Japo tayari ni tajiri ,Mayweather ambae jina lake la utani ni Money, inatarajiwa atapokea zaidi ya dolla millioni $150m na Pacquiao kama millioni $100m.
Pacquiao yeye ametoka jamii ya kimaskini huko Ufilipino na kuna wakati katika maisha yake ya utotoni ambapo hata angelala njaa.
Sasa wa kuangalia kwenye TV kando, wengi wa mashabiki wa huko Marekani wangependa kuona makonde yakirushwa 'LIVE' kwa hivyo wamekubali kutoa ada ya hadi $100 kwa kichwa kushuhudia wakiwa 'LIVE' nje ya ulingo.
Wenye uchu wa kushuhudia pambano hilo 'LIVE' lakini hawajapata tiketi wako tayari kuzipata kwa walionanazo huku dau likiwa limepandishwa kwa kiwango atakacho muuzaji huyo mchuuzi.
Wafilipino kumshangilia Pacquiao
Wakati huo huo wito umetolewa kwa wakaazi wa kisiwa kimoja cha Philippines kwamba watumie kawi kwa kipimo kidogo ili kuihifadhi ndio waitumie kumwangalia katika runinga zao hapo Jumapili shujaa wao m-Filipino mwenzao , Manny Pacquiao (36) atakapokuwa akipambana na Mmarekani Floyd Mayweather (38) kwenye ulingo wa shindano la ndondi linalotajwa kuwa kubwa zaidi mnamo siku za hivi karibuni.
Wakaazi hao wameshauriwa na kampuni ya umeme nchini humo Palawan kuzima vifaa vya matumizi mengine ya nyumbani kama friji, kutotumia mashine za kufua nguo, wala kutopiga pasi ili kuhifadhi kawi hiyo siku hiyo itumike tu kuwashia Runinga zao.
Ushauri huo umetolewa kwani kisiwa hicho hukumbwa na upungufu wa umeme mara kwa mara, hivyo ni sharti wafuate maagizo hayo ili wasikose kushuhudia na kumshangilia kinara huyo wao ataeshiriki pambano hilo litakalo fanyika huko Las Vegas Jumamosi usiku saa za Marekani.
Ndilo pambano lililovutia fedha zaidi kuwahi kutokea.