ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, September 14, 2017

SERIKALI YAANZA JITIHADA ZA KUWAKABILI VIWAVIJESHI HATARI AINA YA FALL ARMYWORM (FAW)


 Kiwavijeshi aina ya Fall Armyworm (FAW)
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema akizungumza wakati akifungua warsha ya siku moja kujadili namna ya kukabiliana na mdudu aina ya Kiwavijeshi
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Mimea, Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bibi Beatrice Palangyo akiwasilisha mada ya utambuzi wa Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wanaojulikana kitaalamu kama Spodoptera Frugiperda wakati wa warsha ya kujenga uelewa juu ya wadudu hao


Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wakishambulia mazao aina ya mahindi
Wadau wa kilimo kutoka Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, USAD, ONE HACKER FUND, Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki  (TPRI), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Mradi wa WEMA wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema akizungumza wakati akifungua warsha ya siku moja kujadili namna ya kukabiliana na mdudu aina ya Kiwavijeshi
 Baadhi ya wadau wa kilimo wakifatilia warsha
Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wakishambulia zao la Mahindi
 
Na Mathias Canal, Dar es salaam 

Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imeanza jitihada za kuwakabili Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wanaojulikana kitaalamu kama Spodoptera Frugiperda ambao wametajwa kuwa na uwezo mkubwa kuharibu mazao mbalimbali hususan mahindi ambayo ndio zao kuu la chakula nchini.

Imeelezwa kuwa Viwavijeshi hao wanapofika kwenye mazao hutoa kemikali ambayo huweza kudanganya mmea kuwa unashambuliwa na magonjwa kama ukungu au fangasi hivyo mmea unapohisi unashambuliwa na hayo magonjwa, hupunguza kinga dhidi ya wadudu hao hatari na kuwa rahisi kushambuliwa. 

Hayo yamebainishwa leo Septemba 14, 2017 na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema wakati akifungua warsha ya siku moja mbele ya Wadau wa Kilimo ambao ni Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani USAD, ONE HACKER FUND, Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki  (TPRI), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Mradi wa WEMA .

Mkutano ulikuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kwa ajili ya kumkabili mdudu huyo aina ya Fall Armyworm (FAW) ambaye anashambulia mazao mbalimbali nchini hususani zao la mahindi.

Alisema Athari ya viwavi jeshi haishii kuharibu majani ya mimea pekee, wadudu hao wanapokula majani na kutengeneza sumu aina ya ‘firenide’ inayodhuru mifugo inapokula majani yaliyoathiriwa.

Bwana Malema amesema tayari Serikali imechukua juhudi za awali kukabiliana na mdudu huyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya utambuzi wa mdudu huyo kwa kuwataka Wananchi kung’oa mazao na kuyachoma pindi wanapobaini uwepo wa mdudu huyo.

Pia tayari dawa tatu zimepitishwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya uchunguzi wa Viatilifu (TPRI) zinazoangamiza wadudu hao ambazo ni Duduba 450, Mupacrone 500 EC na Match Save kutoka Kampuni ya Syngenta hivyo Wananchi wametakiwa kuzitumia haraka pindi wanapoona dalili za kuwepo wa wadudu hao shambani.

Bwana Malema amesema kuwa katika kipindi cha miaka mingi Tanzania imekuwa ikikumbwa na viwavijeshi aina ya African Armywarms ambapo mara zote imekuwa ikiwadhibiti wadudu hao wanapojitokeza kwa kuwapa kiuatilifu kinachosababaisha matumbo ya wadudu hao kujaa na hatimaye kuwasababishia vifo.

Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza Wizara ilipata taarifa ya uvamizi katika shamba la Mwekezaji mkubwa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa mwezi Machi 2017 na walipofuatilia na kupeleka sampuli maabara mdudu huyo alibainika kwa jina la  Spodoptera frugiperda au Fall arymworm ambaye ni hatari na amekuwa akiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Kutokana na unyeti wa suala hilo Wizara ya Kilimo imewasiliana na  Shirika la Chakula Duniani (FAO), kwa ajili ya kuunganisha juhudi za pamoja ili kumdhibiti mdudu huyo kabla hajasambaa kwenye maeneo mengi nchini.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika taarifa yake imesema viwavijeshi hao aina ya Fall armyworm wameonekama pia katika nchi za Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Namibia Afrika ya Kusini na Zambia huku chanzo chake ikiwa ni nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Redio ya Umoja wa Mataifa, FAO bado haijatangaza   kiwango kamili cha uharibifu katika nchi hizo, huku ikiongeza kuwa Shirika hilo na Wadau wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamejadili  udhibiti wa viwavijeshi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Mimea, Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bibi Beatrice Palangyo akiwasilisha mada ya utambuzi wa wadudu hao katika warsha hiyo amesema kuwa katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wadudu hawa walianza kuingia nchini Nigeria na kwa sasa wameenea katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Afrika kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Malawi.

Alisema wadudu hao wanashambulia mazao ya jamii ya nafaka kama mahindi (Corn) wanauwezo wa kushambulia hata magugu pale wanapokosa mazao kama mahindi kwani hawali mazao mengine kama mboga na matunda, wanakula zaidi mahindi na magugu yanayofanana na mahindi.

Zaidi ya Mikoa 15 nchini ikiwemo Zanzibar imeripoti kuwepo kwa kadhia ya mdudu huyo hivyo asilimia 15 ya mazao jamii ya nafaka kama mahindi yameathiriwa, jambo ambalo kama lisingepatiwa ufumbuzi wa haraka, lingesababisha upotevu mkubwa wa mazao mashambani na kutishia upatikanaji wa chakula nchini.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.