusha hewani hotuba yangu ili kuwawezesha watoto wengi waweze kujua kile ambacho ninakihutubia siku hii ya leo. Sina shaka mtatuunga mkono kwa aslimia mia moja.  Nashukuru pia watoto wenzangu kwa kushirikiana nami katika uandaaji wa hotuba hii.

Ndugu watoto wenzangu,                                                    
Kutokana na Takwimu za tafiti mbalimbali zinaonesha ya kuwa asilimia hamsini (50) ya watanzania wote ni watoto na wengi wetu tunafahamu ya kuwa kesho ni leo,je tumejiandaaje na tumeandaliwaje kupokea rasilimali nzuri za nchi yetu? Hakika kila mtu afikirie kwa umakini, apambanue, achambue na afanye maamuzi sahihi, stahiki na magumu kwa ustawi wa nchi yetu hasa katika kutujenga, kutushirikisha na kutuendeleza vyema sisi watoto.

Ndugu watoto wenzangu,
Napenda kuchukua fursa hii kuwaelezea baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakuta watoto wenzetu ambazo zimekuwa ni ukiukwaji wa haki za mtoto. Watoto wenzetu wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kimwili kama vile kupigwa ngumi, mateke na viboko; Ukatili wa kisaikolojia kama vile kutukanwa, kuitwa majina kama vile mbwa, kuku na nguchiro; Ukatili wa kijinsia kama vile kubaguliwa katika kupata elimu na na kazi za nyumbani mfano mtoto wa kiume ndiye anayepewa nafasi ya kusoma, kupumzika na kucheza pia wakati mtoto wa kike akiaachwa nyumbani na kufanyishwa kazi bila ya kupewa muda stahiki wa kupumzika;  na aina nyingine ya ukatili ni ukatili wa  kingono ambapo watoto wenzetu wamekuwa wakibakwa na kulawitiwa na watu wazima na wenye akili timamu.

Ndugu watoto wenzangu,
Matukio mbali mbali ya ukatili kwa watoto tumekuwa tukiyaskia ama kuyaona yakitokea katika jamii zetu. Mkoani Mtwara mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Newala amepata ulemavu wa akili kwa kupigwa na mwalimu wake kwa madai ya kushindwa kulipia kiasi cha pesa cha shilingi 300 iliyokuwa inachangishwa baada ya kitabu cha shule kupotea. Wakati hayo yakitokea mkoani Mtwara huko Mkoani Dododma mama mmoja mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mchanga. Na hapa Jijini Mwanza, mama mmoja alimmwagia mtoto wake maji ya moto na kumsababishia majeraha na maumivu makali sehemu mbali mbali za mwili wake. Kuna matukio mengi ya ukatili kwa watoto zaidi ya hayo ambayo nimeweza kuyataja yakitokea kila siku katika jamii zetu.

Ndugu watoto wenzangu,
Matukio ya ukatili kwa watoto hayafanywi na miti, wanyama wala wadudu bali yanafanywa na watu wenye akili timamu mbaya zaidi wengi wao ni watu wazima na wenye heshima zao katika jamii. Pia matukio hayo hayafanyiki sehemu ambazo wanaishi mbwa, kuku au paka bali hufanyika sehemu ambazo kuna viongozi wanaotawala, kuna wananchi wanaishi na kuna taasisi zinazoweza kutetea na kumlinda mtoto dhidi ya ukatili.  Ni aibu sana kwa matukio ya ukatili kwa watoto kutokea katika jamii zetu ambazo wanaishi binadaamu na wala si wanyama.
  
Ndugu watoto wenzangu,
Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wazazi, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kuwa tayari kuripoti na kupinga matukio ya ukatili kwa watoto. Na serikali iweze kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaofanya ukatili wa aina yoyote ile ili watoto wote waweze kupata haki zao kwa maslahi ya kujenga Tanzania imfaayo kila mtoto. Kuanzia leo, naomba lugha za matusi kwa watoto zikome, vipigo kwa watoto viishe na matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto tuyazike. Kila kiongozi katika eneo lake, tunamwomba ahakikishe kuwa hakuna mtoto hata mmoja anayefanyiwa ukatili. Na kila mzazi katika familia yake, tunamwomba ahakikishe hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili, na kila taasisi katika eneo lake kikazi ihakikishe hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili. Tanzania bila ukatili kwa watoto inawezekana, Pamoja tunaweza!
Mungu ibariki Afrika!
Mungu ibariki Tanzania!
Na Mungu wabariki watanzania wote waweze kutulinda sisi watoto dhidi ya ukatili wa aina yeyote ile.

Ahsanteni sana kwa kunsikiliza!

Ummy Jamaly

Mwenyekiti wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MPANGO WA TAIFA WA DAMU SALAMA TANZANIA WAVUKA MALENGO WA UKUSANYAJI DAMU

Ofisa uhusino na masoko wa Mpango wa Taifa wa damu salama Bw. Rajab Mwenda (kulia) akielezea kuhusu rpoti ya makusanyo ya damu ya robo mwaka na mikakati ya kukusanya damu kipindi cha Novemba- Januari 2013 wakati wanafunzi wakiwa likizo

Na Mwandishi Wetu         

MPANGO wa Taifa wa Damu S
alama Tanzania (NBTS) umevuka malengo ya ukusanyaji  damu   kwa asilimia 110  katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba 2013 ambapo jumla ya chupa 38,552 zilikusanywa na kuvuka malengo ya chupa 35,000 zilizokuwa zikusanywe.
Ofisa Uhusiano na Masoko wa Mpango wa Damu Salama Tanzania Bw. Rajab Mwenda alisema Kanda iliyongoza kwa makusanyo ya damu ni  Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam,Morogoro,Dodoma na Pwani  ambako jumla ya chupa 13,669 zilikusanywa, Kanda inayofuatia kwa ukusanyaji damu ni Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro,Arusha, Manyara, Tanga)  iliyokusanya chupa 6,159.
Alisema katika kipindi cha mwezi oktoba 2012 hadi Septemba 2013 takwimu zinaonyesha chupa za damu 139,676 ambayo ni sawa na asilimia 99.8 ya lengo la kukusanya chupa 140,000 ilifikiwa hata hivyo Mpango wa Taifa wa damu salama unakusanya asilimia 26 ya mahitaji ya damu kwa mwaka.  Mahitaji ya damu kwa mwaka ni wastani wa chupa 400,000- 450,000.
Alisema tofauti iliyoko ya upatikanaji wa damu kwenye hospitali  nchini imekuwa inafidiwa na ndugu wa wagonjwa  katika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mgonjwa.
Bw. Mwenda alisema mbalimbali ambazo zinasababisha mpango kushindwa kukusanya damu kwa 100% toka kwa wachangiaji damu wa hiari kunatoakana na uelewa mdogo katika jamii kuhusu uchangiaji damu kwa hiari kwani mfumo uliozoeleka ni ndugu wa mgonjwa ndiyo wanatoa.
Alisema nyingine  ni uhamasishaji usiotosheleza toka kwa viongozi mbalimbali wa jamii, wanasiasa, viongozi wa dini, uuzwaji wa damu usio halali hospitalini jambo ambalo linawakatisha tamaa wachangia damu wa hiari, matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali  na miundombinu hafifu hususan barabara duni wakati wa kukusanya na kusambaza damu.
Bw. Mwenda alisema Mpango wa Taifa wa Damu salama una wadau mbalimbali ambao hujitokeza kuchangia damu kwa hiari kama taasisi za kidini, majeshi, sehemu za kazi, mikusanyiko ya watu na wanafunzi ambao huchangia asilimia 80 ya damu hapa nchini
Alisema katika kipindi cha Novemba hadi  Januari kila mwaka  ni kigumu katika ukusanyaji damu kwani  wadau wakuu ambao ni wanafunzi wanakuwa likizo ya mwaka hivyo Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeweka  mikakati mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Alisema katika mikakati hiyo ni kufanya  kampeni ya kuhamasisha uchangiaji damu kwa hiari katika jamii na sehemu za makanisani, minadani, stendi za mabasi, misikitini, kwenye masoko na sehemu za kazi.
Alisema wameanza kuhamasisha kambi za jeshi, makundi ya dini na ma wasiliano yamefanyika kwa jumuiya mbalimbali hapa nchini zichangie damu mfano jumuiya ya Khoja shia, Sabato na Jaula.
Pia alisema watatumia vyombo vya habari ili kuikumbusha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchangia damu  na visaidie kutoa elimu na kutangaza ratiba  ya ukusanyaji damu katika vituo vidogo na vikuu.
Alitoa rai kwa Watanzania kujitokeza kuchangia damu kwa hiari katika vituo vya damu salama kwa mtu yoyote mwenye afya mwanamke au mwanaume na mwenye umri kuanzia miaka 18 ajitokeze kuchangie damu.
Alisema uchangiaji wa damu kwa hiari una faida kwa mtoaji kwa vile napunguza hatari ya magonjwa ya moyo, kuwepo kwa madini chuma mengi kupita kiasi katika damu kunakodhoofisha utendaji kazi na kuchangia damu mara kwa mara hurekebisha madini  chuma ya ziada  katika mfumo wa damu.
Alisema faida nyingine ni upimaji wa afya pasipo gharama kwa sababu  wakati unapochangia damu mtaalamu wa tiba daktari au muuguzi atapima shinikizo la damu yako, mapigo ya moyo na kukufanyia vipimo vya afya bure.
 
Alisema kutoa damu kunaongeza utambuzi wa kiwango cha chembe hai nyekundu na chembe na huchochea uzalishaji wa seli damu mpya na kuwaomba wanahabari kuendelea kuhamasisha na kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara kwani ni damu ya mwanadamu pekee inayotumika kumuongezea mgonjwa anayehitaji damu.

Thursday, November 7, 2013

MWANZA YASIMAMA KWA DAKIKA KADHAA.

Wakazi wa jiji la Mwanza leo majira ya saa 4 asubuhi waliwekwa njia panda na kujawa hofu kubwa kufuatia vikosi vya askari kanzu, FFU, askari polisi na zimamoto wakiwa na vifaa sambamba na magari yao walipolivamia jengo la Hotel Gold Crest na kuanza saka saka za kujiweka sawa huku wakiendeleza mapambano na jamaa ambao walijipanga mithili ya wahalifu.
Hali hiyo ilisababisha magari pikipiki kusimama kwa muda huku wananchi wakiingiwa hofu na woga, wengine wakikimbia na baadhi ya wafanyabiashara wakifunga maduka yao wakifananisha na lile la Westgate la jijini Nairobi nchini Kenya
Wateja wa kituo cha mafuta kilichopo karibu na hotel Gold Crest jengo ambalo ndiko zoezi lilikuwa likifanyika pamoja na wateja wa ofisi za PPF, duka la Vodacom Mwanza na Benki ya NMB zilizopo katika jengo hilo walikosa huduma kwa muda huku wengine wakitimka maeneo hayo kwa tahadhari wakidhani ni live.
Watu wakihaha nao polisi wakiweka ulinzi mkali eneo la tukio. 
Harakati zikiendelea eneo la tukio.
Polisi wakiwaweka chini ya ulinzi 'wahalifu bandia' katika zoezi lililozua taharuki kwa kwakazi wa jiji laMwanza.
Hata hivyo mpaka zoezi hilo linamalizika hakuna mwananchi aliyeweza kubaini kuwa tukio hilo lilikuwa ni la uigizaji, kila mmoja alikuwa akisimulia kivyake sekeseke zima, lakini mapango mzima ulikuwa ni kuvinoa vikosi vya polisi na Zimamoto juu ya kukabiliana na uhalifu kwenye majengo makubwa ya huduma mbalimbali. Ama hakika zoezi lilifanikiwa.

Pig up Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza.