ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, July 22, 2023

MAKALA:KAMPUNI YA TAIFA GESI YANUNGANA NA SERIKALI KUDHIBITI WIMBI LA UKATAJI WA MITI MKOA WA PWANI.

 


Na Victor Masangu,Pwani 

Mkoa wa Pwani umetajwa kuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na hii ni kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la wananchi kukata miti ovyo pamoja na kutumia kwa kasi matumizi ya mkaa hali ambayo imesababisha kila kukicha hali ya mazingira kuwa mbaya zaidi na maeneo mengine kuwa kama jangwa.

Mkoa wa Pwani umeonekana kinara zaidi kwa uharibifu wa mazingira na hii yote ni kutokana na  wananchi kuamua kwenda katika baadhi ya maeneo na kuamua kukata miti hiyo kwa ajili ya matumizi ya mkaa,pamoja na kuni kitu ambacho kinachangia zaidi hata kupotea kwa uoto wa asili.


Uchunguzi ambao umefanyika na mwandishi wa habari hizi umeweza kubaini kwamba katika baadhi ya halmashauri tisa ambazo zipo katika Mkoa wa Pwani baadhi yake zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mazingira kuharibika kutokana na changamoto hiyo ya ukataji wa miti ovyo na wengine bila hata ya kuwa na vibali maalumu.

Changamoto ya ukataji wa miti ovyo bila ya kuwa na vibali uchunguzi umebaini  nayo ndio imekuwa ni chanzo kikubwa ya baadhi ya watu hasa katika maeneo ya vijijini kwenda katika maeneo hayo na kukata miti kinyemela hasa katika nyakati za usiku na baada ya hapo kutumia miti hiyo kwa matumizi ya mkaa pamoja na kuni bila kujua madhara yake katika siku za zijayo.


Kutokana na hali hiyo pia imebainika kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakishirikiana na madereva wa pikipiki maarufu (boda boda) kwa ajili ya kusafirisha magunia ya mkaa hasa katika nyakati za usiku wakisafirisha magunia hayo kuyapeleka katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam kwa lengo la kuweza kujipatia kipato.


Pamoja na hali hiyo mwandishi wa habari hizi aliweza kujionea jinsi ya magunia zaidi ya nane hadi kumi yakiwa yamepakiwa katika baadhi ya  boda boda uku wakiwa wanatumia njia za vichochoroni ili kukwepa kukamatwa na mamlaka husika kwani wengine hawana vibali kwa kusafirisha nishati hiyo ya mkaa.

Lakini pamoja na serikali kupiga marufuku uharibifu wa mazingira ovyo bila kuzingatia sheria na taratibu lakini bado kuna baadhi ya madereva wa boda boda kuendelea kushirikiana na baadhi ya watendaji katika kuendelea kukata miti ovyo ili kuweza kupata kuni pamoja na mkaa bila ya  kujali kabisa athari zake.

Kutokana na kuendelea na wimbi hilo la ukataji wa miti ovyo umesababisha pia kwa kiasi kikubwa kuharibu miundombinu ya barabara kutokana na kuchimba mashimo makubwa kwa ajili ya kuweza kuchoma miti hiyo ili kupata mkaa bila kuangalia ni namna gani wananchi wenye makazi yaliyo jirani kutokana na kufuka kwa moshi wakati wa kuni au magogo hayo yanapochomwa moto.

Boda boda hao pia wamekuwa wakivunja sheria za barabarani huku wakiwa wamebeba magunia hayo mpaka wanashindwa kukaa vizuri katika kiti na wakati mwingine wamekuwa wakisababisha ajali na baadhi yao kupata majeraha na vilema vya kudumu kutoka na kazi hiyo wanayoifanya.


Baadhi ya madereva wa boda boda ambao wanajishughulisha na kusafirisha nishati hiyo ya mkaa kwa masharti ya kutotajwa majina yao wamesema kwamba wameamua kujikita katika kazi hiyo kutokana na kukabiliwa na changamoto ya fursa za ajira lakini serikali ikija na mpango wa kuwasaidia wapo tayari kuachana na uharibifu wa mazingira.


Wamesema kwamba wengi wao wamekuwa wakienda katika maeneo ya vijijini na kushirikiana na wahusika katika kukata miti hiyo kwa lengo la matumizi ya nishati ya mkaa pamoja na kuni ambazo zimekuwa zikitumika hasa katika maeneo ya vijijini.


"Kutokana na kazi hii ya kubeba magunia ya mkaa tunapitia changamoto nyingi sana ikiwemo kukamatwa na mamlaka husika TFS na wakati mwingine tunapewa adhabu na kutulipisha faini kwani tumeshakatazwa kufanya kazi hii bila ya kuwa na vibali kwa hiyo serikali ikiweka mazingira vizuri ya nishati mbadala basi sisi tupo tayari kwa matumizi mengine ya gesi,"wamebainisha boda boda hao.

Kadhalika wamebainisha kuwa baadhi ya boda boda hao wamesema kwamba rafiki zao wameshaamua kuachana kabisa na shughuli hizo za kusafirisha mkaa kutokana na kuona athari zake mbali mbali ikiwepo suala la kupata ajari na kukamatwa kila kukicha.

Wakitoa ushuhuda mwingine wameongeza kuwa wakati mwingine wamekuwa wakikimbizana na TFS na kusababisha kuanguka na mwisho wa siku wanataifishwa magunia hayo ya mkaa na hatimaye kujikuta wanaingia hasara kwani wakati mwingine wanapigwa na pikipiki kuchukuliwa.

Mmoja mwingine wa boda boda anayeishi Wilaya ya Kibaha amesema kuwa alishakumbwa na mkasa wa kukamatwa na TFS pindi alipokuwa amebeba mkaa na alipokonywa pikipiki yake lakini alipata msaada wa kupatiwa elimu juu ya matumizi mabaya ya uharibifu wa mazingira.


Aidha dereva huyo akusita baadhi ya wadau mbali mbali ambao waliweza kumsaidi kwa dhati kuweza kumpa elimu zaidi ya madhara ya uharibifu wa mazingira pamoja na umuhimu wa kutumia nishati mbadala ya Taifa gas ili kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa ambao wameachana kabisa na matumizi ya kuni pamoja na mkaa wamesema kuwa ujio wa uwepo wa nishati ya Taifa gas umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa changamoto ya uharibifu wa mazingira katika maeneo mbali mbali.

Pia wananchi hao wameishauri serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi hasa wa vijijini juu ya madhara ya ukataji wa miti ovyo sambamba na kuweka mipango madhubuti ya kuzalisha mitungi ambayo itakuwa na ujazo wa aina tofauti ili kumudu gharama za kununua.

Kwa Upande wao wadau wa mazingira katika Mkoa wa Pwani waliomba mamlaka zote zinazohusika ikiwemo TFS kuongeza nguvu zaidi katika kudhibiti hali ya uharibifu wa mazingira ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji kwa kushirikiana na wananchi wenyewe.

Pia hawakusita kuwatoa mawazo yao kwa kuwataka  Wakala wa misitu TFS kutokaa barabarani kwa ajili kuwakamata madereva wa boda boda na badala yake wafanye ziara katika maeneo husika lengo ikiwa ni kuwadhibiti wale wote ambao wanafanya uharibifu kwa kukata miti ovyo.


Katika kuliona hilo serikali imezindua kampeni maalumu ya utunzaji wa mazingira na matumizi sahihi ya nishati mbadala ambayo imezinduliwa hivi karibuni katika shule ya sekindari Ruvu ambayo itasaidia kuachana na matumizi ya mkaa na miti.

Kuzinduliwa kwa kampeni hiyo kwa kuanzia katika Mkoa wa Pwani imeanza kuzaa matunda kutoka na wadau wa mazingira,halmashauri mbali mbali kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mtaa na vijiji kuanza juhudi za kurudisha hali halisi kwa kuanza kupanda miti.

Pia kumekuwepo na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya hali nchi hivyo serikali kuzindua kampeni hiyo pia itaweza kuwa mkombozi kutokana na ushirikiano ambao umeshaanza kufanyika kuanzia ngazi za chini hadi ngazi za juu.

Nao baadhi ya mama lishe wanaofanya biashara zao katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Pwani wamenufaika na matumizi ya nishati mbadala ya gesi wamesema imeweza kuwasaidia kuondokana na kutumia kuni na mkaa kwani itasaidia kuunga juhudi za serikali katika kutunza mazingira.

Pia Mama lishe hao wameipongeza serikali kwa kuleta nishati mbadala na kuiomba iweze kubuni zaidi mitungi mingine midogo ambayo wataweza kuinunua kwa bei nafuu ili kuweza kuachana kabisa na matumizi ya mkaa na kuni.

"Baadhi yetu hapo awali sisi mama lishe katika miaka ya nyumba tulikuwa tunatumia kwa wingi matumizi ya kuni lakini wakati mwingine madhara yake ni makubwa kutokana na kupuliza moto hivyo ule moshi ulikuwa unatuingia kwenye kifua ni hatari kwa afya hivyo nishati hii mbadala ya gesi  ni sahihi zaidi,"wamesema mama lishe.

Katika kutekeleza kampeni hiyo serikali kupitia Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo amesema kwamba mpango huo utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuwahimiza wananchi waweze kutunza mazingira katika maeneo yao.

Aidha Waziri huyo amesisitiza kwa kunahitajika juhudi za ushirikiano kutoka kwa mamlaka mbali mbali zinazohusika ikiwemo TFS,WWWF, na wadau wengine wa mazingira ili kuweza kufanikisha zoezi la kampeni hiyo ikiwa pamoja na wananchi.


Jafo amebainisha kuwa kuwepo kwa nisgati mbada ya Taifa gesi kutaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kupunguza zaidi wimbi la ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira na kuongeza kuwa serikali itakuwa mstari wa mbele katika kutimiza azma ambayo imejiwekea ya kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Amebanisha hivi karibuni kampeni hiyo imezinduliwa Wilayani Kibaha katika shule ya sekondari Ruvu hivyo ni vema wahusika hususan Taifa gesi wanapaswa kuangalia namna ya kufunga mitambo katika shule za sekondari ili waweze kutumia nishati hiyo mbadala.



"Hivi karibuni niliweza kupata fursa ya kuhudhuria uzinduzi wa kampeni ya utunzaji wa mazingira kwa hivyo sisi kama serikali  ninawaomba wahusika aa Taifa gesi kuweka mipango ya kufunga mitambo ya gesi katika shule mbali mbali za sekondari na taasisi za umma hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira,"amesema Waziri Jafo.



Amefafanua kuwa ana imani kwamba mitambo hiyo ya gesi ikifungwa katika shule hasa za bweni kutakuwa ni njia moja wapo ya juhudi za kupunguza wimbi la ukataji wa miti ovyo na kuondokana na matumizi ya mkaa pamoja na kuni ambapo pia itapunguza gharama za matumizi.


Dk. Jafo amesema kwamba pia kuzinduliwa kwa kampeni hiyo ya utunzaji wa miti   pia itasaidia  kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamekuwa na athari katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo katika Mkoa wa Pwani.

"Bado kuna shule za sekondari bado kwa sasa zinaendelea na matumizi ya nishati ya kuni pamoja na mkaa lakini nina imani kampeni itaweza kuleta mabadiliko chanya ya kuweza kutumia nishati mbadala kuliko kutumia kuni kwani ndio chanzo cha uharibifu wa mazingira,"anasisita Jafo.



Waziri Jafo ameipongeza kwa dhati juhudi ambazo zimefanywa na Kampuni ya Taifa gesi kwa kuanza utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya Nishati Mbadala kwa kuanza kufunga mtambo wa gesi katika shule hiyo.


Jafo meongeza kwamba kati ya mikoa  minne hapa nchini ambayo imeathirika kwa uharibifu wa Mazingira Pwani ni mojawapo ambapo alimpongeza Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge kwa jitihada anazozifanya za kusimamia kampeni ya kupanda miti.


Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewasisitiza zaidi wananchi wa Mkoa wa Pwani na hawatajikita kwenye matumizi ya nishati mbadala mabadiliko ya tabia ya nchi yataendelea kuleta athari kubwa.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson Saimon amebainisha changamoto kubwa iliyopo ya Wilaya yake ipo karibu jirani na Jiji la Dar es Salaam hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira.

Mkuu huyo alisema kuwa hata hivyo bado kuna juhudi za makusudi ambazo zimeshaendelea kufanyika katika kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linafanyika katika halmashauri zote ikiwemo kupanda miti katika maeneo ambayo yameathiliwa zaidi.


 Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakar Kunenge amewataka viongozi na watendaji wote wakiwemo wa Chama kuhakikisha wanatekeleza maelekezo yote ambayo yanatolewa na Rais wavawamu ya sita Dkt.Samia Suluhu katika kujikita katika kupambana na ukataji wa miti ovyo.

"Maagizo ambayo yanatolewa lazima tuyafangie kazi likiwemo hili la Mkoa wetu kukabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na katika hili mimi naomba tulifanyie kazi kuanzia katika ngazi za chini hadi za juu," anasema Kunenge.



Pamoja na hayo Kunenge amewahiza wananchi wote kuachana kabisa na vitendo vya uharibifu wa mazingira  kwa kukata miti na kuchoma mkaa na badala yake  kujikita zaidi kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili.


Mkuu huyo wa Mkoa anasema katika kutimiza mpango wa serikali kwa Sasa tayari wameshaendelea kufanya kampeni ya utunzaji wa mazingira ambapo wameshafanikiwa kupanda miti zaidi ya milioni 9.7.



Katika hatua nyingine anasema kwamba kampeni hiyo ambayo imezinduliwa katika Mkoa wake utaweza kuleta matokeo chanya katika suala zima la kupambana wimbi la ukataji wa miti kiholela na kuweka mipango zaidi katika kupanda miti na kutunza mazingira.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo katika kuunga mkono juhudi za serikali wamepiga marufuku kwa madereva wa boda boda kupakia magunia ya mkaa na kutasafirisha kuelekea Jijini Dar es Salaam.

Kamanda huyo anasisitiza kuwa kumekuwepo kwa ajali nyingi ambazo chanzo chake kinasababishwa na na baadhi ya madereva wa  boda boda kuvunja sheria za barabarani huku wakiwa wamepakia nishati hiyo ya mkaa zaidi ya magunia name.

Jeshi hilo la Polisi Mkoa wa Pwani limesema litaendelea kudhibiti upakiaji holela wa mkaa huo pamoja na kuwakamata wale wote ambao watabainika kwenye kinyume na kuongeza wataendelea kutoa elimu kwa madereva hao juuu ya madhara ya ukataji miti.

Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga  na Rufiji  nao hakusita kuzungumzia madhara ambayo yamewakumba kutokana na tatizo la ukataji wa miti ikiwemo suala la uharibifu wa mazingira pamoja na kupoteza uoto wa asili.


Hivi karibu serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Taifa gasi ilizundua kampeni maalumu kwa ajili ya utunzaji wa mazingira pamoja na matumizi ya nishati mbadala iliyofanyika katika shule ya sekondari Ruvu Wilayani Kibaha mkoani Pwani lengo ikiwa ni kuondokana na kuthibiti matumizi ya kuni na mkaa.

MAFUNZO MAALUMU YA MATIBABU YA UTAPIAMLO MKALI KWA WATOTO YATOLEWA KWA WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO

 Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo Dkt Mohamed Salehe wa tano  kulia mwenye koti akifuatilia kwa umakini  Mafunzo Maalumu yanayohusu matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto yametolewa kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo

Sehemu ya washiriki wa mafunzo wakifuatilia 
Daktari wa Wodi ya Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo Dkt Mwalimu Khalid


Na Oscar Assenga,TANGA.

MAFUNZO Maalumu yanayohusu matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto yametolewa kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo huku yakielezwa kuwa yatakuwa na umuhimu mkubwa kwao.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili,Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo Dkt Mohamed Salehe alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi wakati wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Dkt Mohamed ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga alisema baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo anaimani kwamba washiriki wanakwenda kuwa chachu katika utoaji wa huduma.

Mafunzo hayo yamewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwem kutoka Ustawi wa Jamii, Madaktari, Manesi na maafisa lishe ambayo yanatajwa kwamba yatakuwa chachu katika utoaji wa huduma

Alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa natharia na vitendo huku washiriki wakionekana kuwa na uelewa mzuri na walimu wamekuwa wakitoa mafunzo ya kuwaezesha kutoa matibabu kwa watoto wenye utampiamlo.

“Unampomtibu mtoto mwenye tatizo la utapiamlo linahitaji watu wote waweze kusaidiana na chimbuko la hasa na sababu kuweza kujulikana na kumtibu ndio moja njia pekee ya kuweza kumuondolea huyo mtoto tatizo hilo”Alisema

Dkt Mohamed alisema akiwa ametibiwa Hospitali lakini pia akirudi nyumbani awe ametibika moja kwa moja ikiwemo kupewa matunzo wanaporudi nyumbani baada ya kumaliza matibabu.

“Pamoja na kwamba wanatibiwa Hospital wanahitaji matunzo huko nyumbani watoto wanakaa na wazazi hivyo ni kuwapa mafunzo ya namna ya kuwalea watoto kama hao kwani wanaweza kuwa kama wengine na ndoto zao ila mafunzo kwa wazazi ni jambo la muhimu”Alisema

Awali akizungumza wakati wa mafunzo hayo Afisa Lishe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo Imakula Mwamrefu alisema wapo kwenye mafunzo maalumu yanayohusu matibabu kwa watoto wenye utapiamlo mkali wanaozaliwa katika hospitali hiyo.

Alisema kwamba kwenye hospitali hiyo wana kitengo ndani ya wodi ya watoto 13 na 14 kinachohusika kwa matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto hivyo kutokana na hilo wameona wawe na mafunzo ya kujengeana uwezo namna ya kuwatibu watoto wanapofika hospitalini.

Hata hivyo alisema kwamba mafunzo hayo yatakuwa kwa njia ya kuelekezana na vitendo kuona namna ya kutambua utapiamlo mkali

Naye kwa upande wake Daktari wa Wodi ya Watoto katika Hospitali hiyo Dkt Mwalimu Khalid alisema kwamba mafunzo hayo ya matibabu kwa watoto wenye utapiamlo mkali ni muhimu kutokana na kwamba wanakuwa na miili yenye mabadiliko hivyokuna na utofauti jinsi ya kuwatibu ukilinganisha na wale wa kawaida.

Alisema hiyo kuna umuhimu wa madaktari na manesi wanaopokuwa na wajibu wa kuwaangalia hao watoto wanatakiwa kueleza mafunzo hayo kutokana na watoto hao wanatibiwa tofauti na wengine hivyo daktari anaweza kuwa mzuri sana kutibu watoto lakini akimpata mtoto kama huyo kama hajapata mafunzo anaweza kumtibu tofauti.

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WAASWA KUZINGATIA SHERIA ZA MADINI KUPUNGUZA MIGOGORO - NYAMONGO

 



 Na Mwanahamisi Msangi, Mara 

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Henry Mditi amewaasa Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini Nchini kuzingatia Sheria, Usalama, Utunzaji wa Mazingira na Matumizi salama ya baruti katika uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini ili kupunguza migogoro isiyokuwa na tija migodini.

Mhandisi Mditi ameyasema hayo leo Julai 21, 2023 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Usalama, Afya,Utunzaji wa Mazingira na matumizi salama ya baruti kwa wachimbaji wadogo wa madini, yaliyofanyika Wilayani Tarime  mkoani Mara ambayo yameshirikisha pia  Wakurugenzi, Mameneja, Watumishi kutoka Tume ya Madini, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Viongozi wa Wachimbaji Wadogo na Wachenjuaji wa Madini pamoja na Wafanyabiashara na wamiliki wa migodi wa eneo la Nyamongo.

Mhandisi Mditi amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji, na biashara ya madini zinafanyika kwa kuzingatia Usalama, Afya na Utunzaji wa mazingira kwa kufuata Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa.

“Tunatambua kwamba shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini zina manufaa mbalimbali kwa mchimbaji, wananchi na Taifa kwa ujumla kupitia fursa za ajira, biashara na mapato mbalimbali kwa serikali,” amesema Mhandisi Mditi.

Amesema kuwa mafunzo hayo yameangazia pia utaratibu wa utoaji leseni za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini hususan kwenye usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini.

" Ni muhimu shughuli hizo kufanyika kwa kuzingatia Usalama, Afya na Utunzaji wa mazingira ili kuzifanya kuwa endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo, hivyo mafunzo haya yatiliwe mkazo namna ya kuepuka na ajali migodini, utunzaji wa mazingira, afya na matumizi sahihi ya baruti." amesema Mhandisi Mditi.

 Ameongeza kuwa, “Kupitia mafunzo haya naamini mna wajibu mkubwa wa kuimarisha mfumo wenu wa utendaji kazi kwa kuangalia usalama katika maeneo mnayochimba ili kuhakikisha kuwa taifa halipotezi nguvu kazi ili tuwe na uchimbaji endelevu wa kuimarisha maisha yetu na jamii inayotuzunguka,"

Wachimbaji wa madini 105 kutoka eneo la Nyamongo Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara wameshiriki mafunzo hayo ya siku moja ambapo, wametakiwa kuepuka utoroshaji wa madini kwani kwa kufanya hivyo watasababisha Serikali kukosa mapato na kushindwa kutoa  huduma za msingi za kijamii zenye tija ikiwemo elimu bure na afya.

Thursday, July 20, 2023

NYAMOGA AMSHUKURU NYALUSI KWA KUCHANGIA MILIONI KUMI KWA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO.

 

Mbunge wa Jimbo La Kilolo  Justine Nyamoga akimshukuru Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa  Nancy Nyalusi kwa kuchangia shilingi millioni kumi kwaajili ya kuanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kijiji cha Kimala wilya ya Kilolo
Mbunge wa Jimbo La Kilolo  Justine Nyamoga akimshukuru Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa  Nancy Nyalusi kwa kuchangia shilingi millioni kumi kwaajili ya kuanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kijiji cha Kimala wilya ya Kilolo

Na Fredy Mgunda,Kilolo

Mbunge wa Jimbo La Kilolo Mhe Justine Nyamoga amemshukuru Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa Mhe Nancy Nyalusi wa kuchangia shilingi millioni kumi kwaajili ya kuanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto.

Nyamoga amemshukuru nyalusi leo katika kijiji cha kimala kata ya kimala wakati akifanya mkutano na wananchi wa kijiji hicho ambapo hadi sasa wamama wajawazito walikuwa wanaenda umbali mrefu kwaajili ya kupata huduma 

“ Poleni sana wanakijiji wa kijiji cha Kimala kwa kupata changamoto hii ya kwenda umbali mrefu hadi Kidabaga kwaajili ya kupata huduma mimi nitatoa shilingi milioni kumi kwaajili ya ujenzi wa zahanati na naomba ujenzi huu uanze mara moja kwasababu fedha sasa ipo “ Amesema Nyalusi

Hatahivyo Nyamoga amewataka wananchi waweze kushiriki katika ujenzi wa zahanati hiyo ili ijengwe kwa haraka sana ili iweze kuwa msaada kwa kina mama


UWT TAIFA WAIPONGEZA NACHINGWEA KWA KUTEKELEZA ILANI YA CCM KAMA INAVYOTAKIWA

 

Mwenyekiti wa UWT taifa Merry Chatanda katika akiongea mara baada ya kukagua mradi wa RUWASA wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi na kuridhika na mchakato wake
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na mwenyekiti wa UWT taifa Merry Chatanda wakikagua kichomea taka katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na mwenyekiti wa UWT taifa Merry Chatanda akipata maelezo kutoka kwa mhandisi wa RUWASA Nachingwea Sultan Ndolwa akielezea namna ambavyo serikali ya awamu ya sita ikiwa na nia ya kumtua mwanamke ndoo kichwani



Na Fredy Mgunda,Nachingwea


UMOJA wa wanawake wa chama cha mapinduzi (UWT) wameupongeza uongozi wa wilaya ya Nachingwea Kwa kutekeleza miradi vizuri kama ambavyo ilani ya CCM inavyotaka.

Akizungumza wakati akikagua miradi ya maendeleo mwenyekiti wa UWT taifa Merry Chatanda alisema kuwa amekagua miradi ya maji, ujenzi wa magengo mapya katika hospital ya Nachingwea pamoja,ujenzi wa ofisi ya CCM wilaya Nachingwea na mradi wa kimaendeleo wa UWT Nachingwea wameiona inaendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Chatanda alisema kuwa serikali ya wilaya ya Nachingwea inayoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Mohamed Hassan Moyo imekuwa makini kwa kufanya kazi Kwa umakini mkubwa.

Alisema kuwa chama cha mapinduzi wilaya ya Nachingwea inafanya kazi vizuri na kwa ushirikiano mkubwa na serikali ya wilaya hiyo na kuleta maendeleo ya wananchi kama ambavyo ilivyojionea.

Mwenyekiti wa UWT taifa Merry Chatanda alisema kuwa RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia suluhu Hassan anafanya kazi kubwa hivyo wananchi na Wanachama wa CCM wanatakiwa kumsemea mema anayoyafanya Kwa watu ambao wanambeza.

BENKI YA CRDB YAZINDUA SimBanking App MPYA INAYOTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA KUTAMBUA MAHITAJI YA WATEJA NA KURAHISISHA MIAMALA

 

 
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa SimBanking App inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi inayowezesha kutambua mahitaji ya wateja na kurahisiha hudumana miamala yenye muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence), iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo tarehe 19 Julai 2023.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akiwa mbele ya kifaa kinachotumia teknolojia ya kisasa zaidi inayowezesha kutambua mahitaji ya wateja na kurahisiha huduma na miamala yenye muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence) ambayo inatumika katika SimBanking App mpya iliyozinduliwa leo katika hafla , iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo tarehe 19 Julai 2023.
 
===========   =========   ========== 
 
Wakati dunia ikishuhudia mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayochagiza maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha, leo Benki ya CRDB inayoongoza kwa ubunifu nchini imezindua SimBanking App inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi kutambua mahitaji ya wateja.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema SimBanking App hii mpya imetengenezwa kwa muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence).
“Teknolojia iliyotumika katika SimBanking App hii inampa uwezo mteja kuchagua mpangilio wa huduma kwa namna ambavyo yeye mwenyewe angependelea, teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kutambua ni huduma gani mteja anapendelea zaidi na kumrahisishia namna ya kuipata,” alisema.
 
Nshekanabo alibainisha kuwa teknolojia hiyo mpya ni ya kimapinduzi katika kufikisha huduma za fedha kwa wateja kwani itaongeza wigo wa huduma zinazoweza kutolewa kidijiti huku kasi ya miamala ya wateja ikirahishwa kwa kiasi kikubwa.
 
“Eneo jingine ambalo tumelipa uzito mkubwa katika SimBanking App hii mpya ni ulinzi na usalama wa taarifa na miamala ya wateja. Tunatumia teknolojia ya biometriki kuhakikisha usalama kwa wateja. Hii inatufanya kuwa Benki pekee nchini na kati ya chache barani Afrika inayotumia teknolojia hii,” aliongezea Nshekanabo.
Akizungumzia huduma mpya ambazo zimeongezwa, Meneja Mwandamizi wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu wa Benki ya CRDB, Jacklina Jackson amesema SimBanking App inatoa fursa za uwekezaji kwa wateja kwa kuwawezesha kuwekeza kupitia akaunti za uwekezaji (Fixed Deposit) kidijiti.
 
“Wateja pia sasa hivi wanaweza kupanga uhamisho wa fedha na malipo yanayojiruida au ya mara kwa mara kwa urahisi. Uhamisho unaweza kupangwa kila siku, kila wiki au kila mwezi. Tumeboresha upande wa kumbukumbu za taarifa ya miamala ambapo wateja wanaweza kupata risiti ya miamala yote wakati wowote kwa urahisi,” alisema Jacklina.
 
Katika upande wa malipo, alisema SimBanking App imeboresha malipo kupitia watoa huduma za kidijiti kwa kuwezesha ukusanyaji wa malipo kupitia programu hiyo ambapo mteja ana uwezo wa kutoa ruhusa ya malipo kwa kutumia mfumo wa namba ya siri ya mara moja (one time passcode). 
“Vilevile tumefanya maboresho katika huduma za bima kwa kuongeza kasi na muda wa upatikanaji wa huduma,” aliongezea Jacklina kuhusu huduma hiyo ya bima za vyombo vya moto ambayo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza kupitia SimBanking App mwaka 2020 benki ilipofanya maboresho.
 
Aidha, SimBanking App mpya inakuja na programu ya uaminifu (loyalty program) inayowawezesha wateja kupata kupata alama wanapotumia application na kisha kujishindia zawadi. Wateja pia aplikesheni hii mpya pia inatoa fursa kwa wateja kutoa maoni yao kila wakati wanapokamilisha miamala mfumo unaohusisha uwasilishaji wa maandishi na matumizi ya emoji kuonyesha hisia juu ya huduma.
 
Hii ni mara ya pili kwa Benki ya CRDB kufanya maboresho makubwa katika huduma ya SimBanking baada ya maboresho yaliyofanyika mwaka 2020. Tarifa ya Benki hiyo inaonyesha sasa hivi asilimia 96 ya miamala yote inafanyika kidijitali huku SimBanking ikichangia sehemu kubwa.
 
Huduma ya SimBanking ambayo ilianzishwa mwaka 2022 imekuwa ikitajwa kuwa moja ya huduma bora zaidi za kidijitali ambazo zinatoa mchango mkubwa katika ujumuishi wa kifedha nchini na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi. 
 
SimBanking imepata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo tuzo za Consumer Choice Awards, tuzo za za Global Finance zinazotolewa nchini Marekani, na hivi karibuni imepata tuzo ya huduma bora ya kidijitali katika tuzo za Tanzania Digital Awards.




Wednesday, July 19, 2023

WAZIRI NAPE AMUWAKIA TUNDU LISSU ''ETI MAWAZO YA RAIS NI MATOPE'' TUTAKUONYESHA TUNDU LISSU

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

JEH Kwa kauli za Tundu Lissu inafaa kumuita Rais Samia Rubish ikiwa - Sept 7 alipopigwa risasi, Samia akiwa Makamu wa Rais kwa Serikali ya awamu ya Tano iliyoongozwa na Hayati JPM, Samia ndie kiongozi pekee wa kitaifa alieenda kumsalimia jijini Nairobi bila kujali Boss wake kipindi hicho angelichukuliaje jambo hilo. - Feb 2022 Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Rais wa Nchi alimuomba Tundu Lissu akutane nae Ubelgiji na kutoa maelekezo, arudishiwe stahiki zake zote zilizokua zimezuiliwa akiwa kama Mbunge na akarudishiwa ikiwemo kulipiwa madeni ya matibabu na Tundu Lissu alithibitsha hilo. - Mama samia akiwa rais karudisha demokrasia na tunaona vyama mbalimbali wanakosoa serikali na kutoa maoni yao. JE HAYA YOTE YANAFAA RAIS SAMIA KUITWA RUBBISH?

TUME YA MADINI YATOA SIKU SABA KWA WAMILIKI WA LESENI KUTEKELEZA MASHARTI

 










 Dodoma Julai 19, 2023 

Tume ya Madini imetoa siku saba kwa wamiliki wote wa leseni za madini zikiwemo leseni za utafutaji wa madini, leseni za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa wa madini, leseni za uchenjuaji wa madini, leseni za uyeyushaji wa madini na leseni za usafishaji wa madini kuhakikisha wanatekeleza masharti  ya leseni zao kwa mujibu wa Sheria.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa ya Sekta ya Madini.

Amesema kuwa, zipo kampuni za  madini ambazo zimeaminiwa na Serikali kwa kupewa leseni za madini lakini wamekuwa wakikiuka masharti ikiwa ni pamoja na kutoendeleza maeneo ya uchimbaji wa madini hivyo kukosesha fursa kwa waombaji wengine wenye nia ya kuchimba madini na Serikali kupata mapato yake.

“ Tumetoa muda wa siku saba ( kuanzia tarehe 19 hadi 25 Julai, 2023 kwa wamiliki wote kutekeleza masharti ikiwa ni pamoja na wamiliki wote wa leseni za madini ambao leseni zao zimetoka lakini hawajazichukua kuhakikisha wamezichukua, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka kuhakikisha wamelipia na leseni ambazo hazijaendelezwa kuhakikisha zinaendelezwa ndani ya muda ulioainishwa sambamba na kuwasilisha taarifa ya kuanza kazi na taarifa za kila robo mwaka kuwasilishwa,” amesema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amewataka waombaji wote wa leseni za madini wenye mapungufu kurekebisha mapungufu hayo ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi, maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi  na ada ya pango kwa mwaka.

Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa wamiliki au waombaji wa leseni watakaoshindwa kurekebisha mapungufu ndani ya muda wa siku saba, Profesa Kikula amefafanua hatua hizo kuwa kwa leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka, leseni ambazo haziendelezwi na leseni ambazo  zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria na kwa maombi yote ya leseni ambayo hayakidhi vigezo, yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.

Aidha, Profesa Kikula amesisitiza kuwa dhumuni la Serikali ni kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wawekezaji wote nchini na kuongeza kuwa Serikali haitamfumbia macho mwekezaji wa ndani au kutoka nje ya nchi ambaye ameshikilia maeneo bila ya kuyaendeleza au kuyatumia maeneo hayo kujipatia fedha kisha kuwekeza nje ya nchi.

Pia, Profesa Kikula ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika madini ya kimkakati yanayohusika katika utengenezaji wa vifaa vya kisasa na kieletroniki ikiwemo magari yanayotumia umeme ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Wakati huohuo, Profesa Kikula ameongeza kuwa Serikali imekamilisha kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii za mwaka 2023 ambazo zitasaidia wamiliki wa leseni kuwa na mwongozo wa namna bora ya kutoa huduma kwa jamii zinazozunguka migodi yao.