Kiwavijeshi aina ya Fall Armyworm
(FAW)
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo
ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema akizungumza wakati
akifungua warsha ya siku moja kujadili namna ya kukabiliana na mdudu aina ya Kiwavijeshi
Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi Afya ya Mimea, Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo
Mifugo na Uvuvi, Bibi Beatrice Palangyo akiwasilisha mada ya utambuzi wa Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wanaojulikana
kitaalamu kama Spodoptera Frugiperda wakati wa warsha ya kujenga uelewa juu ya wadudu hao
Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm
(FAW) wakishambulia mazao aina ya mahindi
Wadau wa kilimo kutoka Shirika la
Maendeleo la Watu wa Marekani Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, USAD, ONE HACKER FUND, Taasisi ya Utafiti wa
Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Shirika
la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Mradi wa WEMA wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo
ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema akizungumza wakati
akifungua warsha ya siku moja kujadili namna ya kukabiliana na mdudu aina ya Kiwavijeshi
Baadhi ya wadau wa kilimo wakifatilia warsha
Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm
(FAW) wakishambulia zao la Mahindi
Na
Mathias Canal, Dar es salaam
Wizara ya Kilimo Mifugo
na Uvuvi imeanza jitihada za kuwakabili Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm
(FAW) wanaojulikana kitaalamu kama Spodoptera Frugiperda ambao wametajwa
kuwa na uwezo mkubwa kuharibu mazao mbalimbali hususan mahindi ambayo ndio zao
kuu la chakula nchini.
Imeelezwa kuwa Viwavijeshi
hao wanapofika kwenye mazao hutoa kemikali ambayo huweza kudanganya mmea kuwa
unashambuliwa na magonjwa kama ukungu au fangasi hivyo mmea unapohisi
unashambuliwa na hayo magonjwa, hupunguza kinga dhidi ya wadudu hao hatari na
kuwa rahisi kushambuliwa.
Hayo
yamebainishwa leo Septemba 14, 2017 na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo
ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema wakati
akifungua warsha ya siku moja mbele ya Wadau wa Kilimo ambao ni Shirika la
Maendeleo la Watu wa Marekani USAD, ONE HACKER FUND, Taasisi ya Utafiti wa
Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Shirika
la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Mradi wa WEMA .
Mkutano ulikuwa na lengo
la kujenga uelewa wa pamoja kwa ajili ya kumkabili mdudu huyo aina ya Fall
Armyworm (FAW) ambaye anashambulia mazao mbalimbali nchini hususani zao la
mahindi.
Alisema Athari ya
viwavi jeshi haishii kuharibu majani ya mimea pekee, wadudu hao wanapokula
majani na kutengeneza sumu aina ya ‘firenide’ inayodhuru mifugo inapokula
majani yaliyoathiriwa.
Bwana Malema
amesema tayari Serikali imechukua juhudi za awali kukabiliana na mdudu huyo
ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya utambuzi wa mdudu huyo kwa
kuwataka Wananchi kung’oa mazao na kuyachoma pindi wanapobaini uwepo wa mdudu
huyo.
Pia tayari dawa tatu
zimepitishwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya uchunguzi
wa Viatilifu (TPRI) zinazoangamiza
wadudu hao ambazo ni Duduba 450, Mupacrone 500 EC na Match Save kutoka Kampuni
ya Syngenta hivyo Wananchi wametakiwa kuzitumia haraka pindi wanapoona dalili
za kuwepo wa wadudu hao shambani.
Bwana Malema amesema
kuwa katika kipindi cha miaka mingi Tanzania imekuwa ikikumbwa na viwavijeshi
aina ya African Armywarms ambapo mara
zote imekuwa ikiwadhibiti wadudu hao wanapojitokeza kwa kuwapa kiuatilifu
kinachosababaisha matumbo ya wadudu hao kujaa na hatimaye kuwasababishia vifo.
Ameongeza kuwa kwa
mara ya kwanza Wizara ilipata taarifa ya uvamizi katika shamba la Mwekezaji
mkubwa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa mwezi Machi 2017 na walipofuatilia na
kupeleka sampuli maabara mdudu huyo alibainika kwa jina la Spodoptera frugiperda au Fall arymworm ambaye ni hatari na
amekuwa akiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.
Kutokana na unyeti
wa suala hilo Wizara ya Kilimo imewasiliana na Shirika la Chakula Duniani
(FAO), kwa ajili ya kuunganisha juhudi za pamoja ili kumdhibiti mdudu huyo
kabla hajasambaa kwenye maeneo mengi nchini.
Shirika la Chakula
na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika taarifa yake imesema viwavijeshi hao
aina ya Fall armyworm wameonekama pia katika nchi za Zimbabwe, Malawi,
Msumbiji, Namibia Afrika ya Kusini na Zambia huku chanzo chake ikiwa ni nchini
Marekani.
Kwa mujibu wa
Redio ya Umoja wa Mataifa, FAO bado haijatangaza kiwango kamili cha
uharibifu katika nchi hizo, huku ikiongeza kuwa Shirika hilo na Wadau wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamejadili udhibiti wa viwavijeshi.
Naye Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi Afya ya Mimea, Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo
Mifugo na Uvuvi, Bibi Beatrice Palangyo akiwasilisha mada ya utambuzi wa wadudu
hao katika warsha hiyo amesema kuwa katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara
wadudu hawa walianza kuingia nchini Nigeria na kwa sasa wameenea katika nchi
mbalimbali ikiwemo Tanzania, Afrika kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na
Malawi.
Alisema wadudu hao
wanashambulia mazao ya jamii ya nafaka kama mahindi (Corn) wanauwezo wa
kushambulia hata magugu pale wanapokosa mazao kama mahindi kwani hawali mazao
mengine kama mboga na matunda, wanakula zaidi mahindi na magugu yanayofanana na
mahindi.
Zaidi
ya Mikoa 15 nchini ikiwemo Zanzibar imeripoti kuwepo kwa kadhia ya mdudu huyo
hivyo asilimia 15 ya mazao jamii ya nafaka kama mahindi yameathiriwa, jambo ambalo
kama lisingepatiwa ufumbuzi wa haraka, lingesababisha upotevu mkubwa wa mazao
mashambani na kutishia upatikanaji wa chakula nchini.