Ummy Jamaly Mwenyekiti wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
|
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BARAZA LA
WATOTO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
1OCTOBA 2013
Ndugu
watoto wenzangu,
Awali ya yote napenda
kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujaalia
siku hii ya leo kuwa na afya njema kabisa. Kwa wale watoto wenzangu ambao hali
zenu kiafya si njema nakuombeni sana kwa Mwenyezi aweze kuwajaalia afya njema
“Amina.”
Ndugu
watoto wenzangu,
Kuanzia leo Alhamis
ya tarehe 31/10/2013 nitakuwa nawahutubia ikiwa ni sehemu ya utaratibu wangu
mpya wa kuzungumza nanyi watoto wenzangu. Nitajitahidi kila mwisho wa mwezi
kutoa hotuba yangu katika sehemu tofauti tofauti kama vile shuleni, kwenye
vituo vya watoto, mabaraza ya watoto na hata kwenye ofisi za mashirika ya
watoto kama hii leo ambapo natoa hotuba yangu tokea ndani ya ofisi za shirika
la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza zilizoko Ghana hapa Jijini Mwanza nchini
Tanzania. Shirika hili ndilo ambalo linatuwezesha sisi watoto kuweza kutoa
hotuba kupitia program ya “Hotuba ya watoto” Tunashukuru sana shirika la
Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza kwa kutujali watoto na kutuwezesha sauti
zetu kusikika. Pia tunaomba waandishi wa habari muweze kuirusha hewani hotuba
yangu ili kuwawezesha watoto wengi waweze kujua kile ambacho ninakihutubia siku
hii ya leo. Sina shaka mtatuunga mkono kwa aslimia mia moja. Nashukuru pia watoto wenzangu kwa kushirikiana
nami katika uandaaji wa hotuba hii.
Ndugu
watoto wenzangu,
Kutokana na Takwimu
za tafiti mbalimbali zinaonesha ya kuwa asilimia hamsini (50) ya watanzania wote
ni watoto na wengi wetu tunafahamu ya kuwa kesho ni leo,je tumejiandaaje na
tumeandaliwaje kupokea rasilimali nzuri za nchi yetu? Hakika kila mtu afikirie
kwa umakini, apambanue, achambue na afanye maamuzi sahihi, stahiki na magumu
kwa ustawi wa nchi yetu hasa katika kutujenga, kutushirikisha na kutuendeleza
vyema sisi watoto.
Ndugu
watoto wenzangu,
Napenda kuchukua
fursa hii kuwaelezea baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakuta watoto
wenzetu ambazo zimekuwa ni ukiukwaji wa haki za mtoto. Watoto wenzetu wamekuwa
wakifanyiwa ukatili wa kimwili kama vile kupigwa ngumi, mateke na viboko;
Ukatili wa kisaikolojia kama vile kutukanwa, kuitwa majina kama vile mbwa, kuku
na nguchiro; Ukatili wa kijinsia kama vile kubaguliwa katika kupata elimu na na
kazi za nyumbani mfano mtoto wa kiume ndiye anayepewa nafasi ya kusoma,
kupumzika na kucheza pia wakati mtoto wa kike akiaachwa nyumbani na kufanyishwa
kazi bila ya kupewa muda stahiki wa kupumzika;
na aina nyingine ya ukatili ni ukatili wa kingono ambapo watoto wenzetu wamekuwa
wakibakwa na kulawitiwa na watu wazima na wenye akili timamu.
Ndugu
watoto wenzangu,
Matukio mbali mbali
ya ukatili kwa watoto tumekuwa tukiyaskia ama kuyaona yakitokea katika jamii
zetu. Mkoani Mtwara mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari
Newala amepata ulemavu wa akili kwa kupigwa na mwalimu wake kwa madai ya
kushindwa kulipia kiasi cha pesa cha shilingi 300 iliyokuwa inachangishwa baada
ya kitabu cha shule kupotea. Wakati hayo yakitokea mkoani Mtwara huko Mkoani
Dododma mama mmoja mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa na jeshi la polisi kwa
tuhuma za kumuua mtoto wake mchanga. Na hapa Jijini Mwanza, mama mmoja alimmwagia
mtoto wake maji ya moto na kumsababishia majeraha na maumivu makali sehemu
mbali mbali za mwili wake. Kuna matukio mengi ya ukatili kwa watoto zaidi ya
hayo ambayo nimeweza kuyataja yakitokea kila siku katika jamii zetu.
Ndugu
watoto wenzangu,
Matukio ya ukatili
kwa watoto hayafanywi na miti, wanyama wala wadudu bali yanafanywa na watu
wenye akili timamu mbaya zaidi wengi wao ni watu wazima na wenye heshima zao
katika jamii. Pia matukio hayo hayafanyiki sehemu ambazo wanaishi mbwa, kuku au
paka bali hufanyika sehemu ambazo kuna viongozi wanaotawala, kuna wananchi
wanaishi na kuna taasisi zinazoweza kutetea na kumlinda mtoto dhidi ya ukatili.
Ni aibu sana kwa matukio ya ukatili kwa
watoto kutokea katika jamii zetu ambazo wanaishi binadaamu na wala si wanyama.
Ndugu
watoto wenzangu,
Napenda kuchukua
fursa hii kutoa wito kwa wazazi, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya
habari na jamii kwa ujumla kuwa tayari kuripoti na kupinga matukio ya ukatili
kwa watoto. Na serikali iweze kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wale wote
wanaofanya ukatili wa aina yoyote ile ili watoto wote waweze kupata haki zao
kwa maslahi ya kujenga Tanzania imfaayo kila mtoto. Kuanzia leo, naomba lugha
za matusi kwa watoto zikome, vipigo kwa watoto viishe na matukio ya ubakaji na
ulawiti kwa watoto tuyazike. Kila kiongozi katika eneo lake, tunamwomba
ahakikishe kuwa hakuna mtoto hata mmoja anayefanyiwa ukatili. Na kila mzazi
katika familia yake, tunamwomba ahakikishe hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili,
na kila taasisi katika eneo lake kikazi ihakikishe hakuna mtoto anayefanyiwa
ukatili. Tanzania bila ukatili kwa watoto inawezekana, Pamoja tunaweza!
Mungu ibariki Afrika!
Mungu ibariki
Tanzania!
Na Mungu wabariki
watanzania wote waweze kutulinda sisi watoto dhidi ya ukatili wa aina yeyote
ile.
Ahsanteni sana kwa
kunsikiliza!
Ummy Jamaly
Mwenyekiti wa baraza
la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.