|
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Regina Chonjo akipiga mpira kuashiria ufunguzi Airtel Rising Stars mkoa wa Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri jana. |
|
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Regina Chonjo akikagua timu wakati wa ufunguzi wa Airtel Rising Stars mkoa wa Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri jana. |
Soka ni ajira, DC Moro awambia vijana Airtel Rising
stars
Morogoro, Jumatano Agosti 17 2016 … Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Regina Chonjo amewataka
vijana kuonyesha vipaji vyao vya soka na kutambua kuwa mchezo huo ni fursa
nzuri inayoweza kuwapa maisha bora na kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Chonjo aliyasema hayo
wakati wa ufunguzi wa mashindano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya
Airtel Rising Stars kwa mkoa wa Morogoro uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mchezo huo.
“Napenda kutumia fursa hii kutoa rai
kwa wazazi na walezi kuwahamasisha vijana kushiriki michuano hii ili kuendeleza
vipaji vyao na kusaidia juhudi za serikali za kuinua kiwango cha mchezo wa soka
hapa nchini”, alisema. Zaidi ya wachezaji 120 walihudhuria uzinduzi huo
Alisema mbali ya kuwa burudani, mpira
wa miguu pia hudumisha amani, umoja, urafiki, udugu miongoni mwa viongozi na
wachezaji na kuwafanya vijana kuwa wakakamavu, wachangamfu na wenye afya bora.
“Lakini muhimu zaidi mpira wa miguu ni chanzo cha ajira kwa vijana wengi duniani”,
alisema .
Aliwataka viongozi wa soka mkoa wa Morogoro
kufuatilia kwa karibu michuano hiyo na kuchagua wachezaji wenye vipaji ili
kuuwezesha mkoa huo kufanya vizuri katika fainali za Taifa za Airtel Rising
Stars zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 6 hadi 11.
Alisema michuano ya Airtel Rising
Stars imekuwa ni jukwaa la kusaidia kubaini wachezaji wenye vipaji kutoka
sehemu mbalimbali ambao bila mashindano haya wangeweza kupotea hivi hivi.
Aliwataka viongozi wa soka mkoa humo kushirikiana na shirikisho la soka nchini
(TFF) kuwalea na kuwaendeleza vijana wanaopatikana kupitia Airtel Rising Stars.
Akiongea katika hafla hiyo ya
ufunguzi, mwenyekiti wa wa chama cha Soka mkoani Morogoro Pascal Kihanga ambaye
pia ni Mustahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro aliwataka vijana kucheza kwa
kujituma ili kuweza kuchaguliwa kuunda timu ya mkoa.
Kwa upande wake, Meneja wa Airtel mkoa
wa Morogoro Omar Bongo alisema kuwa kampuni ya Airtel inajivunia kuweza kupata
fursa ya kutoa mchango katika soka la Tanzania. “Airtel Rising Stars imekuwa chimbuko
la wachezaji wa timu za Taifa na klabu hapa nchini”. Tunaona fahari kuweza
kupata fursa ya kudhamini soka nchini Tanzania“alisema Bongo.
Hafla hiyo ya ufunguzi ilishuhudia
mchezo wa ufunguzi kati ya Moro Kids na Techforty ambapo Moro Kids waliibuka na
ushindi wa 2-0. Katika mchezo mwingine, Mwere Kids iliishinda Kizuka 2-1.