ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, October 14, 2024

RAIS SAMIA APOKEA MWENGE WA UHURU KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO MBIO ZA MWENGE WA UHURU MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi wakati akihitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge ambazo kitaifa zimefanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba tarehe 14 Oktoba, 2024.

 "Nimehitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na Wiki ya Vijana hapa mkoani Mwanza. Ninawashukuru wote waliojitokeza kushiriki tukio hili la kihistoria ambapo Mbio za Mwenge wa Uhuru zimefikisha miaka 60."

"Pongezi kwa wote walioshiriki kuukimbiza kwa mwaka huu na kazi nzuri waliyofanya ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo"


"Nimepokea taarifa ya miradi yote iliyotembelewa katika mbio hizi ambayo inakwenda kunufaisha wananchi kwenye kila kona ya nchi yetu. Nimepokea mapendekezo na salamu za wananchi wa maeneo yote ulikopita Mwenge wa Uhuru, na kwa umakini na uharaka tutayafanyia kazi yale yote yaliyoainishwa kwa manufaa ya Taifa letu"

RAIS wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 14, 2024 amewaongoza Viongozi na Wananchi mbalimbali kwenye kilele cha mbio za Mwenge zilizoambatana na Wiki ya Vijana na Nyerere Day katika uwanja CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Rais Samia akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa mbio hizo Ndugu Godfrey Eliakim Mzava kwenye Kilele cha Maadhimisho Mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Matukio mbalimbali katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.


TASAC YAFANYA MAZUNGUMZO NA KANALI MTAMBI KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

 





Katika jitihada zake za kuendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kuzungumzia masuala ya usalama wa usafiri wa majini kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kanali Mtambi ameipongeza TASAC kwa hatua mbalimbali wanazochukua kuimarisha masuala ya usafiri wa majini na ushirikiano wanaoutoa katika Mkoa wa Mara na hususan usalama wa wasafiri katika katika Ziwa Victoria.


Kanali Mtambi ameiomba TASAC kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria na kanuni zinazohusiana na usafiri wa majini kwa wananchi na taasisi za Serikali na binafsi ili kupunguza ajali na athari za ajali za vyombo vya usafiri wa majini.


“Sisi kama Serikali tunatakiwa kuendelea kuwahakikishia usalama watumiaji wa Ziwa Victoria ikiwemo wasafiri wanaotumia vyombo vya usafiri vya majini kuhusiana na usalama wao wanapotumia usafiri wa majini,” amesema Mhe. Kanali Mtambi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira na Usafiri wa Majini, Bi. Leticia Mutaki amesema TASAC inaendelea na jukumu lake la utoaji wa elimu ya usalama wa usafiri majini kwa wadau wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo taasisi na Halmashauri kuhusiana na usimamizi wa usafiri wa majini.


“Tuna mpango wa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Halmashauri zote zinazopakana na ziwa ili Halmashauri zisaidie kusimamia usafiri wa majini kwa niaba ya TASAC,” amesema Bi. Mutaki.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC, Bi. Judith Kakongwe amesema Sheria na kanuni za sasa zinawabana zaidi wenye vyombo vya usafiri kuweka jaketi okozi lakini haziwabani abiria kuzivaa jambo ambalo linaleta changamoto kwa sababu wamiliki wakiweka bila kuvaliwa hazisaidii kama inatokea ajali.


“Tupo kwenye mchakato wa kubadili vipengele vya sheria na kanuni ili abiria nao wabanwe kuvaa jaketi okozi na sio tu wamiliki wa chombo kama ilivyo sasa ili kusaidia kupunguza madhara ajali zinapotokea” amesema Bi. Kakongwe.


TPA kuanza usimamizi wa mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela

 

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatarajia kuanza rasmi usimamizi wa shughuli zote za kibandari katika mwalo wa Kirumba ulipo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kufuatia tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali.

Akitoa taarifa kwa umma Ijumaa Oktoba 11, 2024 kupitia waandishi wa habari, Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa tangazo la Serikali namba 855 la tarehe 24/12/2023 ambalo linaipa TPA mamlaka ya kusimamia mialo yote iliyo rasmi.

Lugenge aliongeza kuwa shughuli za usimamizi wa mwalo huo zitaanza kesho rasmi Jumamosi Oktoba 12, 2024 zikihusisha usimamizi wa usalama wa vyombo vya majini.

Awali mwalo huo ulikuwa ukisimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ukiwa ni miongoni mwa mialo 10 katika Ziwa Victoria iliyotangazwa kusimamiwa na TPA.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza
Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge akitoa taarifa kwa umma kuhusu TPA kuanza kuusimamia mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela.
Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge akizungumza na wanahabari jijini Mwanza.
Tazama Video hapa chini

Thursday, October 10, 2024

KAMATI YA BUNGE YAMPONGEZA RAIS DKT SAMIA SULUHU KWA KUCHOCHEA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI NCHINI

 

 Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Suleiman Jafo akizungumza wakati wa ziara ya  ya siku moja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara ilipotembelea eneo Kituo cha Forodha za Tanzania na Kenya eneo la Mkinga Mkoani Tanga kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mariam Ditopile Mzuzuri akifuatia Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian
 Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mariam Ditopile Mzuzuri akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo



Na Oscar Assenga, MKINGA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imempongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya kuchochea uwekezaji nchini pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara.


Pongezi hizo zilitolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mariam Ditopile Mzuzuri wakati wa ziara ya siku moja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara ilipotembelea eneo Kituo cha Forodha za Tanzania na Kenya eneo la Mkinga Mkoani Tanga.

 

Alisema kwamba mazingira hayo mazuri yamewekwa kwa wafanyabiashara ambao tayari wapo kwenye biashara na viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbal nchini

 

“Leo tumepata fursa ya kuja hapa kituo cha Forodha Horohoro kuona namna kituo hicho cha pamoja baina ya Tanzania na Kenya sisi kama kamati tunawapongeza kwani kituo hiki kazi yake kubwa kukusanya mapato kuhakikisha wafanyabishawa kutoa Kenya wanaoleta bidhaa hawapitia njia za panya wanapitia hapo kutoa ushuru na kodi stahiki pia bidhaa zinazotoka nchini na kwenda nchi jirani zinatoa ushuru stahiki “Alisema

 

Alisema wanawapongeza kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye kituo hicho kwa maana mwaka jana walipanga kukusanya jumla ya sh.Bilioni 77 lakini walikusanya Bilioni 90 na kwa mwaka huu wa fedha wa 2024/2025 kota ya kwanza Julai hadi Sept walipangiwa kukusanya Bilioni 25 lakini wamekusanya bilioni 34 wanaona ni mafanikio.

 

“Sisi kama Kamati tunaiomba serukali na tutalisimamia lazima waongeze ufanisi katika kituo hicho na kikubwa cha kwanza ambacho kimeelezwa ni ununuzi wa scana kwa namna tulivyoona ukusanyaji wa mapato unaridhisha lazima tupate scana na focklift kwa ajili ya kunyanyua mizigo tuweze kuongeza ufanisi na mapat kupanda”Alisema

 

Aidha alisema kwamba inawezekana wanaotumia njia za panya ni kutokana na kukaa muda mrefu wakati wa kupitisha mzigo na hivyo kuona shida kupitishia hapa hivyo tunaiagiza Serikali ndani ya muda mfupi na wizara zote husika na Waziri Dkt Jafo akae na Waziri wa Fedha ili kwa haraka scana na focklift ziweze kupatikana na kuongeza ufanisi na kituo kifanye kazi ile inayokusudiwa chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu na Serikali yake ya wamu ya sita.

 

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Suleiman Jafo amesema kwamba Serikali itahakikisha bidhaa zote zinazopitishwa kwenye vituo vya Forodha katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani zinaendelea kuwa na viwango vinavyokidhi na kudhibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Wakala wa VipimoTanzania ( WMA) na Tume ya Ushindani (FCC).

 

Alisema kwamba lengo la kuhakikisha hilo ni kuwalinda watanzania na walaji wa mwisho wa siku wafanye biashara na kamati imetoa maelekezo kuhakikisha eneo hilo linakuwa na scana ambayo inaweza kuhakikisha mizigo inakwenda kwa haraka sana.

 

“Hili la scana hapa tumelichukua na sio muda mrefu kupitia Wizara ya fedha tutahakikisha Scana hiyo inapatikana pamoja nyenzo za kufanyia kazi ikiwemo Focklift itakayokuwa ikinyanyua mizigo lakini niwashukuru Kamati ya Bunge kwa kazi kubwa na niwaambie serikali itahakikisha mambo yote muhimu yanatekelezwa lengo kubwa ni kuboresha utoaji huduma”Alisema Waziri Jafo.

 

 Aidha alimshukuru R ais Dkt Samia Suluhu kutokana na kazi kubwa inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya kimaendeleo na hata kamati ilivyotembelea eneo la Horohoro imeona kuna mafanikio makubwa kwenye ongezeko la mapato.

 

“Lakini kuona jinsi gani Taasisi zinasaidia kuhakikisha biashara eneo hilo mizigo isafirishwe vizuri baina ya nchi ya jirani kenya na bidhaa zinazopita lazima zinakidhi viwango vilivyowekwa na kuthibitishwa na TBS na WMAna FCC lengo kuwalinda watanzania na walaji mwisho”Alisema Waziri Dkt Jafo.

 

Akizungumzia suala la ubinafsishaji lililofanyika miaka ya nyuma nchini alisema Serikali ilikuwa na nia njema kufanya ubinafsishaji lakini kwa bahati mbaya malengo yalienda tofauti wengi waliopewa viwanda hawakufanya vizuri.

 

“Kama mnakumbuka hivi karibuni Rais Dkt Samia Suluhu alitoa maelekezo kwamba viwanda hivyo vifufuliwe maeneo mbalimbali na nilikuja Tanga na hivi karibuni tumekaa kikao na Hazina kubainisha viwanda vyote na kuona hatua za kuchukua“Alisema

 

Waziri Dkt Jafo alisema mojawapo ya hatua hizo ni kuhakikisha viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi waangalia namna bora ya kufanya kazi kwa utaratibu wa kisheria na wapate wawekezaji wengine au waliokuwepo wahakikishe ndani ya muda mfupi wanafanya uwekezaji ili viwanda viweze kufanya kazi na kutengeneza ajira kwa watanzania.

 

WANANCHI WA BUKOMBE KWA MH.BITEKO WAFURIKA ZOEZI LA UGAWAJI WA MITUNGI YA GESI DARASA LATOLEWA.

 ZAIDI YA MITUNGI YA GESI 1,500 YATOLEWA KWA BEI YA RUZUKU BUKOMBE

Wananchi wametakiwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kuimarisha afya zao sambamba na kutunza mazingira. Wito huo umetolewa Oktoba 10, 2024 Wilayani Bukombe na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage wakati wa Semina maalum ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wakazi wa Wilaya hiyo. "Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia, anatupenda na anafanya kila njia kuhakikisha kila mwananchi anapata bidhaa za nishati safi za kupikia kwa gharama nafuu", alisema Mhandisi Advera.

𝗕𝗨𝗞𝗢𝗠𝗕𝗘 𝗞𝗨𝗠𝗘𝗡𝗢𝗚𝗔....!! 🇹🇿✔️

 


𝗕𝗨𝗞𝗢𝗠𝗕𝗘 𝗞𝗨𝗠𝗘𝗡𝗢𝗚𝗔....!! 🇹🇿✔️


Heka heka za Mwalimu Day wilayani Bukombe zimeanza leo asubuhi kwa jogging moja matata kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya hadi kwenye viwanja vya Kilimahewa tukiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Mbunge wa jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mh. Paskasi Mulagiri na viongozi wengine wa Wilaya pamoja na benki ya CRDB.

Sisi Jembe fm tunafurahi kuwa sehemu ya tukio hili adhimu, maalum kwa ajili ya walimu wetu wapendwa na wananchi wa Bukombe kwa ujumla.
















#Bukombe
#KusemaNaKutenda
#SikuYaMwalimu2024
#crdbbank
@jembefmtz 
@jembenijembe 

Tuesday, October 8, 2024

MAPINDUZI MAKUBWA YAMEFANYIKA TCRA KANDA YA ZIWA - WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA - SEHEMU YA KWANZA

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

Katika muendelezo wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, Leo Oktoba 08, 2024, Jembe Fm imefika katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Ziwa (TCRA) na kuzungumza na meneja wa kanda Mhandisi Imelda Salum, #tcra #samiasuluhuhassan #jembehabari #mwanza

TPA TANGA BILIONI 18 NDANI YA MIEZI 3

 

 

MENEJA wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha akizungumza waandishi wa habari ikiwa ni siku ya wiki ya huduma kwa wateja
Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha kushoto akimkabidhi zawadi Mwandishi Mwandamizi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mkoa wa Tanga Bertha Mwambela ikiwa ni wiki ya huduma kwa wateja mapema leo



Na Oscar Assenga, TANGA

MAMLAKA ya Bandari (TPA) Tanzania Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha miezi mitatu ya robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 wamekusanya Bilioni 18 zilizotokana na ujio wa meli 11 huku asilimia 44.4 ya mapato hayo yakitokana na Meli za Kampuni ya Sea Front Shipping Services kutumia Bandari ya Tanga.

Hayo yalisemwa leo na Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku ya wiki ya huduma kwa wateja ambapo alisema kwamba wanapenda kumshukuru mteja huyo mkubwa na wateja wengine ambao wanaitumia Bandari hiyo.

Alisema kwamba wataendelea kuwashukuru na kushirikiana nao ili wajue changaamoto zinazowakabili ili waweze kuzirekebisha na wahakikishe wanapata huduma bora ya kiwango cha juu kitachowawezeshaa kurudi tena na kupata huduma katika Bandari hiyo na kufikia kwenye lengo walilokusudia.

Akizungumzia kiwango cha shehena ambayo wameihudumia kwa kipindi hicho alisema waliweza kuhudumia shehena ya tani 333,718 na hivyo kuvuka lengo lao waliojiwekea kwa asilimia 17.8 walijiwekea la kuhudumia tani 283,290.

“Utaona ni jinsi gani tumefanikiwa na tusingeweza kufanikiwa bila kutoa huduma bora kwa wateja mwaka jana kwa kipindi cha miezi mitatu kama hii tuliweza kuhudumia tani 200,004 mwaka huu tumehudumia 333,718 utaona namna tumeweza kuvuka lengo ”Alisema

Awali akizungumza Mwakilishi wa Kampuni ya Maersk ofisi ya Tanga Salum Mgaya alisema huduma za bandari ya Tanga hivi sasa zimefanyiwa maboresho makubwa ya vifaa na rasilimali watu na teknolojia imeongezeka ufanisi mkubwa na meli zao zinapoingia zinahudumiwa kwa wakati na makasha ya wateja yanatolewa kwa wakati.

Alisema kwamba hivi sasa meli zinafunga gatini na kuhudumiwa masaa 24 na wamekwisha kuleta meli kubwa yenye kontena 1,000 na imehudumiwa ndani ya wastani wa siku tatu mpaka nne kulingana na vifaa vilivyokuwepo lakini maboresho yaliyofanyika yameongeza ufanisi Bandari ya Tanga.

Naye kwa upande wake Mwakilishi kutoka Kampuni ya Star rock Shipping Vitalis Mokiwa alisema walikuwa wanadili na meli za mafuta na sasa wanadili na meli za mizigo mbalimbali ikiwemo ya kontena na wanaishukuru serikali kwa kuwaboresha bandari ya Tanga.

Alisema kwa sababu mwanzo meli zilipokuwa zinakuja mizigo ilikuwa inashushwa mbali na gatini na hivyo wakijikuta waingia gharama mara mbili lakini sasa kutokana na maboresho ya ujenzi wa gati ambao umewezesha meli kufika gati.


Monday, October 7, 2024

TPA TANGA BILIONI 18 NDANI YA MIEZI 3

 VICTOR MASANGU,PWANI TV

 
Kilio cha walimu wa shule ya  msingi Boko Timiza iliyopo  kata ya Tumbi Halmashauri ya Wilaya ya  Kibaha mji   kilichokuwa kikiwakabiliwa kwa kipindi cha miaka zaidi ya 40  cha kuwepo na  changamoto  sugu ya  ukosefu mkubwa  wa kutokuwa na viti na meza hatimaye kimepatiwa ufumbuzi baada ya baadhi ya wadau wa maendeleo ya elimu kuamua kulivalia njuga suala hilo na kwenda kutoa msaada kutokana na kubaini walimu hao hawana sehemu maalumu ya kukaa.

Hayo yamebainishwa na Kaimu  Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Boko Timiza Rozania Kimate  wakati wa halfa fupi  iliyofanyika shuleni hapo kwa ajili ya kukabidhiwa  msaada huo wa viti na meza kutoka kwa mdau wa maendeleo Selina Koka ambaye pia ni mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini na  Mlezi wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake (UWT)  Wilaya ya Kibaha mjini na kubainisha  msaada huo utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa walimu.

UBIA WA TWIGA WAONGOZA MCHANGO WA TASNIA YA UCHIMBAJI MADINI KATIKA UCHUMI WA TANZANIA

 

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow akiongea katika mkutano na waandishi wa habari ,viongozi wa serikali na wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa bulyanhulu jana,(Kushoto) ni Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa na (kulia) ni Meneja wa Barrick nchini,Melkiory Ngido.
Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa akiongea katika mkutano huo.
Mbunge wa Nyang'hwale,Mh.Hussein Nasor Amar akiongea katika mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu.

Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa, amesema ubia kati ya Kampuni ya Dhahabu ya Barrick na Serikali ya Tanzania ni kielelezo cha mafanikio ya ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwa kuwa unazidi kuleta manufaa nchini na ameomgeza kuwa Serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wenye kuleta mapinduzi chanya katika kukuza uchumi wa nchi .

Akiongea na katika mkutano wa waandishi wa habari wa kupokea taarifa ya utendaji wa migodi ya Barrick na Twiga uliojumuisha wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu, Dk.Kiruswa, alisema ubia huu umekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa migodi yote inayoendeshwa na Barrick uendeshaji wake umekuwa wa uwazi pia mafanikio yake yanaonekana kutokana na kutoa mchango mkubwa kwa Serikali kupitia kodi mbalimbali, kufanikisha miradi ya kijamii kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), kupanua wigo kwa ajira kwa Watanzania na kunufaisha wananchi kupitia utekelezwaji wa sera ya maudhui ya ndani (Local content kwa ufanisi mkubwa) sambamba na uwekezaji katika matumizi ya teknolojia za kisasa cha uchimbaji.

Alisema Serikali haitafumbia macho vitendo vya kuwahujumu wawekezaji wanaofanya vizuri katika uwekezaji wao nchini kwa lengo la kuwakatisha tamaa na kurudisha nyuma mkakati wa Serikali wa kukuza uwekezaji nchini yakiwemo mashirikika yasio ya Kiserikali ya nje ya nchi ambayo yamekuwa yakijifanya kiranja wa kutetea haki za binadamu na kusambaza taarifa za uwongo dhidi ya wawekezaji wa hapa nchini zikijifanya kuwatetea watanzania wanyonge wakati zinatafuta mianya ya kujinufaisha kupitia mgongo wa watanzania.

“Serikali ya Tanzania iko imara na madhubuti katika kusimamia wawekezaji kuhakikisha wanafuata kanuni na sheria zake kupitia taasisi zake mbalimbali zilizoanzishwa kisheria ambazo zinafanya vizuri na wanaokiuka sheria wanachukuliwa sheria na kupewa maelekeza na miongozo hivyo hayo mashiriki yasio ya Kiserikali yaache kuchafua taswira ya nchi kama ambavyo yamekuwa yakifanya kwa muda mrefu kupitia mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara” ,alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na maombi yaliyokuwa yakitolewa kwa Serikali na viongozi wa wananchi katika maeneo ya migodi ya kuwatengea wachimbaji wadogo maeneo na kuyataka makampuni makubwa yenye teknolojia ya uchimbaji kuwasaidia Serikali imeanza kuyafanyia kazi na imeanza mazungumzo na makampuni makubwa kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake zinazosimamia uchimbaji wa madini.

Ubia huo unachangia 51% ya mapato ya Serikali yanayotokana na tasnia ya uchimbaji madini, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mpango wa Uwazi wa Tasnia ya Uchimbaji Madini Tanzania (TEITI). Ubia wa Twiga unajumuisha migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu.

Migodi yote miwili pia iliongoza katika utendaji wa kiusalama wa tasnia hiyo, huku Bulyanhulu ikishinda Tuzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka huu wakati North Mara ikitajwa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Tanzania (OSHA) kuwa kampuni bora katika kuwahudumia wafanyakazi wenye mahitaji maalumu.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema katika mkutano huo kuwa utafutaji wa madini unaoendelea katika maeneo yaliyotumika na kuachwa karibu na migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara unaendelea. Utafiti huo umebainisha fursa zaidi za kuzihuisha na kuzipanua hifadhi za madini ambapo madini yatakwisha au kupungua, jambo litakalosaidia zaidi katika kuongeza uhai na unyumbufu wa migodi hiyo. Aidha, maendeleo mazuri yameshapatikana katika kuyabainisha maeneo mapya ambapo hapakuwahi kuwa na shughuli za uchimbaji madini, yenye uwezo wa kuongeza migodi mipya kwenye kampuni hiyo.

Aidha, Bristow alisema mpango wa Barrick na Twiga wa Kusongesha Mbele Mustakabali wa Elimu umekamilisha awamu yake ya kwanza, ambapo Barrick ilifadhili upanuzi wa miundombinu ya shule zipatazo 64, yenye thamani ya dola milioni 10, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo 396, mabweni yapatayo 97 na majengo ya maliwato yapatayo 600. Awamu ya pili ya mpango huo umepangwa kuanza katika robo ya nne ya mwaka huu kwa uwekezaji mwingine wa dola milioni 10 ambao utafuatiwa na awamu ya tatu ya dola milioni 10.

Wakati huohuo, Chuo cha Barrick, kilichozinduliwa mwanzoni mwa mwaka na Waziri wa Madini kwenye mgodi uliofungwa wa Buzwagi na ambao hivi sasa ni eneo maalum la uzalishaji (SEZ), tayari kimetoa mafunzo kwa mafomeni, wasimamizi na warakibu zaidi ya 1,000 kutoka katika nchi za Afrika na Mashariki ya Kati. Chuo hiki kiko mbioni kufikia lengo lake la kutoa mafunzo kwa zaidi ya watu 2,000 mwaka huu.

Bristow alisema kulingana na dhamira ya uwazi ya Barrick, kampuni hiyo iliwasilisha taarifa za hivi karibuni za mfululizo wa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizokuwa zinatolewa dhidi ya Mgodi wa North Mara kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (CHRGG). Baada ya kutembelea mgodi huo na maeneo ya jirani na kufanya uchunguzi wa kina, tume hiyo ilitoa taarifa iliyothibitisha kwamba hapakuwa na ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu katika mgodi wa North Mara na hivyo kuuondolea mgodi huo tuhuma hizo zilizotolewa na baadhi ya mashirika yasiyo yasiyo ya kiserikali ya nchi za nje.

Viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka wilaya za Kahama, Msalala na Nyang’hwale waliohudhuria mkutano huo, walipongeza mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana kupitia uwekezaji wa Barrick hususani katika kufanikisha miradi mikubwa ya kijamii kupia fedha za uwajibikaji kwa jamii kwenye sekta ya afya na elimu.

Friday, October 4, 2024

Simba SC 2-2 Coastal Union | Highlights | NBC Premier League 04/10/2024

 Coastal Union imelazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Simba katika mchezo wa ligi kuu ya NBC Tanzania Bara uliopigwa kwenye Dimba KMC Complex, Dar es Salaam.

Simba wametangulia kwa magoli mawili kipindi cha kwanza kutoka kwa Mohamed Hussein Zimbwe Jr. na Lionel Ateba kwa penati , lakini Coastal wakacharuka kipindi cha pili na kupata magoli mawili kupitia kwa Abdallah Hassan na Hernest Malonga....

Thursday, October 3, 2024

VIJIJI VYOTE MTWARA VIMEFIKISHIWA UMEME SASA NI ZAMU YA VITONGOJI



📌BILIONI 16.7 KUSAMBAZA UMEME VITONGOJI 150


📌KUNUFAISHA KAYA 4,950

Baada ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 785 Mkoani Mtwara, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 16.7 wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150 utakaonufaisha kaya 4,950 mkoani humo.

Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Deogratius Nagu amebainisha hayo Oktoba, 02, 2024 Wilayani Masasi Mkoani Mtwara mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Kanali Patrick Sawala wakati wa kumtambulisha Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd ya Arusha.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kukamilisha utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 785 mkoani hapa kwa asilimia 100 na sasa ni zamu ya vitongoji ambapo kiasi cha shilingi 16,717,407,821.65 kitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150,” alisema Mhandisi Nagu.

Tukio hilo lilishuhudiwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Nanyumbu, Mtwara na Tandahimba, Kamati za Usalama Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Masasi, Madiwani kutoka Kata mbalimbali Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. 

Akizungumza wakati wa utambulisho wa mkandarasi huyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala alizipongeza REA na TANESCO kwa kuendelea kushirikiana kuhakikisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia Nishati linatimia.

“Wana Mtwara tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwani kwa sasa hapa kila Kijiji kina umeme na sasa wanahakikisha umeme unafika vitongojini,” alisema.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme vitongojini, Mhandisi Nagu alisema kati ya vitongoji 3,427 vilivyopo Mkoani humo, vitongoji 2,200 vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 64 na kwamba vitongoji 150 ambavyo vitapata umeme kupitia mradi huo vitaongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme katika Mkoa wa Mtwara.

Aidha, alibainisha kuwa mradi huo ambao mkandarasi wake ametambulishwa, utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na hivyo kukamilika ifikapo Septemba 2026 na kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mhandisi Nagu alisema mradi utatekelezwa katika majimbo 10 katika wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala, Masasi na Nanyumbu na kwamba katika kila Jimbo Vitongoji 15 vitanufaika.

“Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara ikiwa na lengo la kuwapatia huduma za Nishati wananchi ili kuboresha huduma za jamii maeneo ya vijijini na vijiji-miji,” alisema Mhandisi Nagu.

Kwa upande wake Mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd, Samwel Lema alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi utatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na utakamilika ndani ya muda kama ilivyo katika mkataba.