ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 16, 2026

KAMATI BUNGE YARIDHISHWA MRADI FARU MWEUSI, MBWA MWITU

 Faru mweusi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imesema imeridhishwa na uwekezaji wa mradi wa uhifadhi wa faru mweusi na mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, na kuiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka husika kuendelea kuwalinda wanyama hao ambao walikuwa hatarini kutoweka.

Akizungumza Machi 15 baada ya kutembelea na kukagua mradi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mary Masanja, amesema kamati imefurahishwa na maendeleo ya mradi huo huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwalinda na kuwahifadhi wanyama hao adimu.

Alisema pia ni muhimu kuangalia uwezekano wa kuwahamishia faru katika hifadhi nyingine kadri idadi yao inavyozidi kuongezeka, ili kuwapa nafasi zaidi ya kuishi na kuongeza fursa kwa watalii kuwaona katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini.

“Mradi kwa sasa unaridhisha na ukizingatia kwamba faru ni mnyama aliyekuwa kwenye hatari ya kutoweka. Tunaendelea kuwaalika wananchi watembelee hifadhi hii, na kikubwa tumeielekeza Wizara kuwa mradi huu unahitaji matunzo endelevu. Pale ambapo idadi ya faru itaongezeka, waweze kusambazwa katika hifadhi nyingine ili watalii wanaotembelea maeneo hayo waweze kuwaona kwa urahisi zaidi,” alisema Masanja.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, alisema mradi huo wa faru uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.4 unalenga kuwahifadhi wanyama hao adimu ili waweze kuzaliana na kulinda urithi wa taifa.

Alisema pamoja na juhudi za uhifadhi, mradi huo pia umeongeza thamani ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, kwani watalii sasa wanaweza kufika katika eneo maalumu lenye uzio wa umeme na kupata fursa ya kuwaona faru kwa ukaribu zaidi.

“Kamati wameridhishwa na mradi huu na kutupa maelekezo ya kuendelea kuwalinda wanyama hawa pamoja na kuboresha zaidi mradi huu. Faru waliopo katika mradi huu wamefikia idadi ya 50, hivyo eneo la sasa linaanza kuwa finyu. Kamati imesisitiza kuongeza eneo la uzio, na sisi pamoja na mamlaka husika tunakwenda kulifanyia kazi kwa haraka ili wanyama wapate eneo kubwa zaidi la kuishi na utalii uendelee kuimarika,” alisema Abbasi.

Aidha, aliongeza kuwa Wizara pia inapanga kuongeza magari kwa ajili ya kuwahudumia watalii wanaotembelea eneo la faru pamoja na hifadhi kwa ujumla, kutokana na ongezeko kubwa la watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, hususan wale wanaokuja kuona faru.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo, Asia Halamga, alisema juhudi za Serikali zimewezesha kuongezeka kwa wanyama waliokuwa adimu kama faru na mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kufurahia na kuthamini urithi wa rasilimali za asili uliopo Tanzania.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment